Categories
Habari

Watu 866 waambukizwa COVID 19

Watu 866 wamepatikana kuwa na virusi vya corona na kuzidisha idadi ya maambukizi nchini na kuwa jumla ya watu  87,249.

Kwenye taarifa, waziri wa afya  Mutahi Kagwe, alisema kuwa idadi hii ilipatikana baada ya kupimwa kwa sampuli 7,815 katika muda wa saa  24 zilizopita.

Kaunti ya Nairobi ilizidi kuongoza kwa jumla ya maambukizi mapya 273 huku ikifuatwa na kaunti za Mombasa iliyokuwa na visa  78, kaunti ya Nakuru iliyokuwa na visa 73, kaunti ya Kiambu kwa visa 55, Kirinyaga visa  49, Nyamira visa  35, Kisumu visa 27 huku kaunti za Kilifi na  Kajiado zikinakili visa  23 kila mmoja.  Wagonjwa 1,194 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku wengine  7,984 wakitibiwa nyumbani.

Idadi ya wagonjwa walio katika chumba cha wagonjwa mahututi imeongezeka hadi wagonjwa  77 huku wale walio katika kituo cha  High Dependency Unit wakiwa kumi.

Wagonjwa sita zaidi waliaga dunia na kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa 1,506.

Kinyume na jana wakati taifa hili liliposhuhudia kupona kwa zaidi ya wagonjwa elfu 11, wagonjwa waliopona katika saa 24 zilizopita walikuwa 322.

Idadi jumla ya wagonjwa waliopata nafuu  nchini ni  68,110.

Categories
Kimataifa

Marekani yaitaja China kuwa tishio kubwa kwa demokrasia duniani

Mkurugenzi wa ujasusi wa rais wa Marekani anayeondoka, Donald Trump ametaja China kuwa tishio kubwa kwa demeokrasia na uhuru duniani tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Hata hivyo, China imedokeza kuhusu kuvurujika kabisa kwa uhusiano baina ya nchi hiyo na Marekani.

Mkurugenzi huyo wa shirika la kitaifa la ujasusi, John Ratcliffe amesema China inapania kutamalaki ulimwengu.

Katika makala yake kwenye jarida la Wall Street, Ratcliffe alisema hujuma za kiuchumi zinazotekelezwa na China zinalenga kuiba, kughushi na kubadili sera za kiuchumi.

Ubalozi wa China nchini Marekani umesema makala ya Ratcliffe yanapotosha na yamejikita kwenye fikira za vita baridi.

Aidha, ubalozi huo umedai kuwa seriali ya Marekani pamoja na kampuni zake imehusika kwenye vitendo vya wizi wa kimtandao.

Makala hayo ya Ratcliffe yalichapishwa wakati ambapo vyombo vya habari nchini China vimetilia shaka uhusiano baina ya nchi hizo mbili ambao umedorora zaidi katika miaka ya hivi punde kuhusiana na masuala ya biashara, haki za binadamu, jimbo la Hong Kong na janga la COVID-19.

Categories
Habari

Wenye mapato ya chini wasazwa huku hatua ya kuwapunguzia wakenya ushuru ikitamatika mwakani

Waziri wa fedha Ukur Yatani ametangaza kwamba hatua zilizotangazwa na serikali kuwapunguzia Wakenya ushuru kufuatia hali ngumu kiuchumi wakati wa janga la Covid-19 zitaondolewa kuanzia Januari mosi mwaka 2021.

Yattani alisema wale walio na mapato ya chini ya shilingi elfu-24 wataendelea kufurahia mpango kamili wa kuondolewa ushuru kwa kuto-tozwa ushuru wa mapato yaani “Pay As You Earn” (PAYE).

Alisema uamuzi huo umetokana na kulegezwa kwa baadhi ya masharti yaliyokuwa yamewekwa na serikali na kurejelewa kwa shughuli za kawaida.

Waziri alisema kwamba kuanzia Januari mosi mwaka 2021, kiwango cha ushuru wa mashirika kitapandishwa tena hadi asilimia 30 kutoka asilimia 25 kwa sasa.

Ushuru ziada wa thamani yaani (VAT), utapandishwa tena hadi asilimia 16 kutoka asilimia 14 kwa sasa.

Yattani aliwakumbusha WaKenya kwamba serikali haijatangaza viwango vipya vya ushuru, bali imerejesha viwango vilivyokuwepo kabla ya janga hilo la Covid-19.

