Categories
Michezo

KCB yawafilisi Gor Mahia na kuwapa kipigo cha 4 ligi kuu FKF

Mabingwa watetzi wa ligi kuu ya Kenya Gor Mahia waliendelea kutota baada ya kucharazwa mabao 2 bila jibu na Kenya Commercial Bank katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa Jumapili alasiri katika uwanja wa Kasarani.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizikia sare tasa KCB walirejea kipindi cha pili na mbinu tofauti huku Dennis Simiyu akipigiwa pasi na kupachika bao la kwanza dakika ya 75, huku kipa Bonface Oluoch kimcheza rafu Victor Omondi na kuwazawidi KCB penati iliyofungwa na Omondi akiongeza la pili kunako dakika ya 85 .

Ilikuwa ni mechi ya tano kwa Gor Mahia kupoteza msimu huu na ya pili mtawalia huku wakiteremka hadi nafasi ya 8 ligini kwa pointi 19,alama 16 nyuma ya viongozi Tusker Fc waliosakata mechi nne zaidi.

Katika pambano jingine Kakamega Homeboyz ilipata ushindi wa bao 2-1 ugenini dhidi ya Mathare United inayozidi kurekodi matokeo duni msimu huu.

Categories
Michezo

Mashemeji waogopana ligi kuu FKF

Derby iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na ghamu baina ya  AFC Leopards na Gor Mahia haikuwa na chochote muhimu baada ya timu zote kutoka sare tasa katika pambano la ligi kuu Jumapili alasiri katika uwanja wa Kasarani.

Leopards watajilaumu baada ya kukosa nafasi chungu nzima za kupachika magoli hususan kipindi cha kwanza wakati Kogalo wakicheza kwa tahadhari kuu na kupata pointi hiyo muhimu.

Leopards walikuwa wakisaka ushindi wa kwanza dhidi ya Gor kwenye ligi kuu tangu mwaka 2016 lakini watalazimika kusubiri zaidi.

Pointi hiyo moja inawaweka  Leopards katika nafasi ya 4 kwa alama 19  nao Gor Mahia  wakiwa katika nafasi ya 6 kwa alama 16 kutokana na mechi 9.

Katika mchuano mwingine wa Jumapili Bidco United ilisajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Zoo Fc.

Categories
Michezo

Mashemeji Derby Kasarani bila mashabiki Jumapili

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Kenya Gor Mahia watashuka uwanjani Kasarani Jumapili  Februari 7  kwa mechi ya ligi kuu maarufu kama Mashemeji Derby huku kwa mara ya kwanza mechi ya hiyo ya ubabe na utani mkubwa ikichezwa bila mashabiki uwanjani kutoka na ugonjwa wa Covid 19.

Timu zote zililkuwa zimeiomba wizara ya afya  kuruhusu angaa mashabiki 5,000 ombi lililokataliwa na  kuwalazimu mashabiki kusalia nyumbani wakati wa mchuano huo siku ya  Jumapili .

Katibu mkuu wa Gor Mahia Sam Ochola amesema wamejiandaa vyema huku wakilenga kuzoa alama zote tatu ili kuwakaribia Leopards kwenye jedwali.

“Kikosi chetu kiko  sawa tunatafuta pointi zote tatu ili tuwakaribie Leopards”akasema Ochola

Kwa upande wake mwenyekiti wa Leopards Dan Shikanda ana imani ya kusajili matokeo bora mchuano huo huku akilalama kuhusu kufungiwa nje kwa mashabiki.

“Tulitarajia kuwa by the time tunacheza hii mechi serikali itaruhusu mashabiki lakini kwa sasa tutacheza tu bila mashabiki lakini tunalenga kupata matokeo mazuri”akasema Shikanda

Leopards ni ya 4 ligini kwa pointi 18 wakati Gor Mahia ikishikilia nafasi ya 6 kwa alama 15.

Categories
Michezo

Ulinzi Stars waiangusha Mathare United huku Gor wakiiparuza Zoo Fc ligi kuu FKF

Wanajeshi Ulinzi Stars  na mabingwa watetezi Gor Mahia wamesajili ushindi katika mechi mbili za ligi kuu FKF  zilizosakatwa Jumatano alasiri.

Ulinzi waliipakata Mathare United mabao  2-1 katika uwanja wa Afraha  ,Daniel Waweru akipachika bao la kwanza kwa wenyeji kunako dakika ya 7 akiunganisha mkwaju uliotumwa na Michael Otieno na kumwacha kipa hoi bin taaban.

Kiungo Elvis Nandwa aliongeza bao la pili kwa Ulinzi akiunganisha pasi  murua iliyochongwa na mchezaji Masuta katika dakika ya 70 huku Mathare wakijipatia goli la maliwazo kupitia kwa Daniel Otieno dakika ya 88.

Katika mechi nyingine iliyopigwa katika uchanjaa wa Kasarani, Gor Mahia walirejelea tambo za ushindi na kuititiga Zoo Fc mabao 3 bila jibu ,kiungo Samuel Onyango akipachika la kwanza dakika ya 10, kabla ya nahodha Keneth Muguna kutanua uongozi kwa goli la dakika ya 32 na kisha Onyango akapiga tena bao la tatu kunako dakika ya pili ya muda wa mazidadi.

