Categories
Michezo

Kenya wasajili ushindi wa kwanza kwa kuichakaza Msumbiji vikapu 79-62 mechi za kufuzu Fiba Afrobasket

Timu ya Kenya ya mpira wa kikapu maarufu kama Morans imekamilisha mechi za raundi ya kwanza katika kundi B kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket kwa ushindi baada ya kuwanyuka Msumbiji vikapu 79-62  Ijumaa jioni katika uwanja wa Kigali.

Morans walianza mchuano huo wakijua kuwa ni ushindi tu ungewaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu baada ya kupoteza mechi za kwanza mbili dhidi ya Senegal na Angola na wakalazimishwa kutoka sare alama 19-19 katika robo ya kwanza ya mchezo .

Hata hivyo Msumbiji waliimarika katika robo ya pili  na kuibwaga Kenya pointi 17-14 huku Kenya wakilipiza kisasi na kushinda robo ya tatu alama 23-17 na kudumisha ushindi kwenye  robo ya mwisho vikapu  23-14 .

Tyler Ongwae kwa mara nyingine tena aliibuka mfungaji bora wa vikapu kwa Kenya kwa kufunga 21 akifuatwa na Valentine Nyakinda aliyefunga vikapu 16  huku nahodha Erick Mutoro akirekodi vikapu 15.

Kenya inayofunzwa na kocha Cliff Owuor itarejea nchini mwishoni mwa juma hili ,kujiandaa kwa mechi tatu za raundi ya pili kundini B wakianza dhidi ya Senegal Februari 19 mjini Kigali Rwanda ,kabla ya kukutana na Angola Februari 20 na kufunga ratiba dhidi ya Msumbiji tena tarehe 21 mwezi Februari mwakani.

Timu tatu bora kutoka kundi hilo zitafuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao nchini Rwanda.

Categories
Michezo

Morans wapakatwa na Angola michuano ya kufuzu kwa Fiba Afrobasket

Matumaini ya timu ya taifa ya Kenya katika mpira wa kikapu almaarufu the Morans  kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao yalididimia baada ya kuambulia kichapo cha pointi 66-83 kutoka kwa Angola katika mechi ya pili ya kundi B  ya  kufuzu, iliyosakatwa Alhamisi Alasiri  katika uwanja wa Kigali  Rwanda.

Morans walipoteza robo ya kwanza ya mchezo pointi 10-18 na ya pili 15-21, lakini wakanyong’oyea zaidi katika robo ya tatu walipocharazwa alama 13-29.

Mabadiliko kadhaa  ya kiufundi kutoka kwa kocha Cliff Owuor yaliimarisha mchezo wa Wakenya  waliojizatiti na kunyakua ushindi katika kwota ya mwisho ya mchezo alama 28-15 ingawa tayari maji yalikuwa yamezidi unga.

Reuben Mutoro na Tyler Ongwae walikuwa wafungaji bora wa pointi kwa Kenya ,kila mmoja akizoa alama 18 .

Nahodha wa kenya Mutoro amesema walicheza vizuri dhidi ya Angola kuliko dhidi ya Senegal huku akiahidi kwamba wataimarisha mchezo wao zaidi dhidi ya Msumbiji Ijumaa “Tulicheza vyema katika mechi ya leo kinyume na  mechi ya Jumatano ,naamini kuwa  tutarudi kufanya utafiti na kujitayarisha vyema dhidi ya Msumbiji  ambao nina imani tutaimarika zaidi na kupata ushindi”akasema Mutoro

“Kwetu sisi mechi ya Msumbiji ni kama fainali tutajituma kwa asilimia 100 kwani hatuna kingine cha kuhofia au kutuzuia na baada ya hapo tutangoja raundi ya pili mwaka ujao”akaongeza Mutoro

Kwa upande wake kocha Owuor amesema kuwa alijaribu kurekebisha makosa mengi waliyofanya dhidi ya Senegal ,walipochuana na Angola na ameahidi kwamba analenga ushindi katika mechi ya mwisho Ijumaa dhidi ya Msumbiji kabla ya kurejea kwa raundi ya pili Februari mwaka ujao.

”Tumekuwa na makosa mengi uwanjani ,ukiangalia tumekuwa tukipoteza mpira kwa urahisi na pia walinzi wetu hawajamakinika ipasavyo,lakini nafurahia mchuano wetu wa leo umekuwa bora kuliko ule dhidi ya Senegal.Kwa sasa tunajiandaa kucheza na Msumbiji tutafute matokeo bora halafu turejee tena Februari mwaka ujao kwa raundi ya pili”akasema kocha Owour

Ushinde wa Morans  dhidi ya Angola ulikuwa wa pili mtawalia katika kundi B kwenye mashindano hayo ,baada ya kulazwa pointi 54-97 katika pambano la ufunguzi siku ya Jumatano.

Hii ina  maana kuwa Kenya ni sharti waishinde Msumbiji katika mchuano wa mwisho Ijumaa hii kuanzia saa kumi na mbili jioni ,ili kuwa na fursa ya kutinga mashindano ya Fiba Afrobasket mwakani nchini Rwanda.

Angola wanaongoza kundi hilo baada ya kushinda mechi ya pili walipowaangusha  Msumbiji Jumatano usiku katika mechi ya kwanza.

Katika mechi ya pili Alhamisi Nigeria imeibwaga Sudan Kusini pointi 76-56  katika kundi D.

Mkondo wa kwanza wa mechi za makundi   utakamilika Jumapili ijayo kabla ya mkondo wa pili kuanza Februari 19 mwaka ujao.

Timu tatu bora kutoka kila kundi baada ya mechi 6 za makundi zitafuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao nchini Rwanda.