Categories
Habari

Prof Magoha: Serikali haijaidhinisha nyogeza ya karo ya vyuo vikuu

Waziri wa elimu Professor George Magoha ametoa wito kwa wazazi na wanafunzi wa vyuo vikuu kutokuwa na wasiwasi kuhusiana na madai kuwa serikali inapanga kuongeza karo ya vyuo vikuu kutoka shilingi elfu 16 hadi shilingi elfu 48 kwa mwaka.

Profesa Magoha alisema kuwa licha ya kuwa kuna mazungumzo bungeni kuhusiana na hatua hiyo ya kuongeza karo ya vyuo vikuu, serikali haijakaa na kujadili swala hilo.

Magoha alidokeza kuwa karo hiyo haitaongezwa mara nne kuliko kiwango cha sasa.

Waziri alisema kuwa nyongeza hiyo ya karo haitatekelezwa bila kuwahusisha wadau wote.

Profesa Magoha hata hivyo alielezea kuridhika kwake na viwango vya madawati yaliyowasilishwa shuleni huku akisema kuwa mafundi waliotengeneza madawati hayo watalipwa kupitia kwa simu wiki moja baada ya kutayarishwa stakabadhi.

Magoha aliyasema hayo katika shule ya upili ya Kapsoit katika kaunti ya Kericho alipozuru shule hiyo ili kukagua iwapo inazingatia masharti yaliyowekwa kudhibiti virusi vya Covid-19.

Categories
Habari

kenya yanakili idadi ya juu zaidi ya walipona Covid-19 baada ya watu 11,324 kupata nafuu

Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini imeongezeka na kufikia watu 89,363 baada ya watu 1,253 zaidi kupatikana kuwa na virusi hivyo.

Idadi hiyo ilipatikana baada ya kupimwa kwa sampuli 10,750 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Katibu mwandamizi katika wizara ya afya Dkt. Rashid Aman pia alitangaza kuwa wagonjwa 16 waliaga dunia kutokana na virusi hivyo  na kufikisha idadi jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo kuwa  1,500.

Wakati huo huo, taifa hili limeandikisha idadi ya juu zaidi ya watu waliopona kwa siku hasa baada ya wagonjwa 11,324 kupata nafuu kutokana na virusi hivyo vya corona.

Idadi jumla ya waliopona kutokana na virusi hivyo sasa ni watu 67,788.

Kati ya watu  11,324 waliopona, watu 11,177  walikuwa wakitibiwa nyumbani huku wengine  147 wakiruhusiwa kuondoka katika hospitali mbalimbali kote nchini.

Dkt Aman aliongeza kuwa kwa sasa wagonjwa  1,200 wamelazwa katika hospitali mbalimbali kote nchini.

Wagonjwa  7,755 wanatibiwa nyumbani huku 73 wakiwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi na  31 wakitumia mashini za kuongeza hewa ya Oxygen. 

Nairobi iliandikisha idadi ya juu ya visa vipya huku ikinakili visa 326,  Mombasa 143,   Kilifi 105, Kiambu 86, Murang’a 67, Meru 45, Kirinyaga 43 na  Makueni 36.

Kaunti ya Migori iliandikisha visa 35, Embu 34, Laikipia 32, Nakuru 26, Machakos  25, Kitui 24, Taita Taveta 20, Bungoma 19, Siaya 18 na Lamu 17.

Nyeri  ilikuwa na 17, Uasin Gishu 14, Kajiado 13, Garissa 13, Nandi 12, Kisumu 12, Tharaka Nithi 11, Bomet 11, Homa Bay 10, Busia 7, Kakamega 6, Kwale 6, Samburu 6, Nyandarua 5, Jericho 4, Isiolo 3 na Turkana 2.

Categories
Habari

Afisa wa Polisi aliyemwuua mwanafunzi huko Malaba kwa kutovaa barakoa azuiliwa

Afisa wa Polisi aliyempiga risasi kimakosa mwanafunzi wa kidato cha pili katika eneo la Malaba Ijumaa iliyopita kwa madai ya kutovaa barakoa anazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea.

Hayo yamefichuliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa katika Bunge la Kitaifa, Paul Koinange.

