Categories
Burudani

Coy Mzungu azawadiwa gari

Mchekeshaji wa nchi ya Tanzania Coy Mzungu alizawadiwa gari na usimamizi wa Wasafi Media kampuni inayomilikiwa na Diamond Platnumz na ambayo inadhamini tamasha la Cheka Tu ambalo alianzisha Coy.

Diamond Platnumz mwenyewe ndiye aliwasilisha gari hilo kwa Coy Mzungu jambo ambalo hakutarajia wakati wa awamu ya Mzizima ya tamasha hilo la Cheka Tu.

Coy alikuwa jukwaani na mchekeshaji wa Kenya Eunice Mamito na Diamond akajiunga nao na kutangaza kwamba alikuwa amepitia tu kushukuru wote waliohudhuria tamasha hilo na kumpokeza gari Coy Mzungu.

Kwa mara ya kwanza, ukumbi wa mikutano wa jumba la kibiashara la Mlimani City Jijini Dar es Salaam ulijaa tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo la vichekesho.

Baada ya kutangaza zawadi hiyo, Diamond alimwelekeza Coy na wengine nje ambapo gari lenyewe lilikuwa limeegeshwa. Kwa furaha nyingi alipokea zawadi yake Coy Mzungu na hata kusimama juu ya gari lenyewe huku akishukuru usimamizi wa Wasafi.

Wakati wa kuondoka nchini Tanzania Eunice Mamito alimtania Diamond Platnumz akisema kwamba anastahili kukumbuka kina dada anapogawa magari.

Mamito ni mmoja wa wachekeshaji wa Kenya ambao wamepata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha hilo la vichekesho nchini Tanzania. Wengine ni pamoja na Sammie Kioko, Eric Omondi na Mc Jessy.

Categories
Burudani

Mamito apeleka ucheshi nchini Tanzania

Mchekeshaji wa Kenya Eunice Mamito yuko nchini Tanzania kwa ajili ya kuigiza kwenye tamasha kubwa la vichekesho nchini humo ambalo linajulikana kama “Cheka Tu – Mzizima Edition”.

Tamasha hilo ambalo hudhaminiwa na Wasafi Media litaandaliwa kuanzia saa moja unusu, usiku wa leo tarehe 26 mwezi Februari mwaka 2021 katika jumba la kibiashara la Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Kuna wasanii wengine wengi ambao watatumbuiza kwenye tamasha hilo kama vile wachekeshaji wa Tanzania, Coy Mzungu, Kiredio, Mr. Romantic kati ya wengine na mwimbaji wa nyimbo za injili Christina Shusho ataimba huko.

Kuna wachekeshaji wa Kenya ambao wamepata fursa ya kuhusika kwenye awamu za awali za tamasha hilo kwa jina “Cheka Tu” nao ni Eric Omondi, Mc Jessy, Profesa Hamo na Sammie Kioko.

Mchekeshaji wa nchi ya Uganda Patric Salvado pia amewahi kuhusishwa kwenye tamasha hilo ambalo lilianzishwa na Coy Mzungu kwa jina halisi Conrad Kennedy ambaye hujiita Rais wa uchekeshaji nchini Tanzania.

Mamito ndiye mchekeshaji wa kike wa kwanza kutoka Kenya ambaye amealikwa kutumbuiza kwenye tamasha hilo kubwa la uchekeshaji nchini Tanzania.

Zamu ya Eric Omondi, Mc Jessy na Salvado ambayo ilikuwa tarehe 2 mwezi Januari mwaka huu wa 2021, Diamond Platnumz alihudhuria na wakaigiza pamoja jukwaani.

Coy Mzungu aliweka video ya kuonyesha akimlaki Mamito kwenye uwanja wa ndege na baadaye wanaonekana wote na Eric Omondi na huenda naye yuko nchini Tanzania kwa ajili ya kipindi chake cha “Wife Material” na tamasha hilo ila hajatajwa kwenye mabango.

Categories
Burudani

Eric Omondi apimana nguvu na Diamond Platnumz

Mchekeshaji huyo wa nchi ya Kenya anamtania mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz kwa kile ambacho anakitaja kuwa kushambulia Afrika mashariki kwa kupata wapenzi na watoto.

Eric anasema alimwonya Diamond kwamba atalipiza kisasi lakini hakuamini na kwamba anajua sasa ameshachoka kukimbizana na wapenzi analea watoto.

Diamond Platnumz ana watoto na wapenzi wake wa zamani kwenye nchi zote za Afrika mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania.

Nchini Kenya ana mtoto na msanii Tanasha Donna ambaye anaitwa Naseeb Junior kama yeye na siku yao ya kuzaliwa ni moja, ukienda Uganda ana Zari Hassan ambaye ana watoto wake wawili, Princess Tiffah na Prince Nillan na kwao Tanzania anayejulikana ni Hamissa Mobeto ambaye ana mtoto kwa jina Dillan.

