Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, imethibitisha kwamba karatasi za kupigia kura zimewasili kwenye vituo husika kabla ya chaguzi ndogo za tarehe 15 mwezi huu katika sehemu mbalimbali nchini.
Tume hiyo hiyo imesema kuwa masanduku yenye karatasi hizo yatafunguliwa mbele ya wawaniaji au waakilishi wao kabla ya kupelekwa kwenye vituo vya kupigia kura.
Aidha, IEBC iliandaa kikao na wachunguzi wa chaguzi Jumapili, ikisema tayari imewapatia mafunzo na kuwapa kiapo cha siri maafisa wa chaguzi hizo ndogo.
Tume ya IEBC pia ilishauriana na walemavu ikisema inaazimia kuhakikisha ujumuishaji wa kila mtu katika mchakato wa uchaguzi.
Chaguzi hizo ndogo zitaandaliwa katika Eneo Bunge la Msambweni kwenye Kaunti ya Kwale, Wadi ya Dabaso iliyoko Kaunti ya Kilifi na Wadi ya Kahawa Wendani, Naiorbi miongoni mwa nyingine.
Shughuli za kampeni kwa ajili ya chaguzi hizo zilitamatika usiku wa Jumamosi, masaa 48 kabla ya kura hizo kupigwa.
Uchaguzi mdogo wa Msambweni umeibua ushindani mkali kati ya mgombea wa chama cha ODM Omari Boga na mgombea huru Feisal Bader anayeungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.