Categories
Kimataifa

Mshauri wa Trump kuhusu janga la Korona ajiuzulu

Mshauri wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhuru virusi vya Korona Dkt. Scott Atlas amejiuzulu.

Atlas amemshukuru Rais Trump kwa kumpa fursa ya kuwahudumia Wamarekani, akisema nyakati zote alikuwa akitegemea hatua za hivi punde za kisayasi na ushahidi bila mwingilio au ushawishi wowote wa kisiasa.

Katika kipindi cha miezi minne alichohudumu, Dkt. Atlas alitilia shaka haja ya kuvalia barakoa na hatua nyingine za kukabiliana na janga hilo.

Pia mara kadhaa alitofautiana na wanachama wengine wa jopo la kukabiliana na virusi vya Korona, tangu alipojiunga na jopo hilo mwezi Agosti.

Mbali na kutilia shaka umuhimu wa kuvalia barakoa, Atlas alipinga kufungwa kwa maeneo mbali mbali nchini humo.

Wataalamu wa afya ya umma, akiwamo Dkt. Anthony Fauci wa kituo cha kukabiliana na magonjwa, walimshutumu Atlas kwa kumhadaa na kumpotosha Rais Trump kuhusu virusi vya Korona.

Marekani imenakili takriban visa milioni 13 vya virusi vya Korona na zaidi ya vifo elfu 266.

Categories
Kimataifa

Nitatoka White House baadaye, Trump alegeza msimamo

Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kuondoka kwenye Ikulu ya White House iwapo Joe Biden atathibitishwa kirasmi na jopo la waamuzi kuwa Rais mpya.

Kufikia sasa Rais huyo hajakubali kushindwa kwenye uchaguzi wa Urais wa tarehe 3 mwezi huu.

Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba itakuwa vigumu kukubali matokeo ya uchaguzi huo yanayoashiria kwamba alishindwa na mpinzani wake Biden wa chama cha Democratic.

Kwa mara nyingine, amekariri madai ambayo hayajathibitishwa kuwa kulikuwa na udanganyifu wa kura kwenye uchaguzi huo.

Biden alimshinda Trump kwa kura 306 dhidi ya 232 chini ya mfumo wa jopo la waamuzi ambao hutumiwa kumchagua Rais wa Marekani.

Kura hizo zilizidi 270 ambazo mwaniaji anahitaji ili kutangazwa mshindi wa Urais kwa mujibu wa mfumo wa uchaguzi nchini humo.

Aidha, Biden alimshinda Trump kwa zaidi ya kura million sita za kawaida.

Jopo hilo la waamuzi litakutana mwezi ujao kuidhinisha rasmi matokeo hayo, huku Joe Biden akipangiwa kuapishwa tarehe 20 Januari.

Rais Trump na wafausi wake wamewasilisha kesi kadhaa mahakamani kuhusiana na uchaguzi huo, lakini nyingi kati yazo zimetupiliwa mbali.

Mapema wiki hii, Trump alikubali hatimaye kuruhusu shughuli za kuwaapisha maafisa wapya wa baraza la Biden baada ya sintofahamu iliyodumu kwa wiki kadhaa.

Categories
Kimataifa

Trump ahimizwa na rafikiye akubali kushindwa

Rafiki wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump amemhimiza rais huyo aachane na harakati za kupinga ushindi wa rais mteule Joe Biden.

Chris Christie, aliyewahi kuwa Gavana wa jimbo la New Jersey amelitaka kundi la kampeini la Trump kusitisha kile alichokitaja kuwa fedheha ya kitaifa.

Rais Trump amekataa kukubali kwamba alishindwa kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika hivi majuzi nchini Marekani kwa madai ambayo hayajathibitishwa kwamba kulikuwa na visa vya udanganyifu.

Wafuasi wengi wa chama cha Republican wameunga mkono juhudi hizo za Trump za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Siku ya Jumamosi, juhudi za Trump zilipata pigo wakati Jaji katika jimbo la Pennysylvania  alipotupilia mbali kesi iliowasilishwa na Trump ya kutaka kubatilisha maelfu ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta katika jimbo hilo.

Categories
Kimataifa

Masaibu ya Trump yazidi baada ya mahakama kutupilia mbali kesi dhidi ya kura za Pennyslvania

Jaji mmoja katika Jimbo la Pennyslvania nchini Marekani ametupilia mbali kesi ya maafisa wa kampeini wa Rais Donald Trump ya kutaka kuharamishwa kwa mamilioni ya kura  zilizopigwa kwa njia ya posta katika jimbo hilo muhimu.

Jaji Mathew Brann alisema kuwa madai ya kuwepo kwa udanganyifu kwenye shughuli hiyo hayana msingi wowote.

Hatua hiyo inafungua njia kwa serikali ya jimbo hilo kuthibitisha kura na ushindi wa Rais Mteule Joe Biden katika jimbo hilo muhimu, ambapo alimshinda mpinzani wake Trump kwa  zaidi ya kura 80,000.

Hili ni pigo la hivi punde kwa Rais Trump ambaye anajaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 3 mwezi Novemba.

Hadi sasa Ris Trump amekataa  kushindwa kwenye uchaguzi huo kwa madai kwamba kulifanyika udanganyifu na wizi wa kura kwenye shughuli hiyo.

Hata hivyo hajatoa ushahidi wowote kuthibitiha madai hayo.

Hali hiyo imechelewesha mchakato ambao hufuatwa baada ya kufanywa uchaguzi wa urais nchini Marekani.

Categories
Habari

Viongozi wawili wa kundi la Alshabab wawekewa vikwazo na Marekani

Viongozi wawili wa kundi la wanamgambo wa Somalia, Al-Shabaab waliodaiwa kuhusika na shambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Kenya wamewekewa vikwazo na Marekani.

Mwanajeshi mmoja wa Marekani na wanakandarasi wawili waliuawa wakati wa shumbulizi hilo la mwezi Januari kwenye kambi ya Simba iliyoko katika kisiwa cha Manda kaunti ya Lamu.

Shambulizi hilo lilikuwa la kwanza kutekelezwa na kundi la Al-Shabaab dhidi ya wanajeshi wa marekani.

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Marekani kwenye taarifa imewataja Abdullahi Osman Mohamed na Maalim Ayman kama magaidi wa kimataifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mohamed ni mtaalam mkuu wa vilipuzi wa kundi la Al-Shabaab na pia kiongozi wa kitengo cha Habari cha kundi hilo ilhali Ayman ndiye aliyehusika kupanga shambulizi katika kambi ya Simba.

Aidha taarifa hiyo imewapiga marufuku raia wa Marekani kushirikiana katika biashara ya aina yeyote na wawili hao.

Categories
Kimataifa

Obama atoa wito wa kusitisha migawanyiko Marekani

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama amesema taifa hilo linahitaji kubadili tamaduni ya dhana za hujuma ambazo zimezidisha migawanyiko nchini humo.

Kwenye mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, Obama amesema kuwa Marekani imegawanyika kuliko ilivyokuwa miaka minne iliopita.

Kulingana na Obama, migawanyiko hiyo imedhihirika wakati Donald Trump aliposhinda uchaguzi wa urais.

Amesema kwamba ushindi wa Joe Biden kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2020 ni mwanzo wa juhudi za kuliunganisha tena taifa hilo.

Obamba amesema kuliunganisha taifa hilo hakuwezi kuachiwa wanasiasa, bali kunahitaji pia mabadiliko ya kimuundo na watu kusikilizana na kukubaliana kabla ya kuzua malumbano.

Hata hivyo Obama amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya kihisia ya kizazi kijacho, vijana hawana budi kuwa na matumaini kwamba mambo yatabadilika na kwamba sharti wawe sehemu ya mabadiliko hayo.

Categories
Kimataifa

Wafuasi wa Trump waandamana kupinga matokeo ya uchaguzi Marekani

Maelfu ya wafuasi wa Rais wa Marekani Donald Trump wamejitokeza mjini Washington DC kuunga mkono madai yake ambayo hayajathibitishwa kuhusu wizi wa kura kwenye uchaguzi wa urais wa nchi hiyo.

Shirika la utangazaji la BBC limeripoti kuwa waandamanaji waliokuwa wakibeba mabango waliungana na wanachama wa mrengo ya kulia ambao wengi wao walikuwa wakivalia kofia za kinga na mavazi ya kuzuia risasi.

Wafuasi wa Trump walianzisha maandamano hayo mwendo wa saa sita adhuhuri saa za nchi hiyo karibu na jengo la Freedom Plaza, mashariki mwa Ikulu ya White House, na walitarajiwa kuelekea upande wa mahakama ya juu.

