Categories
Michezo

Simba wa Nairobi wazidisha machungu ya Mathare United baad ya kuilaza 2-0

Klabu ya Nairobi City stars maarufu kama Simba wa Nairobi  imezidisha masaibu ya Mathare United baada ya kuicharaza mabao 2-0 katika pambano la pekee la ligi kuu ya Kenya lililopigwa Jumanne alasiri katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Beki wa pembeni kushoto Bolton Omwenga alipigiwa pasi ndani ya kijisanduku na kupachika bao  la kwanza dakika ya 27 kabla ya nguvu mpya Rodgers Okumu kuongeza la pili dakika ya 89 .

Ushindi huo ulikuwa wa tano kwa City Stars ligini msimu huu wakipanda hadi nafasi ya 8 kwa pointi  19 kutokana na mechi 14 na kuweka hai matumaini ya kuibuka miongoni mwa tano bora.

Mathare nao wanazidi kukabiliwa na hatari ya kushushwa ngazi kutoka ligi kuu wakiwa wamesakata mechi 11 ,kushinda 2,kwenda sare 3 na kushindwa 6 wakiwa katika nafasi ya 16 kwa alama 9.

Categories
Michezo

Ulinzi Stars waiangusha Mathare United huku Gor wakiiparuza Zoo Fc ligi kuu FKF

Wanajeshi Ulinzi Stars  na mabingwa watetezi Gor Mahia wamesajili ushindi katika mechi mbili za ligi kuu FKF  zilizosakatwa Jumatano alasiri.

Ulinzi waliipakata Mathare United mabao  2-1 katika uwanja wa Afraha  ,Daniel Waweru akipachika bao la kwanza kwa wenyeji kunako dakika ya 7 akiunganisha mkwaju uliotumwa na Michael Otieno na kumwacha kipa hoi bin taaban.

Kiungo Elvis Nandwa aliongeza bao la pili kwa Ulinzi akiunganisha pasi  murua iliyochongwa na mchezaji Masuta katika dakika ya 70 huku Mathare wakijipatia goli la maliwazo kupitia kwa Daniel Otieno dakika ya 88.

Katika mechi nyingine iliyopigwa katika uchanjaa wa Kasarani, Gor Mahia walirejelea tambo za ushindi na kuititiga Zoo Fc mabao 3 bila jibu ,kiungo Samuel Onyango akipachika la kwanza dakika ya 10, kabla ya nahodha Keneth Muguna kutanua uongozi kwa goli la dakika ya 32 na kisha Onyango akapiga tena bao la tatu kunako dakika ya pili ya muda wa mazidadi.

Kufuatia matokeo ya Jumatano Gor na Ulinzi wamezoa idadi sawa ya alama 12 ingawa vijana wa KDF wamecheza mechi mbili zaidi.

Categories
Michezo

FKF yapata pigo baada ya mahakama kuzirejesha Mathare United na Zoo Fc ligini

Shirikisho la kandanda nchini  FKF limepatwa na pigo baada ya mahakama ya kutatua migogoro michezoni  nchini SDT kuamuru kurejeshwa ligini timu za Mathare United na Zoo Fc   kusubiri uamuzi wa kesi  iliyowasilishwa dhidi ya FKF na  vialbu hivyo viwili wiki ijayo.

Mwenyekiti wa Mahakama hiyo maarufu kama SDT John Ohaga ametoa uamuzi huo mapema Alhamisi wa kuzirejesha timu hizo mbili kwenye ligi pamoja na kubatilisha uamuzi wa awali wa FKF wa kutamatisha kandarasi za wachezaji wote wa klabu  hizo mbili  .

Pia jaji Ohaga ameagiza Fkf iliruhusu wachezaji na maafisa wa vilabu hivyo kufanyiwa vipimo vya COVID 19 sawa na vilabu vingine  saa 72 kabla ya kuanza mechi zao za ligi kuu .

Wachezaji wa Zoo FC

Baraza kuu la FKF likikutana Desemba 9 na kuamuru kuzipiga marufuku timu hizo hadi pale zitakaposaini mkataba huo wa Star Times.

FKF ilizipiga marufuku timu hizo kushiriki ligi kuu ya FKF baada ya kudinda kusaini mkataba wa Star Times ambao ungewezesha mechi za timu hizo kupeperushwa mbashara na runinga hiyo ya China .

 Wachezaji Mathare United

Shirikisho hilo pia linamchunguza mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier  baada yake kaundika barua kwa Star Times kuondoa barua ya kwanza iliyoandikwa na aliyekuwa katibu mkuu Sam Ochola kusaini mkataba huo .

Zoo FC vs. Kenya Football Federation – Order (17 Dec 2020)

Mkataba wa FKF na Star Times umeibua hisia kali huku vilabu vya Ulinzi Stars,Mathare United ,Gor Mahia na Zoo Fc vikiupinga kwa kukiuka haki zao hatua iliyochangia kupigwa marufuku na kutimuliwa ligini kwa Mathare  United na Zoo Fc .

Timu za Mathare na Zoo zilizuiwa kucheza mechi zao za kufungua msimu wa ligi wiki jana wakati Gor na Ulinzi wakiwa tayari wamecheza mechi 2 na moja mtawalia katika ligi kuu.

Mahakama ya SDT itakutana wiki ijayo kusikiza kesi hiyo na kutoa maelekezo zaidi huku ligi ya FKF ikiangia mechi za mzunguko wa nne mwishoni mwa juma hili.