Eric alitoa video inayomwonyesha akiwa na mwanamuziki na muigizaji wa Tanzania Gigy Money ambaye ni rafiki wa karibu wa Diamond Platnumz anapoanza kulipiza hatua ya Diamond ya kunyakua warembo Afrika Mashariki.

Wimbo ambao ametumia kwenye video hiyo ni “Kwaheri” ambao umeimbwa na Jua Cali na Sanaipei Tande ishara kwamba Gigy amehama Tanzania na kumwacha Diamond na kuja Kenya kwa Eric Omondi japo yote hayo ni uigizaji tu.

Kulingana na maneno, picha na video kutoka kwa Eric Omondi kwenye mitandao ya kijamii, Gigy Money na Betty Kyallo huenda wakawa wahusika kwenye awamu ya pili ya kipindi chake “Wife Material”.

Categories
Burudani

Khaligraph amshinda eric Omondi

Wasanii hao wawili mmoja wa muziki mwingine wa uchekeshaji na uigizaji wamekuwa wakitangaza kwa muda kuhusu pigano hilo la ndondi la leo tarehe 23 mwezi huu wa Februari mwaka huu wa 2021.

Na hii leo waliachilia video za pigano hilo lao ambapo Eric Omondi alishindwa na Khaligraph Jones lakini bado hataki kukubali kwamba alishindwa.

Wiki tatu zilizopita Eric alionekana akinunua jeneza na kuchimba kaburi vitu ambavyo angetumia kumzika Khaligraph baada ya kumshinda hii leo lakini mambo yamekwenda ndivyo sivyo.

Kulingana naye mwamuzi wa pigano lao alikuwa anampendelea mpinzani wake ambaye ni Khaligraph na kwamba Khaligraph alitumia mbinu ambazo hazikubaliki kwenye mchezo huo ndiposa akamshinda.

khaligraph ambaye aliamua kusalia kimya muda wote huo akifanya mazoezi anaonekana kufurahia ushindi wake huku akihimiza Eric achapishe video nzima ya pigani ili watu waone alivyomshinda.

Pigano hilo “Bomba Boxing Match” lilikuwa limedhaminiwa na kampuni ya ubashiri ya Kenya Charity Sweepstake.

Categories
Burudani

Shaffie Weru kulipia Tanasha deni

Mtangazaji Shaffie Weru ameahidi kulipia mwanamuziki Tanasha Donna deni analodaiwa na mpodozi wake. Shaffie anasema yeye na Tanasha ni marafiki wa karibu na anamtetea akisema huenda alishindwa kulipa deni hilo kwa sababu fulani ambayo hajafichua.

Weru ambaye alizungumza jana kwenye kipindi fulani cha mitandaoni, hata hivyo alisema kwamba atalipa deni hilo ikiwa halizidi shilingi elfu 20.

Kulingana naye, ameamua kulipadeni hilo sio kama rafiki ya Tanasha lakini kama mtu ambaye anaelewa hali ya sasa ya biashara ambapo wengi wanashindwa kulipia bidhaa na huduma kutokana na shida zilizoletwa na janga la Corona.

Habari kuhusu deni hilo zilitolewa hadharani na Dana De Grazia ambaye alikuwa akizungumza kwenye kipindi cha Eric Omondi. Kulingana naye, mtaalam huyo wa mapodozi ambaye ni rafiki yake amejaribu kupata pesa zake kutoka kwa Tanasha bila mafanikio.

Anasemekana kutoa huduma hizo za mapodozi wakati Tanasha alikuwa anaandaa video ya muziki lakini mpaka sasa hajalipwa.

Tanasha hajajibu madai hayo ya deni ila alionekana kucheka Dana na Eric kwani aliwasaidia kupata jambo la kuzungumzia kwenye kipindi hicho.

Categories
Burudani

Tanasha amjibu Dana

Jana tulikujuza kuhusu tuhuma za mwanadada aliyekuwa mtangazaji wa runinga ya Ebru Dana De Grazia dhidi ya mwanamuziki Tanasha Donna.

Dana alikuwa mgeni kwenye kipindi cha mchekeshaji Eric Omondi ambapo alidai kwamba Tanasha ana deni la rafiki yake ambalo hajalipa na linatokana na kazi ya mapodozi aliyomfanyia wakati wa kuunda video ya wimbo wake.

Eric Omondi hata hivyo alifuta video hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram na sasa Dana anadai kwamba sio yeye alimwomba Eric aifute bali ni Dona aliomba iondolewe.

Baadaye, Tanasha alipachika picha yake kwenye akaunti ya Instagram akiwa amevaa vazi refu na kuandika “Donna = Content” kuashiria kwamba jina lake linatumika kuendeleza kazi za waigizaji na wengine maarufu mitandaoni.

