Categories
Kimataifa

Trump akabiliwa na tishio la kung’atuliwa mamlakani tena

Bunge la Marekani huenda likapiga kura Jumanne kuhusu azma ya kumng’oa Rais Donald Trump mamlakani, kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa chama cha Democratic.

Wabunge wa chama hicho wamepania kuchukua hatua hiyo kwa misingi kwamba matamshi ya Trump yalichochea ghasia na uvamizi uliofanywa katika jengo la Capitol Hill ambao pia ulisababisha vifo vya watu watano.

Kiranja wa Bunge hilo James Cyburn anasema kuwa hatua zitachukuliwa wiki hii kutokana na kisa hicho.

Hata hivyo huenda wabunge hao wasiwasilishe kifungu kuhusu mchakato huo katika Bunge la Seneti hadi baada ya siku 100 za utawala wa Joe Biden.

Muda huo utampa fursa Biden kuliunda baraza lake jipya la mawaziri na kuzindua sera mpya, zikiwemo za kukabiliana na janga la COVID-19.

Trump hajatoa matamshi yoyote rasmi tangu alipong’atuliwa kutoka mitandao ya kijamii, hasa ule wa Twitter, siku ya Ijumaa.

Hata hivyo taarifa kutoka Ikulu ya White House zilisema kuwa Rais Trump atafanya ziara huko Texas siku ya Jumanne na kuzuru eneo la mpaka wa nchi hiyo na Mexico, ambako aliamuru kujengwa ukuta wakati wa utawala wake ili kuzuia uhamiaji haramu.