Kufuatia matokeo ya Jumatano Gor na Ulinzi wamezoa idadi sawa ya alama 12 ingawa vijana wa KDF wamecheza mechi mbili zaidi.

Categories
Michezo

Gor Mahia wazima Stima Kisumu

Mabingwa watetezi Gor Mahia  wameiteketeza Western Stima  mabao 3-1 katika mechi ya ligi kuu FKF  Jumatatu alasiri katika uwanja Moi kaunti ya Kisumu .

Sammy Onyango alifungua ukurasa kwa bao la dakika ya 23  kabla ya Godfrey Villa Orachaman kuwarejesha wenyeji mchezoni kwa bao la dakika ya 38 huku kipindi cha kwanza kikimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Tito Okello kutoka Sudan Kusini aliwahakikisha Kogalo ushindi kwa mabao ya dakika za  65 na 88 ukiwa ushindi wa tatu kwa Gor msimu huu baada ya kusakata mechi 5 ,wakishikilia nafasi ya 8 kwa pointi 9.

Katika mchuano mwingine vijana wa Mathare United wameipakata  Zoo Fc mabao 2-0 .

KCB wangali kuongoza kwa alama 18 kutokana na mechi 7 wakifuatwa na Tusker Fc kwa pointi 17 huku Kariobangi Sharks ikiwa  ya tatu kwa alama 15.

Categories
Michezo

Gor waangukia NAPSA All Stars kuwania tiketi ya makundi ya kombe la shirikisho

Gor Mahia   wameratibiwa kumenyana na timu ya  National Pension Scheme Authority  Stars (NAPSA) ya Zambia  katika mchujo wa kufuzu kw ahatua ya makundi ya kombe la shirikisho la soka Afrika Caf .

Mkondo wa kwanza wa mechi hiyo utapigwa Februari 14 mjini Nairobi , huku ule wa pili ukisakatwa Zambia Februari 21 huku mshindi wa jumla akifuzu kucheza makundi ya kombe la shirikisho.

Gor walilazimishwa kucheza hatua hiyo baada ya kubandiliwa katika ligi ya mabingwa walipocharazwa mabao 8-1 na mabingwa wa Algeria CR Belouizdad huku  Napsa wakifuzu  kwa sheria ya bao la ugenini dhidi ya UD Songo ya Msumbiji licha ya kutoka sare ya 1-1.

Berkane wakitawazwa mabingwa wa kombe la shirikisho mwaka jana

Mchuano huo  una maana kuwa wachezaji wa zamani wa Gor Shaban Odhoji na Timothy Otieno na  Andrew  Tololwa  zamani akiwa  Mathare United ambao wanaichezea Napsa watarejea kucheza dhidi ya Gor.

Katika mataifa ya Afrika mashariki Namungo ya Tanzania imepangwa dhidi ya  Premeiro De Agosto ya Angola wakati AS Kigali ya Rwanda imenyane na CS Faxien ya Tunisia.

Mechi hizo kuchezwa baina ya Februari 14 na 21 mwaka huu huku washindi 16 kwa jumla wakifuzu kupiga hatua ya makundi ya kombe hilo la shirikisho.

 

 

Categories
Michezo

Gor Mahia kuhitimisha ratiba na wageni Belouizdad

Mabingwa wa Kenya Gor Mahia watakuwa na kibarua cha mwaka katika mechi ya marudio ya mchujo wa pili kuwania taji ya ligi ya mabingwa ,Jumatano alasiri katika uwanja wa taifa wa Nyayo  wakihitaji si ushindi tu, bali ushindi  wa mabao 7-0 ili kufuzu kwa hatua ya makundi .

Gor maarufu kama Kogalo walipoteza mkumbo wa kwanza mabao 6-0 mjini Algiers  wiki mbili zilizopita matokeo yaliyochangiwa na maandalizi duni yaliyoambatana na migomo ya wachezaji  wakiteta kutolipwa mishahara yao.

CR Belouizdad

Belouizdad ambao ni mabingwa wa Algeria wamekuwa na wakati wa kutosha wa kujiandaa tangu wawasili nchini Jumapili iliyopita huku wakihitaji tu kuzuia kufungwa mabao zaidi ya 6 na Gor ili kufuzu kwa hatua ya makundi pia kwa mara ya kwanza .

Bernard Hensel Camille atakuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na   Hensley Danny Petrousse na  Steve Marie huku   Eldrick Matthieu Adelaide akiwa afisa wa nne ilihlai  Mzee Zam Ali kutoka  Zanzibar atakuwa kamisaa wa mechi .

 

 

 

 

Categories
Michezo

Nyumbani ni nyumbani !! Owino Calabar aanza mazoezi na Gor Mahia miaka 6 baadae

Beki wa zamani wa kilabu cha Gor Mahia  David Owino Kalabar ameanza mazoezi na mabingwa hao watatezi wa ligi kuu ya Kenya  mapema Jumatatu baada ya kukamilisha kandarasi yake na Zesco united ya Zambia Disemba 31 mwaka uliopita.