Wengine wanaona kwamba Bi. Dana ambaye aliwahi kuigiza kwa kipindi “Nairobi Diaries” anatumia tu jina la Tanasha Donna kujipatia umaarufu.

Aliondolewa kwenye kipindi hicho miaka minne iliyopita baada ya kuigiza kwenye msimu mzima wa vipindi kumi na tatu.

Hivi maajuzi, ameonyesha picha akiwa ameandika jina la Eric Omondi kwenye sehemu ya nyuma ya mapaja yake isijulikane kama maandishi hayo ni ya kusalia kwenye ngozi yake milele au ni ya kufutika.

Categories
Burudani

Tanasha ameanikwa!

Mwanamuziki Tanasha Donna wa Kenya amejipata pabaya baada ya aliyekuwa mtangazaji wa runinga Dana De Grazia anayejiita Hustle goddess kwenye mitandao ya kijamii kufichua kwamba ana deni la rafiki yake ambalo amekataa kulipa hadi sasa.

Akizungumza kwenye kipindi cha mitandaoni cha mchekeshaji Eric Omondi kiitwacho “Show kwa Choo” Dana alisema kwamba rafiki yake ambaye ni mtaalamu wa mapodozi alimfanyia kazi Tanasha wakati akitayarisha video yake ya muziki ya hivi karibuni.

Dana anasema hapendi watu ambao wanakosea marafiki wake wa karibu na ndio maana alikuwa ameamua kmsukuma kimfano Tanasha kwenye choo cha maji ambacho ndicho kiti kwenye kipindi hicho cha Eric Omondi.

Dana alisema pia kwamba hajali hata kama watu wa Tanzania watamuingilia kwa kujulikanisha jambo hilo kuhusu Tanasha Donna ambaye ana mtoto wa kiume na mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz.

Kwa sababu ya uhusiano wake na Diamond na kazi zake kama mwanamuziki na balozi wa bidhaa mbali mbali wengi hawafikirii kwamba Tanasha anaeza kuwa na deni la mtu.

Eric Omondi ndiye alipachika video hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram akisema anampigia simu Tanasha ambaye ni rafiki yake ili ajibu madai hayo lakini kufikia sasa amefuta video hiyo.

Dana De Grazia alishangaza wengi maajuzi baada ya kuandika jina la Eric Omondi kwenye upande wa nyuma wa miguu yake.

Categories
Burudani

Mercy Atis aingilia biashara ya chakula.

Mwanamuziki Mercy Atis ambaye alijipatia umaarufu kwa wimbo wake kwa jina “I don’t wonna know” sasa ameingilia biashara ya kuuza chakula tayari.

Ijumaa tarehe 5 mwezi Februari mwaka 2021 alifungua rasmi sehemu hiyo ya kuuzia chakula kwa jina “Motherland” huko Kitengela kaunti ya Kajiado karibu na Nairobi.

Kabla ya siku hiyo ya uzinduzi alikuwa ametangaza kwamba watu kadhaa maarufu walikuwa wameahidi kuhudhuria na kusaidia katika uzinduzi wa hoteli yake ambayo pia inauzwa vinywaji.

Alitaja mchekeshaji Eric Omondi ambaye alisema alikuwa ameahidi kufanya kazi kama mshereheshaji yaani MC bila malipo na Amina Rabar mtangazaji wa runinga kati ya wengine wengi.

Mchekeshaji Jalang’o kwa jina halisi Felix Odiwuor alisemekana kuwa na kazi nyingi hiyo ijumaa lakini akatoa ahadi ya kwenda kupata chakula cha mchana katika hoteli hiyo ya Motherland Jumatano wiki hii.

Atis amepata uungwaji mkono kutoka kwa watu wengi nchini Kenya na nje ya Kenya baada ya hadithi ya maisha yake kujulikana.

Alikuwa amekwenda nchini Marekani kwa nia ya kufanya kazi na kubadilisha maisha yake lakini akajikuta matatani na kukaa jela kwa muda wa miaka mitano na kisha kurudishwa Kenya bila chochote hata mavazi.

Anasema waliompeleka Marekani hawakutimiza ahadi ya kumsaidia kujiunga na chuo cha uuguzi akafanya juu chini akajiunga lakini akaacha tena kwani hangeweza kujilipia karo.

Baada ya hapo akajipata akiishi katika eneo moja la watu wasio na makazi nchini marekani katika eneo la California.

Babake alipoaga nchini Kenya, hangeweza kuhudhuria mazishi yake kwa hivyo akaomba ndugu zake wamtumie video ya mazishi.

Alitumiwa video hiyo na wakati mmoja akakuta wenzake aliokuwa akiishi nao wakitazama video hiyo huku wakimcheka, wakamsukuma nje wakafunga mlango.

