Categories
Kimataifa

Afueni kwa Trump baada ya Bunge la Seneti kupungukiwa na kura za kumshitaki

Bunge la Seneti la Marekani limekosa kufikisha thuluthi mbili ya kura ili kumshitaki aliyekuwa rais wa taifa hilo Donald Trump kwa kosa la kuchochea uvamizi wa majengo ya bunge ya Capitol tarehe 6 mwezi Januari.

Maseneta 57 walipiga kura ya kumshitaki Trump, wakiwemo saba wa chama cha Republican, huku 43 wakipinga hoja hiyo.

Kura hiyo ilikosa uungwaji mkono wa maseneta 10 kufikisha angalau kura 67 zilizohitajika kumshitaki Trump.

Baada ya kuondolewa  kesi hiyo, Trump alitoa taarifa akishutumu jaribio hilo, akisema ni jaribio baya zaidi la kutaka kumpata na makosa kiongozi wa taifa katika historia ya taifa hilo.

Hii ilikuwa mara ya pili ya jaribio la kumshitaki Trump.

Iwapo angeshitakiwa, basi hangeweza tena kuwania wadhifa wowote katika Bunge la taifa hilo.

Baada ya kura hiyo, seneta mwandamizi wa bunge la Seneti wa chama cha Republican Mitch MacConnel alisema Trump alichochea uvamizi wa bunge na wafuasi wake na kukitaja kitendo hicho kuwa cha fedheha na utepetevu wa majukumu.

Awali, alipiga kura kupinga kesi hiyo akiitaja kuwa ukiukaji wa katiba kwa kua sasa Trump si kiongozi wa taifa hilo.

Hata hivyo alisema bado Trump anaweza kuwajibishwa na mahakama.

Categories
Kimataifa

Huenda Trump akazuiwa kushikilia wadhifa wa umma

Kesi ya kutaka kumzuia Donald Trump kushikilia wadhifa wowote wa umma kuhusiana na wajibu wake katika ghasia zilizoghubika Jumba la Capitol imepangiwa kuanza juma lijalo kwenye bunge la Seneti, kulingana na wajumbe wa chama cha Democratic.

Siku ya Jumatatu, Bunge la congress litawasilisha uamuzi wake kwa bunge la Seneti, na hivyo kutoa nafasi kwa mjadala katika Bunge hilo lenye viti 100.

Ma-seneta wa chama cha Republican walikuwa wamewasilisha ombi la kuchelewesha mjadala huo, ili wapate fursa ya kujiandaa.

Trump alisafiri hadi Florida baada ya muhula wake kutamatika siku ya Jumatano, huku akikosa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Joe Biden.

Juma lililopita bunge la Congress liliamua kumuwajibisha Trump kuhusiana na ghasia zilizokumba Jumba la Capitol, na hivyo kutoa fursa ya kujadili swala hilo kwenye bunge la Seneti.

Ikiwa atapatikana na hatia,Trump huenda akazuiwa kushikilia wadhifa wowote wa umma siku zijazo.

Seneta maarufu wa chama cha Democratic Chuck Schumer alisema leo kwamba bunge hilo lipokea Jumatatu rufaa ya kumjadili Trump.

Na iwapo chama cha Democratic, ambacho kilitwa uthibiti wa Seneti juma hili, hakitabadili sheria, inamaanisha  mjadala dhidi ya Trump utaanza siku ya Jumanne.

Categories
Habari

Eric Kneedler ndiye balozi mpya wa Marekani hapa nchini

Eric Kneedler ndiye balozi mpya wa Marekani hapa nchini. Uteuzi wake ulitangazwa muda mfupi baada ya kuapishwa kwa Joe Biden kuwa Rais wa 46 wa Marekani.

Baada ya uteuzi wake, Kneedler alitoa wito wa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Kenya na Marekani hususan katika maswala ya  usalama,afya, elimu na biashara.

