Categories
Habari

Rais Kenyatta akutana na Waziri kutoka Japan katika Ikulu ya Nairobi

Rais Uhuru Kenyatta amekutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan anayezuru humu nchini, Toshimitsu Motegi, katika Ikulu ya Nairobi.

Wakati wa mkutano huo, Motegi, ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili humu nchini, ameeleza kuendelea kujitolea kwa Japan kuunga mkono mipango ya maendeleo humu nchini, hasa miradi ya muundo msingi.

Motegi ametaja mradi unaoendelea wa kupanua Bandari ya Mombasa na ustawishaji eneo maalum la kiuchumi la Dongo Kundu kuwa baadhi ya miradi ambayo serikali yake inamakinika kuhakikisha imekamilishwa.

Waziri huyo wa Japan pia amemuarifu Rais Kenyatta kuhusu kongamano la kibiashara kati ya Japan na Kenya ambalo litaandaliwa baadaye mwaka huu nchini Japan na akawasilisha mwaliko wa Waziri Mkuu Yoshide Suga kwake.

Kwa upande wake Rais Kenyatta ameeleza kutambua hatua ya Japan kuendelea kuunga mkono mipango ya maendeleo humu nchini, akisema nchi hii itaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kihistoria na taifa hilo la Bara Asia.

Categories
Kimataifa

Muungano wa Ulaya wasambaza chajo za Corona kwa mataifa wanachama

Muungano wa Mataifa ya Bara Ulaya, EU, umezindua kampeni ya pamoja ya kuchanga raia dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Rais wa tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema kuwa chanjo ya Pfizer-BioNTech tayari imesambazwa kwenye mataifa yote 27 ya muungano huo.

Baadhi ya mataifa ya muungano huo yalianza kutoa chanjo hiyo Jumamosi.

Muungano wa Ulaya kufikia sasa umenakili vifo vya watu 335,000 kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Zaidi ya watu milioni 14 wameambukizwa virusi hivyo, huku maagizo makali yakiendelea kuzingatiwa dhidi ya msambao huo.

Kampeni hiyo ya chanjo inajiri huku aina mpya ya virusi vya Corona ikigunduliwa katika baadhi ya mataifa ya Ulaya pamoja na Canada na Japan.

Categories
Kimataifa

Serikali ya Japan yabuni mbinu ya kuhimiza raia wafanye mapenzi zaidi

Japan inapanga kufadhili michezo ya mitandaoni itakayokutanisha watu ili kuchochea raia wake kufanya mapenzi.

Hatua hiyo inatokana na lengo la serikali ya nchi hiyo kutaka kushughulikia suala la kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa.

Kuanzia mwaka ujao, serikali ya Japan itapiga jeki serikali za majimbo ambazo zinapanga kuanzisha ama zilizoanzisha tayari mifumo ya mitandaoni ya kuunganisha watu.

Mwaka uliopita idadi ya watoto waliozaliwa nchini Japan ilikuwa chini ya elfu 865, idadi ambayo ni ya chini zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Taifa hilo lenye idadi ya juu zaidi ya wakongwe kuliko vijana limekuwa likitafuta mbinu za kubadili hali ya wakazi wake kukosa kuzaana kwa haraka kwa kuboresha utumizi wa teknolojia miongoni mwa mbinu nyingine za hivi punde.

Mwaka ujao, serikali hiyo inapanga kusambazia serikali za majimbo takribani dola milioni 19 za kiMarekani ili kushughulikia swala hilo.

Idadi ya watu nchini Japan inatarajiwa kupungua kutoka  milioni 128 mwaka wa 2017 hadi chini ya millioni 53 kufikia mwisho wa karne hii.

Watunzi wa sera wanajitahidi kuhakikisha usawa kati idadi inayozidi kupungua ya wafanyikazi na gharama inayozidi kuongezeka ya maslahi ya wafanyikazi hao.

Categories
Habari

Rais Kenyatta ampongeza Waziri Mkuu mpya wa Japan Yoshihide Suga

Rais Uhuru Kenyatta amempongeza Yoshihide Suga kufwatia kuchaguliwa kwake kuwa Waziri Mkuu mpya wa Japan.

Suga anachukua nafasi ya Shinzo Abe ambaye alijihuzulu wadhifa huo kutokana na sababu za kiafya.

Kwenye risala yake ya pongezi, Rais Kenyatta amemtakia Suga kila la heri kwenye wadhifa huo.

“Tafadhali pokea pongezi zangu kwa ushindi wako na nakutakia heri ya ufanisi unapochukua majukumu ya wadhifa kama Waziri Mkuu mpya wa Japan.”

Aidha, Rais Kenyatta amemhakikishia Suga kuwa uhusiano mwema uliopo kati ya Japan na Kenya utazidi kudumishwa.

Wakati uo huo, Rais Kenyatta amemuaga Waziri Mkuu anayeondoka mamlakani Shinzo Abe. Kwenye ujumbe wake, Rais Kenyatta amempongeza Abe kwa misaada ya kimaendelo ya Japan kwa Kenya wakati wa utawala wake.

“Nachukua fursa hii kukushukuru kwa kuwa kiongozi mwema na wakutegemewa katika ufufuzi wa uhusiano mwema kati ya Kenya na Japan. Kutokana na msaada wa serikali ya Japan, Kenya imeshuhudia kupungua kwa gharama ya kawi, uimarishaji wa miundo msingi ya uchukuzi na mawasiliano na pia usambazaji wa nguvu za umeme kote nchini,” amesema Rais.