Categories
Burudani

“Nashukuru Mungu kwa kunipa mzazi mwenza kama Zari” Diamond

Mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz au ukipenda Simba au Chibu Dangote amemsifia sana mzazi mwenza kwa jina Zari Hassan.

Akizungumza jana katika kituo cha redio cha Wasafi Fm kwenye kipindi cha ‘The Switch’, mmiliki huyo wa Wasafi Media alifichua kwamba hana uhusiano wa kimapenzi na Zari mzaliwa wa Uganda anayeishi na kufanya biashara nchini Afrika Kusini.

Diamond alikuwa amekwenda kituoni humo jana kwa ajili ya kuzindua kibao walichoshirikiana na Koffi Olomide.

Alisema wanasaidiana tu katika malezi ya wanao wawili na alikuwa amekuja kumletea watoto kwani hakuwa ameonana nao kwa muda wa miaka miwili.

“Miongoni mwa watu ama wazazi wenzangu ambao ninaweza nikawasifia, yaani nasifia katika namna tunajua namna gani ya kuishi kama wazazi ni Zari.” ndiyo baadhi ya maneno aliyasema Diamond.

Alisema pia kwamba anafarijika kuona kwamba watoto wake wana mama kama Zari na alibahatika kuzaa naye na anashukuru Mungu.

Kuhusu wanawe kulelewa na baba mwingine Diamond alisema hakuna tatizo bora aruhusiwe kutagusana na watoto wake anavyotaka.

Wanawe wakiwa nchini Tanzania, Diamond alipata fursa ya kurekodi kibao na mtoto wake wa kike Tiffah na amesema kibao chenyewe kitazinduliwa kabla ya mwisho wa mwaka.

Zari anasemekana kuwa ana mahusiano mengine ya mapenzi naye Diamond akasema bado yuko peke yake hajapata mpenzi.

Sifa alizomimina Diamond kwa Zari zinafanya wanawake wengine ambao ana watoto nao kuonekana vibaya sana. Bwana huyo ana mtoto wa kiume na mwanamitindo wa Tanzania Hamisa Mobeto na mwingine wa kiume na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna.

Categories
Burudani

Zari Hassan asuta kakake Diamond

Mwanamitindo Zari Hassan, mzaliwa wa Uganda anayeishi na kufanya biashara nchini Afrika kusini amegadhabishwa na matamshi ya kaka wa kambo wa Diamond Platinumz kwa jina Ricardo Momo. 

Ricardo alihojiwa na hapo ndipo alimwaga mtama kuhusu mahusiano ya Zari na Diamond Platinumz. Kulingana naye, Zari ndiye alianza kumnyemelea Diamond kwa kutaka kufurahia mali yake na umaarufu. 

Lakini Zari anakana hayo akisema kwamba Ricardo anafaa kufanya utafiti kabla ya kusema mambo kwani sio ukweli anaonelea kuwa kaka huyo wa Diamond anatafuta ufuasi kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia jina lake. 

Hata hivyo Zari amekiri kwamba yeye ndiye kwanza alimpigia Diamond simu akitaka huduma zake kama mwanamuziki kwenye sherehe ambayo alikuwa ameandaa, Diamond akamwelekeza kwa meneja wake na ikatokea kwamba hangeweza kuhudhuria na kutumbuiza kwenye sherehe ya Zari kwani alikuwa na kazi kipindi hicho chote.

Baada ya hapo, Zari anasema walikutana tena kwenye ndege wakisafiri na hapo ndipo walibadilishana nambari za simu na Diamond akawa ndiye mwenye kuwasiliana na Zari kwa sana kwa kutuma jumbe kila mara. Mwanadada huyo anasema alikuwa na pesa hata kabla ya kukutana na Diamond. 

Zari na Diamond walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi ambao una matunda ambayo ni watoto wawili, wa kike Tiffah na wa kiume Nillan.

Walitengana baada ya kile kinachosemekana kuwa uzinzi kwa upande wa Diamond.

Alipohojiwa yapata mwaka mmoja uliopita, Diamond alikiri kwamba yeye ndiye alikuwa na makosa mengi kwenye uhusiano wake na Zari.

Zari pia anakoseshwa kwa kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Peter Okoye mwanamuziki wa Nigeria na mwalimu wake wa mazoezi wakati akiwa kwenye uhusiano na Diamond.

