Categories
Michezo

Morans wanyanyaswa na Senegal 54-92 Fiba Afrobasket nchini Rwanda

Timu ya taifa ya Kenya ya mpira wa kikapu, ilianza vibaya mechi za kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mjini Kigali Rwanda baada ya kucharazwa pointi 92 -54 katika mchuano uliosakatwa katika uwanja wa Kigali Arena Jumatano jioni.

Kenya maarufu kama Morans walianza vyema pambano hilo ,huku wakilazimisha sare ya alama 19-19 katika robo ya kwanza ya mchezo ,kabla ya kulegea katika robo ya pili walipopoteza alama  14-28  na kisha Morans wakasajili ushindi wa pointi  19-14 katika robo ya tatu ikiwa robo pekee ya mechi iliyoshindwa na Kenya.

Hata hivyo  Morans wanaofunzwa na kocha Cliff Owuor walizidiwa maarifa kwenye robo ya mwisho walipozabwa alama 2-34 wakiwa na makosa mengi ya safu ya ulinzi huku pia wakikosa kumakinika wakati wa kufunga na pia zikiwa alama za chini zaidi walizosajili katika robo moja na pia kufungwa pointi nyingi zaidi .

Licha  ya kocha Owuor kuitisha muda wa mapumziko ili kujaribu kuimarisha mchezo, dau la Kenya lilionekana kuzama kila wakati haswa wakipoteza nafasi nyingi za kufunga alama tatu maarufu kama 3 pointer na pia alama 2.

Katika mchuano huo uliorushwa mbashara na runinga ya Kbc Channel 1 , Tyler Ongwae aliibuka mfungaji bora wa Kenya kwa kuzoa pointi 13 huku Ibrahim Faye akiizolea Senegal alama za juu zikiwa 19.

Vijana wa Morans sasa watakuwa na muda wa chini ya saa 24 kujitayarisha na kurekebisha makosa yao, kabla ya kurejea uwanjani kukabiliana na miamba wa Afrika Angola Alhamisi alasiri na  kufunga ratiba dhidi ya Msumbiji Ijumaa.

Kenya hawana budi kushinda angaa mechi moja ili kuwa na nafasi ya kufuzu kwa fainali za mwaka ujao, ambapo timu tatu bora kutoka kila kundi zitacheza kipute cha Fiba Afrobasket.