Akitoa ripoti ya muda bungeni kuhusu hatua zilizopigwa katika uchunguzi wa kisa hicho, Koinange pia amefafanua kuwa Ezekiel Odera aliyeuawa kwa kupigwa risasi alikuwa miongoni mwa kundi la watu waliokuwa wakilalamika baada ya polisi kuwakamata watu wawili kwa kutovaa barakoa na wala siye aliyetuhumiwa kwa kutovaaa barakoa.

Kulingana na  Koinange, ni wakati wa rabsha hizo ambapo jiwe lilirushwa kwa polisi, hali iliyomlazimu mmoja wao kujibu kwa kufyatulia risasi kundi hilo na risasi ikampata Odera na akafariki papo hapo.

Aidha,  Koinange amesema maafisa wa Mamlaka Huru ya kutathmini utenda kazi wa Polisi (IPOA) kwa sasa wako Malaba kuchunguza kisa hicho.

“Imependekezwa kwamba uchunguzi wa kina ufanywe ili kubaini wazi hali iliyosababisha kisa cha kupigwa risasi kwa lengo la kuchukua hatua mwafaka,” amesema Koinange

Rabsha zilikumba mji wa Malaba siku ya Ijumaa kufuatia mauaji hayo yaliyotekelezwa na maafisa wa polisi waliokuwa wakitekeleza kanuni za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

Categories
Habari

Watu 961 zaidi waambukizwa COVID-19 Kenya, 854 wapona huku 10 wakiaga dunia

Wizara ya Afya humu nchini imeripoti visa vipya 961 vya maambukizi ya COVID-19 baada ya kupima sampuli 7,780 katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Kufikia leo, jumla ya visa vilivyoripotiwa imefikia 85,130 kutokana na upimaji wa jumla ya sampuli 901,426 tangu kisa cha kwanza kuripotiwa mnamo Machi 2020.

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, visa hivyo vipya ni pamoja na Wakenya 944 na raia wa kigeni 17.

626 kati yao ni wanaume, ilhali 335 ni wanawake, kati ya umri wa miezi mitano hadi miaka 94.

Kaunti ya Nairobi imeendelea kuongoza kwa visa 203, ikifuatwa na Nakuru kwa visa 118, Kilifi 83, Kirinyaga 71, Kericho 57,Uasin Gishu 52, Mombasa 41, Embu 41, Busia 40, Nyandaru 24, Kiambu 23, Kisumu 22, Isiolo 21, Nyeri 18, Nandi 16, Murang’a 14, Homa Bay 13, Kakamega 12, Nyamira 9, Turkana 8, Kajiado 7, Kwale 7, Trans Nzoia 7, Samburu 6, Vihiga 6, Siaya 6, Baringo 5, Taita Taveta 5, Kisii 5, Machakos 4, West Pokot 4, Mandera 2, Laikipia 2, Algeyo Marakwet 2, Bomet 1, Garissa 1, Bungoma 1, Marsabit 1 na Kitui 1.

Kufikia sasa jumla ya wagonjwa 1,240 wanahudumiwa katika vituo mbali mbali humu nchini huku wengine 7,755 wakiwa kwenye mpango wa uuguzi wa nyumbani.

Kati ya walio hospitalini, 74 wako kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi ambapo 33 wanatumia vifaa vya kusaidia kupumua na 40 wanapokea hewa ya Oksijeni ya ziada.

Wakati uo huo, watu 854 waliokuwa wakiugua COVID-19 wamepona, 686 kati yao walikuwa wakitibiwa nyumbani na 168 hospitalini. Jumla ya waliopona sasa ni 56,464.

Hata hivyo, wagonjwa wengine 10 wamethibitishwa kuaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kufikisha idadi ya waliofariki humu nchini hadi 1,484.

Categories
Habari

Tume ya TSC kuwaajiri walimu 6,674 wa muda

Tume ya TSC imetangaza nafasi za kazi za walimu wa muda 6,674  watakaohudumu katika shule za msingi na upili.

Walimu hao watasaidia kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi madarasani.

Kwenye tangazo lake katika magazeti ya humu nchini, tume hiyo imesema walimu-1,998 watapelekwa katika shule za msingi ilihali-4,676 watafunza katika shule za upili.

Kulingana na tangazo hilo kuajiriwa kwa walimu hao ni mojawapo wa mpango wa kufufua uchumi uliotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kwenye  hotuba yake ya saba kwa taifa kuhusu janga la Covid-19.