Categories
Burudani

Tanasha Donna kuzindua Albamu yake mwakani

Mamake Naseeb Junior Tanasha Donna ametangaza kwamba mwaka ujao atazindua albamu yake ya kwanza.

Bi Donna ambaye pia aliwahi kuwa mtangazaji wa redio, alisema hayo kupitia Instagram ambapo aliandika,

“Mwaka 2020 umekuwa mwaka wa vibao moto.

Vibao saba kwa muda wa chini ya mwaka mmoja, na sio mimi, ni kwa sababu ya upendo na usaidizi ambao mmeendelea kunionyesha. Alhamdulillah. Mwaka 2021 tunaangusha albamu. Albamu yetu. Tuweke historia. Afrika mashariki kwa ulimwengu.”

Mwanzo wa mwaka huu, Tanasha alizindua ‘EP’ yaani “extended play” yake ya kwanza kwa jina “Donnatella” ambayo ilipokelewa vyema na mashabiki.

Kwenye mkusanyiko huo wa nyimbo kuna nyimbo kama vile ‘Gere’ ambao alishirikiana na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platinumz ambaye pia ni baba ya mtoto wake. Wimbo kwa jina ‘La Vie’ ambao amemshirikisha mwanamuziki wa Tanzania Mbosso ambaye yuko chini ya kampuni ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond. Na wimbo ‘Sawa’ kati ya nyingine.

“EP” au Extended Play katika muziki ni mkusanyiko wa nyimbo ambao hautoshi idadi ya kuitwa albamu. Mama huyo wa mtoto mmoja wakati fulani alisemekana kudandia umaarufu wa mpenzi wake wa awali Diamond ili kuendeleza muziki wake.

Tanasha alikiri kwamba uhusiano wake na Diamond ulisaidia kuinua kazi yake lakini hata yeye ametia bidii kwenye fani hiyo. Tanasha pia ni mwanamitindo na aliwahi kufanya kazi na mwanamuziki Ali Kiba wa Tanzania ambaye huchukuliwa kuwa hasidi wa Diamond hata kabla ya uhusiano wake na Diamond.

Binti huyo alionekana kwenye video ya wimbo ‘Nagharamia’ wake Ali Kiba akiwa amemshirikisha Christian Bella.

Categories
Burudani

Mashemeji wamekasirika!

Simba wa muziki nchini Tanzania amejipata pabaya baada ya kuandika chini ya picha ya mtoto wake Naseeb Junior kwa mara ya kwanza tangu atengane na mama mtoto Tanasha Donna.

Akaunti ya Instagram ya Naseeb Junior inaaminika kuendeshwa na mamake Tanasha na jana jioni binti huyo ambaye pia ni mwanamuziki aliweka picha ya Naseeb akiwa amevalishwa nadhifu mavazi ya rangi nyeupe na samawati.

Mtu wa kwanza kuweka ‘comment’ yake kwenye hiyo picha ni babake mzazi Diamond Platinumz au ukipenda Nasibu Abdul.

Wafuasi wa Naseeb Junior wakenya walichukua fursa hiyo kumsuta Diamond kwa kile ambacho wanasema kwamba ni kukosa kuhudumia mtoto huyo kama baba mzazi.

Mmoja kwa jina ‘9585m.ary’ aliandika,

“Tumechoka tuhakikishie kwamba wewe sio baba asiyekuwepo. Sisi wakenya hatupendi wazazi wasiokuwepo kwa maisha ya wanao. Hivi karibuni utakuwa unalia kwenye runinga. Kuwa mzuri ndugu.”

Wengine wanamshauri bwana huyo aoe wanawake wote ambao wamemzalia watoto kama vile ‘Master26788’

ameandika, “Mimi naona uoe wote kaka kwa sababu uwezo unao. si ufanye hivyo kaka unangoja nini jamani? Mke mkubwa Wema, wa pili Zari na wa tatu Tanasha. Najua unaweza tena sana yule tununu kwa sababu mama hamtaki akae atulie mtoto wake atalelewa na Wema.”

Dadake Diamond Esma Platinumz aliandika, “Tom Kaka we miss you jamani.”. Juzi tu Esma alisifia Zari ambaye alikuwa amepeleka watoto kwa baba yao kwa ujuzi wake katika kupika huku akisema wengine ambao ndugu yake amewahi kuwa nao hawakujua kupika kama Zari.

