Categories
Habari

Wauguzi waagizwa kusitisha mgomo wao na kurejea kazini mara moja

Ni afueni kwa Wakenya baada ya chama cha kitaifa cha wauguzi (KNUN) kusitisha mgomo wa wauguzi uliodumu kwa karibu miezi mitatu.

Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako ametaja agizo la Jaji Maureen Onyango kuwa sababu ya kusitisha mgomo huo na akawataka wahudumu wa afya kurejea kazini kufikia Alhamisi, saa kumi na moja jioni.

Chama cha matabibu nchini pia kilitoa sababu iyo hiyo kilipositisha mgomo wake siku ya Jumanne.

“Wale wahudumu wa afya wote wakiwemo wauguzi ambao wanashiriki mgomo warudi kazini mara moja. Na pia [Jaji Onyango] akaagiza kwamba zile nidhamu zozote ambazo serikali zilikuwa zimewapa wale ambao wanashiriki mgomo zimesimamishwa,” akasema Panyako.

 Panyako hasa amewaarifu wauguzi katika Kaunti za Taita Taveta, Kisumu, Kisii na Busia kwamba madai yote ya kufutwa kazi na kufurushwa kutoka nyumba zao yalisitishwa na mahakama na hivyo basi wapasa kurejea kazini bila kukosa.

Amewahakikishia wauguzi kwamba chama hicho kitaendelea kushinikiza masuala ya wahudumu wa afya ambayo waliwasilisha kwenye ilani yao ya mgomo kupitia mahakama kwani kamati za mashauriano zimeagizwa kuwasilisha ripoti mahakamani katika muda wa siku 30.

Wauguzi waligoma tarehe 7 mwezi Disemba mwaka wa 2020 wakilalamikia mazingira duni ya kikazi na marupurupu.

Categories
Habari

Wauguzi 69 wafurushwa kutoka nyumba za serikali ya Kaunti ya Taita Taveta

Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta imeanza operesheni ya kuwafurusha wauguzi 69 kutoka kwa nyumba za serikali baada ya muda wa kuhama waliopewa kukamilika.

Wauguzi hao ni sehemu ya wahudumu wa afya zaidi ya 400 ambao wamegoma tangu mwezi Desemba mwaka uliopita.

Maafisa wa serikali ya kaunti hiyo wamevamia jengo wanamoishi wauguzi hao na kuanza kuwafurusha pamoja na familia zao.

Kundi la maafisa hao lilikuwa likitembea kutoka nyumba moja hadi nyengine wakiwatoa kwa nguvu wauguzi hao pamoja na vyombo vyao vilivyokuwa ndani.

Wakati wa operesheni hiyo, maafisa hao pia wamehakikisha kwamba nyumba hizo ambazo wauguzi hao walikuwa wakiishi zimefungwa baada ya kuwatoa.

Operesheni sawia na hiyo pia ilikuwa inatekelezwa sambamba katika Kaunti Ndogo za Voi, Mwatate, Wundanyi na Taita.

Huko Voi, wauguzi waliofurushwa walikuwa wanahangaika huku wakitafuta makazi mapya na kuitaja hatua hiyo kuwa ya kinyama.

“Hatukupewa hata ilani ya kutoka. Wamewasili tu na kutufurusha,” akasema mmoja wa waathiriwa hao.

Hata hivyo serikali ya kaunti hiyo, kupitia Waziri wa Afya John Mwakima, imekanusha madai hayo na kusema kwamba walitoa ilani na kuwapa wauguzi hao hadi tarehe 5 Februari watafute makazi kwengine.

Mgomo huo wa wahudumu wa afya ulianza mwishoni mwa mwaka uliopita na kulemaza huduma za afya katika kaunti hiyo.

Huduma za maabara na kutoa ushauri ndizo zinazopatikana baada ya madaktari na wafanyikazi wa maabara kutamatisha mgomo wao kufuatia maelewano na serikali hiyo.

Categories
Habari

Magavana waapa kuwapiga kalamu wahudumu wa afya wanaogoma

Magavana wametishia kuwaachisha kazi wahudumu wote wa afya wanaogoma iwapo hawatarejea kazini mara moja.

Magavana hao pia wamefichua kwamba watasambaza majina ya wafanyanyikazi wote watakaofutwa kazi kufuatia mgomo huo katika kaunti zote ili wasiajiriwe tena kwenye kaunti zengine.

Kwenye kikao na wahariri wa habari, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya ameutaja mgomo huo kuwa kinyume cha sheria.

“Tumesikitishwa na uamuzi wa muungano wa wahudumu wa afya kutekeleza mgomo ambao umedumu kwa mwezi mmoja licha ya janga [la COVID-19] na maagizo ya mahakama. Tunaichukulia hatua hii kuwa kinyume cha haki ya maisha na ya kupata viwango vya juu zaidi vya huduma ya afya kama inavyohakikishwa katika katiba,” akasema Oparanya.

Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega, amesema wahudumu hao walipaswa kutamatisha mgomo wao ili kusubiri matokeo ya mashauriano kati ya Wizara ya Leba na ile ya Afya.

Gavana huyo amesema swala la nyongeza ya mishahara kama wanavyodai wahudumu hao ni jukumu la Tume ya kuratibu mishahara ya watumish wa umma, SRC na Wizara ya Fedha nchini.

Oparanya ameongeza kuwa serikali za kaunti zimejitolea kuhakikisha maslahi ya wahudumu wa afya yameshughulikiwa lakini akatahadharisha kuhusu matakwa mengi ya wahudumu hao kwani uchumi wa nchi hii umeathiriwa pakubwa na janga la COVID-19.

Baadhi ya serikali za kaunti, ikiwemo ile ya Mombasa, tayari zimechukua hatua ya kuwaachisha kazi wahudumu wa afya wanaogoma.

Categories
Habari

Muungano wa Watumishi wa Umma wamtaka Rais Kenyatta atatue mgomo wa wahudumu wa afya

Muungano wa Watumishi wa Umma nchini sasa unamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati kwenye mgomo unaoendelea wa wahudumu wa afya ili kupata suluhu la kudumu.

Maafisa wa muungano huo waliozungumzia athari mbaya kwa vituo vya afya ya umma pia wametoa wito kwa pande husika kulegeza misimamo kwa ajili ya Wakenya wanaoteseka.

Wakiongozwa na Naibu Katibu, Jerry Ole Kina, maafisa hao wametoa wito wa mashauriano baina ya pande husika, wakikariri kwamba msimamo huo mkali unawaathiri Wakenya maskini.

Muungano huo umemkosoa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwa kutishia kuwafuta kazi wahudumu wa afya wanaogoma, ukisema iwapo hatua hiyo itatekelezwa itaathiri vibaya sekta ya afya ambayo tayari inakumbwa na changamoto.

Ole Kina amesema changamoto zinazowakumba wahudumu wa afya zilitokana na ugatuzi na suluhisho linaweza kupatikana kwa njia ya mashauriano kati ya serikali kuu na zile za magatuzi.

Wauguzi na matabibu waligoma mnamo tarehe saba mwezi huu wakishinikiza, miongoni mwa maswala mengine, marupurupu ya mazingira hatari ya kazi na hali bora za kazi huku wakiongoza katika vita dhidi ya janga la COVID-19.

Madaktari pia walijiunga kwenye mgomo huo Jumatatu wiki hii wakitoa shinikizo sawa na hizo.

Categories
Habari

Mgomo wa madaktari sasa wanukia

Huduma kwenye Sekta ya Afya huenda zikasambaratika kuanzia usiku wa manane endapo madaktari ambao ni wanachama wa Chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno, KMPDU, watatekeleza tishio lao la kugoma.

Madaktari hao wamesema kuwa mazungumzo baina yao na serikali yamegonga mwamba na hivyo watajiunga na wauguzi na matabibu ambao walianza mgomo wao wiki mbili zilizopita.

Madaktari wanaotarajiwa kugoma ni pamoja na wataalamu wa matibabu, madaktari wa meno, wakurugenzi wa afya katika kaunti, wataalamu wa dawa na madaktari walio mafunzoni.

Wahudumu hao hawatafika kazini kesho baada ya mazungumzo kuvurujika walipoahirisha mgomo wao kwa siku 14.

Mgomo wa madaktari huenda ukasadifiana na ule wa wauguzi na matabibu ambao umedumu kwa siku 14.

Maafisa wa matibabu wamedumisha kuwa wataendelea na mgomo wao licha ya onyo la Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, kwamba watafutwa kazi kwa kukaidi agizo la mahakama la kuwataka warudi kazini.

Wahudumu wa afya wamegoma ili kushinikiza wapewe vifaa bora vya kujikinga na maambukizi, wale walio na changamoto fulani wasiwe kwenye msitari wa mbele, wawe na bima kamili ya matibabu, kuwalipa mshahara wahudumu waliopelekwa katika serikali za kaunti chini ya mpango wa afya kwa wote na kuwianishwa kwa marupurupu ya kuhudumu katika mazingira hatari, miongoni mwa matakwa mengine.

Categories
Habari

Madaktari kuanza mgomo wao Jumatatu huku wauguzi nao wakidinda kurejea kazini

Chama cha Kitaifa cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU) kimetangaza kuwa madaktari wote watagoma kuanzia Jumatatu baada ya mashauri na serikali kugonga mwamba.

