Categories
Burudani

Ruge Mutabaha akumbukwa

Ni miaka miwili tangu Ruge Mutabaha kuaga dunia na wengi wamemkumbuka mwanabiashara huyo ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Clouds Media nchini Tanzania.

Kabla ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo Ruge alikuwa amezamia kazi ya kuandaa tamasha kubwa kati ya biashara nyingine ambazo alikuwa akifanya.

Mmoja wa wale ambao wamemkumbuka Ruge ambaye alifariki tarehe 26 mwezi Februari mwaka 2019 ni mwanamuziki na mtangazaji Baba Levo.

Baba Levo amepachika picha ya marehemu Ruge kwenye akaunti yake ya Instagram na kusema kwamba atakuwa mpuuzi ikiwa hatakumbuka mchango wa Ruge kwenye maisha yao na muziki wao.

Levo ameendelea kwa kusema kwamba Marehemu Ruge Mutabaha ndiye alimtengeneza hata Diamond Platnumz lakini hajui walikosania wapi.

Amemsifia marehemu Ruge akisema alikuwa jasiri muonyesha njia na anaomba Mungu amsamehe makosa yake naaendelee kumweka mahali pema.

Inaaminika kwamba Diamond na marehemu Ruge hawakukosana ila tofauti zilitokana na ushindani wa kibiashara maanake baada ya kupata hela kwa muziki, Diamond aliingilia biashara sawia na ya Ruge ile ya kampuni ya utangazaji ambayo inaitwa Wasafi Media.

Mutahaba alizaliwa huko Berkeley, California nchini Marekani mwaka 1970 lakini akarejea Tanzania ambako alisomea kuanzia darasa la kwanza hadi shule ya upili kisha akarejea Marekani kwa ajili ya elimu ya chuo kikuu.

Categories
Burudani

Eric Omondi apimana nguvu na Diamond Platnumz

Mchekeshaji huyo wa nchi ya Kenya anamtania mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz kwa kile ambacho anakitaja kuwa kushambulia Afrika mashariki kwa kupata wapenzi na watoto.

Eric anasema alimwonya Diamond kwamba atalipiza kisasi lakini hakuamini na kwamba anajua sasa ameshachoka kukimbizana na wapenzi analea watoto.

Diamond Platnumz ana watoto na wapenzi wake wa zamani kwenye nchi zote za Afrika mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania.

Nchini Kenya ana mtoto na msanii Tanasha Donna ambaye anaitwa Naseeb Junior kama yeye na siku yao ya kuzaliwa ni moja, ukienda Uganda ana Zari Hassan ambaye ana watoto wake wawili, Princess Tiffah na Prince Nillan na kwao Tanzania anayejulikana ni Hamissa Mobeto ambaye ana mtoto kwa jina Dillan.

Eric alitoa video inayomwonyesha akiwa na mwanamuziki na muigizaji wa Tanzania Gigy Money ambaye ni rafiki wa karibu wa Diamond Platnumz anapoanza kulipiza hatua ya Diamond ya kunyakua warembo Afrika Mashariki.

Wimbo ambao ametumia kwenye video hiyo ni “Kwaheri” ambao umeimbwa na Jua Cali na Sanaipei Tande ishara kwamba Gigy amehama Tanzania na kumwacha Diamond na kuja Kenya kwa Eric Omondi japo yote hayo ni uigizaji tu.

Kulingana na maneno, picha na video kutoka kwa Eric Omondi kwenye mitandao ya kijamii, Gigy Money na Betty Kyallo huenda wakawa wahusika kwenye awamu ya pili ya kipindi chake “Wife Material”.

Categories
Burudani

Mzee Abdul afungua akaunti ya Instagram

Mzee Abdul ambaye alipata kujulikana na wengi kama baba mzazi wa mwanamuziki Diamond Platnumz sasa amefungua akaunti kwenye mtandao wa Instagram na anataka wafuasi na biashara.

Kwenye video ambayo iliwekwa kwenye akaunti ya Amber Ruty, mzee huyo anasikika akitangaza akaunti yake mpya ambayo ni “Mzee_Abdul_Official” huku akisihi mashabiki wamfuatilie huko na wanaotaka kutangaza biashara zao pia wamtafute huko.