Kneedler anachukua mahala pa Kyle McCarter aliyejiuzulu wadhifa huo baada ya Donald Trump kuondoka wadhifa wa Rais wa Marekani.

Kulingana na afisi ya ubalozi wa Marekani hapa nchini, Kneedler awali alihudumu wadhifa wa naibu wa mkuu wa ujumbe katika balozi ya Marekani jijini Nairobi kuanzia mwezi Aprili mwaka 2019 hadi mwezi January mwaka 2021.

Kneedler alianza majukumu yake Jijini Nairobi mwaka 2017 akiwa mshauri wa maswala ya kisiasa.

Wadhifa huo wa mshauri wa maswala ya kisiasa pia aliushikilia katika ubalozi wa Marekani huko Manila na naibu wa mshauri wa kisiasa katika ubalozi wa Marekani Bangkok.

Kneedler ana shahada kutoka chuo cha Pomona na uzamili ya maswala ya kimataifa kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Categories
Kimataifa

Rais mpya wa Marekani Joe Biden aanza kazi rasmi kwa mageuzi ya sheria

Rais wa Marekani Joe Biden ameanza kazi rasmi kwa kutangua baadhi ya sera za aliyekuwa rais wa nchi hiyo anayeondoka Donald Trump, saa chache baada ya kuapishwa.

Amesema hakuna muda wa kupoteza kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa hilo.

Biden ametia saini miswada 15 ya sheria, za kwanza zikiwa kuimarisha uwezo wa majimbo ya taifa hilo kupambana na athari za ugonjwa wa COVID-19.

Nyingine zinanuiwa kufutilia mbali baadhi ya sera za utawala wa Trump hasa kuhusu mabadililko ya hali ya hewa na uhamiaji.

Biden tayari ameanza kutekeleza majukumu yake muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani.

Sherehe ya kuapishwa kwa Biden ilikuwa ya aina yake, huku vizuizi kadhaa vikiwekwa kutokana na janga la COVID-19 na watu wachache wakiruhusiwa kuhudhuria sherehe hiyo.

Aidha sherehe ya viapo ilihudhuriwa na watu wachache kinyume cha ilivyokuwa awali.

Trump, ambaye kufikia sasa hajawahi kukubali kushindwa, hakuhudhuria sherehe hiyo na hivyo kubeza desturi ambayo imedumu kwa muda mrefu katika historia ya taifa hilo.

Categories
Kimataifa

Trump aondoka katika Ikulu ya Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ameondoka katika Ikulu ya Marekani akiwa ameandamana na mkewe Melania Trump saa chache kabla ya kuapishwa kwa Rais mteule Joe Biden.

Rais huyo na mkewe walielekea katika kambi ya kijeshi iliyoko Maryland ambapo sherehe za mwisho za kuwaaga zilipangiwa kuandaliwa.

Hata hivyo makamu wa Rais, Mike Pence hatahudhuria sherehe za kumuaga Trump lakini anatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Biden na Harris baadae Jumatano.

Rais Trump akiwahutubia wafuasi wake aliwatakia mafanikio Rais mteule Joe Biden na makamu wake Kamala Harris licha ya kuwa hakuwataja wawili hao kwa majina.

Alisema akiwa katika ikulu ya Marekani aliafikia mengi licha ya janga la Covid-19 kuathiri kipindi cha miezi tisa iliyopita cha utawala wake

Vifo vilivyotokana na Covid-19 nchini humo sasa ni zaidi ya 400,000, na idadi ya vifo imeendelea kuongezeka.

Rais Mteule Joe Biden na makamu wake Kamala Harris wanatarajiwa kuapishwa baadaye Jumatano katika hafla itakayoongozwa na jaji mkuu John Roberts.

Sherehe ya kuapishwa kwa Biden itahudhuriwa na marais wa zamani Barack Obama,Bill Clinton na George W Bush.

Biden atakuwa rais wa Marekani wa 46.

