Categories
Burudani

Sakata ya Wasafi?

Afisi ya mkaguzi wa hesabu za matumizi ya fedha serikalini nchini Tanzania, imeripoti kwamba milioni 140 pesa za Tanzania, ambazo wizara ya Mali Asili na Utalii ililipa kampuni ya Wasafi hazikuwa na mkataba wowote.

Inasemekana kwamba pesa hizo zilinuiwa kulipa wasanii walio chini ya usimamizi wa kampuni ya wanamuziki ya Wasafi ili watangaze utalii wa Mikoa ipatayo sita ya Tanzania.

Hata hivyo inasemekana wizara hiyo ilishindwa kubaini kiwango cha kazi ambayo ingetekelezwa na wasanii hao na eneo ambalo walistahili kuhusisha kwenye matangazo yao.

Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya muungano wa Tanzania Charles Kichere ambaye alizungumza na wanahabari jana huko Dodoma, alisema kiasi cha pesa zilizotolewa kwa kampuni ya Wasafi hakiambatani na sheria za matumizi ya pesa za umma.

Kichere alisema pia kwamba hakuna stakabadhi ambazo ziliwasilishwa kwa ukaguzi ili kubaini jinsi pesa zilitumika katika maandalizi ya tamasha za kitamaduni.

Kampuni hiyo ya Wasafi Classic Baby WCB inamilikiwa na mwanamuziki Diamond Platnumz na inasimamia wasanii kadhaa ambao wameafikia ufanisi barani Afrika na hata nje kama vile Zuchu, Mbosso na Rayvanny ambaye amefungua kampuni yake ya muziki maajuzi kwa jina Next Level Music.

Kampuni ya WCB haijatoa tamko lolote kuhusu sakata hiyo kufikia sasa ila kituo cha redio cha Wasafi FM ambacho pia kinamilikiwa na Diamond Platnumz kiliripoti tu kuhusu aliyoyasema Bwana Charles Kichere kwenye kikao na wahabari.

Inabainika kwamba baadhi ya pesa hizo zililipwa vituo vya runinga ili kupeperusha moja kwa moja tamasha la utamaduni lakini matumizi hayo hayakukaguliwa inavyostahili.

Categories
Burudani

Amber Lulu aota kaolewa na Diamond!

Mwanamuziki wa Tanzania ambaye pia ni muigizaji na mwanamitindo, alisisimua wengi jana jioni baada ya kuandika kwenye Instagram Stories kwamba alikuwa amelala mchana kisha akaota kwamba alikuwa akifunga ndoa na Diamond Platnumz.

Anasema kwenye ndoto aliona arusi yao ikiwa kubwa sana na ilifanyika katika uwanja wa taifa.

Lulu aliwahi kuwa mpenzi wa mwanamuziki wa Kenya Prezzo na isijulikane ni kwa nini aliota kuhusu Diamond au alikuwa akiwaza juu yake?

Mwezi mmoja uliopita, mwanadada huyo aliandaliwa sherehe kubwa ya kukaribisha mtoto almaarufu “Baby shower” ambapo alionekana akiwa mjamzito na kufikia sasa inaaminika ana mtoto ila hajatangaza rasmi.

Tukio hilo lilipeperushwa na Bona Tv.

Amber Lulu hata hivyo, ameweka picha ya mkono wa mtoto ukiwa umeshikilia kidole chake.

Kwenye picha hiyo ametaja akaunti nyingine mpya ya Instagram ambayo ina picha yake akiwa mjamzito na inaitwa @iam_arianna26 na inaaminika jina la mtoto ni Arianna.

Kwenye sherehe hiyo, alikataa kufichua baba mtoto ni nani ila wengi walidhania kwamba ni P-Funk Majani jambo ambalo alikana na hata kusema kwamba hata yeye mwenyewe hajui baba mtoto ni nani!

Categories
Burudani

Wasanii wazindua wimbo wa pamoja wa kumuenzi Rais Magufuli

Wasanii wa muziki zaidi ya 20 wa nchi ya Tanzania ambao walikutana usiku wa tarehe 17 mwezi huu kwa ajili ya kuunda wimbo wa mumkumbuka marehemu Rais Magufuli, wamekutana hii leo tena katika studio za Wasafi Fm kuuzindua.

Wimbo huo unaitwa Lala Salama Magufuli na umeimbwa na Tanzania All Stars.

