Maombolezo ya kitaifa ya siku tatu yameanza leo nchini Argentina kufuatia kifo cha gwiji wa soka Diego Maradona Jumatano jioni.
Maelfu ya watu wamejitokeza katika kasri ya Rais kuutazama mwili wa marehemu na kutoa heshima zao za mwisho mapema Alhamisi, huku wengine wakiingia barabarani Jumatano usiku kuomboleza kwa kulia ,kuimba nyimbo ,kuwasha baruti huku wengine wakisherehekea maisha ya marehemu kwa kunywa pombe kwenye barabara za mji mkuu wa Argentina Beunos Aires.
Mashabiki wengi walikusanyika katika uwanja wa Bombonera ambao hutimika na kilabu cha Boca Juniors kuomboleza kifo cha nguli huyo kati ya jumatano usiku na Alhamisi.
Maradona alifarika Jumatano jioni akiwa na umri wa miaka 60 kutokana na mshtuko wa moyo na ameacha kumbukumbu ulimwenguni kwa bao la hand of God lililoipa Argentina ushindi dhidi ya Uingereza kwenye fainali za kombe la dunia mwaka 1986 huku akiiwezesha timu yake kunyakua kombe la dunia kwa mara ya kwanza akiwa nahodha.