Categories
Michezo

Mali yatinga nusu fainali ya CHAN baada ya kuilaza Congo 5-4

Mali walijikatia tiketi kwa nusu fainali ya CHAN kwa mara ya pili katika historia baada ya kuwabandua Congo mabao 5-4 kupitia mikwaju ya penati kwenye nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Jumamosi usiku uwanjani Ahmad Ahidjo mjini Doual Cameroon.

Timu zote zilishindwa kutumia vyema nafasi zao za kupachika magoli huku makipa wakiwa ange na kuzima mashambulizi na kulazimisha kipindi cha kwanza na cha pili kuishia sare tasa.

Mkenya Dkt Peter Waweru aliyesimamia pambano hilo aliamurisha kupigwa dakika 30 za ziada ambazo pia ziliishia sare ndiposa penati zikapigwa kutenganisha timu hizo.

Mikwaju ya penati ilipigwa huku ile ya Congo ikifungwa na Julfin Ondongo, Hardy Binguila, Yann Mokombo na kipa  Pavelh Ndzila huku Prince Mouandzu Mapata akipiga mkwaju wake nje.

Mali waliunganisha penati zote 5 kupitia kwa Issaka Samake, Moussa Kyabou, Makan Samabali, Mamadou Doumba na  Mamadou Coulibaly  ikiwa mara ya pili kwa timu hiyo kufuzu nusu fainali baada ya kufanya hivyo kw amara ya kwanza mwaka 2016 nchini Rwanda.

Mali watapambana katika nusu fainali na mshindi kati ya Guinea na Rwanda watakaovaana kwenye robo fainali ya mwisho Jumapili usiku.

 

Categories
Michezo

Majirani wa Congo wafuzu robo fainali za CHAN

Timu mbili za Congo DR Congo na Congo Brazaville  zilitinga robo fainali ya kombe la CHAN nchini Cameroon baada ya kusajili ushindi Jumatatu usiku katika mechi mbili za mwisho za kundi B .

Congo Brazaville maarufu kama Red Devils waliibwaga Libya bao 1 -0 katika uwanja wa Japoma mjini Doula , baada ya mabeki wa Libya kushindwa kuondosha mpira katika lango lao na kumpa fursa Cautrand Ngouenimba aliyeuchupia na kuwapa Congo bao la uongozi na la  ushindi kunako dakika ya 52.

Awali na baadae timu zote zilikosa nafasi za kufunga magoli huku makipa wakilazimika kujituma na kupangua matobwe kadhaa.

Katika mechi iliyopigwa ugani Ahmad Ahidjo mjini Younde  DR Congo wajulikanao kama Leopards walijiongezea matumaini ya kutwaa kombe la CHAN kwa mara ya tatu baada ya kuhitaji muujiza wa dakika za mwisho kuipiga Niger   magoli 2-1  na kuongoza kundi B kwa pointi 7.

John Kadima aliwaweka kifua mbele DR Congo dakika ya 27 na kuongoza hadi mapumzikoni.

Hata hivyo the Menas ya Niger walijibu bao hilo kupitia kwa nguvu mpya  Mossi Issa Moussa dakika ya 73 baada ya mabeki wa leopards kusinzia na mechi kuonekana kuishia sare.

Kipa wa Niger Abdoul Razak Halidou alijaribu kuondosha pasi ya nyuma aliyopigiwa na difenda wake, lakini ikatua kwa miguu ya mshambulizi wa DR Congo Masasi Obanza aliyepachika bao rahisi dakika ya 90 na kuwapa Wakongomani ushindi muhimu.

DR Congo wameongoza kundi B kwa pointi 7 wakifuatwa na Congo kwa alama 4 huku Niger na Libya wakizoa pointi 2 kila moja.

Kufuatia matokeo hayo DR Congo watashuka uwanjani  Japoma Doula kukabiliana na wenyeji Cameroon kwenye robo fainali ya Jumamosi hii wakati Congo Brazzaville wakisafiri hadi Yaounde katika uwanja wa Ahmad Ahidjo kupambana na Flying Eagles ya Mali kwenye kwota fainali nyingine.

 

 

Categories
Michezo

Chui wa DRC waanza vyema kuwinda kombe la tatu la CHAN

Mabingwa mara mbili wa kombe la CHAN DR Congo wa walianza vyema harakati za kuwania kombe la tatu baada ya kuwadhibu majirani zao Congo Brazzavile bao 1-0 katika mchuano wa kundi B uliopigwa Jumapili usiku katika uwanja wa Japoma mjini Douala Cmaeroon.

DRC maarufu kama Leopards  walitawala mchuano huo kutoka mwanzo hadi mwisho huku wakibuni nafasi nyingi za kupachika magoli lakini Red Devils ya Congo walicheza mchezo wa kujihami na kulazimisha sare tasa kipindi cha kwanza.

