Categories
Kimataifa

Nitatoka White House baadaye, Trump alegeza msimamo

Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kuondoka kwenye Ikulu ya White House iwapo Joe Biden atathibitishwa kirasmi na jopo la waamuzi kuwa Rais mpya.

Kufikia sasa Rais huyo hajakubali kushindwa kwenye uchaguzi wa Urais wa tarehe 3 mwezi huu.

Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba itakuwa vigumu kukubali matokeo ya uchaguzi huo yanayoashiria kwamba alishindwa na mpinzani wake Biden wa chama cha Democratic.

Kwa mara nyingine, amekariri madai ambayo hayajathibitishwa kuwa kulikuwa na udanganyifu wa kura kwenye uchaguzi huo.

Biden alimshinda Trump kwa kura 306 dhidi ya 232 chini ya mfumo wa jopo la waamuzi ambao hutumiwa kumchagua Rais wa Marekani.

Kura hizo zilizidi 270 ambazo mwaniaji anahitaji ili kutangazwa mshindi wa Urais kwa mujibu wa mfumo wa uchaguzi nchini humo.

Aidha, Biden alimshinda Trump kwa zaidi ya kura million sita za kawaida.

Jopo hilo la waamuzi litakutana mwezi ujao kuidhinisha rasmi matokeo hayo, huku Joe Biden akipangiwa kuapishwa tarehe 20 Januari.

Rais Trump na wafausi wake wamewasilisha kesi kadhaa mahakamani kuhusiana na uchaguzi huo, lakini nyingi kati yazo zimetupiliwa mbali.

Mapema wiki hii, Trump alikubali hatimaye kuruhusu shughuli za kuwaapisha maafisa wapya wa baraza la Biden baada ya sintofahamu iliyodumu kwa wiki kadhaa.

Categories
Kimataifa

Joe Biden ahimiza utulivu msimu wa baridi unapoghubika Marekani

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kudumishwa kwa amani  nchini humo hasa wakati huu wa msimu wa baridi unaondamana na msambao wa  virusi vya  Corona.

Kwenye hotuba ya kuadhimisha likizo ya kutoa shukrani,Biden alisema  sasa ni wakati wa kupambana na virusi vya Corona na siyo kugawanyika.

Aliwahimiza raia wa nchi hiyo kuzingatia maagizo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Hayo yanajiri huku Rais Donald Trump akiwahimiza wafuasi wake kufanya kila juhudi kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais nchini humo.

Akiongea kwa njia ya simu kutoka ikulu ya White House wakati wa hafla ya wabunge wa chama cha Republican huko  Pennsylvania, Trump alirejelea madai yake kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari tele.

Trump alikuwa ametarajiwa kuhudhuria hafla hiyo lakini akaahirisha safari hiyo baada ya wandani wawili wa wakili wake Rudy Giuliani kuambukizwa virusi vya Corona, lakini Giuliani alihudhuria hafla hiyo.

Juhudi za Rais Trump za kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo zimegonga mwamba katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo.

Categories
Kimataifa

Trump ahimizwa na rafikiye akubali kushindwa

Rafiki wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump amemhimiza rais huyo aachane na harakati za kupinga ushindi wa rais mteule Joe Biden.

Chris Christie, aliyewahi kuwa Gavana wa jimbo la New Jersey amelitaka kundi la kampeini la Trump kusitisha kile alichokitaja kuwa fedheha ya kitaifa.

Rais Trump amekataa kukubali kwamba alishindwa kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika hivi majuzi nchini Marekani kwa madai ambayo hayajathibitishwa kwamba kulikuwa na visa vya udanganyifu.

Wafuasi wengi wa chama cha Republican wameunga mkono juhudi hizo za Trump za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Siku ya Jumamosi, juhudi za Trump zilipata pigo wakati Jaji katika jimbo la Pennysylvania  alipotupilia mbali kesi iliowasilishwa na Trump ya kutaka kubatilisha maelfu ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta katika jimbo hilo.

Categories
Kimataifa

Masaibu ya Trump yazidi baada ya mahakama kutupilia mbali kesi dhidi ya kura za Pennyslvania

Jaji mmoja katika Jimbo la Pennyslvania nchini Marekani ametupilia mbali kesi ya maafisa wa kampeini wa Rais Donald Trump ya kutaka kuharamishwa kwa mamilioni ya kura  zilizopigwa kwa njia ya posta katika jimbo hilo muhimu.

Jaji Mathew Brann alisema kuwa madai ya kuwepo kwa udanganyifu kwenye shughuli hiyo hayana msingi wowote.

Hatua hiyo inafungua njia kwa serikali ya jimbo hilo kuthibitisha kura na ushindi wa Rais Mteule Joe Biden katika jimbo hilo muhimu, ambapo alimshinda mpinzani wake Trump kwa  zaidi ya kura 80,000.

Hili ni pigo la hivi punde kwa Rais Trump ambaye anajaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 3 mwezi Novemba.

