Categories
Habari

Rais Kenyatta awataka viongozi wa kidini kukemea maovu nchini

Rais Uhuru Kenyatta amewahimiza viongozi wa kidini kuzungumza wazi kuhusu mienendo na vitendo visivyofaa vinavyohujumu maendeleo humu nchini.

Rais amesema ni kupitia ushirikiano wa Wakenya wote, wakiwemo viongozi wa kidini, ambapo nchi hii itaweza kushinda maovu kama vile ufisadi ambao ameutaja kama kikwazo kikuu cha maendeleo.

“Zungumzeni wazi wazi dhidi ya maovu yote yanayorudisha taifa hili nyuma. Jukumu letu katika ujenzi wa taifa ni ushirikiano; sote tunahudumia watu wale wale. Sisi tunashughulikia maswala ya fizikia ya wananchi na nyinyi mnawapa lishe la roho,” amesema Rais.

Amewapongeza viongozi wa kidini kwa juhudi zao wanazoendelea kufanya katika vita dhidi ya ufisadi na akawataka wazidishe juhudi hizo.

“Nausifia uongozi wa makanisa katika vita vya kupambana na ufisadi. Hata hivyo, bado kunayo nafasi ya hatua zaidi kutoka kwa kanisa. Ni vita vya jamii yote wala si vya serikali pekee,” ameongeza.

Rais amesema haya kutoka Ikulu ya Nairobi kwenye mkutano na viongozi wa kidini ambao walikuwa wamembelea.

Wakati uo huo, Rais na viongozi hao wamekubaliana kuandaa maombi ya kitaifa Jumamosi tarehe 10 mwezi ujao ili kuombea vita nchi hii dhidi ya COVID-19 na maswala mengineyo yanayoihusu nchi hii.

Aidha, Rais Kenyatta amewashauri waendelee kuwahubiria Wakenya jumbe za tumaini bila kuegemea mirengo ya kisiasa.

“Kuhusu maswala ya kisiasa, nafahamu kanisa linabaki juu ya siasa. Lakini sote tuko na jukumu la kuwasaidia watu wetu watambue kwamba hatuwezi kubaki taifa lililopagawa na siasa kila wakati.”

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Fred Matiang’I, Ukur Yattani wa Fedha, Prof. George Magoha wa Elimu, Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki na Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt. Joseph Kinyua miongoni mwa viongozi wengine wakuu serikalini.

Categories
Habari

Ruto asema hatakoma kusaidi makundi ya Kidini na kuinua vijana

Naibu Rais William Ruto amesema hatashurutishwa kukoma kusaidia makundi ya kidini na shughuli za kuwainua vijana.

Akihutubia viongozi wa makanisa waliomtembelea nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu, hapo jana, naibu rais alisema haoni aibu kumtumikia Mungu na wala hajutii imani yake.

Aidha alisema imani yake ndiyo ya kwanza mbele ya mamlaka ya kisiasa na akawataka wale wanaotatizika na shughuli zake za kusaidia makanisa, makundi ya kiislamu na juhudi za kuwainua vijana na wanawake kutafuta shughuli za kufanya.

Alisema viongozi walichaguliwa kuwapa uwezo wakenya miongoni mwa sababu nyingine akiongeza kuwa ni kupitia kwa miradi kama ile anayounga mkono ambapo maisha ya wakenya wa kawaida yanaweza kuimarishwa.