Categories
Habari

Rais Kenyatta akutana na Waziri kutoka Japan katika Ikulu ya Nairobi

Rais Uhuru Kenyatta amekutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan anayezuru humu nchini, Toshimitsu Motegi, katika Ikulu ya Nairobi.

Wakati wa mkutano huo, Motegi, ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili humu nchini, ameeleza kuendelea kujitolea kwa Japan kuunga mkono mipango ya maendeleo humu nchini, hasa miradi ya muundo msingi.

Motegi ametaja mradi unaoendelea wa kupanua Bandari ya Mombasa na ustawishaji eneo maalum la kiuchumi la Dongo Kundu kuwa baadhi ya miradi ambayo serikali yake inamakinika kuhakikisha imekamilishwa.

Waziri huyo wa Japan pia amemuarifu Rais Kenyatta kuhusu kongamano la kibiashara kati ya Japan na Kenya ambalo litaandaliwa baadaye mwaka huu nchini Japan na akawasilisha mwaliko wa Waziri Mkuu Yoshide Suga kwake.

Kwa upande wake Rais Kenyatta ameeleza kutambua hatua ya Japan kuendelea kuunga mkono mipango ya maendeleo humu nchini, akisema nchi hii itaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kihistoria na taifa hilo la Bara Asia.

Categories
Habari

Rais Kenyatta amuomboleza Profesa wa Matibabu James Kagia

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa faraja kwa familia, jamaa na marafiki wa Profesa James Kagia aliyeaga dunia Jumatatu.

Profesa Kagia ni mumewe Ruth Kagia ambaye ni Naibu Msimamizi wa Wafanyikazi anayeshughulika na maswala ya sera na mikakati katika Ikulu ra Rais.

Kwenye salamu zake za rambi rambi, Rais amemtaja Profesa huyo kama daktari mtimilifu wa Kenya, msomi na mhadhiri wa chuo kikuu ambaye huduma zake kwa taifa hili zitakosekana sana.

Kiongozi wa Taifa amesikitishwa sana na kifo cha Kagia, mtaalamu wa afya ya umma mwenye tajriba kuu, wakati ambao nchi hii inahitaji sana weledi wake katika vita dhidi ya janga la Corona.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba tumempoteza Profesa Kagia wakati ambao nchi hii inahitaji huduma zake zaidi, hasa kukabiliana na mgogoro wa kiafya unaotokana na COVID-19 ambao umeathiri ulimwengu mzima,” akaomboleza Rais.

Profesa Kagia alifunza somo la Afya ya Umma kwa miaka mingi katika Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya kuhudumu kama Daktari wa Matibabu katika Hospitali za John Hopkins na Georgetown nchini Marekani.

Rais Kenyatta amewaombea faraja Mjane Ruth Kagia na familia yote ya mwendazake wakati huu wa maombolezo.

Categories
Habari

Rais Kenyatta asifu ushirikiano serikalini katika utoaji huduma

Rais Uhuru Kenyatta amesema jitihada za pamoja za serikali zimeimarisha utoaji huduma kwa wananchi.

Rais amesema ijitaha hizo zimesaidia katika ukamilishaji miradi ya maendeleo, kuhakikisha kuna matumizi bora ya fedha za maendeleo pamoja na uwajibikaji kwa wale wanaotekeleza miradi hiyo.

Kiongozi wa taifa amesema hatua hiyo pia imewezesha serikali kuchukua hatua mwafaka kuhusiana na janga la COVID-19.

Kenyatta amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hatua kubwa zimepigwa katika kukamilisha miradi ya maendeleo, matumizi bora ya fedha za maendeleo, pamoja na uwajibikaji kwa mashirika yanayohusiana na miradi hiyo.

Amesema jitihada za pamoja za serikali zimewezesha kuwepo kwa ushirikiano kuhusiana na janga la Covid-19.

“Jitihada hizi za pamoja serikalini zimekuwa nguzo katika ushirikiano wa utawala katika kukabiliana na janga la COVID-19 na zinaendelea kusaidia katika juhudi za kupona kutokana na janga hilo,” amesema Rais.

Rais Kenyatta alikuwa akizungumza katika Ikulu ya Nairobi wakati alipoongoza hafla ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano wa kimtandao wa kubadilishana maoni kuhusu utaoaji huduma barani Afrika, kwa ushirikiano wa Benki ya Maendeleo Barani Afrika pamoja na Taasisi ya Tony Blair .

Hatua hiyo ni kuambatana na agizo la rais nambari moja lililotolewa mwezi Januari mwaka wa 2019, ambalo  lilibuni kamati kuhusu maendeleo ya kitaifa.

Categories
Habari

Rais Kenyatta aidhinisha sheria mpya ya uteuzi wa makamishna wa IEBC

Rais Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria, mswada nambari tatu wa mwaka 2019 wa marekebisho ya sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.

Sheria hiyo mpya inatoa nafasi ya kubuni jopo la uteuzi la kusimamia mchakato wa kujaza nafasi za makamishna zilizoachwa wazi katika tume hiyo.

Aidha sheria hiyo inaratibu mfumo wa uteuzi wa makamishna wa tume ya IEBC na kufafanua masharti ya kuhitimu kwa wanachama wa jopo hilo la uteuzi.

Tume ya IEBC iliyo na idadi inayohitajika ya makamishna inatarajiwa kusimamia kura ya maamuzi ya marekebisho ya katiba mwaka ujao.

