Categories
Burudani

Niliitwa tena na BASATA, Gigy Money

Msanii wa kike wa Tanzania Gigy Money ambaye kwa sasa amefungiwa asijihusishe na kazi yoyote ya sanaa na Baraza la Sanaa la Tanzania ameelezea kwamba mara tu aliporejea Tanzania baada ya kipindi cha Wife Material kukatizwa ghafla aliitwa kwenye afisi za BASATA.

Pale ndipo aligundua kwamba kufungiwa kwake ni ndani na nje ya Tanzania.

Anasema aliamua kusafiri nje kutafuta kazi ili ajipatie riziki nchini Kenya kupitia kipindi hicho cha Eric Omondi ambacho kilisimamishwa.

Yeye na Eric walikubaliana kwamba wafanye kipindi kikipata wafadhili amlipe lakini hilo halikutimia kwani kipindi kilisimamishwa hata kabla ya kuanza.

Wakati alifungiwa mwanzo wa mwaka huu na kituo cha runinga cha Wasafi nacho kikafungiwa, anasema alikutana na Diamond Platnumz akamwondolea lawama kwamba sio yeye alisababisha runinga yake ifungiwe.

Gigy alibubujikwa na machozi akihojiwa kwa mara ya kwanza tangu kufungiwa akielezea jinsi hawezi kulipa kodi ya nyumba anayoishi na mtoto wake hajaenda shuleni kwani hana hela za kumlipia karo.

Kazi ambazo amekuwa akitegemea za kutangaza biashara za watu imepungua kwani hakuna anayetaka kujihusisha na msanii ambaye amefungiwa.

Alisimulia alivyoumia akiona wasanii wakiomboleza kifo cha Rais Magufuli kwa kutunga na kuimba nyimbo na yeye asiweze.

Alisisitiza kwamba hajawahi kuwa uchi hadharani ingawaje hilo ndilo kosa limesababisha afungiwe kwa miezi sita, adhabu inayostahili kukamilika mwisho wa mwezi wa sita mwaka huu.

Gigy yuko tayari kufanya lolote ili afunguliwe aendeleze sanaa yake ajipatie mapato.

Categories
Burudani

Gigy Money amefilisika?

Mwanamuziki wa Tanzania Gigy Money anaonekana kupitia wakati mgumu kifedha kutokana na maneno ambayo amekuwa akiandika kwenye akaunti yake ya Instagram.

Mwanadada huyo alipachika picha yake kwenye Instagram na kuandika “Sijui niuze mawigi yangu au niuze gari langu? Au niwauze marafiki zangu?

Ikumbukwe kwamba mwanamuziki huyo anaendelea kutumikia adhabu kutoka kwa Baraza la Sanaa la Tanzania-BASATA baada ya kukiuka maadili ya utumbuizaji mwisho wa mwaka jana kwenye tamasha la Wasafi.

BASATA ilimfungia msanii huyo asitekeleze kazi yoyote ya sanaa kwa muda wa miezi sita baada yake kuonekana jukwaani na kwenye runinga akiwa na vazi ambalo lilionyesha mwili wake visivyo.

Anahitajika pia kulipa faini ya shilingi milioni moja pesa za Tanzania.

Alifungiwa wakati mmoja na kituo cha runinga cha Wasafi ambacho kilifungiwa pia na mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA kwa miezi sita kutokana na kupeperusha moja kwa moja tumbuizo la Gigy.

Runinga hiyo hata hivyo imeshafunguliwa baada ya kuomba msamaha na kutimiza masharti.

Gigy amekuwa akizungumza kuhusu kupungukiwa kwake kifedha hadharani kwani hawezi kutumbuiza popote ili apate kulipwa mpaka muda wa marufuku uishe.

Wakati alihudhuria sherehe ya kutuza Amber Lulu aliyekuwa akitarajia mtoto mwezi jana, Gigy aliwaingilia wasanii wengine waliokuwepo ambao hawakuwa wamemtunuku Amber akisema wao hawajafungiwa kazi naye amefungiwa na bado anaweza kutuza mama kijacho.

Akiomboleza kifo cha Rais Magufuli Gigy alipachika picha ya hayati na kuandika; ” Mwanao Naumia, siwezi kukuimbia Nyimbo ya kuomboleza Na kukuenzi, siwezi kushiriki kwenye jambo lolote kama msanii, sipo ata Chato mwanao Naumia sana kwamba ata vocha ya king’amuzi sina ila ulituachia TBC Taifa ndio naangalia msiba huu mzito wa Taifa letu . Baba pia watoto wako tunakukumbuka sana PUMZIKA KWA AMANI (ahsante wasanii wenzangu mliotamani nishiriki lakini sababu zilizo nje ya uwezo wangu sijaweza) Rest In Peace Baba”

Categories
Burudani

Sio kipindi cha familia!

Mchekeshaji na muigizaji Eric Omondi ana matumaini kwamba kufikia sasa watu wote wameelewa kwamba kipindi chake cha “Wife Material” sio kipindi cha familia nzima.

Kulingana naye, kipindi hicho sasa kimeorodheshwa “PG” yaani “Parental Guidance” kumaanisha kwamba wazazi watatakiwa kuelekeza watoto wao wanapokitazama.

Eric ametoa onyo kali kwa wote kuzingatia tangazo hilo wakati wanajitayarisha kurejesha kipindi hicho ambacho ni cha mtandao wa You Tube.

Awali kipindi hicho kilisimamishwa baada ya Omondi kukamatwa na makachero wa DCI kwa ushirikiano na wale wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini KFCB.

Bodi hiyo hata hivyo iliamua kutatua kesi dhidi ya Omondi nje ya mahakama lakini alilazimika kulala korokoroni usiku mmoja.

Mkurugenzi mkuu wa KFCB Daktari Ezekiel Mutua alibuni kamati ya kusikiliza na kuamua kesi hiyo ya Eric ambayo ilihusu ukiukaji wa taratibu za kutayarisha na kusambaza kazi ya sanaa.

Mchekeshaji huyo alikuwa anaandaa na kusambaza kazi ya sanaa bila leseni na kwamba kazi yenyewe haikuwa imepitishwa na KFCB.

Wahusika kwenye kipindi hicho kutoka nchi za Uganda na Tanzania walirejea kwao na wakati mmoja eric alitangaza kwamba mmoja wa wasichana hao raia wa Uganda alikuwa amekataa kurudi nyumbani.

Baadaye tena alisema kwamba kifo cha Rais wa Tanzania ni mojawapo ya sababu za kucheleweshwa kwa kipindi hicho kwani ana wahusika kutoka taifa hilo kama vile Gigy Money.

Categories
Burudani

Ringtone amwonya Eric Omondi

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili ambaye husema yeye ndiye mwenyekiti wa wanamuziki wa nyimbo za injili ametoa onyo hilo kufuatia kuanzishwa kwa awamu ya pili ya kipindi cha Eric Omondi kiitwachwo “Wife Material”.

Ringtone alipachika video kwenye akaunti yake ya Instagram asubuhi ya leo ambapo anazungumzia kipindi hicho ambacho kulingana naye kinawakosea heshima wanawake. Anashindwa ikiwa Eric ana mama, dada au hata shangazi maishani mwake ilhali anaacha mabinti za watu wakimng’ang’ania kisa na maana anatafuta mke.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili ambaye pia wakati fulani alizunguka na bango akisema anatafuta mke, anasema kwamba atamwonya Eric mara ya tatu na ikiwa hatakatiza kipindi chake, atamwombea na kitu kibaya kitamfanyikia.

Awamu ya kwanza ya kipindi hicho ilihusu kina dada wa nchi ya Kenya na ya pili inahusisha wanawake tisa, watatu kutoka kila nchi ya Afrika Mashariki ambazo ni Kenya Uganda na Tanzania.

Jana, mchekeshaji huyo ambaye pia hujiita rais wa wachekeshaji wote Afrika, aliamua kupeleka kina dada hao kwenye sehemu moja ya burudani jijini Nairobi kwa ajili ya kuwakutanisha na mashabiki na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Wakiwa kwenye sehemu hiyo ya burudani, wanadada wawili akiwemo Gigy Money wa Tanzania walianza kupigana huku wakivunja glasi na chupa za pombe ikabidi waondolewe kwenye sehemu hiyo na maafisa wa polisi.