Kwenye taarifa ya umma, chama cha KMPDU kimesema hatua hiyo inatokana na masuala ambayo hayajasuluhishwa baada ya mashauriano ya miezi minane.

“Madaktari watasitisha huduma zao kutokana na masuala ambayo hayajasuluhishwa baada ya miezi minane ya mashauriano kati ya KMPDU na serikali,” imesema taarifa hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo, makundi ya madaktari watakaogoma kuanzia tarehe 21 mwezi huu ni wanagenzi wa matabibu, wanagenzi wa taaluma ya dawa, wanagenzi wa taaluma ya wataalamu wa meno na matabibu.

Wengine ni wataalamu wa dawa, wataalamu wa matibabu ya meno, wataalamu wa utoaji huduma maalum za matibabu na wasimamizi wote wa maafisa wa huduma za utabibu.

Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuwaonya wahudumu wa afya wanaogoma kurejea kazini la sivyo wafutwe kazi.

Wauguzi na matabibu wamekuwa wakigoma tangu Jumatatu juma lililopita, wakishinikiza bima bora ya afya na kupewa vifaa vya kujikinga wanapokuwa kazini, miongoni mwa masuala mengine.

Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako amepuuzilia mbali agizo la Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuwa warejee kazini.

Panyako alikuwa akiongea huko Kakamega wakati wa mazishi ya Wycliffe Alumasa, ambaye ni muuguzi aliyepoteza maisha yake kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Alisema hakuna agizo lolote la mahakama ambalo litawalazimisha kurejea kazini kuambatana na mazingira yaliyoko sasa, ambapo hakuna vifaa vya kujikinga wala mpango wa bima ya matibabu.

Categories
Habari

Kamati ya Bunge kuhusu Afya yaandaa kikao cha kutatua changamoto za sekta ya afya nchini

Kamati ya Bunge kuhusu afya inatarajiwa kukutana na wadau wa sekta ya afya katika juhudi za kutafuta suluhisho la mzozo unaoendelea katika sekta hiyo humu nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Sabina Chege amesema kuwa watakutana na maafisa kutoka Wizara ya Afya, wawakilishi wa kaunti na maafisa kutoka vyama mbali mbali vya wahudumu wa afya ili kujadili swala hilo.

Chege, ambaye ni Mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Muranga, amesema kuwa  kulaumiana kunapaswa kukomeshwa na suluhisho la haraka kupatikana ili kuwaepusha Wakenya na mateso na kero ya kutafuta huduma za afya, kutokana na mgomo wa wauguzi na matabibu unaoendelea.

“Inasikitisha kwamba Wakenya hawawezi kupata huduma za matibabu kwa sababu ya mchezo wa lawama. Tunataka kuwasikiza washirika wote na tutambue shida ilipo, na pia nawasihi wahudumu wa afya wanaoendelea na mgomo kuwatilia maanani Wakenya maskini na wawe tayari kwa mashauriano,” akasema Chege.

Chege amesema kuwa fedha zilizotengewa juhudi za kupambana na janga la COVID-19 zinaweza kutumika kutatua baadhi ya changamoto zinazowakumba wahudumu wa afya wanaogoma.

Mwenyekiti huyo pia amesema itakuwa vyema kama vifaa vya kujikinga kutokana na ugonjwa huo vilivyoko katika Halmashauri ya Usambazaji Madawa (KEMSA) vitatolewa kwa wahudumu wa afya wanaohudumia wagonjwa wa COVID-19.

Mgomo huo ulioanza siku ya Jumatatu umewasababishia matatizo makubwa wagonjwa waliokuwa wakitegemea hospitali za umma kote nchini.

Maafisa kutoka vyama mbali mbali vya wahudumu wa afya wameapa kuendeleza mgomo huo hadi mahitaji yao yatakaposhughulikiwa.

Categories
Habari

Viongozi wa KNUN Muranga, Kiambu na Nyeri matatani kwa kuwakataza wauguzi kushiriki mgomo

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi kimesema kitawasimamisha kazi wawakilishi wa chama hicho katika kaunti za Muranga, Kiambu na Nyeri kwa kuwanyima wanachama wao haki ya kushiriki kwenye mgomo unaoendelea wa wauguzi.

Akiwahutubia waandishi wa habari jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako amesema kuwa wakuu wa chama hicho katika kaunti hizo tatu watapokonywa majukumu yao iwapo watakosa kuwaruhusu wanachama hao kujiunga na wenzao kwenye mgomo kufikia Jumatano jioni.

Panyako amesema ni makosa kwa wawakilishi hao kuwanyima wanachama wao haki ya kushinikiza kuimarishwa kwa maslahi yao pamoja na wenzao katika kaunti nyingine ambao wangali wamegoma.

