Categories
Kimataifa

Polisi nchini Nigeria waamriwa kukomesha ghasia nchini humo

Mkuu wa Polisi nchini Nigeria ameamuru kutumiwa rasilimali zote za idara ya polisi kukomesha ghasia na wizi wa ngawira nchini humo.

Mohamed Adamu amesema wahalifu wanatumia nafasi ya maandamano ya kupinga ukatili wa polisi kusababisha ghasia, jambo ambalo halikubaliki.

Maafisa wa polisi wameamriwa kukomesha ghasia, mauaji, uporaji na uharibifu wa mali ya umma.

Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi yalianza tarehe 7 mwezi Oktoba.

Maandamno hayo ambayo yalijumuisha hasa sana vijana, yalitaka kikosi maalum cha polisi cha kukomesha wizi wa kimabavu SARS  kibanduliwe.

Rais Muhamaddu Buhari aliamuru kubanduliwa kwa kikosi hicho, ambacho kimelaumiwa kwa kusababisha mauaji ya kiholela, mateso na unyang’anyi wa mali.

Hata hivo baada ya siku kadhaa maandamano ya kutaka marekebisho makubwa yafanywe  yangali yanaendelea nchini humo.

Categories
Habari

Hatutaruhusu ghasia kwenye mikutano ya hadhara – Mutyambai

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai amekariri kuwa Tume ya Huduma za Polisi itaidhinisha kufanyika kwa mikutano baada tu ya kuthibitisha wazi kuwa hakutatokea fujo.

Akijibu maswala ya Wakenya kwenye mtandao wake wa kijamii katika ushirikishi wake na wananchi kila wiki, Mutyambai amesema amepokea malalamishi kuhusu ubaguzi wa utekelezaji wa sheria kuhusu mikutano ya hadhara.

“Tukiona uwezekano wa hatari, basi idhini haitatolewa ili kulinda watu na mali katika eneo la maandalizi ya mkutano. Kuna makundi ambayo hayajashuhudiwa yakizua ghasia zozote na kuna mengine yamemezua ghasia, kwa hivyo ruhusa itatofautiana,” amesema.

Mutyambai pia amewakumbusha Wakenya kuhusu msako wa madereva walevi kote nchini ili kukabiliana na ongezeko la ajali za barabarani zinazotokana na ulevi wa waendeshaji magari.

Amesema viwango vya kileo katika damu ya madereva kitaasisiwa na madaktari hospitalini kwa kuzingatia kikamilifu sheria za COVID-19.

Kuhusu maswala ya ufisadi katika shughuli za mahojiano na kupandishwa vyeo katika Idara ya Polisi maeneo tofauti tofauti nchini, Mutyambai amewataka wale ambao wana ushahidi wa kulaghaiwa kupiga ripoti kwa uchunguzi.

Amesema kuzingatia sheria za COVID-19 ni jukumu la kibinafsi na akawaonya Wakenya dhidi ya kutoa hongo kwa maafisa wa polisi.

“Chini ya kanuni za COVID-19, magari ya uchukuzi wa umma yanapaswa kusafirisha abiria asilimia 60 ya nafasi zao. Polisi hawawezi kuchunguza magari yote, kuwajibika kibinafsi ni muhimu. Maafisa wanapaswa kuhakikisha sheria hizo zinazingatiwa,” akasema.

Mutyambai ameongeza kuwa wafasiri wa lugha tayari wamepokea mafunzo ili kuwasaidia wale wasio na uwezo wa kusikia, akisema kuwa tayari maafisa wengine wameanza kufanya kazi katika Kituo cha Polisi cha Central, Nairobi.

Categories
Habari

Ruto ataka waanzilishi wa ghasia za Murang’a wachukuliwe hatua

Naibu Rais William Ruto ameitaka Idara ya Polisi iwachukulie hatua wale waliohusika katika kupanga ghasia zilizoshuhudiwa huko Murang’a Jumapilizilizopelekea watu wawili kuaga dunia.

Ruto amesema wahusika hao wanajulikana vizuri na wanapaswa kuadhibiwa bila kuzingatia misimamo yao ya kisiasa.

“Vyombo vya usalama vinawajua wale walioanzisha hizo ghasia. Lazima wachukuliwe hatua bila kujali msimamo wao wa kisiasa,” amesema.

Amesema ghasia hizo za Murang’a zilikuwa ni mwendelezo wa yale yaliyotukia Kaunti ya Kisii mwezi uliopita ambapo kundi la vijana lilipelekwa eneo hilo kuzusha vurugu wakati wa ziara yake ya kimaendeleo.

“Hii ilitukia Kajiado pia siku chache zilizopita ambako utawala wa eneo hilo ulitumika kutishia wananchi ili wasihudhurie hafla yangu,” akasema.

Ruto amesema haya nyumbani kwake Karen kwenye mkutano na zaidi ya viongozi 2,000 wa nyanjani kutoka Kaunti ya Narok.

Amesema licha ya vitisho hivyo, hatasita kutekeleza wito wa kuwainua wananchi kupitia miradi mbali mbali na akaahidi kuongeza juhudi zaidi.

“Najua ni vigumu lakini lazima tuwe na mjadala huu. Tutazidisha juhudi hizi ili kuwezesha kila mmoja,” akahoji.

Ruto amesikitishwa na madai kuwa polisi wanazidi kutumika kutekeleza maswala ya kisiasa na akamsihi Inspekta Jenerali wa Polisi asalie upande wa haki na kuwahudumia Wakenya wote sawa sawa bila ubaguzi.