Watatu kati ya wanaowania kuwa mke wa Eric ambao ni Gigy Money, Sumaiyah A.K na Kyler wote kutoka Tanzania wamelala katika kituo cha polisi.

Eric amekwenda kuwachukua asubuhi ambapo aliahidi kuwapeleka Saluni na baadaye awapeleke sehemu kupata chamcha.

Categories
Burudani

Eric Omondi apanua wigo anapotafuta mke!

Mara ya kwanza alihusisha tu wanawake kutoka taifa la Kenya akitafuta wa kuoa kulingana na kipindi chake cha mitandaoni kwa jina “Wife Material”. kipindi hicho kilifika mwisho ambapo alimalizia kufunga ndoa na mwanadada mmoja kutoka Band Beca ingawaje wengi walihisi kwamba Shakila ndiye angeshinda.

Zamu hii mchekeshaji huyo ambaye hujiita Rais wa wachekeshaji barani Afrika amepanua wigo na kuhusisha mataifa ya Afrika mashariki ambayo ni Tanzania na Uganda katika kipindi hicho cha kutafuta mke na anakiita “Wife Material 2”.

Mabinti ambao wanashiriki shindano hilo kutoka mataifa Ya Uganda na Tanzania waliwasili nchini jana Jumapili tarehe 7 mwezi Machi mwaka 2021 na walipokelewa na washindani wao wa nchi ya Kenya ambao ni Manzi wa Kibera, Sherlyne Anyango na Dj Coco.

Kundi la watatu kutoka Tanzania linahusisha Gigy Money ambaye ni mwanamuziki na muigizaji ambaye kwa sasa amegubikwa na utata nchini Tanzania. Amefungiwa na Baraza la Sanaa la Tazania BASATA asijihusishe na sanaa yoyote hata kutumbuiza hadharani kwa muda wa miezi sita hadi mwezi Juni mwaka huu na anahitajika pia kulipa faini.

Gigy aliwasili Nairobi akiwa amevalia sidiria tu na kujifunika Bendera ya Tanzania.

Haya yanatokana na tuhuma za kutumbuiza jukwaani akiwa na vazi ambalo lilionyesha umbo lake kabisa kana kwamba alikuwa uchi wakati wa Wasafi Festival mwisho wa mwaka jana mjini Dodoma nchini Tanzania.

Kitendo chake kilisababishia kituo cha runinga cha Wasafi Tv adhabu sawia kutoka kwa mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA, kwa kuwa kilikuwa kinapeperusha tamasha hilo moja kwa moja.

Hata hivyo adhabu dhidi ya kituo hicho ilipunguzwa na kikarejelea upeperushaji wa vipindi mwanzo wa mwezi huu wa Machi.

Categories
Burudani

Wasafi Tv yarejea hewani

Kituo cha runinga cha Wasafi cha Tanzania kilianza kurusha matangazo na vipindi saa sita usiku wa kuamkia leo baada ya marufuku ya miezi miwili.

Kituo hicho kilisimamishwa mwezi Januari mwaka huu wa 2021 kwa kile ambacho mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA ilitaja kuwa kukiuka maadili ya utangazaji baada ya kuonyesha mwanamuziki na muigizaji Gigy Money akitumbuiza jukwaani huku akiwa amevalia mavazi yasiyostahili.

Lakini wiki tatu zilizopita, TCRA ilitangaza kwamba imepunguza adhabu dhidi ya Wasafi Tv kutoka miezi sita hadi miezi miwili baada ya kusikiliza rufaa kutoka kwa usimamizi wa Wasafi Media.

Mkurugenzi mkuu wa TCRA James Kilaba hata hivyo alionya kwamba ikiwa kituo hicho cha runinga hakitafuata kanuni zilizowekwa kitachukuliwa hatua kwa mara nyingine.

Usiku mzima kituo hicho cha runinga kilipeperusha video za nyimbo mbali mbali hasa za wasanii wa Bara Afrika.

Mtangazaji wa Wasafi Fm Baba Levo alishukuru serikali ya Tanzania kwa kupunguza adhabu dhidi ya Wasafi Tv huku akiahidi mashabiki kwamba vipindi vyote ambavyo wanavipenda vitarejelewa.

