Categories
Michezo

Ingwe waikwaruza Homeboyz ligi kuu FKF

Miamba wa soka Kenya Afc Leopards walisajili ushindi wa pili mtawalia kwenye ligi kuu FKF chini ya kocha mpya Patrick Auseems kutoka Ubelgiji walipowaadhibu Kakamega Homeboyz magoli 2-1 katika pambano la Jumapili uwanjani Bukhungu ukiwa ushindi wa kwanza kwa Leopards katika uga huo.

Clyde Senaji aliwaweka wageni Ingwe uongozini kwa goli la kwanza dakika ya 10, kabla ya lvis Rupia kuongeza la pili huku wakiongoza 2-0 kufikia mapumzikoni.

Allan Wanga alifunga bao la kufuta machozi kwa wenyeji na mechi kumalizika kwa ushindi wa Leopards 2-1.

Katika michuano mingine Bandari Fc pia walizidisha makali yao kwa kuinyoa Ulinzi Stars mabao 2-0 katika uwanja wa Kericho Green,Sofapaka wakasajili ushindi wa mabao 2-1 ugenini kwa Posta Rangers nao Kariobangi Sharks wakawafilisi KCB kwa kuwazabua mabao 3-0.

Tusker Fc waliolimwa na Bidco United Jumamosi wangali kushikilia kukutu uongozi wa ligi hiyo kw alama 32 baada ya mechi 14,wakifuatwa na KCB kwa pointi 26,pointi moja zaidi Bandari Fc iliyo ya tatu na AFC Leopards katika nafasi ya 4 wakati Kariobangi Sharks wakihitimisha tano boar kwa alama 24.

Categories
Michezo

Rupia aubuka mchezaji bora ligi kuu FKF Disemba

Mshambulizi wa AFC Leopards  Elvis Rupia ametawazwa mwanasoka bora kwenye ligi kuu ya  FKF Kenya mwezi Disemba mwaka jana .

Rupia aliwapiku kipa wa KCB Joseph Okoth na mshambulizi wa Kariobangi Sharks  Eric Kapaito  na kuwa mshindi wa kwanza wa tuzo hiyo inayoandamana na shilingi 50,000.

Mshambulizi huyo alikuwa na msimu bomba akipachika wavuni maboa 6 katika mechi 4 za ufunguzi kufikia Disemba akifunga bao moja katika ushindi wa Leopards wa   mabao 2-1 dhidi ya  Tusker FC,na kufunga mengine mawili dhidi ya Bidco United kabla ya kufunga magoli 3 dhidi ya Sofapaka .

Tuzo hiyo itakuwa ikitolewa kila mwezi ikiwashirikisha kocha na mchezaji bora.

Categories
Michezo

Sofapaka waongeza masaibu ya Zoo Fc baada ya kuwakung’uta 2-0 FKFPL

Klabu ya Sofaka ilirejelea tambo za ushindi na kuzidisha masaibu ya Zoo Fc ilipowachara mabao 2-0 katika mechi ya pekee ya ligi kuu FKF iliyopigwa Jumatano jioni katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Batoto Ba Mungu walipachika mabao yote kunako kipindi cha kwanza kupitia kwa Lawrence Juma dakika ya 10 na  Kepha Aswani dakika ya 28.

Ushindi huo ulkuwa wa nne kwa Sofapaka baada ya mechi 10 huku wakishikilia nafasi ya 9 kwa alama 14 wakati Zoo FC wakikabiliwa na hatari ya kushushwa ngazi kwani hawajasajili ushindi hata mmoja kati ya mechi  8 walizopiga wakishika mkia kwa pointi 2 pekee.

Categories
Michezo

Kocha Auseems ahudhuria mazoezi ya kwanza ya Ingwe

Kocha mpya wa AFC Leopards Patrick Auseems alihudhuria mazoezi ya  kwanza  ya timu hiyo Jumanne asubuhi saa chache baada ya kusaini mkataba wa kuifunza timu hiyo .

Mbelgiji huyo ambaye zamani alitwaa ubingwa wa ligi kuu  Tanzania akiwa  na  Simba SC  msimu wa mwaka 2018/2019  na  kufikia robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika ,ana leseni ya  EUFA PRO na anatwaa mikoba  ya ukufunzi kutoka kwa  Antony Kimani.

Kocha huyo aliye na umri wa miaka 55 pia amewahizifunza timu za Al Hilal ya Sudan akishinda kombe la Super na kunyakua ligi kuu nchini Congo na AC Leopards mwaka 2014 na amefanya ukufunzi kwa miaka 30 barani ualaua na Afrika.