Diamond hajasema lolote kuhusu maneno ya wafuasi wake na wa mtoto wake kwenye Instagram. Mwezi wa sita mwaka huu Bi. Tanasha alifichua kwamba Diamond hakuwa anagharamia malezi ya mtoto wao.

Categories
Burudani

Diamond Platinumz kuzuru Kenya

Msanii wa nchi ya Tanzania Diamond Platinumz au ukipenda Chibu Dangote au Simba anatarajiwa kutua nchini Kenya hii leo kwa kile ambacho kinasemekana kuwa ziara ya mapumziko.

Ama kweli miezi michache ambayo imepita imekuwa ya kazi nyingi kwa msanii huyo kiasi cha kwamba sasa anahitaji mapumziko.

Mwezi Septemba alikuwa anajihusisha na kazi ya kutoa muziki na Bi. Zuchu ambaye alikuwa amejiunga na kampuni ya WCB anayomiliki Diamond. Wawili hao walitoa nyimbo kama vile ‘Cheche’ na ‘litawachoma’ ambazo zilizua minong’ono chungu nzima kwenye mitandao ya kijamii.

Swali ambalo wengi walikuwa wanajiuliza ni la uhusiano kati ya wawili hao kwa jinsi walicheza kwenye video za nyimbo na kuandamana karibu kila sehemu.

Baada ya hapo Diamond na wanamuziki wengine wa WCB waliingilia Kampeni ambapo walikuwa wakikipigia debe chama cha CCM na hasa Rais John Pombe Magufuli.

Uchaguzi ulipokamilika alifanya tamasha nchini Sudan Kusini na nchini Malawi. Aliporejea nyumbani Tanzania alitembelewa na mpenzi wake wa zamani Zari Hassan na watoto wao Tiffah na Nillan. Hakuwa ameonana na watoto hao kwa muda wa miaka miwili.

Na sasa ametangaza likizo yake nchini Kenya ila wengi wanaonelea kwamba anakuja kuona mtoto wake na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna ambaye ni somo wake kwa jina Naseeb Junior.

Ukurasa wa Facebook kwa jina ‘Wasafi News’ unaoaminika kuwa wa Wasafi Media kampuni inayomilikiwa na Diamond Platimumz ndio umetangaza ziara yake ya Kenya na kupachika picha ya awali ya Diamond na Tanasha.

Categories
Burudani

Video ya “Ushamba” wimbo wa Konde Boy

Harmonize aliutambulisha wimbo huo rasmi usiku wa tarehe mosi mwezi huu wa Novemba wakati wa tamasha la “Ushamba Night Party” ila kwa wakati huo ulikuwa ni sauti tu na jana tarehe nane mwezi Novemba ameachia video ya wimbo huo.

Maneno ya wimbo huo kwenye ubeti wa pili yanaonekana kuingilia anaoshindana nao katika ulingo wa muziki nchini Tanzania na kwenye video inadhihirika wazi kwamba anayemzungumzia ni Simba au ukipenda Diamond Platinumz.

Amemtumia jamaa fulani ambaye anafanana na Diamond Platinumz ambaye hujiita “Diamond wa Buza” kwenye video katika sehemu ya wimbo ambayo inazungumzia Simba. Ni katika ubeti huo wa pili na maneno ni ” … Halina meno hilo simba likila demu lazima litangaze …”.

Diamond wa Buza anaonekana akiwa kwenye kidimbwi cha kuogelea akiwa na mwanadada na wanapiga picha, taswira ya matukio yaliyozua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii wakati ambapo Diamond Platinumz alionekana akiogelea nyumbani kwake na mwanamuziki Mimi Mars.

Hayo yalifanyika siku chache baada ya Diamond Platinumz kukiri kwamba anampenda dada huyo wa mwanamuziki Vanessa Mdee.

Harmonize amefuata nyayo za Ali Kiba kwa kutoa wimbo wa kukejeli washindani baada yake kutoa wimbo kwa jina “Mediocre” na tafsiri yake ni “ujinga”. Hata hivyo Ali Kiba alikana tetesi kwamba wimbo huo ulilenga washindani wake ambao ni Diamond na Harmonize.

Diamond kwa upande mwingine anaonekana kuridhika na ushindani huo katika ulingo wa muziki maanake alipohojiwa katika kituo chake cha redio “Wasafi Fm” tarehe 27 mwezi Oktoba mwaka huu alisema ushindani huo ni muhimu unafanya fani iendelee.