Msanii Gigy Money naye alifungiwa na Baraza la Sanaa la Tanzania asijihusishe na kazi zozote za kuigiza au kutumbuiza kwa muda wa miezi sita na marufuku hiyo bado inaendelea.

Wakati huo kwenye tamasha kwa jina “Wasafi Festival” huko Dodoma, Gigy Money aliingia jukwaani akiwa amevalia dera na baadaye akalivua na kubakia na vazi la kunata mwili ambalo rangi yake inafanana na rangi ya ngozi yake ungedhania yuko uchi.

Anahitajika kulipa faini ya shilingi milioni moja pesa za Tanzania.

Categories
Burudani

Eric Omondi apimana nguvu na Diamond Platnumz

Mchekeshaji huyo wa nchi ya Kenya anamtania mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz kwa kile ambacho anakitaja kuwa kushambulia Afrika mashariki kwa kupata wapenzi na watoto.

Eric anasema alimwonya Diamond kwamba atalipiza kisasi lakini hakuamini na kwamba anajua sasa ameshachoka kukimbizana na wapenzi analea watoto.

Diamond Platnumz ana watoto na wapenzi wake wa zamani kwenye nchi zote za Afrika mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania.

Nchini Kenya ana mtoto na msanii Tanasha Donna ambaye anaitwa Naseeb Junior kama yeye na siku yao ya kuzaliwa ni moja, ukienda Uganda ana Zari Hassan ambaye ana watoto wake wawili, Princess Tiffah na Prince Nillan na kwao Tanzania anayejulikana ni Hamissa Mobeto ambaye ana mtoto kwa jina Dillan.

Eric alitoa video inayomwonyesha akiwa na mwanamuziki na muigizaji wa Tanzania Gigy Money ambaye ni rafiki wa karibu wa Diamond Platnumz anapoanza kulipiza hatua ya Diamond ya kunyakua warembo Afrika Mashariki.

Wimbo ambao ametumia kwenye video hiyo ni “Kwaheri” ambao umeimbwa na Jua Cali na Sanaipei Tande ishara kwamba Gigy amehama Tanzania na kumwacha Diamond na kuja Kenya kwa Eric Omondi japo yote hayo ni uigizaji tu.

Kulingana na maneno, picha na video kutoka kwa Eric Omondi kwenye mitandao ya kijamii, Gigy Money na Betty Kyallo huenda wakawa wahusika kwenye awamu ya pili ya kipindi chake “Wife Material”.

Categories
Burudani

Wasafi Tv kurejea mwisho wa mwezi!

Adhabu iliyotolewa kwa kituo cha runinga cha Wasafi nchini Tanzania imerekebishwa. Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA ilitangaza hayo leo kupitia kwa mkurugenzi mkuu Bwana James Kilaba.

TCRA inasema ilipokea rufaa kutoka kwa usimamizi wa Wasafi Tv inayomilikiwa na msanii Diamond Platnumz kuhusu adhabu hiyo na baada ya kutathmini wameamua kwamba marufuku hiyo ambayo ingekamilika mwezi Juni mwaka huu wa 2021 ikamilike tarehe 28 mwezi Februari mwaka huu wa 2021.

Tangazo la kufungwa kwa kituo hicho lilitolewa na TCRA tarehe tano mwezi Januari mwaka huu na tarehe 21 mwezi huo, usimamizi wa Wasafi Tv ukaandikia TCRA kuomba adhabu yao irekebishwe. Tarehe 28 mwezi Januari, wasimamizi hao wa runinga ya Wasafi walirejea tena TCRA ambapo walipata kusikilizwa.

Bwana Kilaba anasema kwamba Wasafi Tv ilikiri kukiuka kanuni fulani za maadili.

Sababu kuu ya Wasafi Tv kupoteza leseni ya kupeperusha matangazo ni hatua yao ya kupeperusha moja kwa moja tumbuizo la mwanamuziki Gigy Money ambaye anasemekana kuvaa mavazi ambayo yalionyesha umbo lake visivyo.

Msanii huyo Gigy money pia aliadhibiwa na BASATA au ukipenda “Baraza la Sanaa la Taifa” ambapo alifungiwa asiwahi kufanya kazi yoyote ya sanaa kwa muda wa miezi sita.

