Categories
Habari

Magavana waapa kuwapiga kalamu wahudumu wa afya wanaogoma

Magavana wametishia kuwaachisha kazi wahudumu wote wa afya wanaogoma iwapo hawatarejea kazini mara moja.

Magavana hao pia wamefichua kwamba watasambaza majina ya wafanyanyikazi wote watakaofutwa kazi kufuatia mgomo huo katika kaunti zote ili wasiajiriwe tena kwenye kaunti zengine.

Kwenye kikao na wahariri wa habari, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya ameutaja mgomo huo kuwa kinyume cha sheria.

“Tumesikitishwa na uamuzi wa muungano wa wahudumu wa afya kutekeleza mgomo ambao umedumu kwa mwezi mmoja licha ya janga [la COVID-19] na maagizo ya mahakama. Tunaichukulia hatua hii kuwa kinyume cha haki ya maisha na ya kupata viwango vya juu zaidi vya huduma ya afya kama inavyohakikishwa katika katiba,” akasema Oparanya.

Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega, amesema wahudumu hao walipaswa kutamatisha mgomo wao ili kusubiri matokeo ya mashauriano kati ya Wizara ya Leba na ile ya Afya.

Gavana huyo amesema swala la nyongeza ya mishahara kama wanavyodai wahudumu hao ni jukumu la Tume ya kuratibu mishahara ya watumish wa umma, SRC na Wizara ya Fedha nchini.

Oparanya ameongeza kuwa serikali za kaunti zimejitolea kuhakikisha maslahi ya wahudumu wa afya yameshughulikiwa lakini akatahadharisha kuhusu matakwa mengi ya wahudumu hao kwani uchumi wa nchi hii umeathiriwa pakubwa na janga la COVID-19.

Baadhi ya serikali za kaunti, ikiwemo ile ya Mombasa, tayari zimechukua hatua ya kuwaachisha kazi wahudumu wa afya wanaogoma.

Categories
Habari

Seneta Malala amtaka Ruto ajitoe kwenye kinyang’anyiro cha Urais

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ametoa wito kwa Naibu Rais William Ruto kutupilia mbali azma yake ya kuwania wadhifa wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Malala amemtaka Ruto badala yake amuunge mkono kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi katika azma hiyo.

Akiongea katika Kaunti ya Uasin Gishu, Seneta huyo amesema Naibu Rais bado ana umri mdogo na ataweza kuwania wadhifa huo katika siku za usoni.

Ametoa wito kwa wakazi wa Uasin Gishu kumuunga mkono Mudavadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wakati uo huo, Malala amemhimiza Ruto kuunga mkono hadharani mchakato wa BBI bila masharti yoyote, akisema mchakato huo unashughulikia maslahi ya Wakenya.

Amewataka Wakenya kudumisha amani huku taifa hili likijianda kwa kura ya maamuzi ya marekebisho ya katiba.

Categories
Habari

Serikali ya Kakamega yatakiwa kuwafidia wahudumu wa afya waliofariki kutokana na Covid-19

Wahudumu wa afya kaunti ya Kakamega wametoa ilani ya mgomo ya siku 21,ikiwa serikali ya kaunti hiyo haitawafidia maafisa wa afya ambao wameaga dunia kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Kwenye barua kwa afisa mkuu wa afya katika kaunti hiyo Dkt. Collins Matemba,tawi la Kakamega la chama cha kitaifa cha wauguzi na watalaamu wa afya,limesema serikali ya kaunti hiyo imepuuza wito wao wa kuimarishwa kwa mazingira ya kazi kufwatia changamoto ambazo zimetokana na janga la korona.

Wamesema hawawezi kusalia kimya,huku idadi kubwa ya wahudumu wa afya wakiendelea kuambukizwa korona,na wengine kupoteza maisha wakipambana na  ugonjwa huo.

Kufikia sasa jumla ya wahudumu wa afya 102 wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19,na wengine kadhaa kuaga dunia miongoni mwao msimamizi  wa wafanyakazi katika kaunti ya kakamega Robert Sumbi na mbunge wa Matungu Justus Murunga.