Wasafi news pia asubuhi ya leo wameandika wakisema Harmonize anamlenga bosi wake wa zamani ambaye ni Diamond Platinumz. Harmonize aligura WCB kampuni ya muziki ya Diamond Platinumz ila hajakamilisha taratibu za kujiondoa kabisa.

Tazama video ya wimbo Ushamba hapa chini;

Categories
Burudani

Octopizzo apendekezwa kuteuliwa kuwania tuzo za Grammy

Octopizzo ambaye ni mwanamuziki wa nchi ya Kenya ana raha baada ya kupiga hatua katika sanaa yake. Hii ni baada ya kupendekezwa kuteuliwa kuwania tuzo za kifahari za nchi ya marekani za Grammy.

Mwanamuziki huyo kwa jina halisi Henry Ohanga sasa yuko kwenye orodha ya wasanii wanaofikiriwa katika kuwania tuzo za Grammy mwaka 2021.

Hii huwa hatua ya kwanza katika tuzo hizo na baada ya hapo washirika katika “Grammy Academy” watapiga kura kuteua wawaniaji wa tuzo kutoka kati ya wengi waliopendekezwa.

Wimbo wake kwa jina “Another Day” unapendekezwa kuwania tuzo la rekodi bora ya mwaka, huku “Kamikaze ukipendekezwa kuwania tuzo la “Best melodic rap” pamoja na huo wa “Another day”.

Wimbo wake ambao amehusisha Sailors kwa jina “Che che” unapendekezwa kuwania tuzo la “Best Rap Performance”.

Octopizzo alitangaza hayo kupitia akaunti yake ya Twitter.

Wasanii wa Afrika Mashariki ambao pia wako kwenye orodha ya wanaofikiriwa kuwania tuzo za Grammy ni wanamuziki wa kampuni ya Wasafi au ukipenda WCB nchini Tanzania, Diamond Platinumz, Zuchu, na Rayvanny.

Nyimbo za Diamond “Jeje” na “Baba Lao” zinapendekezwa kuwania tuzo la Video bora ya mwaka huku albamu ya Rayvanny kwa jina “Flowers” ikipendekezwa kuwania tuzo la Albamu ya muziki wa dunia bora ya mwaka.

Zuchu anapendekezwa kwa kuwania tuzo la mwanamuziki bora mpya.

Alipohojiwa na Grammys Diamond alisema ikiwa atashinda tuzo la Grammy kwanza ataomba na kushukuru Mungu kwa wiki nzima kisha aandae onyesho kubwa bila malipo nchini Tanzania.

Categories
Burudani

Esma Platinumz akiri kwamba ndoa yake imesambaratika

Dadake mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platinumz ambaye hujiita Esma Platinumz alithibitishia mashabiki wake kusambaratika kwa ndoa yake na Bwana Msizwa baada ya minong’ono kusheheni.

Mwezi mmoja uliopita dada huyo alizima maneno ya kuvunjika kwa ndoa yake ambapo alisema kwamba wako sawa na akakana pia swala la kuwa mjamzito.

Alikuwa ameolewa kama mke wa tatu na inasemekana wake wenza mmoja anaishi nchini Afrika Kusini na mwingine Tanzania. Ikumbukwe kwamba hii ni ndoa ya pili ya Esma ambayo imevunjika, na alipoingia kwenye ndoa hiyo miezi mitatu iliyopita, alisema kwamba aliona kitu kizuri na cha kipekee kwa mume wake Msizwa.

Esma alisema haya kupitia mtandao wa Instagram ambapo alialika mashabiki wake wamuulize maswali na akayajibu kupitia “Insta Stories”.

Alizungumzia mambo mengi tu kwenye kipindi hicho cha maswali na majibu na wafuasi wake. Aliulizwa kuhusu jinsi amekuwa akiishi na wake wenza ikiwa wamewahi kuzozana na akasema hajawahi kukosana nao.

Kuhusu kile ambacho wafuasi wake wanakiita ushamba wa mume wake kwa umaarufu, Esma alisema anaishi naye vile vile ila akizido anamkwepa yasije yakawa kama ya mwanamuziki Shilole na mume wake Uchebe ambao sasa wametalikiana.

Mwanadada huyo pia alizungumzia wanawake wote ambao kakake Diamond amekuwa kwenye mahusiano nao na akasema aliwapenda wote.