Akizungumza studioni humo msanii Diamond Platnumz alielezea kwamba ni wazo ambalo lilimjia ghafla na alipowasiliana na wengine kama Juma Jux wakakubaliana nalo na wakaamua kukutana kwenye studio za wanene kuunda wimbo huo.

Kulingana na mkurugenzi huyo mkuu wa Wasafi Media, wasanii wengine walimaliza kutia sauti asubuhi ya tarehe 18 ambayo ni jana na moja kwa moja wakaingilia uundaji wa video ya wimbo huo.

Mrisho Mpoto anayejulikana kwa muziki wa aina ya kipekee, alisema kwamba wameumia sana kwa kupoteza Rais Magufuli ambaye alitambua sana sanaa.

Kuhusu kuingia mamlakani kwa mama Samia Suluhu Hassan, Queen Darleen alisema kwamba kwa kweli sio raha kwamba ameingia uongozini kwani wote wanaomboleza lakini kuna nguvu fulani ambayo imedhihirika kutokana na kupata Rais wa kike.

Wasanii wote hao wanakubaliana kwamba Rais Magufuli alikuwa zawadi kwao na wakamsifia kwa kutanguliza Mungu kila mara katika uongozi wake.

Mwanamuziki kwa jina Abby Chams alisema Magufuli ni shujaa na hata kama ameondoka watamkumbuka milele.

Wimbo huo unaanzishwa na Mbosso na Christina Shusho na wengine wanaingilia kila mmoja na ubeti wake.

Categories
Burudani

“Siwezi kutafutia Diamond mke!” asema Shilole

Baada ya kioja cha siku ya Jumatatu ambapo Shilole alimkutanisha Diamond Platnumz na mwanadada shabiki wake kutoka ufaransa kitu ambacho kilimkera mamake Diamond, mwanamuziki huyo amejitetea.

Siku hiyo, Diamond na kikosi kizima cha WCB walikuwa wamekamilisha kikao na wanahabari ambapo walitangaza uzinduzi rasmi wa albamu ya Mbosso na walipokuwa wakitoka, Shilole akawasimamisha na kumjulisha dada huyo ambaye hangeweza kusema kiswahili ambaye alitaka tu kupiga picha na Diamond.

Akizungumza kwenye mahojiano na Wasafi Tv, Shishi ambaye mara ya kwanza alikuwa amekataa kusema na mwanahabari, alisema kwamba Diamond sio mtoto mdogo amezaa na wanawake wengi kwa hivyo yeye hana uwezo wa kumtafutia mke.

Shilole hata hivyo aliomba msamaha kwa mamake Diamond ambaye pia humrejelea kama mama akisema ikiwa alikosea basi anaomba msamaha.

Maneno yake yanafuatia msomo aliopata kutoka kwa mama mzazi wa Diamond ambaye alimwonya akome kumtafutia mtoto wake wanawake.

Mamake Diamond naye alihojiwa jana ambapo alisema kwamba mwanadada huyo anayedai kuwa shabiki sugu wa Diamond kutoka Ufaransa, awali alikuwa amemtumia watu akitaka kukutana naye na Diamond na mama Dangote anasema aliwafukuza.

Aliongeza kusema kwamba Shilole angemtafuta Diamond kwingineko badala ya kumfuata mahali alikuwa na waandishi wa habari.

Mpenzi wa mama Dangote aitwaye Uncle Shamte naye alizungumza akisema kwamba kitendo kile kilihatarisha usalama wa Diamond kwani kuna watu wanaweza kuvaa glovu za sumu na wakamdhuru.

wengine wanahisi kwamba Shilole alilipwa hela nyingi na mwanadada huyo kutoka Ufaransa ili amkutanishe na Diamond.

Categories
Burudani

Wasanii wakesha studioni kuandaa wimbo wa maombolezo

Kufuatia kifo cha Rais wa muungano wa Tanzania jana jioni, wasanii wengi tajika nchini Tanzania waliamua kuingia studioni kuandaa wimbo kwa ajili ya kumlia kiongozi huyo.

Kulingana na picha na video zilizochapishwa na Wasafi Tv wasanii ambao walikuwa studioni kwa pamoja usiku ni kama vile Diamond Platnumz, Khadija Kopa, bintiye Zuchu, Mbosso, Ben Pol, Christina Shusho na wengine wengi.