Haya yanajiri baada ya wahudumu wa afya kaunti ya Bomet kuanza mgomo siku ya Alhamisi

Categories
Habari

Vijana wahimizwa kuunga mkono BBI kwa manufaa yao ya kiuchumi

Vijana kote nchini wamehimizwa kusoma na kuelewa ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI, kabla ya kufanya maamuzi yoyote kuhusu.

Chama cha wabunge vijana nchini kinasema ripoti hiyo ina uwezo mkubwa wa kunufaisha vijana nchini lakini lazima wajizindue na kushinikiza ajenda zao.

Kundi hilo lilizungumza wakati ambapo kuna maoni tofauti kuhusu ripoti hiyo huku baadhi ya vijana katika Kaunti ya Kitui wakitaka eneo la Mwingi liwe kaunti kiviake.

Wakati uo huo, Mbunge wa Butere, Tindi Mwale ameanza kuwaongoza baadhi ya vijana wa eneo la Magharibi mwa nchi kuunga mkono ripoti ya BBI.

Mbunge huyo anasema ripoti hiyo ni njia bora ya kujumuisha vijana kikamilifu katika maswala ya  utawala.

Katika Kaunti ya Kakamega, baadhi ya vijana wa eneo hilo wameapa kuunga mkono ripoti ya BBI wakisema inashughulikia uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi wa kizazi kipya nchini.

Hata hivyo, kundi hilo linawalaumu wale wanaopinga ripoti hiyo, likiwarai Wakenya kujitenga na watu wachache wanaotumia mchakato huo kuigawanya nchi hii.

Categories
Habari

Afisa mkuu wa wafanyikazi kaunti ya Kakamega afariki kutokana na Covid-19

Afisa mkuu wa wafanyikazi katika kaunti ya Kakamega Robert Sumbi amefariki. Sumbi aliaga kutokana na matatizo yanayohusiana na ugonjwa wa COVID-19 leo asubuhi.

Duru zinaeleza kuwa alifariki wakati alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti.

Alikuwa miongoni mwa wafanyikazi wa kaunti, ambao walikuwa wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19 jambo ambalo lilimfanya  gavana Wycliffe Oparanya kukomesha shughuli zote katika makao makuu ya kaunti.

Bunge kadhaa za Kaunti zimesimamisha shughuli zao kutokana na maambukizi ya viusi vya covid-19. Bunge hizo za Kaunti ni pamoja na Kericho,Mombasa,Kakamega na Bungoma miongoni mwa zingine

Nchi hii tangu majuzi imenakili idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Siku ya Jumatano kaunti ya Kakamega ilirekodi visa vinne vipya vya COVID-19

Categories
Habari

Oparanya aibuka Gavana mchapa kazi bora zaidi

Gavana wa Kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya ametajwa kuwa gavana anayetenda kazi kwa ubora zaidi kwenye orodha ya hivi punde zaidi iliyotolewa leo na kampuni ya Infotrak.

Kulingana na matokeo ya utafiti huo uliochunguza utenda kazi wa magavana katika kipindi cha mwaka 2019/2020, Oparanya alipata asilimia 82.3, akifuatwa na Gavana wa Kwale, Salim Mvurya kwa asilimia 77.1, naye Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana ni wa tatu kwa asilimia 74.4.

Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o ni wa nne akifuatwa na Alfred Mutua wa Machakos.

Nao John Lonyangapuo wa Pokot Magharibi, Jackson Mandago wa Uasin Gishu, Muthomi Njuki wa Tharaka Nithi, Josphat Nanok wa Turkana na Hillary Barchok wa Bomet wanafuata kwa mpangilio huo.

Kampuni hiyo ya utafiti imewaorodhesha magavana kuambatana na vigezo vikuu vya utenda kazi kuhusiana na majukumu yaliyogatuliwa yakiwemo Afya, Elimu, Kilimo, Huduma za Kijamii, Usimamizi wa Maji, Mazingira na Rasilimali Asili.

