Categories
Habari

Gavana Nyong’o asema Kisumu i tayari kwa sherehe za Madaraka

Gavana wa Kaunti ya Kisumu Profesa Anyang Nyong’o amesema maandalizi ya sherehe zijazo za siku kuu ya Madaraka yamekamilika.

Profesa Nyong’o amesema sherehe hizo zitakazohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta zitaandaliwa katika uwanja wa michezo wa Jaramogi Oginga Odinga.

Nyong’o amesema kazi kwenye barabara za kutoka kati kati ya mji wa Kisumu inaendelea katika juhudi za kupandisha hadhi barabara hizo ili kutumika na wageni watakaohudhuria sherehe hizo.

Gavana huyo amesema hoteli nyingi kuu mjini Kisumu tayari zimelipiwa zote na wageni watakaohudhuria sherehe hiyo mnamo  tarehe moja mwezi Juni.

Nyong’o amesema serikali ya kaunti hiyo itaweka runinga mbili kubwa katika sehemu ya Kirende na uwanja wa Raila ili kuwawezesha wakazi ambao hawatapata fursa ya kuingia uwanjani humo kufuatia sherehe hizo kwa uzingativu wa kanuni za kuzuia msambao wa COVID-19.

Categories
Habari

Kaunti ya Kisumu kuandaa sherehe za mwaka huu za Madaraka Day

Kaunti ya Kisumu itaandaa makala ya mwaka huu ya sherehe za Madaraka Day Juni mosi katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ambao kwa sasa unaendelea kujengwa.

Akiongea wakati wa kukagua shughuli ya ukarabati inayoendelea katika uwanja huo, mwenyekiti wa kamati andalizi ya sherehe za kitaifa aliye pia katibu katika wizara ya usalama, dakta  Karanja Kibicho, alisema kwamba uwanja huo utakaogharimu shilingi milioni-600 unatarajiwa kukamilika kufikia katikati ya mwezi Mei ili kujiandaa kwa hafla hiyo.

Tayari ujenzi wa barabara ya Mamboleo ambayo ni sehemu ya barabara ya kilomita 63 ya Mamboleo, Miwani kuelekea Chemelil, Muhoroni na Kipsitet inajengwa kwa kima cha shilingi bilioni 4.9 kabla ya kuandaliwa kwa sherehe hiyo.

Kutokana na kanuni za ugonjwa wa Covid-19, Kibicho alisema hafla hiyo itaandaliwa kwa njia ya mtandao ambapo ni wageni wachache walioalikwa wataruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Alisema wakazi wanapaswa kufuatilia sherehe hiyo katika maeneo yaliyotengwa huku wakenya wengine wakifuatilia hafla hiyo kwenye matangazo ya moja kwa moja kwenye runinga.

Kibicho alisema rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wanatarajiwa kuongoza sherehe hiyo.

Tangu mwaka 2015, kaunti zimekuwa zikiandaa sherehe za kitaifa.

Categories
Habari

Eneo la kiuchumi kujengwa katika kaunti ya Kisumu

Serikali ya taifa imetenga eneo la ekari 1,000 ambako kutajengwa eneo la kiuchumi mjini Kisumu. Ardhi hiyo ni sehemu ya ardhi ya kiwanda cha sukari cha Miwani kilichosambaratika.

Hatua hiyo itafanikisha utekelezaji wa mradi huo ambao mipango ya utekelezaji wake imekuwa ikiendelea kwa miaka mitatu iliyopita.

Katibu mwandamizi wa wizara ya viwanda David Osiany amesema mchakato wa kuhamisha umiliki wa ardhi hiyo umeimarishwa.

“Tumepiga hatua kuhusu swala hili na sasa linasubiri kuidhinishwa na baraza la mawaziri,” alisema Osiany.

Awali eneo hilo lilipangiwa kubuniwa katika sehemu ya Ombeyi kaunti ndogo ya Muhoroni lakini mpango huo ulipingwa na jamii ya eneo hilo ambao walisema wanataka mgao wa ardhi hiyo.

Osiany amesema eneo hilo jipya linafaa ikizingatiwa kuwa liko karibu na kiwanda cha sukari cha Miwani na kuna muundo msingi bora katika eneo hilo.

Alisema eneo maalum la kipekee la umma katika eneo la Magharibi ya nchi ambalo lina uwezo wa kufufua viwanda vilivyosambaratika na kubuni nafasi za ajira kwa wakazi.

Categories
Habari

Maambukizi ya Covid-19 yanapenyenza katika kaunti zilizo nje ya zile zilizofungwa

Mwenyekiti wa kamati ya afya ya baraza la magavana Profesa Anyang’ Nyong’o, ameonya kwamba kaunti zilizo nje ya zile zilizofungwa kutokana na idadi kubwa ya visa vya maambukizi ya COVID-19, zimeanza kunakili ongezeko la visa vya ugonjwa huo.