Marehemu Rais wa Tanzania John Joseph Pombe Magufuli alitambua sana wanamuziki nchini humo kwa kazi yao ambayo wanafanya. Na ndio maana wakati wa kampeni za kutafuta kuchaguliwa tena mwaka jana, alitumia wanamuziki hao kwenye mikutano ya kampeni.

Aliposhinda aliwahusisha pia katika sherehe ya uapisho wake.

Wengi wa wasanii hao pia wamemwomboleza liongozi huyo wa taifa kwa namna ya kipekee kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii. Msanii Harmonize au ukipenda Konde Boy alipachika video inayomwonyesha akiangua kilio kwenye Instagram stories baada ya kupashwa habari kuhusu kifo cha Magufuli.

Harmonize aliwahi kubadilisha wimbo wake ambao alikuwa amefanya na Diamond Platnumz uitwao Kwangwaru na kuuita Magufuli akisifia utendakazi wake.

Sio yeye tu ambaye ana wimbo wa kusifia marehemu Rais, wengi tu walitunga na kuimba nyimbo za aina hiyo akiwemo malkia wa WCB Zuchu.

Categories
Burudani

Masharti ya Simba!

Mmiliki wa kampuni ya Wasafi Classic Baby ambaye pia ni msanii wa Bongo Fleva Diamond Platnumz ametoa mwelekeo wa mavazi kwa wale wote ambao wanapanga kuhudhuria uzinduzi wa albamu ya Mbosso, “Definition Of Love”.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Diamond ametangazia waalikwa na wale ambao wanaendelea kununua tikiti au wameshanunua kwamba mavazi yatakayokubalika kwenye hafla hiyo ni ya rangi ya bluu yaani samawati na rangi nyeusi.

Diamond ambaye pia hujiita Simba anasema kwamba mtu akiongeza rangi nyeupe kwenye vazi lake hakutakuwa na tatizo na hata akapachika picha za watu waliovaa mavazi ya rangi hizo kama kielelezo.

Kulingana naye yeyote ambaye atafika langoni Mlimani City Jumamosi tarehe 20 mwezi huu wa Machi mwaka 2021 akiwa amevaa mavazi ya rangi tofauti na alizozitaja hatoruhusiwa kuingia na hatarejeshewa hela ya tikiti.

Kuna tiketi za bei tofauti kwa ajili ya tukio hilo, ya kwanza ni ya milioni 5 pesa za Tanzania ambayo ni sawa na 236,739.97 za Kenya.

Tiketi ya pili ni ya shilingi milioni 3 pesa za Tanzania, sawa na 142,043.98 za Kenya, Kuna ya Milioni moja za Tanzania ambayo ni sawa na 47,347.99 pesa za Kenya, ya laki moja ya Tanzania sawa na 4,734.80 za kenya na ya mwisho ni ya shilingi elfu hamsini za Tanzania, sawa na 2,367.40 za Kenya.

Mbosso tayari ametoa albamu hiyo ya “Definition of Love” kwenye majukwaa kadhaa ya muziki mtandaoni na inaonekana kupokelewa vyema na mashabiki.

Categories
Burudani

Wema Sepetu bado anatafuta mbwa wake

Muigizaji huyo wa nchi ya Tanzania ambaye wakati mmoja aliibuka mshindi katika shindano la ulimbwende nchini humo alitangaza kwa mara ya kwanza kuhusu kupotea kwa mbwa wake ambaye amempa jina la “Vanilla Manunu” siku nne zilizopita.

Hata aliweka zawadi ya shilingi milioni moja pesa za Tanzania kwa yeyote ambaye angempata mbwa huyo na kumrejeshea. Baadaye aliongeza zawadi hiyo hadi milioni mbili.

Wengi walikanganyika na picha aliyoipachika Wema kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa amembeba mbwa huyo wakidhani keshampata na sasa amelazimika kufafanua kwamba hajampata na hiyo picha ni ya kitambo.

Ilibidi pia mwanadada huyo aelezee alivyopotea mbwa wake na aliandika haya kwenye akaunti yake ya Instagram;

“Mimi naishi karibu na Kigamboni na kila siku gari ya Production huja mpaka nyumbani na kunichukua kwa ajili ya Kwenda Location… Juzi ilivyokuja nikawa sijaingia kwenye gari cause nilikuwa sina Scenes za kushoot so I told the driver aende tu kuwapitia watu wengine Kambini…. So kilichotokea since Vanilla ameshazoea naendaga nae location without her knowing gate lilivyofunguliwa kuruhusu gari litoke, mbwa nae akaanza kufata gari, kaikimbiza na mpaka sasa sijui bado kama aliikimbiza mpaka wapi, ni majirani tu ndo wamesema kuwa alikuwa anakimbiza gari…. So thats the story… Sijui bado kama mbwa wangu yupo hai au amekufa…”

Kuhusu wanaosema anamtafutia umaarufu mbwa wake, Wema alijitetea akisema mbwa huyo tayari ni maarufu kwani ana ufuasi wa elfu 15 tayari kwenye akaunti yake ya Instagram.