Hadi sasa Ris Trump amekataa  kushindwa kwenye uchaguzi huo kwa madai kwamba kulifanyika udanganyifu na wizi wa kura kwenye shughuli hiyo.

Hata hivyo hajatoa ushahidi wowote kuthibitiha madai hayo.

Hali hiyo imechelewesha mchakato ambao hufuatwa baada ya kufanywa uchaguzi wa urais nchini Marekani.

Categories
Kimataifa

Pigo kwa Trump huku wabunge wa Michigan wakidinda kubatilisha ushindi wa Biden

Rais Donald Trump amepata pigo jingine kwenye azma yake ya kupinga matokeo ya kura za urais nchini Marekani baada ya wabunge katika jimbo la Michigan kusema hawana nia ya kushinikiza kubatilishwa kwa ushindi wa Joe Biden katika Jimbo hilo.

Wabunge wawili wa chama cha Republican wameahidi kufuata utaratibu uliowekwa kubaini kura hizo baada ya mkutano ulioandaliwa katika ikulu ya white house.

Siku ya Ijumaa, Rais Trump alipata pigo katika jimbo la Georgia baada ya jimbo hilo kubaini ushindi wa Biden.

Biden wa chama cha Democrat anatarajiwa kuchukua hatamu za kuiongoza Marekani tarehe 20 Januari mwakani akiwa rais wa 46 wa taifa hilo.

Biden alishinda kwenye uchanguzi huo kwa kuzoa kura 306 za majimbo dhidi ya kura 237 za rais Trump.

Kura za majimbo ndizo hutumiwa kubaini mshidi wa urais nchini Marekani ambako mgombeaji anahitaji kupata kura 270 au zaidi kutangazwa rais mteule.

rump ambaye hajaonekana hadharani mara kwa mara tangu tangu uchaguzi wa tarehe-3 mwezi huu jana alidai kwa mara nyingine kuwa yeye ndiye mshindi kwenye uchaguzi huo.

Trump amedai kuwepo kwa kwa udanganyifu mkubwa kwenye uchanguzi huo japo hajathibitisha madai hayo

Categories
Burudani

Lil Wayne akabiliwa na tishio la kufungwa jela

Mwanamuziki wa Marekani wa mtindo wa rap Dwayne Michael Carter Jr maarufu kama Lil Wayne huenda akahukumiwa kifungo cha hadi miaka kumi gerezani kwa kosa la kupatikana na silaha hata baada yake kushtakiwa kwa kosa sawia awali.

Haya yalibainika jumanne katika mahakama moja ya Florida.

Tarehe 23 mwezi Disemba mwaka 2019 polisi walifanya msako kwenye ndege ya kibinafsi ya mwanamuziki huyo na kupata bastola na risasi kwenye mizigo yake. Alipatikana pia na dawa za kulevya ila hajashtakiwa kwa hilo.

Polisi hao pia waliripoti kwamba Wayne alionekana mlevi kutokana na jinsi alikuwa akizungumza na kushindwa kufungua macho vizuri wakati wa msako huo wa mwaka jana.

Wakili wa Lil Wayne Howard Srebnick hata hivyo amethibitisha kwamba mwanamuziki huyo hajakamatwa na hakujatolewa maagizo ya kumtia mbaroni. Kulingana naye hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba mteja wake alikuwa ananuia kutumia silaha hiyo.

Wayne naye alijitetea akisema bastola hiyo ilikuwa zawadi aliyokabidhiwa kwenye siku ya kusherehekea kina baba ulimwenguni. Wayne anatarajiwa kufika mahakamani tareje 11 mwezi Disemba mwaka huu.

Yapata miaka kumi iliyopita, Lil Wayne alishtakiwa huko New York kwa kosa la silaha na akafungwa jela kwa muda wa miezi nane. Sheria ya Amerika, inazuia wakosaji kumiliki silaha.

Siku chache kabla ya uchaguzi wa Urais nchini Marekani, Lil Wayne alijitokeza na kuunga mkono Rais Donald Trump hatua ambayo ilisababisha mpenzi wake ambaye ni mwanamitindo kwa jina Denise Bodot amuache.

Categories
Kimataifa

Trump amfuta kazi afisa wa kukabiliana na uhalifu wa kimtandao Chris Krebs

Rais wa Marekani Donald Trump amesema amemwachisha kazi afisa wa ngazi za juu wa uchaguzi aliyepinga madai ya rais huyo kwamba uchaguzi wa urais nchini humo ulikumbwa na wizi wa kura.

Afisa mkuu wa shirika la kukabiliana na uhalifu wa kimtandao nchini humo Chris Krebs aliachishwa kazi kufuatia kile Trump alichotaja kuwa madai yasiyo ya kweli kuhusu uadilifu wa uchaguzi huo.

Trump amekataa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi huo na ametoa madai ambayo hayajathibitishwa kwamba ulikumbwa na wizi mkubwa wa kura.

Maafisa wa uchaguzi hata hivyo wamekanusha madai hayo. Krebs ndiye afisa wa serikali kuachishwa kazi hivi majuzi kufuatia kushindwa kwa Trump.

Waziri wa ulinzi Mark Esper pia aliachishwa kazi huku kukiwa na tetesi kwamba Trump alitilia shaka uaminifu wake.

Wadadisi wanakadiria kwamba kabla ya kuondoka afisini, Trump atawaachisha kazi mkurugenzi wa shirika la ujasusi, CIA, Gina Haspel na mwenzake wa FBI Christopher Wray.

Categories
Burudani

Kanye West bado yuko nchini Marekani

Mwanamuziki Kanye West wa nchi ya Marekani alionekana hivi maajuzi akifika kwenye studio yake ya kurekodi muziki iliyoko katika eneo la Calabasas, Los Angeles.

Kanye alikuwa ametishia kuhama nchi ya Marekani ikiwa mshauri wake wa maswala ya siasa ambaye ni Rais Donald Trump angeshindwa kwenye uchaguzi.

Kufikia sasa, matokeo ya uchaguzi nchini Marekani yanaonyesha kwamba Rais Trump ameshindwa na mwaniaji wa chama cha Democrat Joe Biden ingawaje hajakubali rasmi ushinde huo.

Mume huyo wa mwanamitindo Kim Kardashian, naye alikuwa kwenye kinyanganyiro cha Urais nchini Marekani ambapo alijizolea kura elfu sitini kwenye majimbo 12 baada ya jina lake kuondolewa kwenye karatasi za kura kwenye majimbo mengine kwa kukosa kutimiza masharti.

Kanye huwa na tatizo la msongo wa mawazo ambalo husababisha aseme na kufanya mambo kwa njia isiyoeleweka na baadaye kubadilika.

Watu wa karibu kwa mke wake Kim Kardashian wanasema Kim hawezi kukubali kuhama Marekani na watoto wake kwani huko ndiko wamezoea. Duru hizo pia ziliarifu kwamba Kim amezoea matendo ya mume wake na anajua atabadili msimamo huo baadaye.

Taarifa zingine zinaonyesha kwamba Kanye alikuwa na matumaini ya kupata kazi ya Uwaziri kwenye serikali ya Donald Trump muhula wa pili ili ajitayarishe kuwania Urais mwaka 2024.

Kwa vile yote hayo yanaonekana kugonga mwamba, Kanye anahisi Marekani hakukaliki. Inasubiriwa kuona hatua ambayo mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwanasiasa atachukua siku za usoni.

Categories
Kimataifa

Obama atoa wito wa kusitisha migawanyiko Marekani

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama amesema taifa hilo linahitaji kubadili tamaduni ya dhana za hujuma ambazo zimezidisha migawanyiko nchini humo.

Kwenye mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, Obama amesema kuwa Marekani imegawanyika kuliko ilivyokuwa miaka minne iliopita.

Kulingana na Obama, migawanyiko hiyo imedhihirika wakati Donald Trump aliposhinda uchaguzi wa urais.

Amesema kwamba ushindi wa Joe Biden kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2020 ni mwanzo wa juhudi za kuliunganisha tena taifa hilo.

Obamba amesema kuliunganisha taifa hilo hakuwezi kuachiwa wanasiasa, bali kunahitaji pia mabadiliko ya kimuundo na watu kusikilizana na kukubaliana kabla ya kuzua malumbano.

Hata hivyo Obama amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya kihisia ya kizazi kijacho, vijana hawana budi kuwa na matumaini kwamba mambo yatabadilika na kwamba sharti wawe sehemu ya mabadiliko hayo.

Categories
Kimataifa

Uchaguzi wa Marekani uliokamilika watajwa kuwa salama zaidi katika historia ya nchi hiyo

Maafisa wa uchaguzi nchini marekani wamesema kuwa uchaguzi wa mwaka huu wa urais nchini humo ndio uliokuwa salama zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Maafisa hao aidha walipinga madai ya Rais Donald Trump kwamba  uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

Kamati hiyo ilitangaza  kwamba hakukuwa na ushahidi wowote kwamba mtambo wowote wa uchaguzi ulifuta au kupoteza kura, kubadili kura au kuvurugwa kwa njia yoyote ile.

Trump alidai kwamba kura zake milioni 2.7 zilifutwa kwenye uchaguzi wa wiki iliyopita bila kutoa ushahidi.

Hajakiri kushindwa na mwaniaji wa chama cha Democratic, Joe Biden aliyetangazwa mshindi.

Rais mteule Joe Biden aliimarisha ushindi wake kwenye uchaguzi huo kwa kushinda katika jimbo la Arizona Alhamisi jioni.

Ushindi wa Biden huko  Arizona umempa mwaniaji huyo kura 290 za taasisi ya uchaguzi ambazo hubaini mshindi kumaanisha ana zaidi ya kura 270 zinazohitajika kushinda.