Utangazaji wa bidhaa au huduma kupitia mitandao ya kijamii umegeuka kuwa kitega uchumi kwa watu wengi maarufu ulimwenguni na sasa mzee huyo naye ameamua kufuata njia hiyo.

Mzee abdul Juma amejaribu pia muziki ila inaonekana fani hiyo hakuipendelea maanake imekuwa muda wa mwaka mmoja sasa tangu kibao kwa jina “Dudu la Yuyu” ambacho alimshirikisha Sungura Madini kizinduliwe.

Picha ya kwanza ambayo alipachika kwenye akaunti yake mzee Abdul ni yake akiwa amebanwa na kina dada wawili na mmoja ni Amber Ruty.

Anamshukuru Ruty kwa kumjali siku zote na kukashifu wasiomjua kwa undani kwani yeye ni mtu mzuri hayuko vile wengi wanamdhania.

Amber Ruty, mume wake na rafiki yao wa kiume waliachiliwa kutoka gerezani maajuzi baada ya kuweza kulipa faini kwa koosa la kuchapicha video yao ya ngono.

Tangazo la akaunti ya Mzee Abdul limejiri yapata mwezi mmoja tangu mamake Diamond akiri kwamba yeye siye baba mzazi wa mwanamuziki huyo Diamond Platnumz.

Kabla ya hapo wengi walikuwa wamemsuta Diamond sana kwa kutosaidia babake Mzee Abdul ambaye picha zake zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo alionekana akiabiri gari la uchukuzi wa umma akiwa amebeba gunia.

Categories
Burudani

Baba Levo amshukuru Diamond Platnumz

Mwanamuziki na mtangazaji wa kituo cha redio cha Wasafi Fm nchini Tanzania Revokatus Kipando maarufu Baba Levo anamshukuru mwanamuziki Diamond Platnumz kwa kumsaidia kuendelea umaarufu wake jambo ambalo limemletea mengi mazuri.

Kupitia Instagram mtangazaji huyo aliandika, “KUWA KARIBU NA WEWE IMETOSHA KUNIPA PESA AMABAYO SIKUTEGEMEA KUJA KUISHIKA NA UZEE HUU.. Naomba Niweke wazi Kwa Mashabiki Wangu Kwamba Kabla Ya Mwezi Huu Kuisha Nitakuwa Nimesain Mikataba Na MAKAMPUNI TISA MAKUBWA Yote Yanataka Niwe BALOZI Wao Kwenye Bidhaa Zao Tofauti Tofauti… Niseme Tena ASANTE @diamondplatnumz Asante Sanaaa..”

Diamond alijibu usemi huo wa Baba Levo akimwita “Fundi Majumba” na kisha kuweka ishara ya moto na kilipuzi kuonyesha kwamba amekubali shukrani zake.

Wiki tatu zilizopita msanii huyo alizua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii kwa kusema kwamba yeye angekuwa mwanamke kama Zuchu, angemzalia Diamond watoto watatu.

Usemi huo ulisababisha wengi kumrejelea Baba Levo kama chawa jina ambalo analikubali kwa kuwa mara nyingi huwa yuko karibu sana na Diamond Platnumz ambaye ni mkubwa wake kikazi.

Huwa anazungumzia utajiri wa Diamond Platnumz hadharani huku akisema kwamba anakubali kamzidi kifedha lakini atatumia umaarufu wake ili naye aendelee.

Categories
Burudani

Vifaa vya Zoom ni vyangu!

Msanii wa muziki nchini Tanzania Harmonize mmiliki wa kampuni ya usimamizi wa wasanii maarufu kama Konde Music amedai kwamba yeye ndiye mmiliki halisi wa vifaa vinavyotumika kwenye studio za kutayarisha muziki kwa jina “Zoom Extra” ambayo awali iliitwa “Zoom”.

Konde Boy anasema vifaa hivyo ambavyo hutumika huko Wasafi au ukipenda WCB alikogura ni vyake kwani alifungua studio ya Zoom akiwa bado WCB.

