Categories
Habari

Wabunge washinikiza kuimarishwa kwa biashara kati ya Kenya na Tanzania

Kamati ya Bunge kuhusu Ushirikiano wa Kanda ya Afrika Mashariki imeweka mikakati ya kuimarisha biashara kati ya Kenya na Tanzania.

Akiongea wakati wa ziara mjini Isebania, Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo Ruweida Mohamed amesema biashara kupitia mpaka wa Kenya na Tanzania imekumbwa na changamoto ambazo zimeathiri mazingira ya utendaji biashara baina ya mataifa husika.

Hata hivyo, Ruweida ameeleza kuridhika na upimaji wa ugonjwa wa Korona kwenye mpaka huo ambao umeimarika kwa kiasi kikubwa licha ya changamoto za kisera kwenye mataifa husika.

Aidha ameeleza kufadhaishwa na ukosefu wa ushirikiano kati ya serikali ya taifa na ile ya Kaunti.

Wafanyabiashara wa humu nchini walikuwa wanalalamikia kuhangaishwa na maafisa wa usalama wa Tanzania na kufutiliwa mbali kwa leseni zao za kuhudumu.

Awali, katibu katika idara ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kevit Desai, alisema serikali imejitolea kuwakinga wafanyabiashara dhidi ya athari za ushuru wa juu.