Categories
Burudani

Sukari, Zuchu

Zuchu mwanamuziki anayeangaziwa zaidi katika kampuni ya WCB nchini Tanzania ana kibao kipya kwa jina “Sukari” ambacho alikiachia rasmi kwenye You Tube tarehe 20 mwezi Januari mwaka 2021.

Wimbo huo ulikuwa umesubiriwa kwa hamu na ghamu kutokana na namna alikuwa amefanya matayarisho ya ujio wake kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Alitafuta usaidizi wa watu kadhaa maarufu nchini Tanzania ambao wana umuhimu kwenye jamii kwa jumla ambao walirekodi video fupi kuhusu wasifu wao na mwisho wote wanamalizia kujirejelea kama sukari.

Mamake mzazi ambaye pia ni msanii kwa jina Khadija Omar Kopa ni kati ya waliosaidia kutangaza ujio wa kibao hicho cha Sukari. Kwenye video yake, Khadija anasifia burudani yake ambayo anasema ikosekanapo watu hutaharuki na watu huwa tayari kuigharamia wakati wowote. Onyesho zuri la usaidizi wa mama kwa mwanawe hasa katika kuendeleza talanta.

Mwingine kati ya watu hao mashuhuri ni muigizaji Wema Sepetu ambaye alisema kwamba urembo wake ndio ulimjengea jukwaa analosimamia kwa sasa tangu mwaka 2006 baada ya kushinda shindano la ulimbwende wakati huo na kutawazwa “Miss Tanzania”.

Aligusia pia kipaji chake cha uigizaji ambacho anasema ni cha hali ya juu zaidi na kwamba yeye ni sukari.

Kabla ya kuachilia kibao hicho, Zuchu naye alitoa video akisema kwamba anaamini kila mwanadamu ana umuhimu wake katika jamii. Umuhimu huo ndio anafananisha na ladha ya sukari huku akijirejelea kama sukari ya Zanzibar alikozaliwa.

Zuchu alikwenda kuhojiwa katika kituo cha redio cha Wasafi Fm katika kipindi cha jioni kwa jina Mgahawa ambapo alionyesha waliokuwepo jinsi ya kuuchezea wimbo huo.

Ikumbukwe kwamba alipoingia WCB alimhusisha mkubwa wake Diamond kwenye nyimbo kadhaa ambazo zilisababisha minong’ono kwamba wana uhusiano wa kimapenzi.

Walikuwa wakiandamana kwenye maonyesho kadhaa lakini zamu hii Zuchu alikuwa peke yake alipokwenda kuhojiwa. Alisema Diamond alimpa ahadi ya kumshika mkono alipokuwa akianza lakini pia alimwambia kwamba kuna wakati atamwachilia afanye kazi peke yake.

Kama ilivyo mazoea nchini Tanzania, wengi wamerekodi video wakichezea wimbo huo mpya wa Zuchu kwa jina sukari na amechapisha hizo video kwenye akaunti yake ya Instagram.

Categories
Burudani

Zuchu afurahia kukutana na babake mzazi

“Mwaka 2020 ndio mwaka naupenda zaidi maishani. Babangu mzazi. Mwenyezi Mungu atuweke karibu leo mpaka milele. Amani ambayo ninahisi hakuna anayeelewa. Sijawahi kujihisi mkamilifu hivi. Yaliyopita yamepita Mungu atingoze kwenye yajayo. Ninafurahia sana.”

Ni tafsiri tu ya maneno aliyoandika Malkia wa lebo wa muziki ya Wasafi nchini Tanzania Zuchu kwenye picha yake na babake mzazi.

Zuchu anafurahia kukutana na babake mzazi kwa jina “Othman Soud” aliyejitokeza maajuzi na kutangaza kwamba yeye ndiye baba mzazi wa Zuchu.

Hata baada ya kujulikanisha hilo, Othman alisema anajizuia kumtafuta bintiye kwani wengi wataona kwamba anataka kushiriki ufanisi ambao Zuchu amepata maishani baada ya kutokuwa naye kwa muda mrefu.

Zuchu kwa jina lingine Zuhura Othman ni mtoto wa muimbaji wa taarab bi Khadija Kopa. Wakati wa mahojiano, Bwana Othman alimsihi Khadija asiwe kikwazo kati yake na binti yake.

Ishara kwamba Khadija amekuwa akizuia uhusiano wa karibu kati ya Zuchu na babake mzazi. Alipohojiwa miezi kadhaa iliyopita, Khadija Kopa alisema kwamba muziki wake unamlipa vizuri kiasi cha kumwezesha kulea watoto wake kuonyesha kwamba alikuwa akiwalea pasi na baba yao.

Mashabiki wa Zuchu wamemsifia kwa hatua yake ya kwenda kukutana na babake mzazi, kumsamehe na kumwonyesha mapenzi kwani siku zote damu ni nzito kuliko maji.

Zuchu ameinula katika ulingo wa muziki nchini Tanzania mwaka huu baada ya kujiunga na kampuni ya muziki ya WCB au ukipenda Wasafi ambayo inamilikiwa na Diamond Platinumz.

Categories
Burudani

Cheche za Zuchu na Diamond zi wapi?

Video ya wimbo wa mwanamuziki wa Tanzania Zuchu akiwa amemshirikisha Diamond kwa jina “Cheche” ilitolewa kwenye youtube.Video hiyo ilipotea mtandaoni baada ya kupata kutizamwa zaidi ya mara milioni mbili na nusu.

Tangu kuzinduliwa video hiyo imezua hisia mbali mbali miongoni mwa mashabiki wa wawili hao.

Wakosoaji hawakupendezwa na jinsi Zuchu na Diamond walikuwa wakicheza kwenye video hiyo. Ila mamake Zuchu Khadija Kopa ambaye pia ni mwanamuziki aliwasuta wakosoaji akisema ile ilikuwa tu kazi.

 

Diamond na Zuchu

Akizungumza kwenye kituo cha redio cha Wasafi muda mfupi baada ya kituo hicho kurejelea vipindi vyake, Zuchu alisema anakasirika akisikia watu wakisema kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na Diamond.

Ni maneno yalioanza kusambazwa kutokana na jinsi Zuchu na Diamond walicheza kwenye video ya “cheche”.

Zuchu alisema pia kwamba video hiyo itarudishwa kwenye mtandao kwani Wasafi ni timu kubwa na kwamba wataalamu wanashughulika.

Wimbo “Cheche” pia ulisababisha mvutano kati ya Zuchu na Diamond na Tanasha Donna wa Kenya kwa kile ambacho Tanasha anasema kwamba Zuchu aliiba maneno ya mwanzo kwenye wimbo wake “cheche” kutoka kwa wimbo wa Tanasha na Khaligraph uitwao “ride”.

Wajuaji wanashuku video hiyo ya Cheche imetolewa youtube kwa sababu ya mgongano wa haki miliki na Tanasha Donna anahusika.