Katika sekta ya afya, utafiti huo ulizingatia uwezo wa serikali za kaunti kutoa huduma za kimatibabu kwa wakazi kwa bei nafuu na kuhakikisha kwamba vituo vya afya viko na vifaa vya matibabu na madawa ya kutosha.

Katika sehemu hizo zote zilizozingatiwa, Gavana Oparanya alipata alama za kuridhisha.

Kaunti ya Makueni inayosimamiwa na Kivutha Kibwana iliorodheshwa kuwa iliyoimarika zaidi baada ya kutoka nambari 40 kwenye utafiti wa mwaka 2015.

Kaunti zilizodorora zaidi ni Taita Taveta iliyoteremka hadi nambari 36 kutoka 9 mwaka 2015, Samburu imeorodheshwa nambari 44 kutoka 21 na Homa Bay iliorodheshwa nambari 39 kutoka 18.

Kaunti za Tana River, Wajir na Isiolo ndizo zilizoshikilia nafasi tatu za mwisho.

Watafiti hao walielezea kwamba katika baadhi ya kaunti, utoaji huduma unaridhisha kuliko umaarufu wa magavana husika.

Utafiti huo uliofanywa kati ya mwezi Desemba 2019 na Januari 2020 pia unaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanasema ugatuzi unafanikiwa.

Categories
Habari

Mwanamume ajitia kitanzi kwa kushindwa kulipa deni Kakamega

Hali ya simanzi imeghubika Wadi ya Eshiambitsi huko Navakholo, Kaunti ya Kakamega baada ya mwanamme wa umri wa makamo kujiua kwa kushindwa kulipa mkopo wa shilingi 13,000 aliochukua miezi kadhaa iliyopita

Mwili wa Solomon Ayindi umeonekana na majirani ukining’inia kwenye dari ya nyumba yake baada ya kujitia kitanzi.

Akizungumza kwa niaba ya familia yake, mamaye Alice Omwenje amesema mwendazake alikuwa na msongo wa mawazo kutokana na mkopo huo wa rehani.

“Tumemuita lakini hakuitika, tukabomoa mlango tukapata kijana amejinyong’a,” ameeleza Omwenje.

Omwenje amesema mwendazake alikuwa alilipa sehemu ya mkopo huo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi lakini mdeni wake akamshinikiza kulipa pesa zilizosalia, hali iliyomsababishia kukata tamaa ya maisha.

“Alianza kulipa lakini ikabaki elfu saba na akaacha kulipa mwezi wa tatu, wakaweka riba na ikafikia 13,200,” akasema.

Wazee wa jamii hiyo wakiongozwa na mjombake Japhet Kataka wamesema watafuata utamaduni kwa sababu wale wanaojiua hawafai kupelekwa katika hifadhi ya maiti lakini kaburi linafaa kuchimbwa mahali walikofariki na nyumba yake kuteketezwa moto.

Visa vya matatizo ya kiakili vimekuwa vikiongezeka humu nchini kutokana na athari za ugonjwa wa Covid 19.

Categories
Habari

Wakazi waliokuwa na ghadhabu wateketeza kituo cha polisi Kakamega

Wakazi wa kaunti ya   Kakamega  waliokuwa na ghadhabu, waliteketeza  kituo kimoja  cha polisi baada  ya kukabiliana na maafisa wa polisi. 

Kulingana na kamanda wa polisi katika eneo la  Magharibi,  Peris Kimani, ghasia zilizuka  baada  ya afisa mmoja wa polisi  kwenye kituo cha  polisi cha  Mbururu  kudaiwa kumdhulumu  mwanamume  mmoja  kwa  jina, Dennis Lusavu ambaye  pia hutambuliwa kwa jina  Bazenga kwa  kosa la kutovaa  maski.

Mtu huyo ametoweka tangu kisa hicho, na hajapatikana.

Kisa hicho kiliwakasirisha wakazi  ambao waliamua kuelekeza  gahdhabu kwa kituo hicho na kukiteketeza.

Kimani alisema kuwa umati wa takriban watu  300 ulivamia kituo hicho  na kuwashinda nguvu maafisa sita wa polisi waliokuwepo kisha wakakiteketeza.

“Tumepoteza silaha zote zilizokuwemo katika kituo hicho cha polisi baada ya wakazi hao kukichoma moto,” alisema Kimani

Kamanda huyo wa polisi alifichua kuwa  afisa mkuu wa polisi wa kituo hicho  alijeruhiwa  kwenye kisa hicho  na akapelekwa hospitalini.

Maafisa wa polisi kutoka kikosi cha GSU walipelekwa kurejesha hali ya utulivu.

Categories
Habari

Maraga: Tunaazimia kuwa na mahakama kuu katika kila kaunti

Jaji mkuu David Maraga amesema kuwa idara ya mahakama imejitolea kuimarisha miundo misingi ya mahakama nchini katika juhudi za kuboresha huduma.  

Maraga, ambaye alikuwa akiongea alipokuwa akizindua jengo la mahakama katika mahakama ya Kakamega, alisema kuwa wanakaribia kuafikia maazimio ya kuwa na mahakama kuu katika kila kaunti.

Hii ni baada ya kuorodhesha katika gazeti rasmi la serikali vituo vine vya mahakama kuu katika kaunti za Isiolo, Vihiga, Kwale na Nandi juma lililopita.

Alifichua kuwa ujenzi wa jengo hilo ulifadhiliwa na benki ya dunia kupitia mradi wa kuimarisha utendakazi wa idara ya mahakama kwa kima cha shilingi milioni  388.7.

Jaji  Maraga alisema kuwa kaunti za Samburu, Pokot magharibi, Wajir, Mandera na  Elgeyo Marakwet hazijapata vituo vya mahakama kuu.

Alisema kuwa wameorodhesha mahakama 17 mpya za hakimu ambazo zitaongeza idadi ya mahakama hizo kutoka 127 hadi 144 na kufanya kaunti zote ndogo 290 nchini kuwa na mahakama ya hakimu.

Alisema kuwa jengo hilo la kisasa litahifadhi sekta zote muhimu za idara ya mahakama ikiwemo afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma, afisi za magereza na afisi za polisi.

 

Categories
Habari

Shule za Msingi na Upili za umma kupokea madawati zaidi

Shule za msingi zitapata madawati elfu-360 yatakayotengenezwa kwa gharama ya shilingi milioni- 900 huku zile za sekondari zikipokea meza na viti 263,157 vitakavyotengenezwa kwa gharama ya shilingi bilioni moja chini ya mpango wa serikali wa muundomsingi wa shule.

Akiongea alipozuru kaunti ya Kakamega kukutana na mafundi watakaotengeneza madawati hayo, waziri wa elimu Prof.  George Magoha alisema kuwa mafundi wa eneo lolote husika ndio watahusishwa na kwamba hakuna zabuni zozote zilizotolewa kwa sasa.

Profesa Magoha alisema kuwa serikali inaazimia kuhakikisha kwamba madawati hayo yatakuwa shuleni kufikia mwisho wa mwezi ujao.

Waziri huyo alisema kuwa serikali inategemea mafundi wa humu nchini kuwasilisha madawati hayo mapya.

Waziri aliyaonya makundi ya walaghai yanayonuia kupora mali ya umma kwamba hawatapa fursa hiyo na kwamba yeyote atakayepatikana akijaribu kupora pesa hizo atachukuliwa hatua kali.

Kulingana na Magoha hatua ya kuwapa mafundi wa humu nchini kazi hiyo, ni katika juhudi za serikali za kuwapa uwezo vijana katika sekta hiyo na kwamba wale watakaopewa fursa ya kuwasilisha madawati hayo ni sharti watengeneze samani za hali ya juu zinazotimiza viwango vilivyowekwa.