Categories
Burudani

Ushauri wa Professor Jay

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Tanzania ambaye pia ni mwanasiasa Professor Jay kwa jina halisi Joseph Haule ametoa ushauri kwa wanamuziki nchini Tanzania.

Ushauri huo aliupa mada ya “Shule ya Bure” kasha akaandika “Sio lazima kila siku uimbe matusi na mambo ya kitandani ili wimbo wako uwe mkubwa na upendwe, bali unaweza kuimba wimbo wenye mafunzo mema kwa jamii na wadau wakakushika mkono kwa kiwango cha juu kabisa. Kwa pamoja tunaweza kuokoa kizazi hiki.”

Jay anaonekana kukwama kwenye maadili yaliyokuwepo kwenye fani ya muziki tangu wakati walianza muziki.

Bidii yake ya kutafuta kurejesha maadili inaonekana kushabihiana na ile ya mashirika mbali mbali ya serikali nchini Tanzania kama vile BASATA.

Maajuzi Professor Jay amerejelea muziki baada ya mapumziko ya zaidi ya miaka mitano wakati akihudumu kama mbunge wa eneo la Mikumi.

Wimbo wake na Stamina kwa jina Baba unaendelea kufanya vyema kwenye mitandao ya kijamii.

Unagusia uhusiano kati ya mvulana na babake na maadili kwa jumla. Mvulana huyo anamkosea babake heshima kwa sababu ya ufukara na baadaye babake anamfichulia kwamba yeye sio babake mzazi ila ni baba mlezi.

Muda mfupi baada ya uzinduzi wa wimbo huo, ndipo habari zilichipuza kuhusu baba mzazi wa mwanamuziki Diamond Platnumz na wengi wanashangaa ikiwa Jay na Stamina walikuwa na habari kuhusu hilo.

Categories
Burudani

Professor Jay arejelea muziki

Joseph Haule maarufu kama Professor Jay amerejelea muziki baada ya kugonga mwamba kwenye siasa na uongozi nchini Tanzania.

Jay ambaye ana umri wa miaka 45 sasa ni mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Aliendeleza kazi hiyo ya muziki iliyompa umaarufu hadi mwaka 2015 alipowania kiti cha ubunge katika eneo la Mikumi na kushinda.

Akihudumu kama mbunge kazi ya muziki aliisimamisha kabisa. Mwaka jana kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Professor Jay na wengine wengi wa chama cha “CHADEMA” walibwagwa. Aliyemshinda katika ubunge wa Mikumi ni Dennis Lazaro wa chama cha CCM.

Tangu wakati huo amesalia kimya hadi maajuzi alipojitokeza tena kwenye ulingo wa muziki kupitia kwa mwanamuziki mwenzake Stamina.

Stamina amemshirikisha Jay kwa ngoma yake mpya kwa jina “Baba” ambayo ilizinduliwa rasmi jana tarehe 13 mwezi Januari mwaka 2021.

Professor Jay alitangaza ujio wa kibao hicho kipya kwenye akaunti yake ya Instagram huku akihimiza mashabiki wakakitazame kwenye akaunti ya Stamina ya You tube.

Duru zinaarifu kwamba sasa jay ambaye anaigiza kama babake Stamina kwenye video ya wimbo huo amerejelea muziki kikamilifu.

Stamina anafungua wimbo huo akimpigia babake simu huku akimzomea na kumlaumu kwa matatizo anayopitia maishani.

Anamuuliza ni kwa nini hakumpeleka mamake akaavye mimba yake kwani anasikia aliikataa hiyo mimba.

Analaumu babake pia kwa ufukara anashangaa ni kwa nini wanaishi nyumba ya kupangisha na hamiliki hata shamba.

Anapoingia babake, anamwelezea kwamba vipimo vilionyesha kwamba yeye sio babake mzazi ila aliamua tu kumlea kama baba mzazi na anashangaa ni kwa nini hakusoma ajitengenezee maisha mazuri.

 

Categories
Burudani

Mwanamuziki Professor Jay ashindwa kutetea kiti cha ubunge

Joseph Haule almaarufu Professor Jay mwanamuziki ambaye aliingilia siasa nchini Tanzania alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge wa eneo la Mikumi katika uchaguzi mkuu ulioganyika jumatano.

Jay wa chama cha CHADEMA alibwagwa na Dennis Lazaro wa chama cha CCM ambaye alizoa kura 31,411 na Professor Jay akapata kura 17,375.

Kiongozi wa chama chake Bwana Tundu Lissu anaonekana kutoridhishwa na shughuli nzima ya uchaguzi akisema ilikumbwa na udanganyifu kwani maajenti wake walizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupiga na kuhesabu kura.

Haule amekuwa mbunge wa Mikumi kwa miaka mitano sasa na alishinda uchaguzi wa mwaka 2015 kupitia chama chake cha CHADEMA.

Wakati huo alijizolea kura 32,259.

Professor Jay ana umri wa miaka 44 sasa na amekuwa kwenye fani ya muziki tangu mwaka 1989 akiwa mmoja wa wasanii katika kundi la “Hard Blasters” na wakati huo alikuwa anajiita “Nigga J”.

Kundi hilo lilizindia albamu ya kwanza iliyojulikana kama “Funga Kazi” na baadaye wakaibuka washindi wa tuzo la kundi bora la muziki wa hip hop.

Alianza kuimba peke yake mwaka 2001 na kufikia sasa ana albamu sita ambazo ni “Machozi, Jasho na Damu”, “Mapinduzi Halisi”, “J.O.S.E.P.H”, “Aluta Continua”, “Izack Mangesho” na “Kazi Kazi” ya mwaka 2016 wakati akiwa mgeni bungeni.

Akiwa anahudumia watu wa Mikumi kama Mbunge, Profesor Jay alionekana kupunguza kazi ya muziki kidogo na sasa inasubiriwa kuona ikiwa atarejea kikamilifu kwenye fani hiyo.