Categories
Michezo

Kenya Morans wajikaza kisabuni lakini waambulia kichapo dhidi ya Senegal

Timu ya taifa ya Kenya ya mpira wa Kikapu maarufu kama Morans ilijizatiti katika mechi yake ya kwanza ya kundi B Ijumaa adhuhuri kabla ya kusakamwa na vigogo Senegal pointi 51-69 katika mechi iliyopigwa katika ukumbi wa Palais Polyvalent des Sports  mjini Yaounde Cameroon.

Morans walipoteza  robo ya kwanza alama 18-21 kabla ya kuimarika na kunyakua robo ya pili pointi  13-6 ikiwa pia mara ya kwanza kwa Kenya kushinda robo ya mchezo dhidi ya Senegal.

Hata hivyo maji yalizidi unga kwenye robo ya tatu ,Kenya wakiadhibiwa alama 10-25 na kisha wakalazwa  robo ya mwisho 10-17.

Licha ya kupoteza mchuano huo kocha wa Kenya Liz Mils amesema amejivunia mchezo wa Morans ikilinganishwa na mwaka jana nchini Rwanda katika mzunguko wa kwanza wa kufuzu walipocharazwa na Senegal pointi 92-54.

“mimi najivunia mchezo wa timu yangu  haswa katika robo mbili za mchezo huo,na ile ya pili,ukilinganisha na nchini Rwanda mwaka jana tulijituma ,na wakati mwingine  tukikutana na Senegal mambo yatabadilika”akasema Mils

Morans watarejea uwanjani Jumamosi usiku kukabiliana na timu ya pili bora Afrika, Angola,kabla ya kuhitimisha ratiba dhidi ya Msumbiji Jumapili Jioni.

Kenya ni ya tatu katika kundi B kwa pointi 4 baada ya kushindwa na Angola na Senegal na kuishinda Msumbiji katika mkondo wa kwanza wa mechi hizo za kufuzu ulioandaliwa Kigali Rwanda mwaka uliopita.

Timu 16 zitafuzu kushiriki makala ya 30 ya mashindano ya FIBA Afrobasket mjini Kigali  baina ya Agosti24 na Septemba 5  mwaka huu.

Categories
Michezo

Kenya wasajili ushindi wa kwanza kwa kuichakaza Msumbiji vikapu 79-62 mechi za kufuzu Fiba Afrobasket

Timu ya Kenya ya mpira wa kikapu maarufu kama Morans imekamilisha mechi za raundi ya kwanza katika kundi B kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket kwa ushindi baada ya kuwanyuka Msumbiji vikapu 79-62  Ijumaa jioni katika uwanja wa Kigali.

Morans walianza mchuano huo wakijua kuwa ni ushindi tu ungewaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu baada ya kupoteza mechi za kwanza mbili dhidi ya Senegal na Angola na wakalazimishwa kutoka sare alama 19-19 katika robo ya kwanza ya mchezo .

Hata hivyo Msumbiji waliimarika katika robo ya pili  na kuibwaga Kenya pointi 17-14 huku Kenya wakilipiza kisasi na kushinda robo ya tatu alama 23-17 na kudumisha ushindi kwenye  robo ya mwisho vikapu  23-14 .

Tyler Ongwae kwa mara nyingine tena aliibuka mfungaji bora wa vikapu kwa Kenya kwa kufunga 21 akifuatwa na Valentine Nyakinda aliyefunga vikapu 16  huku nahodha Erick Mutoro akirekodi vikapu 15.

Kenya inayofunzwa na kocha Cliff Owuor itarejea nchini mwishoni mwa juma hili ,kujiandaa kwa mechi tatu za raundi ya pili kundini B wakianza dhidi ya Senegal Februari 19 mjini Kigali Rwanda ,kabla ya kukutana na Angola Februari 20 na kufunga ratiba dhidi ya Msumbiji tena tarehe 21 mwezi Februari mwakani.

Timu tatu bora kutoka kundi hilo zitafuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao nchini Rwanda.