Categories
Habari

Idara ya Upelelezi kuwahoji Wabunge Ndindi Nyoro na Alice Wahome kuhusu ghasia za Kenol

Idara ya Upelelezi wa Maswala ya Jinai imemuita Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Kandara Alice Wahome ili kuwahoji kuhusu ghasia za Jumapili huko Murang’a zilizosababisha vifo vya watu wawili.

Wabunge hao wametakiwa kufika katika afisi za idara hiyo zilizoko Nyeri ili kutoa taarifa zitakazowasaidia maafisa wa upelelezi wanaochunguza kisa hicho kilichotokea muda mchache kabla ya ziara ya Naibu Rais William Ruto katika eneo la Kenol.

Kufuatia ghasia hizo, watu wawili waliaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati makundi mawili ya vijana yalipozozana.

Jumapili, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai aliamuru kukamatwa mara moja kwa wawili hao kwa madai ya kuhamasisha watu wanaoaminika kutekeleza uhalifu huo.

Wakati uo huo, Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani NTSA imewaita wasimamizi wa kampuni mbili za usafiri Neo Kenya Mpya Commuters na Joy Kenya Services ili kutoa habari zaidi kuhusu tukio hilo.

Inaaminika kuwa magari ya kampuni hizo yalikodishwa na kubeba watu hadi eneo la Kenol kulikotokea ghasia hizo.

“Baada ya mashauriano na Inspekta Jenerali, mamlaka hii imewataka wasimamizi wa kampuni hizo kufika mbele yake kueleza kuhusu tukio hilo lililoshuhudiwa katika eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a Jumapili tarehe 4 Oktoba, 2020,” imesema mamlaka hiyo.

 

Categories
Habari

Mutyambai aamuru uchunguzi kuhusu ghasia za Murang’a

Idara ya Polisi imeanzisha uchunguzi kuhusu ghasia zilizotokea katika eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a zilizosababisha vifo vya watu wawili.

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa katika ghasia hizo zilizotokea alfajiri ya Jumapili kufuatia ugomvi kati ya makundi mawili ya vijana, masaa machache kabla Naibu Rais William Ruto kuzuru eneo hilo.

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ameamuru maafisa wa upelelezi kufanya uchunguzi kuhusiana na kisa hicho na kuwakamata wahusika wa ghasia hizo.

Mutyambai aidha ametoa onyo kali kwa wanasiasa dhidi ya kuwachochea Wakenya akihoji kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

“Tunawasihi wanasiasa waache kujihusisha na maneno na vitendo vya uchochezi. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayehusika katika upangaji na utekelezaji wa vitendo vilivyo kinyume na sheria,” akasema.

Maafisa wa Polisi waliowasili katika eneo hilo nje ya Kanisa la AIPCA Kenol waliloazimika kutumia vitoa machozi ili kuutawanya umati.

Baadaye Ruto aliwasili katika kanisa hilo wakati ghasia zilipotulia na kuhudhuria ibada huku maafisa wa usalama wakishika doria katika sehemu mbali mbali karibu na kanisa hilo.

Ghasia hizo zilianza baada ya kundi la vijana kuziba barabara katika eneo hilo na kuanza kufukuzana na kundi pinzani.

Magari kadhaa yaliharibiwa huku barabara kuu ya kuelekea Nyeri ikikumbwa na msongamano mkubwa kwa masaa kadhaa.

Mutyambai ameongeza kuwa vitendo kama hivyo havitavumiliwa na akaahidi kutumia sheria kulinda maisha ya wananchi na rasilimali.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi imejitolea kufanya kazi kulingana na sheria ili kutekeleza majukumu yake yanayojumlisha kulinda maisha na rasilimali.”

Ruto ameshtumu ghasia hizo huku akilaumu wapinzani wake kwa kusababisha hali hiyo.

Amesema kuwa atabaki katika chama cha Jubilee na kwamba hatatishika na wale wanaotaka kuondolewa kwake kama naibu kinara wa chama hicho.

Categories
Habari

Ghasia zashuhudiwa katika mkutano wa Ruto huko Murang’a

Ghasia zimezuka mapema Jumapili katika eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a, masaa machache kabla Naibu Rais William Ruto kuzuru eneo hilo.

Kufuatia ghasia hizo, mtu mmoja ameripotiwa kuaga dunia na wengine kujeruhiwa baada ya maafisa wa polisi kurusha vitoa machozi nje ya Kanisa la AIPCA Kenol ili kutuliza umati katika hafla ambayo Ruto alitarajiwa kuhudhuria kwa ajili ya mchango.

Ghasia hizo zimeanza baada ya kundi la vijana kuziba barabara katika eneo hilo na kuanza kufukuzana na kundi pinzani.

Hata hivyo, maafisa wa polisi wameapa kufanya uchunguzi wa kujua chanzo halisi cha ghasia hizo.

Magari kadhaa yameharibiwa huku barabara kuu ya kuelekea Nyeri ikikumbwa na msongamano mkubwa kwa masaa kadhaa.

Baadaye Ruto akawasili katika kanisa hilo wakati ghasia hizo zilipotulia na kuhudhuria ibada huku maafisa wa usalama wakishika doria katika sehemu mbali mbali karibu na kanisa hilo.

Ruto ameshtumu ghasia hizo huku akilaumu wapinzani wake kwa kusababisha hali hiyo.

“Nashtumu vikali hali hii. Hatupaswi kutumia vijana wetu kwa ajili ya vitendo hivyo vya kujinufaisha kibinafsi. Wanasiasa waache kuwaingiza vijana wetu katika hali hizi. Murang’a itajiamulia yenyewe,” amesema Ruto kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter.