Categories
Michezo

Shikanda ateuliwa kocha mpya wa Nzoia Sugar FcC

Klabu ya Nzoia Sugar Fc inayoshiriki ligi kuu ya Kenya imemteua  Ibrahim Shikanda kuwa kocha mpya ambapo atakuwa akisaidiwa na Sylvester Mulukurwa ambaye amekuwa akihudumu katika nafasi ya kaimu kocha .
Shikanda awali amekuwa na timu ya Nairobi Stima ikishiriki ligi ya Nsl na pia amekuwa naibu kocha wa Bandari Fc hadi mwishoni mwa msimu uliopita .
Timu hiyo yenye makao yake magharibi mwa Kenya ni ya 13 katika jedwali la ligi kuu  kwa alama 4 baada ya kwenda sare  mechi 4 kati ya 6 ilizocheza.
Mtihani wa kwanza kwa Shikanda katika benchi ya Nzoia Sugar Fc ni mwishoni mwa juma hili watakapochuana na Western Stima Fc.
Categories
Michezo

Bidco United yaikaanga Vihiga United huku Tusker na Sopaka wakitoka nguvu sawa

Bidco United walisajili ushindi wa kwanza ligini msimu huu, baada ya kuilaza Vihiga United bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu Fkf iliyochezwa Jumapili alasiri katika uchanjaa wa Moi kaunti ya Kisumu.

Bao la pekee na la ushindi kwa Bidco iliyopandishwa ngazi msimu huu lilipachikwa na Nelson Chieta kunako dakika ya 37.

Katika mechi nyingine  iliyopigwa kiwarani Kasarani Tusker Fc walitoka sare ya bao 1-1 na wageni Sofapaka Ellie Asieche akifunga bao la Sofapaka dakika ya 6  kabla Tusker kurejea mchezoni kwa bao la Luke Namanda dakika ya 25.

Katika uga wa Utalii Wazito Fc iliwapachika Nairobi sity stars magoli 2-1 huku Bandari pia ikiwazima Western Stima mabao yayo hayo 2-1 katika uga wa Mbaraki.

Timu za Mathae United na Zoo fc hazijacheza mechi za ufunguzi huku Gor Mahia wakicheza mechi mbili pekee wakati timu nyingi zikiwa zimesakata michuano 6 kila moja.

 

Categories
Michezo

Ulinzi watoshana nguvu na Sharks

Ulinzi Stars na Kariobangi Sharks waliumiza nyasi bila lengo maalum baada ya kuambulia sare tasa Jumamosi alasiri katika mojawapo wa mechi mbili za ligi kuu iliyochezwa uwanjani Kasarani.

Katika uwanja wa Bukhungu pia jumamosi  wenyeji Nzoia Sugar  walitoka sare kapa dhidi ya Kakamega Homeboyz .

Ratiba ya Jumapili

1. Wazito vs Nairobi City Stars (Utalii Grounds, 3 pm)
2. Tusker FC vs Sofapaka (Kasarani Stadium, 3 pm)
3. Vihiga United vs Bidco United (Mumias Sports Complex, 3 pm)
4. Bandari vs Western Stima ( Mbaraki Grounds, 3 pm)

Categories
Michezo

FKF yapata pigo baada ya mahakama kuzirejesha Mathare United na Zoo Fc ligini

Shirikisho la kandanda nchini  FKF limepatwa na pigo baada ya mahakama ya kutatua migogoro michezoni  nchini SDT kuamuru kurejeshwa ligini timu za Mathare United na Zoo Fc   kusubiri uamuzi wa kesi  iliyowasilishwa dhidi ya FKF na  vialbu hivyo viwili wiki ijayo.

Mwenyekiti wa Mahakama hiyo maarufu kama SDT John Ohaga ametoa uamuzi huo mapema Alhamisi wa kuzirejesha timu hizo mbili kwenye ligi pamoja na kubatilisha uamuzi wa awali wa FKF wa kutamatisha kandarasi za wachezaji wote wa klabu  hizo mbili  .

Pia jaji Ohaga ameagiza Fkf iliruhusu wachezaji na maafisa wa vilabu hivyo kufanyiwa vipimo vya COVID 19 sawa na vilabu vingine  saa 72 kabla ya kuanza mechi zao za ligi kuu .

Wachezaji wa Zoo FC

Baraza kuu la FKF likikutana Desemba 9 na kuamuru kuzipiga marufuku timu hizo hadi pale zitakaposaini mkataba huo wa Star Times.

FKF ilizipiga marufuku timu hizo kushiriki ligi kuu ya FKF baada ya kudinda kusaini mkataba wa Star Times ambao ungewezesha mechi za timu hizo kupeperushwa mbashara na runinga hiyo ya China .

 Wachezaji Mathare United

Shirikisho hilo pia linamchunguza mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier  baada yake kaundika barua kwa Star Times kuondoa barua ya kwanza iliyoandikwa na aliyekuwa katibu mkuu Sam Ochola kusaini mkataba huo .

Zoo FC vs. Kenya Football Federation – Order (17 Dec 2020)

Mkataba wa FKF na Star Times umeibua hisia kali huku vilabu vya Ulinzi Stars,Mathare United ,Gor Mahia na Zoo Fc vikiupinga kwa kukiuka haki zao hatua iliyochangia kupigwa marufuku na kutimuliwa ligini kwa Mathare  United na Zoo Fc .

Timu za Mathare na Zoo zilizuiwa kucheza mechi zao za kufungua msimu wa ligi wiki jana wakati Gor na Ulinzi wakiwa tayari wamecheza mechi 2 na moja mtawalia katika ligi kuu.

Mahakama ya SDT itakutana wiki ijayo kusikiza kesi hiyo na kutoa maelekezo zaidi huku ligi ya FKF ikiangia mechi za mzunguko wa nne mwishoni mwa juma hili.

 

 

 

Categories
Michezo

Zoo FC yaelekea mahakamani kupinga mkataba wa FKF na Star Times

Kilabu ya Zoo Fc imewasilisha kesi ya dharura katika mahakama ya kutatua migogoro michezoni SDT  kutaka iruhusiwe kucheza mechi zake ligi kuu ya Fkf ,bila kupeperushwa kupitia runinga ya Star Times  baada ya kudinda kusaini mkataba huo .

Zoo fc yenye makao yake katika kaunti ya Kericho imesusia kucheza mechi zake mbili za ufunguzi za ligi kuu kutokana na kutokubaliana na mkataba huo, huku ikijiunga na timu za Ulinzi Stars,Mathare United na Gor Mahia ambazo zimesusia kusaini  pia mkataba huo wakidai una vipengee vyenye utata.

Mwenyekiti wa Zoo fc Ken Ochieng’ amemtaka Rais wa FKF kukomesha vitisho na kuonyesha mfano mwema wa uongozi akisema hawako tayari kuachilia haki zao za runinga kwa shirikisho.

“Vitisho na unyanyasi havina nafasi  haswa wakati wa swala linalohusu haki za matangazo ya runinga kwa kilabu ,tumeambiwa tupeane haki zetu kwa miaka saba huku tukilipwa  kiwango cha chini cha pesa na hakuna kipengee cha kujiondoa ukisha Saini mkataba huo ,ni mkataba ambao hauna faida yoyote kiuchumi kwa timu”akasema Ochieng’

Timu zote zilizotia saini mkataba huo zimepokea shilingi milioni 2 .

Fkf imeratibu timu za Gor Mahia na Ulinzi Stars kucheza mechi yao ya ufunguzi Jumamosi hii huku Zoo  Fc na Mathare united zikiachwa nje.

Baraza kuu la Fkf linatarajiwa kukutana kuamua hatima ya vilabu hivyo vine huku ikidokezwa kuwa huenda timu hizo zikatimuliwa ligini.

Categories
Michezo

Chui watoa kucha ligini na kudumisha rekodi ya 100%

Miamba wa soka nchini Kenya Afc Leopards waliendeleza msururu wa matokeo mazuri kwa kulilaza Bidco United mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu iliyosakatwa Jumapili Jioni katika uwanja wa Kasarani.

Leopards walihitaji mabao 2 ya mshambulizi Elvis Rupia kunako kipindi cha pili ili kuwatema Bidco waliopandishwa ngazi ligini msimu huu na kudumisha rekodi ya asilimia 100 baada ya michuano miwili kwani pia wakikuwa wameilaza Tusker Fc mabao 2-1 katika pambano la ufunguzi.

Sofapaka wakiwa Kilifi waliwateketeza Western Stima mabao 3-1 ,Ellie Asieche akicheka na nyavu mara mbili ,moja kila kipindi huku naye Kepha Aswani akafunga kazi kwa  Batoto Ba Mungu kwa goli la 3 huku lile la maliwazo kwa wageni Stima likifungwa na Samuel Odhiambo.

Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Sofapaka waliopoteza pambano la ufunguzi  bao 1-0 ugenini kwa Bandari Fc.

Kwenye  matokeo mengine wana Mvinyo Tusker watazidi kusubiri ushindi wa kwanza ligi, baada ya kukabwa koo na Bandari Fc kwa kutoka sare kapa huku Kakamega Homeboyz wakishindwa kutamba nyumbani na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Posta Rangers.

Leopards wanaongoza jedwali kwa pointi 6  sawia na KCB baada ya mechi mbili .

Categories
Michezo

KCB FC na Wazito FC zaibuka kidedea

Baada ya kuambulia kichapo katika mechi za raundi ya kwanza ya ligi kuu wiki jana,timu ya Wazito Fc imesajili ushindi wa kwanza leo kwa  kuwalemea Vihiga United mabao 3-1 katika mchuano wa ligi kuu uliosakatwa  Ijumaa alasiri katika uwanja wa kaunti ya Narok,.

Wazito walichukua uongozi wa pambano hilo kunako dakika ya 12 ya mchezo kupitia kwa  mshambulizi Boniface Omondi kabla ya beki Dennis Ng’ang’a kuongeza la pili robo saa baade huku wakiongoza 2-0 kufikia mapumziko.

Mshambulizi wa zamani  Leopards Wyvone Isuza aliongeza bao la tatu katika dakika ya 54 lakini  Norman Werunga  akapachika goli la kufutia machozi kwa wageni  katika  dakika ya 64.

Iilikuwa mechi ya pili mtawalia  kwa Vihiga united kupoteza tangu warejee kwenye ligi kuu ,baada ya kuangushwa pia kwa bao moja kwa sifuri na Kakamega Homeboyz wiki jana.

Wahifadhi hela KCB waliibwaga Nairobi City Stars  goli 1-0 katika mchuano mwingine wa Ijumaa uwanjani Kasarani.

Bao la pekee na la ushindi kwa Kcb ilikipachikwa kimiani na Difenda Henry Onyango kunako dakika ya 43.

Mechi mbili zaidi za mzunguko wa pili wa ligi kuu kupigwa Jumamosi Nzoia Sugar wakiwaalika Kariobangi Sharks uwanjani Sudi kuanzia saa tisa huku Tusker Fc na Bandari fc wakimenyana uwanjani Kasarani kaunzia saa tisa pia.

Categories
Michezo

Mvutano kati ya FKF na timu 4 watishia kuathiri msimu mpya wa ligi kuu

Shirikisho la kandanda nchini Fkf litaziadhibu  timu ambazo hazitasaini mkataba wa  kupeperusha mechi za ligi kuu inayotazamiwa kuanza Jumamosi hii.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi  mapema Alhamisi ,mwenyekiti wa Fkf Nick Mwendwa amesuta vilabu vinne ambavyo havijasaini mkataba huo wa matangazo ya runinga akisisitiza kuwa vimepewa nafasi ya mwisho kubatilisha misimamo yao mikali na kuruhusu ligi kuanza bila tashwishwi.

Rais wa FKF Nick Mwendwa akizungumza wakati wa kuzindua mkataba baina ya FKF na Star Times

“Sisi tuko tayari kuanza ligi Jumamosi bila hizo timu nne ambazo hazijasaini mkataba huo,lakini pia tunawapa nafasi ya kufikiria upya kuhusu uamuzi wao ,la sivyo tutachukua hatua kama shirikisho wiki ijayo,hakuna vile timu hizo zitazuia ligi kuanza”akasema Mwendwa

Mwendwa amekariri kuwa haki zote za ligi ya Kenya zinamilikiwa shirikisho na wala sio za vilabu inavyodaiwa .

“Fkf ndio wameliki wa haki zote za soka humu nchini na pia ligi ya Fkf Premier League,kwa hivyo tusidanganyane ,si bado tunaomba timu za Zoo Fc,Gor Mahia ,Mathare United na Ulinzi Stars kutafakari na kubadilisha msimamo wao ligi ianze vijana wapate doo”akaongeza Mwendwa

Nick mwendwa akiwa na CEO wa Star Times  Hanson Wang katika uzinduzi wa mkataba ligi kuu FKF

Fkf imezindua mkataba wa miaka 7 na kampuni ya Star Times ya kutoka China ili kupeperusha mechi za ligi kuu ambapo inatarajiwa kuwa angaa mechi 100 zitarushwa kwenye runinga kila msimu .

Hata hivyo kwenye mahojiano na Kbc kwa njia ya simu mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier ameapa kuelekea mahakamani kusimamisha mkataba huo wa runinga na kupinga hatua ya Fkf Kumiliki haki zote za vilabu.