Akisema kuwa hali hiyo inatokana na maambukizi ya kijamii, Prof. Nyong’o alizihimiza kaunti zote kuzingatia kanuni za wizara ya afya, zikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji, kuvalia barakoa katika maeneo ya umma, na kutokaribiana.

Hata hivyo alisema kuwa kaunti zimejiandaa ipasavyo kushughulikia ongezeko lolote la visa vya maambukizi ya COVID-19, akisema kwamba kaunti 32 zimeongeza idadi ya vitanda katika muda wa juma moja lililopita.

Prof. Nyong’o, alisema kuwa serikali za kaunti zinatekeleza hatua za kuhakikisha kwamba watu wanaolengwa katika awamu ya kwanza wanapata chanjo katika kipindi kilichowekwa.

Aliihimiza wizara ya afya kuongeza idadi ya vipimo vinavyosambazwa, ili kutimiza lengo hilo na kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

Wakati huo huo, Profesa Nyong’o alisema kuwa usambazaji wa mapato kwa kaunti, umesalia kuwa changamoto, kwani wizara ya afya imetoa shilingi bilioni-19.8, huku wizara hiyo ikiwa bado haijatoa shilingi bilioni-66.

Aliihimiza wizara ya fedha kutoa pesa hizo, ili kuziwezesha serikali za kaunti kuendeleza shughuli zake na kulipa bili, kwa wawasilishaji bidhaa na huduma.

Categories
Habari

Atwoli apewa tano tena COTU bila pingamizi

Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyikazi (COTU), Francis Atwoli, amechaguliwa tena kuhudumu kwa hatamu ya tano.

Atwoli amechaguliwa bila kupingwa na wajumbe wa chama hicho kwenye hafla iliyoandaliwa leo katika Chuo cha Ufanyikazi cha Tom Mboya, Kaunti ya Kisumu.

Kwenye ujumbe wake katika kitandazi cha Twitter, Atwoli amewashukuru wafanyikazi humu nchini kwa imani yao katika uongozi wake kwa kumpa fursa nyingine kuwahudumia kama msemaji wao.

“Nawashukuru wafanyikazi wote wa Kenya kwa kunichagua tena bila kupingwa kupitia wawakilishi wao, kuwa Katibu Mkuu wa COTU. Naahidi kuwahudumia kwa nguvu zangu zote na sitasaliti imani mlioidhihirisha kwangu,” akasema Atwoli.

Atwoli ameahidi kuwahudumia wafanyikazi kwa kujitolea katika hatamu hiyo ya miaka mitano ijayo.

Atwoli amekuwa Katibu Mkuu wa COTU tangu mwaka wa 2001 alipochukua wadhifa huo kutoka kwa marehemu Joseph Joy Mugalla.

Hatamu yake ya sasa ilitarajiwa kukamilika tarehe 26 mwezi Mei.

Atwoli alichaguliwa tena tarehe 26 Mei mwaka wa 2016 kwa hatamu ya miaka mitano.

Categories
Habari

Kijana aliyemkata kichwa nyanyake kuzuiliwa korokoroni kwa siku saba zaidi

Mshukiwa wa miaka 19 ambaye anadaiwa kumkata kichwa nyanya yake katika mtaa wa  Nyalenda kaunti ya Kisumu, atazuiliwa kwa siku saba akisubiri kukamilika kwa uchunguzi wa polisi.

Mahakama iliamua kuwa mshukiwa huyo kwa jina Kelvin Akal, anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla yake kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 19 anadaiwa kumkata kichwa nyanya yake baada yao kuzozana. Baadaye alipeleka kichwa hicho katika kituo cha polisi cha Central Kisumu

Maiti ya mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 70 ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya  Jaramogi Oginga Odinga teaching and referral.

Mwanaume huyo ambaye anasemekana kuachiliwa maajuzi kutoka gereza moja la watoto huko  Kakamega anazuiliwa katika kituo cha polisi cha  Kisumu Central huku uchunguzi wa kubaini lengo la mauaji hayo ukiendelea.

Categories
Habari

Magoha kutangaza matokeo ya KCPE wiki mbili zijazo

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema huenda matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) yakatangazwa katika muda wa majuma mawili yajayo.

Magoha amesema zoezi la usahihishaji wa mtihani huo linaendelea vizuri na kwamba matokeo hayo huenda yakawa tayari siku chache zijazo iwapo mipango yote itaenda kama ilivyopangwa.

Profesa Magoha ameeleza kuwa karatasi za kuchagua majibu ya A hadi D tayari zimekamilika kusahihishwa na sasa zimebaki tu zile za miandiko ya Insha na ‘Composition’.

Magoha spoke in Kisumu County where he supervised the distribution of Day 6 KCSE 2020 examination materials.