Gigy siku hiyo kwenye tamasha la Wasafi Media, aliingia jukwaani akiwa amevaa dera kisha baadaye akalivua na kubakia na vazi la kushikilia mwili ambalo rangi yake ilikaribia kufanana na rangi ya ngozi yake ungedhania yuko uchi.

Usimamizi wa Wasafi haujasema lolote kuhusu kupunguziwa adhabu.

Categories
Burudani

Gigy Money amlaumu Beyonce

Baada ya mwanamuziki wa Tanzania kwa jina Gigy Money kupata adhabu kali kutoka kwa Baraza la Sanaa nchini Tanzania – BASATA mwanadada huyo sasa anajuta akimlaumu mwanamuziki wa Marekani Beyonce.

Kwenye akaunti yake ya Instagram akiweka video fupi ya Beyonce na mume wake Jay Z wakitumbuiza jukwaani huku Beyonce akiwa amevalia vazi sawa na lililomtia mashakani.

Ishara kwamba huwa anajifunza kwa Beyonce. Kwenye video hiyo Gigy ameandika, “Role Model umeniponza @Beyonce”. Gigy amefuta kila kitu kwenye hiyo akaunti yake ya Instagram isipokuwa video hiyo ya Beyonce na Jay Z.

Gigy amesimamishwa asijihusishe na tamasha zozote kwa muda wa miezi zita na amepigwa faini ya shilingi milioni moja za Tanzania ambazo ni sawa na elfu 47, 184 za Kenya.

Kilichomletea matatizo Gigy Money ni vazi lake akitumbuiza kwenye tamasha la mwaka mpya la Wasafi Media ambalo lilikuwa linapeperushwa moja kwa moja kenye runinga ya Wasafi.

Gigy aliingia jukwaani akiwa amevalia dera na baadaye akalivua na kubakia na vazi ambalo linanata mwili wote na kuonyesha maungo yake.

Kitendo hiki kilisababishia kituo cha Runinga cha Wasafi matatizo kwani pia kimesimamishwa kisirushe matangazo kwa miezi sita na mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania.

Wasafi Media kampuni kuu ya kituo cha redio cha Wasafi fm, kituo cha runinga cha Wasafi Tv na kampuni ya muziki ya Wasafi Classic Baby – WCB inamilikiwa na Diamond Platnumz.

Categories
Burudani

Wasafi Tv yafungwa kwa miezi sita

Kituo cha runinga kwa jina Wasafi Tv cha Tanzania kinachomilikiwa na mwanamuziki Diamond Platnumz kimefungiwa kisipeperushe vipindi na matangazo kwa muda wa miezi sita na mamlaka ya mawasiliano nchini humo TCRA.

Inasemekana kwamba kituo hicho kilikiuka kanuni na maadili wakati kilipeperusha tamasha moja mubashara ambapo msanii kwa jina Gigy Money alionyeshwa akiwa uchi jukwaani wakati wa tamasha la Wasafi Media huko Dodoma.

Msanii Gigy Money naye amezuiwa kujihusisha na shughuli zote za sanaa kwa muda wa miezi sita.

Kaimu mkurugenzi wa TCRA Bwana Johannes Kalungule ndiye alitangaza hayo na kuutaka usimamizi wa kituo hicho cha runinga kuomba umma msamaha.

Kulingana na Kalungule uamuzi huo wa kukifunga kituo hicho cha runinga uliafikiwa baada ya mkutano kati ya pande hizo mbili.

Kufikia sasa usimamizi wa kituo hicho haujasema lolote hata kuomba msamaha kulingana na maagizo.

Hii sio mara ya kwanza kampuni ya Wasafi inajipata pabaya, mwaka jana kituo chake cha redio kwa jina Wasafi fm kilifungiwa kwa muda wa siku saba kwa sababu sawia ya kukiuka maadili.

Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa tarehe 12 mwezi septemba mwaka jana na usimamizi wa kituo hicho uliamua kupeleka watangazaji wake katika eneo la wasafi village ambapo walikumbushwa maadili ya kazi na kupata muda pia wa kujiliwaza.

Watangazaji wa vipindi vya “The Switch” na “Mashamsham” wanasemekana kutumia maneno ambayo yalikuwa kinyume na maadili kati ya tarehe mosi na tarehe nne mwesi Agosti mwaka 2020.