Categories
Burudani

Ezekiel Mutua ataka Eric Omondi akamatwe

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya Daktari Ezekiel Mutua sasa anataka mchekeshaji Eric Omondi akamatwe.

Kulingana naye, Eric amekuwa akiendesha danguro kwenye kipindi chake cha mitandaoni kwa jina “Wife Material” huku akikisingizia kuwa mpango wa ushauri kwa wasichana hao.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mutua anamkosesha Eric kwa kuonekana wazi akibusu wasichana tofauti kati ya waliokuwa kwenye shindano hilo, ilhali kuna ugonjwa wa Covid 19.

Analaumu mmoja wa walioalikwa kufundisha wasichana hao kwa kuwafunza jinsi ya kujamiiana na Eric Omondi akitaja kitendo hicho kuwa cha kishetani.

Kulingana naye, studio ambazo Eric Omondi alizindua katika eneo la Lavington hazisaidii vijana jinsi alikuwa amepanga lakini zinatumika kudhulumu wasichana. Anahimiza makachero wa DCI kuzuru eneo hilo na kumkamata mmiliki .

Ezekiel pia analaumu makundi ya kutetea haki za wanawake akisema yako kimya wanawake wenzao wakidhulumiwa. Bwana Ezekiel Omondi huwa anaendesha kampeni ya kuhakikisha kwamba video chafu au ambazo zinavuruga maadili na hata muziki havionyeshwi hadharani.

Ezekiel na Eric wamewahi kujipata wakizozana tena pale ambapo Ezekiel alimkosoa Eric kwa kupiga picha akiwa nusu uchi.

Wakati huo Eric alikuwa anajitayarisha kufungua studio zake ambazo anasema zitahudumia vijana bure bila malipo kwa nia ya kuendeleza sanaa na talanta.
Baadaye Eric alimfokea Mutua akimwambia aache kutaja jina lake.

Categories
Burudani

Studio za Eric Omondi zafungwa

Studio za Eric Omondi ambazo mchekeshaji huyo alizindua hivi maajuzi zimefungwa na shirika la kusimamia eneo la jiji la Nairobi NMS.

Kulingana na NMS, studio hizo ambazo pia zina afisi za kampuni ya Eric Omondi ziko katika eneo la makazi la Lavington na hivyo anahitajika kuzihamishia kwingine.

Kupita Instagram Eric alijulikanisha hilo akisema kwamba haendi popote atasalia katika eneo hilo, kwani kufikia sasa wamepokea maombi kutoka kwa vijana wengi ambao wangependa kurekodi nyimbo zao katika eneo hilo na ni bila malipo.

Eric anaashiria pia kwamba kuna mwanamke mmoja ambaye anamshuku kwa kuandika maneno ya kuharamisha biashara yake kwenye lango la kuingia akimpa ilani ya kufuta maneno hayo na kuomba msamaha.

Anasema mwanamke huyo alihudhuria hafla ya kuzindua studio hizo na hajui anayemtumia mwanadada huyo.

Mchekeshaji huyo pia anashangaa ni kwa nini biashara yake pekee ndiyo inamulikwa katika eneo la makazi ambalo lina shule kadhaa, studio za Coke na afisi za Azam Tv.

Haya yanajiri siku chache baada ya Eric Omondi kutofautiana na Dakta Ezekiel Mutua Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya KFCB.

Mutua anafahamika kwa kujaribu kuhakikisha maadili yanaendelezwa kwenye ulingo wa burudani nchini Kenya na alizungumza dhidi ya vitendo vya Eric ambapo amekuwa akisambaza picha na video akiwa nusu uchi.

Baadaye Eric alimfokea Bwana Mutua akimwambia aache kutamka jina lake kila mara.

Categories
Habari

KFCB: Wanaohusika na utovu wa maadili miongoni mwa vijana kunaswa

Serikali kupitia bodi ya uorodheshaji filamu hapa nchini-KFCB imezindua shughuli ya kitaifa ya kusaka biashara na watu wanaohusika na ongezeko la visa vya utovu wa maadili miongoni mwa vijana.

Mkurugenzi wa bodi ya KFCB Ezekiel Mutua alisema kwamba kuna ongezeko la utovu wa maadili ambapo alikariri haja ya kumakinika katika kuwalinda watoto.

Kwenye taarifa, Mutua alisema kampeni hiyo inanuiwa kuhamasisha umma kuhusu madhara ya kuwaingiza watoto katika masuala ya watu wazima na umuhimu wa jamii kuwajibika katika kulinda maslahi ya watoto.

Alisema miongoni mwa mikakati iliyochukuliwa na bodi hiyo, ni pamoja na kuzichukulia hatua za kisheria kampuni zinazowahusisha watoto katika masuala yasiyofaa.

Aidha bodi hiyo ilionya vituo vya utayarishaji video vinavyoshirikisha watoto katika biashara hiyo, akisema kwamba vitafungwa, leseni zao kufutwa na wamiliki kushitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema bodi hiyo inashirikiana na kitengo cha kukabiliana na uhalifu mitandaoni na ile ya Google kuhakikisha kwamba hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wafanyibiashara wa mtandaoni hapa nchini wanaohusisha watoto katika masuala ya watu wazima.