Owino aliye na umri wa miaka 32 aliichezea Gor baina ya mwaka 2012 na 2014 kabla ya kujiunga na Zesco United inayoshiriki ligi kuu nchini Zambia ambako amecheza kwa takriban miaka 6 akiwa mwanandinga wa kwanza kupiga soka ya kulipwa katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Haijabainika endapo Kogalo watamrejesha kikosini difenda huyo ambaye kando na kuichezea  Mathare United kabla ya kuhamia Zesco , amekuwa tegemeo katika timu ya taifa Harambee Stars.

Categories
Michezo

David Owino Calabar aibwaga manyanga ya Zesco United

Klabu ya Zesco United imemruhusu Difenda wa Kenya  David Owino Odhiambo almaaarufu Calabar,kuondoka baada ya kutamatisha kandarasi yake  ya sasa inayokamilika disemba 31 mwaka 2020.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Zesco ,klabu hiyo imempongeza beki huyo kwa huduma zake katika kipindi cha miaka 6 akiwa  nao ambapo ameshinda mataji matano ya ligi kuu Zambia mataji matatu ya kombe la Absa na mataji mawili ya ngao ya jamii .

Calabar aliye na umri wa miaka 33  alijiunga na Zesco akitokea Gor Mahia  huku afisa mkuu mtendaji wa Zesco  Richard Mulenga akimpongeza kwa kujitolea na kujituma.

“kwa niaba ya klabu ya soka ya Zesco ,ningependa kuchukua fursa hii kumshukuru Odhiambo kwa kujitolea kwake .                              Kamwe hatutamsahau na mchango wake kwa ufanisi wa timu”akasema Mulenga

Odhimbo alikuwa  mchezaji wa kwanza wa soka kutoka Kenya  kucheza soka ya kulipwa nchini Zambia na pia alikuwa katika kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki michuano ya Afcon mwaka jana nchini Misri.

Wanandinga wengine wa Kenya wanaosakata soka ya kulipwa nchini Zambia ni Jesse Were, John Mark Makwata na Ian Otieno walio Zesco united ,Haron Shakava aliye Nkana Fc  ,na Musa Mohammed aliye Lusaka Dynamos Fc.

 

Categories
Michezo

Gor kukabana koo na wenyeji Belouizdad Jumamosi usiku

Mabingwa wa Kenya Gor Mahia watashuka uwanjani Jumamosi usiku kupambana na mabingwa wa Algeria CR Belouizdad katika mkondo wa kwanza wa  mchujo wa pili kuwania kombe la ligi ya mabingwa Afrika katika uwanja wa Stade 5 Julliet mjini Algiers .

Gor waliosafiri na wanandinga 18 huku wakimtema mshambulizi matata Nicholas Kipkurui wakati nahodha Keneth Muguna akisalia nchini kutokana na jeraha, itahitaji angaa sare au bao la ugenini ili kuwa na fursa ya kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia yao .

CR Belouizdad kwa kirefu Chabab Riadhi de Belouizdad ni mojawapo wa timu zilizo na ufanisi mkubwa ikibuniwa mwaka 1962 na tayari imetwaa ubingwa wa ligi kuu mara 7 nchini Algeria na vikombe 8 vya shirikisho la soka nchini humo.

Ni mara ya kwanza kwa kilabu hicho kucheza ligi ya mabingwa tangu mwaka 2002 walipobanduliwa katika raundi ya kwanza na mapema mwaka huu walibanduliwa na Pyramids ya Misri katika kombe la shirikisho la soka katika raundi ya pili .

Pambano la marudio kupigwa hapa nchini Kenya  huku mshindi wa jumla akifuzu hatua ya makundi.

Sadfa ni timu zote mbili hazijafuzu hatua ya makundi ya kombe la ligi ya mabingwa Afrika huku kila mmoja akilenga kuandikisha historia .

kikosi kamili cha Gor kilichosafiri ni kama kifuatacho:-

1.Gad Mathew
2.Philemon Otieno
3.Michael Apudo
4.Charles Momanyi
5.Juma Andrew
6.Ernest Wendo
7.Sydney Ochieng
8.Samuel Onyango
9.Tito Okello
10.Jules Ulimwengu
11.Geoffery Ochieng
12.Bonface Oluoch
13.Kevin Wesonga
14.Joachim Oluoch
15.Nicholas Omondi
16.Benson Omalla
17.Frank Odhiambo
18.Clifton Miheso

Maafisa wa kiufundi

1. Samuel Omollo
2. Patrick Odhiambo
3. Jolawi Obondo
4. Willis Ochieng
5. Victor Nyaoro
6. Frederick Otieno

maafisa wa timu
1. Dolfina Odhiambo

Kiongozi wa ujumbe
1. Gerphas Okuku

Mechi hiyo iliahirishwa kutoka Jumatano usiku baada ya Gor kukumbwa  na utata wa usafiri na kuwaandikia CAF kutaka mechi iahirishwe ombi lililoitikiwa na CAF.

Mchuano  huo utang’oa nanga saa 10: 45  usiku wa Jumamosi.