Harmonize alikuwa akihojiwa ambapo alifunguka na kuelezea kwamba alinunua vifaa hivyo nchini Afrika Kusini, na aliporudi akamtafuta Ken the Producer wakaanzisha studio hiyo na baadaye wakaamua kumhusisha Diamond ili asilalamike kwamba anafanya mambo kivyake.

Mwanamuziki huyo anasema kuondoka kwake WCB sio kitu ambacho alipanga na hajawahi kuambia umma kilichomsukuma atoke lakini akaacha Ken kwenye Wasafi wakati huo ndio hiyo studio ilibadilishwa jina ikawa “Zoom Extra”.

Alipohojiwa kwenye kituo cha redio cha Wasafi Fm mwezi Septemba mwaka 2019 Ken alisema kwamba yeye ndiye msimamizi wa Zoom Production hata baada ya Harmonize kusema kwamba Jose wa Mipango ndiye alikuja na wazo la Zoom Production.

Ken alisema pia kwamba Zoom Production iko katikati yaani inafanya kazi na kampuni zingine ambazo zinachagua kufanya kazi nayo.

Watangazaji siku hiyo walisoma wasifu wa Diamond Platnumz kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo ameorodhesha kampuni ambazo aliasisi na anazisimamia na Zoom Extra ni moja yao.

Categories
Burudani

Lava Lava kuzindua nyimbo zake Kesho

Mr. Love Bite mwanamuziki wa Tanzania ambaye anajulikana na wengi kama Lava Lava ametangaza kwamba kesho Ijumaa ataachilia msururu wa nyimbo zake ambazo kwa jumla amezipa jina la “Promise”.

Kazi hiyo ambayo inalenga msimu wa mapenzi kwani nyimbo nyingi ni za mapenzi itazinduliwa kesho tarehe 12 mwezi Februari mwaka 2021 huku siku ya ya wapendanao ikiadhimishwa jumapili tarehe 14.

Lava Lava ambaye jina lake halisi ni Abdul Juma Idd, amepachika picha ya nje ya kazi hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram na kulingana naye, orodha kamili ya nyimbo hizo itatolewa kesho pia.

Lava Lava alijiunga na Wasafi Classic Baby ya Diamond Platnumz mwaka 2015 lakini akatangazwa rasmi mwezi mei mwaka 2017 wakati wa kuzindua kibao chake kwa jina, “Tuachane”.

Alitangulia kuzindua audio ya kibao hicho na siku mbili baadaye akazindua video yake.

Kabla ya kujiunga na WCB, Lava Lava na Mbosso walikuwa marafiki wa karibu lakini baadaye ukaribu huo ukatoweka na ndipo mashabiki wao wakaanza kukisia kwamba wamekosana.

Lakini alipohojiwa mwezi Oktoba mwaka 2020, Mbosso alielezea kwamba wanamuziki wa WCB huwa hawaonekani pamoja mara nyingi kwa sababu kila mmoja hufanya kazi zake binafsi na wanakutana wakati wa kuwasilisha kazi hizo.

Jambo lingine ambalo alifichua ni kwamba wanamuziki wote hupiga kura ili kuchagua kibao ambacho kitazinduliwa mwanzo.

Kulikuwa pia na usemi kwamba Zuchu anapendelewa sana na usimamizi wa WCB kuliko wanamuziki wengine ambao wanasimamiwa na kampuni hiyo.

Categories
Burudani

Sijawahi kumroga mume wangu!

Ndivyo alivyojitetea mwanamuziki wa Tanzania Queen Darleen ambaye kwa muda mrefu alichukuliwa kuwa dadake Diamond Platnumz kuhusu uhusiano wake na mume wake Isihaka.

Minong’ono ilikuwa imesheheni mitandao ya kijamii awali kwamba kamshikia dawa ya mapenzi ndiposa anampenda na kusahau mke wake wa kwanza.

Queen ni mke wa pili wa Isihaka na wakati fulani kulinuka ugomvi kati yake na mke wa kwanza ambaye anaitwa Sabra na wakati fulani alipohojiwa Darleen akasema anajua ameolewa yeye peke yake wengi wakadhani labda mke wa kwanza kaachwa.