“Mimi kwa sasa sina wakati wa kujibizana na Fkf lakini nitafuata mkondo wa sheria ambapo nitaelekea mahakamani kutaka kusimamishwa kwa mkataba huo kwa sababu haki za vilabu hazipaswi kutwaliwa na shirikisho”akasema Rachier

Utata huo huenda ukaibuka mvutano mkubwa kwenye ligi kuu ambayo iliratibiwa kuanza Jumamosi hii ambapo jumla ya mechi 3 zimeratibiwa kupeperushwa kupitia Runinga ya Star Times.

 

Categories
Michezo

Gor Mahia yampiga marufuku katibu mkuu Sam Ochola kwa ‘kuuza timu’

Kilabu cha Gor Mahia kimempiga marufuku katibu mkuu wake Sam Ocholla kwa kusaini barua ya mkataba wa kupeperusha mechi la ligi kuu FKF baina ya kampuni ya Star Time na FKF.

Akitangaza  kumpiga marufuku ya  Ocholla,mwenyekiti wa Gor Ambrose Rachier amesema kuwa ilikuwa kinyume cha sheria kwa katibu huyo kusaini barua hiyo bila kushauri usimamizi mkuu wa timu na tayari wameandika barua kwa kampuni ya Stars Times kujitenga na mwafaka huo.

Kulingana na Rachier uamuzi huo sio wa kuchukuliwa na mtu binafsi.

“kulingana na katiba ya  kilabu ibara ya 15 mkataba wowote kama huo unaweza ukatiwa saini tu mwenyekiti wa timu,na hatuko tayari kuuza haki zetu kwa huo mkataba kwani hatujaona  kandarasi kati ya FKF na Stars Times ndio maana hatukubaliani na mkataba huo”akasema  Rachier

Rachier amesisitiza kuwa wako tayari kushiriki ligi kuu inayotazamiwa kuanza tarehe 28 mwezi huu,lakini hawatauza haki zao kwa kusaini mkataba huo.

”Sisi tuko tayari kaunza ligi lakini kile hatutafanya ni kuuza haki zetu,kile FKF wanafanya ni kinyume cha sheria kwa vilabu kupokonywa haki zao”akaongeza Rachier

Hata hivyo Ochola ameitisha kikao na wanahabari Jumatano kujitetea akidokeza kuwa uamuzi huo wa kusaini barua ya mkataba aliuafikia baada ya kupewa idhini na baraza kuu la kilabu.

Kampuni ya Star Times yenye makao yake nchini China ilisaini mkataba wa miaka 7 na Fkf kumiliki haki zote za matangazo ya runinga ya ligi kuu ,mechi za timu za taifa za wanaume na wanawake na mechi 30 za ligi ya NSL.

Vilabu vinne vimedinda kusaini mkataba huo vikiwemo Gor Mahia,Ulinzi Stars ,Mathare United na Zoo Fc kwa misingi ya kutofahamu yaliyimo kwenye kandarasi hiyo.

 

 

 

Categories
Michezo

Ligi ya Nsl kung’oa nanga Disemba 5

Shirikisho la soka nchini FKF  limeahirisha tarehe ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya daraja ya pili nchini kenya NSL hadi tarehe 5 mwezi ujao.

Kulingana na Fkf ligi hiyo imesukumwa mbele kwa wiki moja kutoka tarehe  ya awali, baada ya  ligi kuu ya FKF kuahirishwa kutoka Novemba 20 hadi Novemba 27.

Ligi ya NSL itashirikisha timu 17 msimu huu kinyume na 19 za msimu jana baada ya Chemilil Sugar Fc na Ushuru Fc kuvunjiliwa mbali kutokana na ukosefu wa pesa  na hivyo basi kutoa fursa kwa  Silibwet  Leos Fc,Soy United na Mwatate United Fc kupandishwa ngazi kucheza ligi hiyo.

Timu mbili bora kutoka ligi hiyo hupandishwa ngazi kucheza ligi kuu ya FKF huku ile ya tatu ikicheza mchujo dhidi ya timu ya 16 katika ligi kuu ambapo mshindi hushiriki ligi kuu.

Wachezaji wa vilabu vyote vya ligi kuu wanapitia vipimo vya Covid 19 kwa mjibu wa matakwa ya serikali kabla ya ligi kuanza rasmi.

Ligi kuuu ya Fkf msimu wa mwaka 2020-2021 uantazamiwa kuanza mwishoni mwa juma  hili kwa mechi tatu Afc Leopards wakipambana na Posta Rangers katika uwanja wa Nyay,o huku Mathare united ikifungua dimba dhidi ya Kakamega Homeboyz nao  Bandari Fc waanze msimu nyumbanio dhidi ya Zoo Fc.