Akizungumza leo katika Kaunti ya Kisumu wakati aliposhuhudia usambazaji wa karatasi za siku ya sita ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE), Magoha ametoa tahadhari kwa watu wanaowasaidia watahiniwa kudanganya kwenye mtihani huo.

Waziri huyo amesema wapo walaghai wanaosambaza karatasi bandia za mtihani wa KCSE kupitia makundi ya mitandao ya kijamii, hivyo kusababisha sintofahamu miongoni mwa watahiniwa.

Magoha amewahimiza walimu wakuu na maafisa wa usalama kuwa waangalifu zaidi ili kukomesha visa vya udanganyifu.

Ametoa onyo kwa watahiniwa kwamba yeyote atakayefumaniwa akijaribu kudanganya kwenye mtihani huo atachukuliwa hatua mwafaka pindi atakapokamilisha mtihani wake.

Categories
Habari

Rais Kenyatta aomboleza na familia ya Obama kufuatia kifo cha Mama Sarah Obama

Rais Uhuru Kenyatta ameomboleza na familia ya Obama kufuatia kifo cha Mama Sarah Onyango Obama.

Mama Sarah, ambaye ni mke wa tatu wa babuye Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama, ameaga dunia mapema leo huko Kisumu akiwa na umri wa miaka 99.

Kwenye rambi rambi zake, Rais amemtaja Mama Sara Obama kama nguzo ya maadili mema katika jamii na mkarimu ambaye mchango wake kwa ufanisi wa taifa utakumbukwa daima.

Rais amesema kifo cha mama huyo ni pigo kwa taifa hili, kwani mbali na kuwa nguzo muhimu katika familia yake, alikuwa kielelezo cha maadili ya kifamilia nchini.

Mama Sarah alifariki leo asubuhi katika hositali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga ambapo alilazwa hapo jana asubuhi.

Jina la Mama sarah Obama liligonga vichwa vya habari kufuatia kuchaguliwa kwa mjukuu wake Barack Obama kuwa Rais wa Amerika mwaka 2008.

Atakumbukwa kwa ukarimu wake wa kusaidia watoto na wasiojimudu katika jamii.

Categories
Habari

Mama Sarah Obama aaga dunia

Mama Sarah Obama, ambaye ni nyanyake aliyekuwa Rais wa Marekani Barrack Obama, ameaga dunia.

Kwa mujibu wa familia yake, Sarah amefariki alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu, akiwa na umri wa miaka 99.

Mama Sarah alikuwa amejitolea katika maisha yake kuhudumia yatima na watoto wenye mahitaji kupitia kwa wakfu wake.

Risala za rambi rambi zinaendelea kumiminika kupitia mitandao tangu kifo cha mama huyo kutangazwa.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amemuomboleza Sarah Obama kuwa kielelezo cha ujasiri wa wanawake wa Kiafrika, mwenye uwezo wa kipekee wa kukabiliana na changamoto za maisha.

Amemsifu kwa juhudi zake maishani, ikiwemo uwezo wa kuiongoza familia yake tangu mumewe alipoaga dunia.

Mipango ya mazishi tayari imeanza, huku tarehe ya mazishi ikitarajiwa kutangazwa baadaye.

Categories
Habari

Maafisa tisa wa kaunti ya Kisumu waliomdhulumu mchuuzi mwanamke washtakiwa

Maafisa tisa wa utekelezaji sheria katika kaunti ya Kisumu wamekanusha mashtaka ya kusababisha majeraha mabaya kwa mchuuzi mwanamke.

Maafisa hao ambao walifikishwa mbele ya hakimu Martha Agutu waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu-80.

Maaskari hao tisa wa jiji walishtakiwa kwa kumvuruta Beatrice magolo mwenye umri wa miaka 38 kwa gari aina ya pick-up lililokuwa likiendeshwa kwa kasi siku ya Jumatano pamoja na wenzao ambao hawakuwepo mahakamani.

Wakili Gerald Kadede ambaye aliwaakilisha washukiwa, alidai kwamba wateja wake walikuwa wakitekeleza majukumu yao kama ilivyoratibitiwa kwenye kandarasi za kuwaajiri.

Aliomba wateja wake waachiliwe kwa dhamana kwani wote ndio huwa wanatafutia familia zao riziki.

Kesi yao itatajiwa tarehe 13 mwezi Aprili huku kesi hiyo ikisubiriwa kusikizwa tarehe 20 mwezi huo wa Aprili.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma alisema kitendo kilichotendewa mwanamke huyo ni uhalifu mbaya ambao ulikiuka haki zake za kibinadamu na adhabu ya hukumu ya kifungo cha maisha gerezani yapasa kutolewa.

Kundi la mawakili linamwakilisha mlalamishi likiwemo tawi la Kisumu la shirikisho la wanawake mawakili-FIDA, chama cha wanasheria nchini na tume ya haki za binadamu nchini.