Watakaopelekwa katika shule za msingi watalipwa  shilingi alfu 15 kwa mwezi ilhali wale wa shule za upili watalipwa shilingi alfu 20 kila mwezi.

Walimu hao watahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja na watatunukiwa vyeti mwishoni mwa kipindi hicho.

Ili kufuzu kwa ajira hiyo, mtahiniwa sharti awe Mkenya halisi, awe na Stashahada ya elimu na awe amesajiliwa na tume ya TSC.

Kwenye mipango ya ufunguzi wa shule, TSC imesema itatoa mafunzo kuhusu mtaala mpya wa elimu CBC kwa walimu 118,000 kwa gharama ya shilingi bilioni  moja.

Categories
Habari

Watu 5 zaidi wafariki kutokana na COVID-19 huku wengine 551 wakiambukizwa

Wizara ya Afya imethibitisha visa vipya 551 vya maambukizi ya virusi vya Korona kutokana na sampuli 4,675 zilizopimwa katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Jumla ya visa 84,169 vya maambukizi ya Korona vimethibitishwa hapa nchini tangu kubainishwa kwa kisa cha kwanza mwezi Machi mwaka huu, ikiwa ni baada ya jumla ya sampuli 893,646 kupimwa.

Kati ya visa hivyo vipya, 525 ni Wakenya ilhali 26  ni raia wa kigeni.

Kijinsia, 301 ni wanaume na 250 ni wanawake, huku mgonjwa wa umri mdogo zaidi akiwa mtoto wa umri wa siku saba na yule wa umri mkubwa zaidi akiwa na miaka 100.

Kaunti ya Nairobi kwa mara nyingine imeongoza kwa maambukizi mapya kwa kunakili visa 212, ikifuatwa na Kilifi kwa visa 39, Mombasa 35, Nyeri 33, Embu 30, Nandi 25, Machakos 22, Siaya 21, Kajiado 19, Kiambu 18, Lamu 16, Nyandarua 14, Turkana 11, Uasin Gishu 8, Taita Taveta 7, Kisumu 7, Meru 6, Garissa 6, Kwale 5, Samburu 5, Murang’a 3, Mandera 2, Nakuru 2, huku kaunti za Busia, Laikipia, Kakamega, Wajir na Tharaka Nithi vikiripoti kisa kimoja kimoja.

Jumla ya wagonjwa 8,070 wako chini ya mpango wa kuhudumiwa nyumbani huku 1,275 wakilazwa katika vituo mbali mbali vya afya, 71 katika vyumba vya matibabu maalumu, 36 wanatumia vipumuzi na 34 wanaongezewa hewa ya oksigeni.

Hayo yamejiri huku wagonjwa 266 wakithibitishwa kupona, 206 chini ya mpango wa uuguzi wa nyumbani na 60 kutoka vituo mbali mbali vya afya nchini.

Hata hivyo, wagonjwa watano wameaga dunia na kuongeza idadi jumla ya vifo hadi 1,474.

Categories
Burudani

Mshauri wa Trump kuhusu Covid-19 Scott Atlas, ajiuzulu

Mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu virusi vya Korona anayekumbwa na utata, Dakta Scott Atlas,amejiuzulu.

Akimshukuru Rais Trump kwa kumpa fursa ya kuwahudumia Wamarekani akisema  nyakati zote alikuwa akitegemea hatua za hivi punde za kisayasi na ushahidi bila mwingilio au ushawishi wowote wa kisiasa.

Katika kipindi cha miezi minne akihudumu, Dkt Atlas alitilia shaka haja ya kuvalia barakoa  na hatua nyingine za kukabiliana na janga hilo.

Pia mara kadhaa alitofautiana na wanachama wengine wa jopo la kukabiliana na virusi vya Korona.

Daktari huyo alijiunga na jopo hilo mwezi Agosti. Mbali na kutilia shaka umuhimu wa kuvalia barakoa pia alipinga kufungwa kwa maeneo mbali-mbali.

Wataalam wa afya ya umma akiwamo Dkt Anthony Fauci wa kituo cha kukabiliana na magonjwa walimshutumu Atlas kwa kumhadaa na kumpotosha Rais Trump kuhusu virusi vya Korona.

Marekani imenakili takriban visa millioni 13 vya virusi vya Korona  na zaidi ya vifo elfu 266.