Categories
Habari

Eric Kneedler ndiye balozi mpya wa Marekani hapa nchini

Eric Kneedler ndiye balozi mpya wa Marekani hapa nchini. Uteuzi wake ulitangazwa muda mfupi baada ya kuapishwa kwa Joe Biden kuwa Rais wa 46 wa Marekani.

Baada ya uteuzi wake, Kneedler alitoa wito wa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Kenya na Marekani hususan katika maswala ya  usalama,afya, elimu na biashara.

Kneedler anachukua mahala pa Kyle McCarter aliyejiuzulu wadhifa huo baada ya Donald Trump kuondoka wadhifa wa Rais wa Marekani.

Kulingana na afisi ya ubalozi wa Marekani hapa nchini, Kneedler awali alihudumu wadhifa wa naibu wa mkuu wa ujumbe katika balozi ya Marekani jijini Nairobi kuanzia mwezi Aprili mwaka 2019 hadi mwezi January mwaka 2021.

Kneedler alianza majukumu yake Jijini Nairobi mwaka 2017 akiwa mshauri wa maswala ya kisiasa.

Wadhifa huo wa mshauri wa maswala ya kisiasa pia aliushikilia katika ubalozi wa Marekani huko Manila na naibu wa mshauri wa kisiasa katika ubalozi wa Marekani Bangkok.

Kneedler ana shahada kutoka chuo cha Pomona na uzamili ya maswala ya kimataifa kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Categories
Habari

Marekani kutoa huduma za mtandao kwa shule zilizoko mashinani hapa nchini

Balozi wa Marekani nchini  Kyle McCarter ameahidi kushirikiana kwa karibu na serikali za kaunti kuzisaidia shule zilizoko katika maeneo ya mashinani kupata huduma za mitandao.

Balozi huyo alisema kuwa changamoto zilizosababishwa na janga la corona ndizo zilizoifanya serikali ya Marekani kuingilia kati kuzisaidia shule za maeneo ya mashinani kupata huduma za mitandao.

Alisema kuwa ushirikiano huo baina ya serikali ya Marekani na serikali ya Kenya utawawezesha wanafunzi mashinani kupata huduma za mitandao.

Akiwahutubia wanahabari katika kaunti ya Kiambu baada ya kukutana na gavana James Nyoro, balozi  McCarter alisema kuwa anafahamu changamoto zinazokumba mataifa mengi katika kuwahifadhi wanafunzi shuleni hasa wakati huu wa janga la corona.

Alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma za mitandao katika maeneo ya mashinani hasa katika kuwasaidia vijana kutafuta nafasi za ajira za kujitegemea.

Kuhusu uwekezaji, balozi huyo alisema kuwa serikali ya Marekani itawaleta wawekezaji wa kibinafsi humu nchini ili kusaidia serikali za kaunti kujitegemea na kuimarisha maisha ya wakazi badala ya kutegemea misaada ya kigeni.

Categories
Habari

Wakazi wa Pokot Magharibi wanufaika na barakoa kutoka ubalozi wa Marekani nchini

Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umetoa mchango wa barakoa elfu-100 kwa kaunti ya Pokot Magharibi kama sehemu ya juhudi zake za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Barakoa hizo zitasambaziwa watoto wa shule katika eneo hilo.

Akiongea huko Kapenguria wakati wa kuwasilisha barakoa hizo balozi wa Marekani nchini Kenya Kyle McCarter alisema uhusiano wa kirafiki ulioko baina ya Kenya na Marekani ungali imara.

Balozi huyo aliongeza kuwa barakoa hizo zenye maandishi ya “USA Marafiki” ni mradi unaodhamiria kuhakikisha kwamba watoto wanarudi shuleni wakiwa salama.

Wakati huo huo balozi huyo alitembelea miradi miwili inayofadhiliwa na ubalozi wa Marekani, na kuwataka wakaazi waanzishe miradi ya kuwaletea mapato.

Kundi la kujisadia la kina mama la “Ewan Kiror” ambalo lilinufaika na chumba cha kuwawezesha kukuza Pili Pili ndani ya ukumbi liliomba usaidizi zaidi ili kujenga kumbi nyingine za kukuza mazao mbali mbali kama vile nyanya.

Mwenyekiti wa kundi la kina mama la Otupo katika eneo la Kapkoris- Elizabeth Keriso, aliitisha ufadhili zaidi ili wajihusisha na mradi wa ufugaji kuku na kufaidi wanachama wengi zaidi.

Categories
Habari

Balozi wa Marekani ashtumu hatua ya kutumia vijana kuzua vurugu humu nchini

Balozi wa Marekani humu nchini Kyle McCarter amesema nchi yake haitabakia kimya na kutazama vijana wakiendelea kuchochewa na wanasiasa kuzua vurugu humu nchini.

Wakati uo huo, Kyle amekanusha madai kwamba nchi yake inapanga kufutilia mbali hati za Visa za maafisa wa ngazi za juu serikalini, kwa kukatiza uhuru wa kujieleza, kutangamana na kujikusanya pamoja humu nchini.

Balozi huyo ambaye alikuwa akiongea wakati wa ziara ya kutoa mchango wa barakoa kwa utawala wa Kaunti ya Kirinyaga, amesema hafahamu lolote kuhusu habari hizo huku akitaja madai hayo kuwa ya uongo.

Akiwa ameandamana na Gavana wa Kirinyaga Ann Mumbi Waiguru, Kyle pasipo kutoa maelezo zaidi amesema hakuna uamuzi wowote kama huo ambao umeafikiwa na nchi yake, na akahimiza WaKenya kupuuza uvumi wa aina hiyo.

Pia amesema kwamba wale watakaopatikana na hatia kufuatia kupotea kwa fedha za kupambana na janga la COVID-19, watakabiliwa na hatua kali kutoka kwa serikali yake.

Kuhusu usalama, Kyle amesema kwamba serikali za Marekani na Kenya zinashirikiana kwa karibu ili kushinda kundi la kigaidi la Al-Shabaab.