Kocha Patrick Auseems akiongoza mazoezi ya AFC Leopards

Kibarua cha kwanza kwa kocha huyo akiwa usukani ni mechi ya raundi ya 64 bora kuwania kombe la FKF Jumapili ijayo mjini Wundanyi dhidi ya Taita Taveta Stars.

Auseems alikuwa difenda wa zamani wa klabu cha Stadard Liege nchini Ubelgiji.

 

Categories
Michezo

Mashemeji waogopana ligi kuu FKF

Derby iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na ghamu baina ya  AFC Leopards na Gor Mahia haikuwa na chochote muhimu baada ya timu zote kutoka sare tasa katika pambano la ligi kuu Jumapili alasiri katika uwanja wa Kasarani.

Leopards watajilaumu baada ya kukosa nafasi chungu nzima za kupachika magoli hususan kipindi cha kwanza wakati Kogalo wakicheza kwa tahadhari kuu na kupata pointi hiyo muhimu.

Leopards walikuwa wakisaka ushindi wa kwanza dhidi ya Gor kwenye ligi kuu tangu mwaka 2016 lakini watalazimika kusubiri zaidi.

Pointi hiyo moja inawaweka  Leopards katika nafasi ya 4 kwa alama 19  nao Gor Mahia  wakiwa katika nafasi ya 6 kwa alama 16 kutokana na mechi 9.

Katika mchuano mwingine wa Jumapili Bidco United ilisajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Zoo Fc.

Categories
Michezo

Mashemeji Derby Kasarani bila mashabiki Jumapili

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Kenya Gor Mahia watashuka uwanjani Kasarani Jumapili  Februari 7  kwa mechi ya ligi kuu maarufu kama Mashemeji Derby huku kwa mara ya kwanza mechi ya hiyo ya ubabe na utani mkubwa ikichezwa bila mashabiki uwanjani kutoka na ugonjwa wa Covid 19.

Timu zote zililkuwa zimeiomba wizara ya afya  kuruhusu angaa mashabiki 5,000 ombi lililokataliwa na  kuwalazimu mashabiki kusalia nyumbani wakati wa mchuano huo siku ya  Jumapili .

Katibu mkuu wa Gor Mahia Sam Ochola amesema wamejiandaa vyema huku wakilenga kuzoa alama zote tatu ili kuwakaribia Leopards kwenye jedwali.

“Kikosi chetu kiko  sawa tunatafuta pointi zote tatu ili tuwakaribie Leopards”akasema Ochola

Kwa upande wake mwenyekiti wa Leopards Dan Shikanda ana imani ya kusajili matokeo bora mchuano huo huku akilalama kuhusu kufungiwa nje kwa mashabiki.

“Tulitarajia kuwa by the time tunacheza hii mechi serikali itaruhusu mashabiki lakini kwa sasa tutacheza tu bila mashabiki lakini tunalenga kupata matokeo mazuri”akasema Shikanda

Leopards ni ya 4 ligini kwa pointi 18 wakati Gor Mahia ikishikilia nafasi ya 6 kwa alama 15.

Categories
Michezo

Gor Mahia yawashika mateka Bandari Fc ,wakati Tusker ikiwalewesha Mathare

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Kenya  Gor Mahia walikosa heshima ugenini walipoilabua Bandari Fc magoli 3-1 katika mechi ya ligi iliyopigwa Jumapili alasiri katika uchanjaa wa Mbaraki kaunti ya Mombasa.

Mrundi Jules Ulimwengu alipachika mabao 2 ,la kwanza kunako dakika ya 36 kabla ya Bernard Odhiambo kurejesha goli hilo  dakika ya 40  kwa Bandari ,wakati Ulimwengu akiwarejesha Kogalo uongozini kwa bao la dakika ya 45  na kuenda mapumzikoni kwa uongozi wa mabao 2-1.

Nicholas Kipkurui alipachika bao la tatu dakika ya 91  na kuwapa wageni ushindi maridhawa.

Katika uwanja wa Ruaraka wagema mvinyo Tusker Fc waliilewesha Mathare United kwa kuwabinikiza bao 1-0 ,Luke Namanda akitikisa nyavu dakika ya 7,5 huku  Hillary Wandera akifunga penati mbili katika ushindi wa Nzoia Sugar Fc wa mabao 2-1 dhidi ya wageni Zoo Fc ambao pia walipata goli la kufutia machozi kupitia penati.

Tusker wangali kushikilia kukutu uongozi wa ligi hiyo kwa alama  23 baada ya mechi 10 ,pointi 1  zaidi ya KCB iliyo ya pili wakati Wazito Fc ikiwa imezoa alama 20 katika nafasi ya tatu.