Categories
Kimataifa

Vitengo vya usalama nchini Marekani kukabiliana na maandamano mapya ya wafuasi wa Trump

Maafisa wa usalama nchini Marekani wamejiandaa kukabiliana na msururu wa maandamano ya wafuasi wa Rais Donald Trump.

Inadaiwa kuwa wafuasi hao wamepanga kufanya maandamano katika siku zilizosalia kabla ya kuapishwa kwa Rais Mteule Joe Biden tarehe 20 mwezi huu.

Majimbo kadhaa yakiwemo California, Michigan, Pennsylvania, Kentucky na Florida yameweka maafisa wa usalama kwenye hali ya tahadhari ili kukabiliana na maandamano hayo.

Maafisa katika jimbo la Washington DC pia wameajiandaa kwa ghasia hizo baada ya tukio la tarehe sita mwezi huu ambapo wafuasi wa Rais Trump walivamia majengo ya bunge.

Usalama umeimarishwa baada ya shirika la upelelezi la FBI kuonya vitengo vya usalama kuhusu kutokea kwa wimbi jipya la maandamano katika majimbo yote 50 nchini Marekani hadi siku ya ambayo Biden ataapishwa.

Wataalamu wanadai kuwa maandamano hayo yatakuwa makali zaid katika majimbo ya Wisconsin, Michigan, Pennsylvania na Arizona.

Vuguvugu moja linalojiiita “Boogaloo” limetangazwa kuwa litaandaa maandamano katika majimbo yote 50.

Categories
Kimataifa

Trump akabiliwa na tishio la kung’atuliwa mamlakani tena

Bunge la Marekani huenda likapiga kura Jumanne kuhusu azma ya kumng’oa Rais Donald Trump mamlakani, kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa chama cha Democratic.

Wabunge wa chama hicho wamepania kuchukua hatua hiyo kwa misingi kwamba matamshi ya Trump yalichochea ghasia na uvamizi uliofanywa katika jengo la Capitol Hill ambao pia ulisababisha vifo vya watu watano.

Kiranja wa Bunge hilo James Cyburn anasema kuwa hatua zitachukuliwa wiki hii kutokana na kisa hicho.

Hata hivyo huenda wabunge hao wasiwasilishe kifungu kuhusu mchakato huo katika Bunge la Seneti hadi baada ya siku 100 za utawala wa Joe Biden.

Muda huo utampa fursa Biden kuliunda baraza lake jipya la mawaziri na kuzindua sera mpya, zikiwemo za kukabiliana na janga la COVID-19.

Trump hajatoa matamshi yoyote rasmi tangu alipong’atuliwa kutoka mitandao ya kijamii, hasa ule wa Twitter, siku ya Ijumaa.

Hata hivyo taarifa kutoka Ikulu ya White House zilisema kuwa Rais Trump atafanya ziara huko Texas siku ya Jumanne na kuzuru eneo la mpaka wa nchi hiyo na Mexico, ambako aliamuru kujengwa ukuta wakati wa utawala wake ili kuzuia uhamiaji haramu.

Categories
Kimataifa

Trump asema yuko tayari kwa mpito wa amani

Rais wa Marekani Donald Trump ameelezea kujitolea kwake kuondoka afisini kwa njia ya amani.

Huku akisema utawala mpya utaapishwa tarehe 20 Januari, Rais huyo wa chama wa Republican alihimiza kuwepo maridhiano.

Trump  alisema alighadhabishwa na ghasia, uvunjaji sheria na machafuko yaliyoshuhudiwa  ya siku ya Jumatano na kwamba ni muhimu kutuliza hisia na kurejesha utulivu.

Licha ya kuwa matamshi hayo ya Trump hayakugusia madai yake ya awali kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu, yaliashiria kukubali kwake kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Urais ulioandaliwa tarehe 3 mwezi Novemba mwaka jana.

Hotuba hiyo ya Trump kwa njia ya video ilichapishwa kwenye ukrasa wake wa tweeter, ambao ulifufuliwa siku ya alhamisi baada ya kufungwa kufuatia ghasia hizo wakati wa kikao cha pamoja cha Mabunge ya taifa hilo.

Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu wanne na wengine 68 kutiwa nguvuni.

Hayo yalijiri huku wapinzani wa Rais huyo anayeondoka katika mabunge yote mawili ya Marekani wakitoa wito wa kuondolewa kwake ofisini kufuatia uvamizi wa bunge na kundi la wafuasi wake.

Seneta Chuck Schumer wa chama cha Democratic alisema Trump anapaswa kuondolewa ofisini mara moja.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge Nancy Pelosi alisema iwapo hatang’atuka huenda akaondolewa kwa nguvu.

Hata hivyo kuondolewa kwa Trump kutahitaji usaidizi wa wajumbe wa chama cha Republican na hadi sasa ni wachache tu ambao wameunga mkono hatua hiyo. Katika hotuba yake kwa njia ya video,

Categories
Kimataifa

Watu 4 wafariki baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge

Maafisa wa polisi Jijini Washington DC wamethibitisha kuwa watu wanne wamefariki baada ya wafuasi wa Rais Donald Trump kuvamia ukumbi wa kikao cha kuidhinishwa kwa Joe Biden kuwa Rais mpya wa Marekani.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimearifu kwamba mwanamke aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa uvamizi huo alikuwa mkaazi wa San Diego, Ashli Babbitt, ambaye aliwahi kuhudumu katika jeshi la wana-anga la nchi hiyo.

Hadi sasa, zaidi ya watu 52 wametiwa nguvuni, – 47 kati yao kwa ukiukaji wa sheria za kafyu.

Afisa mmoja wa usalama alisema vifaa viwili vilivyoshukwia kuwa vilipuzi vilipatikana na kuteguliwa na maafisa wa FBI kwa kushirikiana na polisi.

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameshtumu vikali uvamizi huo wa wafuasi wa Donald Trump kwenye bunge la Congress,  huku akimtaka Rais huyo anayeondoka “kujitokeza hadharani” na kukashfu ghasia hizo.

Trump, ambaye  alikuwa amehimiza waandamanaji hao kuelekea kwenye bunge la Congress, baadaye aliwashauri kurudi nyumbani.

Katika matukio ya kushangaza yaliyopeperushwa moja kwa moja kwa njia ye televisheni kote duniani, uvamizi huo ulifanya wajumbe katika bunge la Congress kujificha chini ya viti huku milio ya risasi na vitoza machozi ilisikika.

Kikao cha pamoja cha kuidhinisha ushindi wa Joe Biden tayari kimerejelewa baada ya kusitishw akutokana na vurumai hilo.

Rais Donald Trump amekataa kukubali kushindwa na Biden katika uchaguzi mkuu ulioandaliwa tarehe 3 November mwaka jana huku akidai uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu bila kutoa ushahidi wowote.

Categories
Kimataifa

Trump aonywa dhidi ya kutumbukia mtegoni kuhusu madai ya vita kati ya Marekani na Israeli

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amemhimiza Rais wa Marekani Donald Trump asiangukie mtego kuhusu madai ya njama ya Israeli ya kuzusha vita kwa kushambulia vikosi vya Marekani nchini Iraq.

Alitoa onyo hilo wakati wa maadhimisho ya mauaji yaliyotekelezwa na Marekani nchini Iraq ya Jenerali Qassem Soleimani wa Iran kwa shambulizi la ndege isiyoendeshwa na rubani.

Israeli haikutoa maoni mara moja kuhusu madai hayo.

Marekani inawalaumu wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya mizinga katika vituo vya Marekani nchini Iraq, ikiwa ni pamoja na shambulizi lililotekelezwa karibu na Ubalozi wa Marekani.

Ujasusi wa hivi punde kutoka Iraq unadokeza kuwa maajenti wa Israeli wanapanga njama ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani ili kuchochea vita na Marekani.

Afisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na wizara ya mashauri ya kigeni ya Israeli hazijatoa maoni kuhusu madai hayo.