Mshambulizi Chico Ushindi wa Kubanza alitumia vyema udhaifu wa safu ya nyuma ya Congo na kufyatua tobwe lililotua kimiani katika dakika ya 46 ya mchezo huku bao hilo likidumu hadi kipenga cha mwisho .

Ilikuwa ni mechi ya kulipiza kisasi kwa Leopards baada ya kufungiwa nje ya makala ya CHAN mwaka 2018 na Red Devils.

Katika pambano la awali la kundi hilo Niger walipoteza nafasi nyingi huku wakiambulia sare tasa na mabingwa wa mwaka 2011 Libya .

Msimamo wa makundi ya A na B baada ya mechi za mzunguko wa kwanza ni kama ufuatao;

Cameroon wanongoza kundi A kwa alama 3 wakifuatwa na Mali pia kwa pointi tatu huku Zimbabwe na Burkinafasso wakiwa bila alama.

DR Congo wanaongoza kundi B kwa alama 3 wakifuatwa na Libya na Niger kwa pointi 1 kila moja wakati Congo ikishika mkia bila alama.

 

 

Categories
Burudani

Akon aingilia biashara ya madini nchini Congo

Mwanamuziki wa Marekani wa mtindo wa R&B Aliaune Damala Badara Akon Thiam maarufu kama Akon ameingilia biashara ya kuchimba madini katika nchi ya Congo.

Kampuni yake imeingia kwenye mkataba na kampuni ya serikali ya Congo ya kuchimba madini – Sodimico, ambapo atatoa usaidizi wa kifedha katika eneo moja la kuchimba madini.

Mwanamuziki huyo ambaye ana asili ya Senegal barani Afrika amekuwa akijihusisha na biashara tofauti na mipango ya usaidizi barani Afrika kwa miaka ya hivi karibuni.

Anajenga jiji lake nchini Senegal kwa gharama ya dola bilioni sita za marekani na anamiliki biashara ya hela kwa jina Akoin.

Kampuni anayosimamia Akon iliyosajiliwa nchini Marekani ‘White Waterfall LLC’ imekubaliana na serikali ya Congo, kutoa dola milioni mbili za Marekani ambazo zitatumika katika kuendesha shughuli kwenye sehemu ya kuchimba madini inayoitwa Kimono katika mkoa wa Haut Katanga nchini Congo.

Nchi ya Congo ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa madini ya Copper barani Afrika na inaongoza kwa uzalishaji wa madini ya Cobalt ulimwenguni.

Cobalt hutumika kuunda betri za gari.

Kulingana na maelezo kwenye tovuti yake, kampuni ya White Waterfall LLC huwekeza kwenye kampuni za kuchimba madini lakini hakujatolewa orodha ya kampuni ambazo imewahi kushirikiana nazo.

Categories
Burudani

Wazito wa Rhumba ambao Watoto walifuata nyayo zao

Muziki wa Rhumba ambao asili yake ni nchini Congo unapendwa sana ulimwenguni kote na vizazi vyote lakini wengi wanaoushabikia ni watu wa umri mkubwa.

Wale ambao walipata nafasi ya kuhudhuria tamasha za wanamuziki kama vile Franco wakiwa vijana. Wengi wa wanamuziki tajika katika fani hiyo wameshaiaga dunia lakini miziki yao bado iko hai.

Huwezi kukosa kumtaja Franco Luanzo Luambo Makiadi unapozungumzia rhumba kwani alitawala muziki nchini Congo kwa muda mrefu na wadadisi wanasema kwamba yeye alikuwa na tabia ya kunyakua kila kipaji kipya ambacho kilikuwa kikichipuza wakati huo na kukiweka chini ya kundi lake la TPOK Jazz.

Hata baada ya kung’aa kwa namna ya kipekee, hakuna mtoto wake, kati ya wote 18, ambaye alifuata nyayo zake katika muziki.

Mwanawe wa kiume kwa Emongo Luambo anaishi mjini Brussels nchini Ubelgiji ambapo anasemekana kuendeleza biashara ya familia yao.

Gwiji mwingine wa muziki wa Rhumba ni Madilu System au ukipenda Jean De Dieu Makiese ambaye alitamba sana. Sio mengi yanafahamika kuhusu familia yake ila inasemekana aliacha mke kwa jina ‘Biya’ na watoto.

Tofauti na hao wawili wa kwanza kulikuwa na Tabuley Rochereau anayefahamika sana kwa kibao “Muzina” ana mtoto ambaye alirithi taaluma yake ya muziki. Mtoto huyo ni wa kiume kwa jina “Pegguy Tabu” ambaye ana kazi nyingi tu za muziki.

Pegguy Tabu

Pegguy pia aliwahi kushirikiana na Koffi Olomide kwa kufanya upya kibao cha marehemu babake kwa jina “Mokolo Nakokufa” maanake “siku nitakufa”.

Pegguy ana kazi nyingine nyingi za muziki. