Categories
Habari

Kuria amtaka Rais aunde kamati ya Bunge ili kuokoa mapendekezo muhimu ya BBI

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, sasa anamtaka Rais Uhuru Kenyatta kubuni kamati maalum ya Bunge ili kujadili namna ya kupitisha mapendekezo yenye manufaa katika mpango wa BBI.

Kuria amesema hatua hiyo itasaidia kuepusha hali ya mpango huo kutupiliwa mbali kwa kukosa uungwaji mkono.

Kuria amedumisha kwamba nchi hii haistahili kupoteza mapendekezo kadhaa muhimu katika mpango wa BBI, kama vile kuongezwa kwa kiwango cha fedha zinazotolewa kwa kaunti na kubuniwa kwa maeneo bunge mapya kwenye kaunti ambako hakuna uwakilishi wa kutosha.

Amekariri kwamba juhudi za kuandaa kura ya maamuzi kuambatana na hali ilivyo sasa humu nchini zitasababisha BBI kukosa uungwaji mkono wa kutosha kote nchini.

Akiongea katika eneo la Gatundu Kaskazini baada ya hafla ya mazishi katika Kijiji cha Kang’oo, Kuria ametoa wito kwa kiongozi wa taifa kuandaa mkutano wa kundi la wabunge wa vyama mbali mbali ili kujadili uwezekano wa kupitisha bungeni mapendekezo muhimu kwenye ripoti hiyo ya BBI.

Amesema ijapo ripoti hiyo ni nzuri, taratibu zinazohitajika kabla ya kufanyia katiba marekebisho hazijafuatwa.

Aidha, Kuria amesema inasikitisha kuona kwamba kutokana na tamaa za kibinafsi, baadhi ya wanasiasa wametumia ripoti ya BBI kama chombo cha kuzua ghadhabu miongoni mwa Wakenya wengi.