Lakini jana wanandoa Isihaka na Darleen walifafanua kwamba wako wote kwenye ndoa hiyo na ndipo alisema kwamba hajawahi kumtafutia mume wake dawa ya mapenzi ili awe naye. Aliendelea kwa kusema kwamba akiamua kumroga basi atakuwa mke pekee kwenye ndoa hiyo.

Walikuwa wakihojiwa kwenye kituo cha redio cha Wasafi FM ambacho kinaendeleza mahojiano ya wapenzi na wanandoa mwezi huu wa mapenzi.

Isihaka alisema kwamba huwa anagawa siku zake za wiki kati ya wake zake wawili, siku nne kwa mke mkubwa na tatu kwa mke mdogo.

Darleen naye alielezea kwamba anamjali mume wake sana ndio maana lazima amheshimu mke mwenza kwani mume wake anampenda sana mke mkubwa. Hiyo alisema ndiyo sababu aliacha kupachika picha za Isihaka kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kila mara.

Mwanadada huyo ambaye ni mwanamuziki chini ya Kampuni ya WCB ya Diamond Platnumz alisifiwa sana na mume wake ambaye alisema kwamba anajua sana kutekeleza majukumu yake kama mke na kwamba anapokuwa nyumbani yeye sio Queen Darleen bali ni Mwanahawa kwani hata mavazi hubadilika wakiwa pamoja.

Categories
Burudani

Diamond Platnumz afanya ziara fupi nchini Kenya

Jana jioni mwanamuziki Diamond Platnumz toka Tanzania aliweka video ikimwonyesha akiabiri ndege huku akisema kwamba anaelekea jijini Nairobi nchini Kenya.

Watu wake wa karubu kama vile Romy Jons walikuwa naye kwenye ndege hiyo ya kibinafsi kulingana na picha walizopachika kwenye akaunti zao za Instagram.

Romy liweka picha akiwa ameketi karibu na Diamond ndani ya ndege na kuandika maelezo kwamba walikuwa kwenye uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi.

Alitumia majina ya kuonyesha ukoo wao yaani Romeo Nyange na Naseeb Nyange, baada ya mamake Diamond kutangaza kwamba marehemu Salum Nyange ndiye baba mzazi wa Diamond.

Lakini hakuna yeyote kati yao alitangaza sababu ya ujio wao nchini Kenya.

Muda mfupi baada yao kuwasili Kenya, mamake Diamond Bi. Sanura Kasimu ambaye hujiita Mama Dangote kwenye Instagram alipachika video tatu fupi kwenye Instagram zikionyesha Diamond akiwa na mtoto wake na Tanasha Donna kwa jina Naseeb Junior ndani ya gari la kifahari.

Na usiki ulipowadia, Diamond akapachika video nyingine ikimwonyesha akiabiri ndege hiyo yake ya kibinafsi na kuelezea kwamba alikuwa amemaliza alichikuja kufanya Nairobi na anarejea Tanzania.

Kwenye tangazo lake la kwanza la kusema kwamba anakuja Nairobi, alitaja kampuni ya kutengeneza soda ya Pepsi isijulikane kama alikuwa amekuja kwa ajili ya biashara na kampuni hiyo.

Ziara yake nchini Kenya ilidumu takriban saa tisa pekee.

Categories
Burudani

Wasafi Tv kurejea mwisho wa mwezi!

Adhabu iliyotolewa kwa kituo cha runinga cha Wasafi nchini Tanzania imerekebishwa. Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA ilitangaza hayo leo kupitia kwa mkurugenzi mkuu Bwana James Kilaba.

TCRA inasema ilipokea rufaa kutoka kwa usimamizi wa Wasafi Tv inayomilikiwa na msanii Diamond Platnumz kuhusu adhabu hiyo na baada ya kutathmini wameamua kwamba marufuku hiyo ambayo ingekamilika mwezi Juni mwaka huu wa 2021 ikamilike tarehe 28 mwezi Februari mwaka huu wa 2021.

Tangazo la kufungwa kwa kituo hicho lilitolewa na TCRA tarehe tano mwezi Januari mwaka huu na tarehe 21 mwezi huo, usimamizi wa Wasafi Tv ukaandikia TCRA kuomba adhabu yao irekebishwe. Tarehe 28 mwezi Januari, wasimamizi hao wa runinga ya Wasafi walirejea tena TCRA ambapo walipata kusikilizwa.