Alikiri kupenda watoto wote wa kakake. Esma na Diamond ni watoto wa mama mmoja lakini baba zao ni tofauti. Diamond ana dada mwingine ambaye ni mwanamuziki kwa jina Queen Darleen ambaye wana baba mmoja ila mama ni tofauti.

Categories
Burudani

Tanasha Donna kutembezwa Tanzania na mtangazaji Mwijaku

Mtangazaji wa redio na muigizaji nchini Tanzania kwa jina Mwijaku amesema kwamba atamwalika na kumtembeza mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna huko Tanzania.

Akizungumza katika tamasha kwa jina “Ushamba Night Party” lililoandaliwa na mwanamuziki Harmonize mtangazaji huyo alidokeza kwamba kwa sasa uhusiano kati yake na Tanasha ni mwema na anapania kumpeleka nchini humo na wafanye kazi kubwa.

Mwijaku alisema kwamba uchaguzi mkuu wa Tanzania ambao ulikamilika mwisho wa mwezi jana ndio ulichelewesha ziara hiyo ya Bi. Tanasha.

“Sasa nasubiri tu Rais mteule John Pombe Magufuli aapishwe ndio nimlete Tanasha.” aliendelea kusema Mwijaku.

Wawili hao walikaribia kukosana wakati fulani baada ya Mwijaku kudai kwamba yeye ndiye baba ya mtoto wa Tanasha na sio Diamond Platinumz.

Tanasha aligadhabishwa na hilo na kutishia kumchukulia hatua za kisheria ndipo akaombamsamaha na kuai kwamba alieleweka vibaya.

“Nilikuwa namaanisha kwamba hapa kwetu mtoto ni wa jamii kwa hivyo mtoto wa Diamond ni kama wangu tu. Wakenya walinielewa vibaya.” Mwijaku alisema.

Mwanamuziki wa muda mrefu wa Bongo Flavour Ray C alimkosoa Mwijaku wakati huo akimweleza kwamba jambo kama hilo halikuwa rahisi kama alivyokuwa akilichukulia. Alihimiza Tanasha kuchukua hatua za kisheria.

Inasubiriwa kuona ikiwa ni ukweli atakuwa mwenyeji wa Tanasha nchini Tanzania ili amtembeze hadi kwenye mbuga za wanyama ambazo anasema Tanasha hajawahi kujionea.

Categories
Burudani

Rayvanny Kuondoka Wasafi?

Fikra kuhusu uwezekano wa mwanamuziki kwa jina la usanii “Rayvanny” au ukipenda “Vanny Boy” kuondoka kwenye kampuni ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platinumz, zinatokana na usemi wa Diamond mwenyewe.

Wakati wa mahojiano yake kwenye kipindi cha ‘The Switch’, kwenye Wasafi FM siku ya jumanne, Diamond alifichua kwamba hivi karibuni Rayvanny anazindua kampuni yake ya kusimamia wanamuziki.

Diamond alisema ameona Studio ambazo Rayvanny anaandaa na kulingana naye zikizinduliwa zitakuwa bora kuliko zote nchini Tanzania.

Alipoulizwa kuhusu uhuru wa wanamuziki walio chini ya Wasafi kuondoka na kujiendeleza, Dianond alisema wana uhuru wa kufanya vile.

Mwimbaji huyo wa kutokea eneo la Tandale alisema kila mara huwa anawahimiza wanamuziki walio chini yake waishi vizuri na watu na watafute kujiendeleza kifedha.

“Iwe mfano ni mimi, nimefika hapa nilipo halafu wakati mmoja unikute kule Tandale nakuomba shilingi mia jamani! ikiwa ni mimi sitakupa!” Alisema mwanamuziki huyo.

Maneno yake yanaonekana kuwa kinaya kwani hadi sasa, kampuni ya Wasafi haijamwachilia kikamilifu mwanamuziki Harmonize ambaye aligura na kuanzisha kampuni yake kwa jina “Konde Music”.

Harmonize alifichua kwamba mkataba wake na WCB unamhitaji alipe milioni mia tano pesa za Tanzania kabla apate hakimiliki za nyimbo zake na kuandikisha hakimiliki yake mwenyewe.

Kulingana naye amelazimika kuuza mali nyingi kulipa deni hilo lakini bado hajalimaliza.

Inasubiriwa kuona ikiwa Rayvanny atagura Wasafi au atasalia tu akiendeleza biashara yake kando au atagura na ikiwa atagura safari yake itakuwa rahisi au ngumu kama ya Harmonize?