Categories
Burudani

Maggy Bushiri arejea Tanzania

Mwanamuziki Maggy Bushiri amerejea nchini Tanzania kutoka Marekani anakoishi kwa ajili ya kuzindua nyimbo kadhaa.

Alikuwa ameandamana na mpenzi wake kwa jina Martin Classic ambaye pia ni mwanamuziki na wameshirikiana katika nyimbo kadhaa. Wawili hao waliwasili wakiwa wamevalia barakoa nyeusi ila walizivua mara tu walipolakiwa na wenyeji wao.

Barakoa hazitumiki nchini Tanzania hasa baada ya serikali nchini humo kutangaza mwaka jana kwamba ugonjwa wa Covid 19 ulikuwa umeisha humo.

Maggy Bushiri ni mzaliwa wa Congo, ila alilelewa nchini Tanzania kwa muda kidogo na baadaye yeye, ndugu zake na mamake wakahamia marekani kama wakimbizi.

Kulingana naye, aliondoka Tanzania akiwa na umri wa miaka miwili kuelekea Mozambique na baadaye wakaelea Marekani.

Alipohojiwa mwaka 2019 nchini Tanzania, alielezea kwamba babake aliaga dunia kabla wagure Tanzania na mamake akaaga dunia mwaka 2009 wakiwa nchini Marekani.

Kwenye mahojiano hayo pia alifichua kwamba alikuwa mwanafunzi wa chuo cha Los Angeles anakoishi na anasomea mambo ya uanahabari hasa uundaji wa vipindi.

Mwaka 2018 alihojiwa na jarida la Los Angeles kwa jina “VoyageLA” ambapo alifichua kwamba haikuwa rahisi kuingilia muziki kwani mara nyingi aliambiwa hatoshi.

Wimbo wake ambao anasema ulifanya ajulikane zaidi ni “Swing Your Body”. Wakati huo alifichua mipango yake ya siku za halafu, ile ya kufungua kampuni ya mavazi ambapo rangi kuu itakuwa Zambarau au ukipenda Purple.

Anapenda sana rangi hiyo naye hujiita “The Purple Queen” ila alipowasili Tanzania jana, hakuwa na nywele za rangi ya Zambarau kama siku za awali.

Alizungumzia pia mipango ya kurejea alikozaliwa na kuanzisha kituo kikubwa ambacho kitakuwa makazi ya kuhudumia mayatima.

Inasubiriwa sasa kuona mazuri ambayo ameletea mashabiki wake wa Tanzania mwaka huu wa 2021.

Categories
Burudani

Tarehe mpya ya tuzo za Grammy

Wasimamizi na waandalizi wa tuzo kubwa zaidi za muziki ulimwenguni Grammy wamebadili tarehe ya kutuza washindi wa mwaka 2021.

Awali hafla ya kutuzwa kwa washindi ilikuwa imepangiwa kufanyika tarehe 31 mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Sherehe hiyo sasa itafanyika tarehe 14 mwezi Marchi mwaka huu wa 2021.

Kwenye taarifa ya pamoja, Harvey Mason Junior ambaye ni kaimu msimamizi wa “Recording Academy”, Jack Sussman naibu msimamizi wa kituo cha CBS na Ben Winston wa Fulwell 73 Productions walisema kwamba sababu kuu ya kuahirisha tuzo za Grammy ni ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Covid 19 katika eneo la Los Angeles.

Watatu hao wanasemekana kuafikia uamuzi huo baada ya kushauriana na maafisa wa serikali na wale wa afya wa eneo hilo.

Katika eneo la Los Angeles hospitali zimejaa wagonjwa na hata vyumba vya wagonjwa katika hospitali hizo vimejaa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid 19.

Usalama wa wanamuziki tajika wanaolengwa kwenye tuzo hizo, waandalizi na wengine wanaohusika umepatiwa kipaumbele.

“Tunashukuru wanamuziki wote wanaohusika, wafanyikazi wa Recording Academy inayoandaa tuzo za Grammy, wafanyibiashara na hasa walioteuliwa kuwania tuzo za mwaka huu kwa utulivu na kujitolea kwao kufanya kazi nasi na kutuelewa tunapopitia kipindi kigumu cha janga la Corona.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye taarifa ya pamoja ya waandalizi wa tuzo za Grammy.