Categories
Habari

Viongozi wa kisiasa kuwaelimisha wakenya kuhusu ripoti BBI

Viongozi wa vyama vya kisiasa wameahidi kuwaelimisha wakenza katika juhudi za kuwahamasisha kuhusu fursa zilizopo kwenye ripoti ya BBI.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao waliwahimiza wakenya kuweka kando tofauti zao na kushirikiana katika kujenga kenya bora kwa vizazi vijavyo.

Kuhakikisha sauti ya kila mkenya inasikika na kuwezesha kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake, tutawaelimisha wakenya ili kuwahamasisha kuhusu fursa zilizopo katika taifa hili kupitia mpango huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Viongozi hao waliokutana katika Ikulu ya Nairobi siku ya Alhamisi, walielezea mpango wa kuwa na mkutano wa pamoja kati ya wabunge na viongozi wa kaunti tarehe 9 mwezi Machi mwaka huu.

Huku wakishukuru mabunge ya kaunti kwa kuunga mkono mswada wa BBI, viongozi hao wa vyama vya kisiasa walisema hatua hiyo ya mabunge hayo iliweka msingi ambapo taifa hili litaboresha usawa wa kijinsia, usawa wa fursa kwa wote sawia na kila mkenya kufurahia ufanisi unaoafikiwa nchini.

Jinsi wawakilishi wa kaunti walivyodhihirisha, sasa ni wakati kwa wakenya wote kuweka kando tofauti zao na kuungana pamoja katika kuboresha taifa hili, kwetu sisi, watoto wetu na kwa vizazi vya nchi hii vijavyo,” walisema viongozi hao.

Categories
Habari

BBI yapita magatuzini, sasa yaelekea Bunge la Kitaifa

Mswada wa marekebisho ya katiba ya mwaka 2020 kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa (BBI) umetimiza uungwaji mkono wa mabunge 24 yanayohitajika kikatiba ili uelekezwe katika Bunge la Kitaifa kujadiliwa.

Hii ni baada ya mabunge ya Kaunti 12 zaidi kupitisha mswada huo siku ya Jumanne na hivyo kutimiza matakwa ya kikatiba ya kupitishwa na angalau mabunge ya kaunti 24 ambayo ni zaidi ya nusu ya mabunge yote ya kaunti 47 nchini.

Kufikia Jumatatu alasiri, mabunge 12 yalikuwa tayari yamepitisha mswada huo, yakiwemo Homabay, Siaya, Kisumu, Pokot Magharibi, Busia, Trans Nzoia, Kajiado, Kisii, Vihiga, Nairobi, Laikipia na Samburu, huku kaunti ya Baringo ikiwa ya pekee iliyokataa mswada huo.

Mabunge mengi ya kaunti yalikuwa yameratibu kujadili mswada huo Jumanne huku yale ya Kakamega, Narok, Makueni, Nyamira, Taita Taveta, Murang’a, Bungoma, Kitui, Nyeri, Lamu, Nyandarua na hivi sasa Garissa pia limepitisha mswada huo na kutimiza idadi ya 24.

Haya yanajiri huku kaunti zengine zikiendelea kujadili msawa huo na zengine zikiwa bado zinachukua maoni ya wananchi.