 

Categories
Michezo

Homeboyz wazidiwa Uzito ligi kuu FKF

Klabu ya Wazito Fc imeendeleza msuru wa matokaeo mazuri  kwa kushinda mechi tano mtawalia,ilipowaangusha Kakamega Homeboyz goli 1 bila jibu katika mechi ya pekee ya ligi kuu FKF iliyochezwa Ijumaa alasiri katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Michael Owino alipachika kimiano bao hilo la pekee na la ushindi kwa wenyeji kunako dakika ya 41 .

Ushindi huo unaikweza Wazito Fc hadi nafasi ya tatu ligini baada ya mechi 10 ,wakishinda 6 kwenda 2 na kupoteza mbili wakiwa wamezoa alama  20 sawia na Tusker Fc iliyo ya pili ,pointi 1 nyuma ya viongozi KCB.

Ligi hiyo kuendelea Jumamosi kwa jumla ya mikwangurano minne ,City Stars wakifungua kazi Kasarani saa saba unusu dhidi ya Kariobangi Sharks,kabla ya Sofapaka kumenyana na Vihiga United katika uchanjaa wa Mumias Complex saa tisa .

Wahifadhi hela KCB watakuwa na mtihani mgumu huko Afraha dhidi ya wanajeshi Ulinzi Stars kisha  AFC Leoaprds wakamilishe ratiba  saa tisa alasiri dimbani Kasarani dhidi ya Posta Rangers.

Categories
Michezo

Ulinzi Stars waiangusha Mathare United huku Gor wakiiparuza Zoo Fc ligi kuu FKF

Wanajeshi Ulinzi Stars  na mabingwa watetezi Gor Mahia wamesajili ushindi katika mechi mbili za ligi kuu FKF  zilizosakatwa Jumatano alasiri.

Ulinzi waliipakata Mathare United mabao  2-1 katika uwanja wa Afraha  ,Daniel Waweru akipachika bao la kwanza kwa wenyeji kunako dakika ya 7 akiunganisha mkwaju uliotumwa na Michael Otieno na kumwacha kipa hoi bin taaban.

Kiungo Elvis Nandwa aliongeza bao la pili kwa Ulinzi akiunganisha pasi  murua iliyochongwa na mchezaji Masuta katika dakika ya 70 huku Mathare wakijipatia goli la maliwazo kupitia kwa Daniel Otieno dakika ya 88.

Katika mechi nyingine iliyopigwa katika uchanjaa wa Kasarani, Gor Mahia walirejelea tambo za ushindi na kuititiga Zoo Fc mabao 3 bila jibu ,kiungo Samuel Onyango akipachika la kwanza dakika ya 10, kabla ya nahodha Keneth Muguna kutanua uongozi kwa goli la dakika ya 32 na kisha Onyango akapiga tena bao la tatu kunako dakika ya pili ya muda wa mazidadi.

Kufuatia matokeo ya Jumatano Gor na Ulinzi wamezoa idadi sawa ya alama 12 ingawa vijana wa KDF wamecheza mechi mbili zaidi.

Categories
Michezo

Ingwe yaichuna Sharks huku KCB wakiwazima Western Stima

AFC Leopards waliwakwaruza Kariobangi Sharks mabao 2-0 katika mchuano wa ligi kuu uliopigwa Jumapili alasiri  katika uwanja wa Kasarani.

Elvis Rupia alipachika bao la kwanza dakika ya 11 huku wakiongoza kwa goli hilo kufikia mapumziko.

Kipindi cha pili pande zote zilicheza kwa tahadhari huku wageni Ingwe wakilazimika kumaliza mechi na wachezaji 10 uwnajani kufuatia kupigwa kadi nyekundu kwa Fabrice Mugheni  dakika ya 89.

Kadi hiyo nyekundu haikuwatamausha Leopards walioongeza mashambulizi na  Jefari Odeny akaongeza bao la pili kunako dakika ya 92  ukiwa ushinde wa pili kwa Sharks msimu huu.

Katika mikwangurano mingine  Kakamega Hombeboyz wakiwa nyumbani Bukhungu waliikung’uta Bidco United magoli 2-0 Ali Bhai na Moses Mudavadi wakipachika  mabao yote katika kipindi cha kwanza wakati KCB wakiiparuza Western Stima mabao 3-1 katika uga Moi kaunti ya Kisumu.

Kcb wangali kushikilia kukutu uongozi wa ligi hiyo kwa pointi 21 baada ya michuano 8 wakifuatwa na Tusker Fc kwa alama 20 huku Wazito Fc wakifunga orodha ya tatu bora kwa alama 17.