Categories
Habari

Waumini wa Kisii walalamikia ongezeko la visa vya makanisa kuteketezwa

Wakazi wa Kata Ndogo ya Otamba katika Kaunti ya Kisii wamelalamikia visa vya mara kwa mara vya uteketezaji wa makanisa ya eneo hilo.

Wakazi hao wanasema kanisa lingine liliteketezwa siku ya Jumamosi na watu wasiojulikana, hivyo kufikisha matano; idadi ya makanisa yaliyoteketezwa katika muda wa wiki moja.

Kanisa la Otamba PAG ndilo la hivi punde kuteketezwa baada ya makanisa ya Katoliki, SDA, Worldwide Ministries na Legio Maria kuteketezwa ampema wiki hii.

Kerubo Orang’I, ambaye ni muumini, alitilia shaka malengo ya wateketezaji hao, akisema watu hao ambao hutekeleza maovu yao nyakati za usiku pia hujihusisha katika matendo ya kustaajabisha.

Mzee mmoja kwa jina Eric Ratemo alitaka hatua za haraka kuchukuliwa na taasisi za usalama ili kukomesha uovu huo kabla haujakithiri zaidi.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kisii Jebel Munene amewaambia waandishi wa habari kwamba polisi wanafuatilia vidokezi muhimu ambavyo karibuni vitawezesha kukamatwa kwa washukwia.

Categories
Habari

Viongozi wa Makanisa watakiwa kukomesha siasa katika ibada

Viongozi wa makanisa wametakiwa kukoma kuwapa wanasiasa kipau mbele wanapohudhuria ibada au hafla nyingine za kidini.

Askofu Stanley Michael Michuki wa Kanisa la Hope Restoration International amewashtumu baadhi ya wachungaji na maaskofu kwa kuwa na mazoea ya kuwapa wanasiasa viti vyao kila wanapohudhuria ibada katika makanisa yao.

“Mchungaji au Askofu asisimame na kumpa kiti chake mwanasiasa; wabaki kwenye viti vyao na wanasiasa wanaweza kuongea kama watapewa nafasi lakini sio maswala ya siasa,” akasema Michuki.

Alikuwa akiongea katika uwanja wa Mweiga katika kaunti ya Nyeri wakati wa kuwekwa wakfu kwa Askofu Erastus Njoroge wa Kanisa la Four Way na kumfanya kuwa Askofu Mkuu.

Askofu Michuki amesema kuwa wanasiasa hawapaswi kuruhusiwa kupiga siasa makanisani na wanapaswa kushughulikiwa kama waumini wa kawaida.

“Ni vigumu kuzuia wanasiasa kuingia kanisani lakini hilo ni swala tofauti na kuwaambia wasipige siasa,” akaongeza.

Hata hivyo mewatetea viongozi wa makanisa dhidi ya shutuma kuwa wanatumia vibaya injili kwa manufaa ya kifedha.

Askofu Michuki ametoa wito kwa serikali kukabiliana vikali na wachungaji walaghai.

Akiongea wakati wa hafla hiyo, Askofu Erastus Njoroge amekosoa uhusiano wa karibu ambao umeibuka kati ya wanasiasa na kanisa huku akionya kuwa huenda ikawa vigumu kwa kanisa kuwakosoa wanasiasa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa.

Categories
Habari

Ruto asema hatakoma kusaidi makundi ya Kidini na kuinua vijana

Naibu Rais William Ruto amesema hatashurutishwa kukoma kusaidia makundi ya kidini na shughuli za kuwainua vijana.

Akihutubia viongozi wa makanisa waliomtembelea nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu, hapo jana, naibu rais alisema haoni aibu kumtumikia Mungu na wala hajutii imani yake.

Aidha alisema imani yake ndiyo ya kwanza mbele ya mamlaka ya kisiasa na akawataka wale wanaotatizika na shughuli zake za kusaidia makanisa, makundi ya kiislamu na juhudi za kuwainua vijana na wanawake kutafuta shughuli za kufanya.

Alisema viongozi walichaguliwa kuwapa uwezo wakenya miongoni mwa sababu nyingine akiongeza kuwa ni kupitia kwa miradi kama ile anayounga mkono ambapo maisha ya wakenya wa kawaida yanaweza kuimarishwa.