Waamuzi wawili wa humu nchini Dkt Peter Waweru Kamaku na Gilbert Cheruiyot wameteuliwa kusimamia makala ya 6 ya fainali za kombe la CHAN nchini Cameroon kuanzia Jumamosi Januari 16 mwaka huu.
Dkt Waweru ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Kilimo na Teknolojia JKUAT ni miongoni mwa marefa 18 wa katikati ya uwanja walioteuliwa kusimamia mechi 32 za dimba la CHAN ikiwa mara ya pili kupewa jukumu hilo na shirikisho la soka Afrika Caf ,baada ya kusimamia fainali za AFCON mwaka 2019 nchini Misri pia kwa mara ya kwanza.
Waweru ni mhadhiri wa Applied Mathematics katika chuo kikuu cha JKUAT na pia ni mkurugenzi wa michezo katika chuo hicho .
Dkt WaWeru pia alisomea katika chuo hicho pia akachezea timu ya soka ya JKUAT kando na kuwa kiongozi wa michezo katika muungano wa wanafunzi JKUSO mwaka 2005 .
Kufikia sasa mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 39 amesimamia mechi 12 za kimataifa barani Afrika zikiwemo mechi za kombe la shirkisho la Caf baina ya vilabu,ligi ya mabingwa Caf,kombe la Afccon kwa chipukizi, mechi za kirafiki ,mechi za kufuzu kombe la Afcon kwa chipukizi na pia alisimamia mechi ya kombe la AFCON mwaka 2019 nchini Misri baina ya Ivory Coast dhidi ya Namibia akiwa miongoni mwa waamuzi 27 wa kati kati ya uwanja .
Katika mechi 12 za kimataifa alizosimamia Dkt Waweru ametoa kadi 20 za manjano na mbili nyekundu.
Kwa upande wake Gilbert Cheruiyot atakuwa mmoja wa marefa wasaidizi 17 kusimamia fainali za Chan nchini Cameroon, baada pia ya kusimamia mechi ya AFCON mwaka 2019 nchini Misri na itakuwa mara ya pili kusimamia mechi za Chan baada ya kuwa refa wa katikati ya uwanja mwaka 2016 nchini Rwanda.