Tume hiyo kwa sasa ina makamishna watatu baada ya makamishna wanne kujiuzulu.

Rais pia ametia saini kuwa sheria mswada wa mwaka huu wa kudhibiti matangazo ya nje katika kaunti.

Sheria hiyo inalenga kulainisha matangazo ya nje katika maeneo ya kaunti kwa kuhakikisha masuala ya kibiashara, mazingira na usalama wa umma yanazingatiwa kwa usawa.

Sheria hiyo inatambua umuhimu wa matangazo ya nje kama chanzo cha mapato kwa serikali za kaunti na inatoa leseni kwa usawa katika kaunti zote 47.

Miswada hiyo iliwasilishwa kwa Rais na Wakili Mkuu wa Serikali Ken Ogeto ili kutiwa saini katika Ikulu ya Nairobi.

Shughuli hiyo imeshuhudiwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka, Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt. Joseph Kinyua, Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya, miongoni mwa viongozi wengine serikalini.

Categories
Kimataifa

Trump athibitishwa kuwa hawezi kueneza tena COVID-19

Daktari wa Ikulu ya White House nchini Marekani Sean Conley amethibitisha kuwa Rais Donald Trump hawezi tena kusambaza virusi vya Korona.

Hii ni taarifa ya kwanza rasmi kutolewa na daktari huyo kuhusu afya ya Rais Trump tangu Alhamisi wiki hii.

Hapo jana, Trump alihutubia wafuasi wake kutoka ubaraza wa Ikulu ya White House katika hotuba yake ya kwanza tangu alipoondoka hospitalini alikokuwa akitibiwa ugonjwa wa COVID-19.

Kumekuwa na wasi wasi kuwa huenda Trump akaeneza virusi hivyo baada ya kulazwa hospitalini kwa siku tatu tu kisha akaruhusiwa kuondoka.

Taarifa ya daktari huyo inabaini kuwa hakuna ushahidi kwamba Rais Trump anaweza kuambukiza watu virusi vya Korona kwani amepata nafuu.

Siku chache zilizopita, Trump alishtumiwa na madaktari nchini humo baada ya kuondoka hospitalini alipokuwa anatibiwa COVID-19 na kuwahutubia wafuasi nje ya hospitali hiyo akiwa kwenye gari lake.

Madaktari hao walimushtumu Trump kwa kitendo hicho wakisema kuwa kilihujumu kanuni zilizowekwa za kudhibiti msambao wa ugonjwa huo.

Categories
Habari

Rais Kenyatta aidhinisha sheria ya ugavi wa mapato kwa kaunti

Rais Uhuru Kenyatta ametia sahihi mswada wa ugavi wa mapato kwa kaunti 2020/2021 kuwa sheria.

Hatua hii inatarajiwa kuidhinisha usambazaji wa mgao wa shilingi bilioni 369 kutoka serikali kuu hadi kwa zile za magatuzi.

Mswada huo umewasilishwa kwa Rais na Spika wa Bunge la Seneti Ken Lusaka katika hafla ya Ikulu ya Nairobi mapema leo iliyohudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Waziri wa Fedha Ukur Yattani.

Viongozi wa wengi katika mabunge yote mawili Poghisio na Amos Kimunya pia wamehudhuria hafla hiyo pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt. Joseph Kinyua miongoni mwa viongozi wengineo.

Bunge la Seneti lilipitisha mfumo wa ugavi wa mapato kwa kaunti mwezi Septemba na kukomesha mzozo ambao ulisababisha ukosefu wa pesa kwa serikali za kaunti kwa miezi kadhaa.

Mzozo kuhusu mswada wa ugavi wa mapato kwa kaunti nusura usababishe kulemaa kwa huduma katika serikali za magatuzi kutokana na ukosefu wa fedha.

Categories
Habari

Rais Kenyatta atangaza siku tatu za maombi ya kitaifa

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza wikendi ijayo kuwa ya maombi ya kitaifa kuanzia Ijumaa tarehe 9 hadi Jumapili tarehe 11 Oktoba, 2020.

Wakati huo, Wakenya wamehimizwa kuombea nchi hii katika sehemu zao za kawaida za ibada, kwa kuzingatia kanuni za kuzuia msambao wa COVID-19.

Jumamosi tarehe 10, Rais Kenyatta atakuwa na maombi ya pamoja na waumini wa dini tofauti tofauti kwenye ibada itakayoandaliwa katika Ikulu ya Nairobi kuanzia saa nne asubuhi.

Ibada hiyo itapeperushwa moja kwa moja na vituo vikuu vya runinga na redio humu nchini.

Haya yanajiri siku chache baada ya hotuba ya 12 ya Rais kuhusu hali ya kitaifa ya janga la COVID-19 ambapo sehemu za maabudu zilitakiwa kuruhusu waumini hadi thuluthi moja ya majengo yao.

Hii inamaanisha kuwa kanisa linaloweza kuingia watu elfi 30 linaruhusiwa kukubali watu elfu 10, bora kuwe na uwezekano wa kuzingatia umbali unaokubalika.

Rais Kenyatta amesisitiza Wakenya kuendelea kuzingatia kanuni za COVID-19 ili nchi hii iweze kushinda kikamilifu vita dhidi ya janga hilo.

“Kama tumeshinda sehemu moja ya vita dhidi ya COVID-19, basi hatujashinda vita hivyo,” akasema.