Categories
Kimataifa

Bara la Ulaya laongeza juhudi za kukabiliana na maambukizi ya COVID-19

Jamhuri ya Czech inaweka kizuizi cha kadiri cha wiki tatu, huku ikifunga shule, baa na vilabu wakati Ulaya ikijitahidi kudhibiti kuongezeka kwa visa vya maradhi ya COVID-19.

Shule, baa na vilabu vitasalia kufungwa hadi tarehe tatu mwezi ujao huku migahawa ikiruhusiwa tu kuwasilisha chakula kwa wateja au kukiuza kwa kuwapakia, hadi saa mbili usiku kila siku.

Mabweni ya vyuo vikuu pia yanafungwa kwa muda, na masomo yataendeshwa wanafunzi wakiwa nyumbani kupitia mtandao.

Shule za chekechea zitasalia kufungwa na mikakati maalum kuwekewa watoto wa wafanyakazi wa kutoa huduma muhimu.

Kumerekodiwa vifo 1,051 vya kutokana na maradhi ya COVID-19 katika Jamhuri ya  Czech tangu tarehe mosi mwezi Machi, wakati taifa hilo lilipothibitisha kisa cha kwanza cha maradhi hayo.

Uholanzi pia iliamuru kufungwa kwa migahawa na unywaji wa pombe kwenye maeneo ya umma umepigwa marufuku na sharti barakoa zivaliwe katika maeneo hayo.

Naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwenye hotuba ya televisheni kuwa atatangaza vizuizi zaidi.

Chancella wa Ujerumani Angela Merkel amesikitishwa na  hali inayozidi kuzorota Barani Ulaya.

Categories
Kimataifa

Uingereza yamwondoa balozi wake nchini Belarus

Uingereza imemrejesha nyumbani Balozi wake aliye nchini Belarus kutokana na zogo la kisiasa linalokumba nchi hiyo.

Maafisa wa serikali jijini Minsk wamekabiliana na waandamanaji wanaopinga utawala wa Rais Alexander Lukashenko anayedai kuwa mshindi wa uchaguzi tata ulioandaliwa mwezi Agosti, mwaka uliopita.

Waziri wa maswala ya kigeni, Dominic Raab amesema, hatua hiyo inaambatana na msimamo uliochukuliwa na nchi za Poland na Lithuania, ambazo ni wakosoaji wakali wa Rais Lukashenko.

Siku ya Ijumaa, Belarus iliwatimua maafisa-35 wa Kibalozi kutoka nchi hizo mbili jirani.

Raab alikashifu hatua hiyo akisema itasababishwa kutengwa kwa raia wa nchi hiyo.

Nchi nyingine saba za Ulaya zikiwamo Ujerumani, Romania na Jamhuri ya Czech pia zimewaondoa mabalozi wao kutoka Belarus.

Mzozo huo wa kidiplomasia umezidisha uhasama kati ya Belarus na nchi za Ulaya.

Wiki iliyopita, jumuia ya Ulaya iliungana na Uingereza na Canada kuwawekea vikwazo maafisa wakuu wa serikali ya Belarus wanaodai kuchochea ukiukaji wa haki za binadamu hususan dhidi ya waandamanaji wa upinzani