Waandamanaji hao wamekuwa wakitumia majina tofauti tofauti kwa maandamano hayo kama vile Million MAGA March wakitumia ufupi wa wito wa Trump wa “Make America Great Again” na pia “March for Trump and Stop the Steal DC”.

Trump hajakubali kuwa mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden alishinda uchaguzi huo wa tarehe tatu mwezi Novemba.

Categories
Kimataifa

Bush ampongeza Biden kwa ushindi wa kura za Urais Marekani

Aliyekuwa  Rais wa Marekani George W. Bush amempongeza Rais Mteule wa Marekani Joe Biden na Makamu wake mteule Kamala Harris kwa kuchaguliwa  kwao.

Katika taarifa, Bush amesema alimpigia simu Biden kumshukuru kwa ujumbe wa kizalendo alioutoa katika hotuba yake ya kukubali kuchaguliwa kwake.

Alimpigia simu Kamala Harris pia na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kwa kihistoria kuwa makamu wa rais wa kwanza wa kike.

Akikubali tofauti za kisiasa baina yao, Bush anasema anamjua Biden kuwa mtu mzuri, ambaye ataongoza na kuwaunganisha Wamarekani.

Ujumbe wa Bush umetokea wakati wabunge wengi wa chama tawala cha Republican kwenye Bunge la Congress wakiwa wangali hawajamtambua Biden hadharani kama rais mteule.

Katika taarifa yake, Bush pia amempongeza Trump kwa kampeni aliyoiendesha kwa bidii, akitaja kura zaidi ya milioni 70 alizopata kama ishara ya mafanikio ya kisiasa ambayo sio rahisi kuafikia.

Categories
Kimataifa

Biden ashinda Urais nchini Marekani

Mgombea Urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic Joe Biden ndiye rais mpya wa Marekani.

Hii ni baada ya kufikisha kura 273 kati ya 270 ambazo mgombea anahitaji ili atawazwe mshindi katika kinyang’anyiro hicho.

Shughuli ya kuhesabu kura hizo zilizopigwa Jumanne bado inaendelea lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani, Biden ndiye atakayetawazwa mshindi wa uchaguzi huo ulioibua hisia mseto ulimwenguni kote.

Haijabainika kama Rais wa sasa Donald Trump atakubali kushindwa na kuachilia mamlaka mnamo Januari mwaka wa 2021 ambapo Biden anatarajiwa kuapishwa.

Tayari Trump ameonekana kutilia shaka matokeo ya uchaguzi huo Jumatano alipohutubia wafuasi wake na kusema ataelekea mahakamani kusimamisha shughuli za kuhesabu kura hizo.

Ushindi huo wa Biden utamfanya mgombea mwenzake Kamala Harris kuwa Makamo wa Rais wa kwanza wa jinsia ya kike nchini humo.

Categories
Kimataifa

Biden akaribia Ikulu ya White House

Mgombea wa Urais nchini Marekani Joe Biden amesema tena kuwa ana uhakika wa ushindi kwenye uchaguzi nchini humo.

Biden anakaribia kumshinda Rais Donald Trump kufuatia kura zilizoandaliwa Jumanne iliyopita.

Biden sasa ana kura 253 kati ya kura 270 za wajumbe ambazo zinazohitajika kumuingiza Ikulu chini ya mfumo wa uchaguzi wa Marekani, huku Trump akiwa na kura 214.

Biden pia anaongoza katika hesabu ya kura katika  majimbo muhimu ya Georgia, Nevada, Pennsylvania na Arizona.

Ushindi wa Biden utamfanya Rais Trump kuondoka afisini mnamo mwezi Januari mwaka wa 2021 baada ya kutawala kwa miaka minne.

Ikiwa Biden atatangazwa mshindi wikendi hii, maafisa wake wanatarajiwa kuanza mchakato wake wa mpito mnamo Jumatatu ijayo.

Kikosi cha kulinda mafisa wakuu wa serikali kimetuma maafisa katika eneo la Delaware ambako Bidem anaishi ili kuimarisha usalama wake.

Nayo huduma ya uchukuzi wa ndege nchini humo imepiga marufuku ndege kupaa kwenye anga ya Wilmington aliko Biden.

Hata hivyo, hakuna dalii kuwa Rais Trump atakubali ushindi wa mpinzani wake katika muda mfupi ujao.