Bwana Kilaba anasema kwamba Wasafi Tv ilikiri kukiuka kanuni fulani za maadili.

Sababu kuu ya Wasafi Tv kupoteza leseni ya kupeperusha matangazo ni hatua yao ya kupeperusha moja kwa moja tumbuizo la mwanamuziki Gigy Money ambaye anasemekana kuvaa mavazi ambayo yalionyesha umbo lake visivyo.

Msanii huyo Gigy money pia aliadhibiwa na BASATA au ukipenda “Baraza la Sanaa la Taifa” ambapo alifungiwa asiwahi kufanya kazi yoyote ya sanaa kwa muda wa miezi sita.

Gigy siku hiyo kwenye tamasha la Wasafi Media, aliingia jukwaani akiwa amevaa dera kisha baadaye akalivua na kubakia na vazi la kushikilia mwili ambalo rangi yake ilikaribia kufanana na rangi ya ngozi yake ungedhania yuko uchi.

Usimamizi wa Wasafi haujasema lolote kuhusu kupunguziwa adhabu.

Categories
Burudani

Kibao cha Harmonize na Anjella kuzinduliwa siku ya wapendanao

Harmonize anayemiliki kampuni ya wanamuziki kwa jina Konde Music aligonga vichwa vya habari mwishi wa mwaka jana baada ya kuomba kufanya kazi na msanii anayeibukia nchini Tanzania kwa jina Anjella.

Anjella anaishi na ulemavu na amekuwa tu akitumbuiza kwa kurudia nyimbo za wasanii wengine wakubwa na hapo ndipo Harmonize alifurahishwa na uwezo wake wa kuimba.

Kinyume na matarajio ya wengi Harmonize msanii mkubwa alimtumia Anjella ujumbe kwenye Instagram akimwomba afanye kazi naye jambo ambalo Anjella hakuamini.

Lakini baadaye wasanii hao wawili walikutana na kuanza kupanga mikakati ya kushirikiana kikazi na kazi hiyo inaonekana kukamilika kulingana na tangazo la Harmonize kwamba kibao chao kitaanguka tarehe 14 mwezi huu wa Februari siku ya wapendanao.

Awali Harmonize alikuwa amepanga kwamba kazi yake na Anjella iwe ya kwanza ya mwaka huu lakini anaonekana kubadili mipango kwani tayari amezindua wimbo mwingine kwa jina “Anajikosha” na amemhusisha Anjella kwenye video.

Wimbo wao unaitwa “All Night” na kwenye tangazo lake, Harmonize anadai kwamba ni wimbo mzuri sana na utamuinua Anjella sana. anamshukuru pia kwa kazi yake na kukubali kufanya kazi naye.

Harmonize amebadilisha muonekano wa Bi. Anjella ambaye awali alikuwa anavaa tu kawaida na hakuwa anatumia vipodozi.

Anjella alivyokuwa akionekana awali na anavyoonekana sasa

Wanaofuatilia muziki nchini Tanzania wanaonelea kwamba hatua ya Harmonize ya kuleta Anjella na kufanya naye kazi ni ya kujaribu kushindana na Diamond Platnumz ambaye alimchukua Zuchu akaanza kufanya naye kazi na sasa Zuchu anafanya vywema.

Awali Harmonize alikuwa chini ya usimamizi wa Diamond kwenye WCB lakini akagura na kuanzisha kampuni yake ya muziki kwa jina “Konde Music”. Kila mara huwa anatoa nyimbo na kusema maneno ambayo wengi huwa wanahisi yanamlenga Diamond ila Diamond hajawahi kujibu.

Wakati mmoja Harmonize alikiri heshima na mapenzi yake kwa Diamond na Diamond hakujibu. Juzi juzi akihojiwa kwenye kituo cha Wasafi Fm, Diamond alisema hakujibu utambuzi wa Harmonize kwani alihisi kwamba yeye sio mkweli na huwa anatumia jina lake kujitafutia umaarufu.