Panyako ameelezea imani kwamba mashauriano yanayoendelea na serikali kuhusiana na shinikizo zao yatakomesha mgomo huo hivi karibuni.

“Wale viongozi ambao wamesababisha wafanyikazi wasianze mgomo katika hizo kufikia jioni ya leo watakuwa wamesimamishwa kama viongozi wa chama hiki na tutaweka kaimu viongozi katika kaunti hizo ili kuendesha shughuli za chama hiki,” amesema Panyako.

Wakati uo huo, wahudumu wa afya katika Kaunti ya Makueni waliokuwa wamegoma kudhihirisha umoja na wenzao wamesitisha mgomo katika kaunti hiyo kwa muda wa siku 30 zijazo.

Uamuzi huo uliafikiwa baada ya viongozi wa kaunti hiyo kusema watashughulikia shinikizo zao katika muda wa siku  30 zijazo.

Categories
Habari

Mgomo wa Wauguzi nchini waanza

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) kimesisitiza kwamba mgomo wao uliopangwa kuanza Jumatatu bado ungalipo.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako, amesema kipindi cha makataa ya mgomo wao kilimalizika Jumapili na wameanza mgomo leo hadi kutimizwa kwa matakwa yao.

“Mgomo kote nchini uliopangwa kuanza Jumatatu tarehe saba Desemba, 2020, bado ungalipo. Tunawahimiza wanachama wetu waungane tunapotetea haki zetu,” amesema Panyako.

Panyako amesema swala la pekee ambalo limeshughulikiwa kwa kiwango fulani ni kutangazwa kwa janga la COVID-19 kuwa hatari kwa afya.

Ameweaagiza maafisa katika matawi yote kushiriki na kuhakikisha ufanisi wa mgomo huo.

Miongoni mwa maswala yanayoibuliwa na chama hicho cha wauguzi ni pamoja na kuwalipa wauguzi wote shilingi elfu 30 kama marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira hatari, wauguzi wote kulipwa fedha zote za mishahara na pia fedha walizokatwa kuwasilishwa kwa taasisi husika.

Pia wanataka wauguzi wote vibarua kuajiriwa kwa masharti ya kudumu na kuajiriwa kwa wauguzi elfu saba zaidi ili kusaidia katika vita dhidi ya COVID-19.

Chama hicho kinataka wauguzi kupewa vifaa vya kutosha vya kujikinga kwani wao hua wa kwanza kukutana na wagonjwa wanapowasili kwenye taasisi za afya.

Aidha, wauguzi wanataka kukamilika kwa mkataba wa pamoja kuhusu nyongeza ya mishahara.

Wanataka pia kuwepo mpango makhsusi wa bima ya matibabu kwa wauguzi kutokana na magonjwa yote ukiwemo ule wa COVID-19 na kufidiwa haraka kwa familia za zaidi ya wauguzi 18 ambao hadi sasa wamefariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Pia wanataka kujumuishwa kwa pendekezo la kubuni Tume ya Kuajiri wahudumu wa sekta ya afya miongoni mwa mapendekezo mengine ya mpango wa BBI.

Categories
Habari

Madaktari waahirisha kuanza kwa mgomo wao hadi tarehe 21 Desemba

Chama cha Kitaifa cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU) kimefutilia mbali mgomo uliopangiwa kuanza leo.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Chibanzi Mwachonda amesema Baraza la Kitaifa la Ushauri kwa chama hicho lilikutana na kuamua kutoa ilani mpya ya siku 14 ya mgomo ili kutoa fursa ya mashauriano kuhusu matakwa yao.

Chama hicho kinasema ikiwa maswala ambayo wameibua hayatashughulikiwa katika muda huo wa siku 14, basi mgomo huo utaanza tarehe 21 Desemba.

Katika taarifa kwa wanachama, Mwachonda amewahimiza Madaktari kutohatarisha maisha yao popote ambako hakuna vifaa vya kujikinga hasa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Uamuzi wa kusimamisha mgomo huo umeafikiwa baada ya mabunge yote mawili kuonyesha kwamba kamati zao za afya zinapanga kukutana tarehe 9 na 10 Desemba kujaribu kusuluhisha masuala yaliyozua utata.

Miongoni mwa masuala yanayozozaniwa ni pamoja na kuwapa vifaa vya kutosha vya kujikinga, maafisa wote walioorodheshwa miongoni mwa makundi ya walio hatarini kutojumuishwa katika majukumu ya mstari wa mbele, kuwepo mpango makhsusi wa bima ya matibabu, kupandishwa vyeo, kuorodheshwa kulingana na majukumu yao na kuwianishwa kwa marupurupu yao ya kufanya kazi katika mazingira hatari.