Mercy alichukua hatua ya kuwacha moto nje ya mlango huo ambao ulilazimisha wenzake kumfungulia na kuuzima na ndipo alikamatwa kwa kosa la kuharibu mali kwa moto.

Mwanadada huyo anakumbuka na kushukuru wote ambao wamekuwa wakimsaidia tangu arejee nchini Kenya na sasa anaweza kujisimamia.

Mfanyibiashara wa Saluni kwa jina Diana Aketch ambaye wakati fulani alimwalika Mercy Atis kazini kwake na kumpa sura mpya naye alihudhuria shughuli ya kufungua mkahawa huo.

Binti ya Diana Sketch, Mercy Atis, Diana Aketch na mwenzao

Categories
Burudani

Eric Omondi amtetea Churchill

Mchekeshaji Eric Omondi amejitokeza kumtetea Daniel Ndambuki maarufu kama Churchill kutokana na shutuma dhidi yake kuhusiana na wachekeshaji ambao wamewahi kutumia jukwaa lake na kukosa kuendelea.

Omondi ambaye alikuwa akihojiwa kwenye kituo kimoja cha redio alisema ni lazima mchekeshaji afungue macho afikirie zaidi ili anufaike na fursa ya kuonekana kwenye kipindi cha Churchill.

Alisimulia kwamba wakati fulani, wachekeshaji waliitisha mkutano na Churchill wakitaka kwamba waongezewe marupurupu ya kuwa kwenye kipindi chake kwani wanaona yeye anaendelea ananunua magari mazuri ilhali wao hawana chochote.

Kulingana naye, mkutano huo ulikwisha hata kabla uanze kwani alimuuliza Dan Ndambuki mbele ya hao wachekeshaji ikiwa aliwahi kumlipa hata shilingi moja akiwa mmoja wa wachekeshaji wa kipindi chake ambapo Churchill alikana.

Omondi alisema kwamba alijua jukwaa la Churchill lingemwezesha kusonga mbele maishani kwa hivyo anahimiza wachekeshaji wengine wajikakamue ili waweze kupata kazi zingine huku nje kutokana na kazi yao kwenye kipindi cha Churchill.

Huku haya yakijiri, Omondi ameshangaza wengi baada ya kununua jeneza na kuchimba kaburi ambalo anasema atamzika mwanamuziki Khalighraph Jones.

Kulingana na matangazo kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii, wawili hao watakuwa na shindano la ndondi tarehe 23 mwezi huu wa Februari mwaka 2021.

OG kwa upande wake anaendeleza tu mazoezi kimya kimya.

Categories
Burudani

Shosholites, Eric Omondi

Baada ya kumalizana na kipindi cha awali ambacho kilichanganya wengi kwa jina “Wife Material” muigizaji Eric Omondi amezamia kingine kwa jina “Shosholites”.

Kwenye wife material alihusisha mabinti wengi wakidhani kwamba kweli alikuwa akitafuta mke kikweli. Alichagua binti mmoja mwimbaji katika Band Beca mpaka wakafunga arusi ambayo wengine walidhania ni ya ukweli ila yote yalikuwa maigizo tu.

Kwa muda sasa, Eric omondi amekuwa akiachilia picha na video zinazoonyesha kina mama wazee ambao wanajaribu mitindo ya kisasa ambayo inachukuliwa na wengi kuwa ya wanawake wa umri mdogo kama vile kujipodoa.

Kwenye maelezo ya hizo picha na video Eric alionekana kuhimiza wafuasi wake kumtumia video za nyanya zao wakifanya mambo yasiyo ya kawaida kwa umri wao na huenda wakajishindia hela.

Mshindi atapatiwa laki moja, atakayeibuka wa pili atajinyakulia shilingi elfu hamsini, wa tatu elfu thelathini na nambari nne atapatiwa majani chai ya mwezi mzima na kampuni ya Old Farm.

Kampuni hiyo ya Old Farm Tea ndiyo inadhamini kipindi hicho cha Eric Omondi kwa jina Shosholites ambacho kinazinduliwa leo kwenye akaunti ya Eric Omondi ya Youtube.

Kulingana naye, hili litakuwa shindano la kipekee la talanta.

Eric Omondi na wachekeshaji wengine wanaonekana kugeukia mitandao ya kijamii ili kuendeleza fani yao kutokana na masharti mengi ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya korona.

Masharti hayo yamepiga marufuku mikutano mikubwa na ile ya usiku maanake kuna kafyuu ya saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri.

Lakini maajuzi yeye na Mc Jessy wametumbuiza nchini Tanzania ambapo hakuna masharti makali baada ya serikali nchini humo kutangaza mwaka jana kwamba ugonjwa wa Covid 19 ulikuwa umeisha.