Wema Sepetu ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Diamond Platnumz, husema kwamba amejaribu mara nyingi kupata mtoto bila mafanikio, humrejelea mbwa wake kama mtoto wake.

Categories
Burudani

Mamake Diamond amuonya Shilole

Mama huyo wa msanii Diamond Platnumz Sanura au Sandra Kassim ambaye hujiita Mama Dangote kwenye Instagram hakuridhishwa na kitendo cha Shilole ambaye pia ni mwanamuziki.

Jana baada ya Diamond na kikosi kizima cha WCB kukamilisha kikao na wanahabari hotelini Hyatt Regency ambapo walitangaza uzinduzi rasmi wa albamu ya Mbosso, Shishy Baby alimsimamisha Diamond kisa na maana kumkutanisha na shabiki wake mmoja ambaye alikuwa amesafiri kutoka ufaransa kwa ajili ya kumwona Diamond na kupiga naye picha.

Shilole alijielezea haraka ambapo pia alitamka kwamba binti huyo ambaye anazungumza kifaransa alikuwa tayari kumlipa yeyote ambaye angemfikisha kwa Diamond.

Diamond hakusema lolote ila alisimama tu na kutimiza hitaji la shabiki huyo wake. Baadaye Shilole alizungumza na wanahabari ambapo alisema Diamond ambaye humrejelea kama kakake mdogo hana mpenzi na labda wangeskizana na dada huyo.

Hilo ndilo jambo ambalo limemkasirisha mamake Diamond ambaye amechukua picha ya Diamond, ya Shilole na video ya shilole akisema na wanahabari akazipachika kwenye Instagram kwa pamoja na kuandika maneno yafuatayo;

“Kama mzazi hakuna anayefurahia kuona mwanae analetewa mwanamke ovyo ovyo bila kuzingatia staha ya mtu kama mtu, au imani zetu. Ukizingatia huyo mtu kashatangaza hadi pesa ili apige picha na mwanangu ila kwa kuwa tunajua nia yake ni ovu hatukumpa nafasi hiyo. mwanangu ni tafsiri halisi ya jamii( kioo cha jamii) yenye nidhamu tofauti na alivyo au ulivyomchukulia @officialshilole usirudie tena na siyo maisha kuchukuliana poa watu wakiwa kazini…hakuna msanii anayekubali kila mtu anayesema ni shabiki yake kirahisi..sisi ni wazoefu wa kushuhudia mashabiki ila siyo huyo au aina hiyo ya shabiki sijapenda”.

Diamond Platnumz ana watoto na wanawake watatu ambao wanajulikana ila hajaoa na kwa sasa hayuko kwenye uhusiano wa kimapenzi asemavyo na wengi wanahisi kwamba mamake mzazi hudhibithi mahusiano ya mwanamuziki huyo.

alipokuwa kwenye uhusiano na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna, wengi waliamini kwamba wangefunga ndoa lakini wakatengana mara tu mtoto wao alipozaliwa ndipo uvumi ukaenea kwamba mamake Diamond hakumpenda Donna.

Categories
Burudani

Mbosso kuzindua rasmi albamu yake

Usimamizi wa kampuni ya muziki ya Wasafi Classic Baby au ukipenda WCB ya Tanzania imetangaza kwamba mwanamuziki wake Mbosso atazindua rasmi albamu yake kwa jina “Definition Of Love” Jumamosi tarehe 20 mwezi huu wa Machi mwaka 2021.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam, msanii wa muziki Diamond Platnumz ambaye pia ndiye mkurugenzi wa Wasafi alisema kwamba walijitokeza kutangaza uzinduzi wa albamu ya Mbosso kama njia moja ya kusimama naye kwani wanaelewa huenda ana shauku kwa kuwa ndiyo albamu yake ya kwanza.

Diamond alisema shughuli hiyo itaanza saa moja jioni huku akiwashukuru waandishi wa habari kwa jinsi walitangaza uzinduzi wa mwanamuziki Zuchu awali.

Mbosso naye aliwashukuru waandishi wa habari kwa kuitikia mwito wa leo na kusema kwamba tayari hiyo ni “Definition of Love”.

Mwingine aliyezungumza kwenye kikao hicho cha wanahabari ni Mbunge wa eneo la Morogoro Kusini Hamisi Shaban Taletale au ukipenda Babu Tale ambaye pia ni msimamizi wa wasanii katika WCB.

Babu Tale alimpigia debe Mbosso akisema anastahili kupatiwa kazi ya ubalozi wa Utalii wa Tanzania kwa jinsi alitumia maeneo mbali mbali ya kuvutia nchini Tanzania katika video za nyimbo zake.

Anasema watu wengi tayari wameonyesha nia ya kuzuru Tanzania kutokana na picha ambazo wameona kwenye video za muziki wa Mbosso na kwa hilo akaalika wasimamizi wa wizara ya mali asili na utalii nchini Tanzania kwenye uzinduzi wa albamu hiyo ya Mbosso.

Albamu ya Mbosso Definition of Love ina vibao 12 ambavyo ni; Mtaalam, Kiss Me, Baikoko ambao amemhusisha Diamond Platnumz na Tulizana ambao aliimba na Njenje wa bendi ya Kilimanjaro.

Wimbo wa tano kwenye albamu hiyo unaitwa Yalah, wa sita Sakata ambao aliimba na Flavour, wa saba Pakua aliouimba na Rayvanny ambaye pia ni wa kundi la WCB na wa nane ni Karibu ambao aliimba tena na Diamond.

Nyimbo nyingine ni Your Love ambao aliimba na Liya, Kadada alouimba na Darassa, Yes wake na Spice Diana na Nipo Nae ambao ameimba peke yake.

Aliongezea nyimbo nyingine mbili ambazo anarejelea kama “Bonus Tracks” mmoja unaitwa Limevuja na mwingine Kamseleleko ambao alimshirikisha Baba Levo.

Categories
Burudani

Diamond amsifia Rayvanny

Msanii wa muziki toka nchini Tanzania ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Wasafi ambayo ina Label ya wanamuziki WCB, Kituo cha redio Wasafi Fm na kituo cha runinga Wasafi Tv Diamond Platnumz amemsifia sana mwanamuziki mwenza Rayvanny.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo kwenye hafla ya kuzindua rasmi kampuni ya Rayvanny ya kurekodi muziki na kusimamia wanamuziki, Diamond alisema kwamba Rayvanny ni msanii ambaye ni mpole hata baada ya kufanikiwa kwa kupata mauzo ya kiwango cha juu cha muziki.

Kulingana na Diamond, Rayvanny angekuwa na dharau sana kutokana na pesa nyingi alizonazo lakini ni mpole na akatumia nafasi hiyo kusuta wanamuziki ambao wanadhania kwamba ili wafanikiwe lazima watengeneze ugomvi na wengine.

Diamond alisema mkakati huo umepiitwa na wakati.

Aligusia kisa cha hivi karibuni ambapo Rayvanny alinunua gari jipya aina ya Toyota Prado na hakutangaza kwenye mitandao ya kijamii wafanyavyo watu wengine.

Simba aliahidi kuhakikisha kwamba Kampuni ya Rayvanny ambayo inafahamika kama “Next Level Music, NLM” inafahamika na kuendelea zaidi ili hata kampuni yake ya Wasafi isitukanwe.

Nembo ya NLM

Makao makuu ya Next Level Music yako katika eneo la Mbezi Beach Rainbow Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na ni jumba la orofa la rangi nyeupe. Ukiingia ndani unapata mapambo ya rangi yeupe na nyeusi na afisi hizo zimepambwa na picha watu ambao Rayvanny anawaenzi pamoja na tuzo ambazo amewahi kushinda kama msanii.

Kati ya picha hizo kuna ya Diamond Platnumz na ya Babu Tale.

Diamond na Rayvanny walikuwa wamevalia suti za rangi yeupe na mapambo ya rangi nyeusi ambazo ni rangi za Kampuni hiyo ya Rayvanny.

Katika hotuba yake Diamond alisema kwamba wao ni watoto ambao walilelewa kwa umasikini na wanajitahidi kudaidia wengine kutoka kwenye umasikini kupitia muziki.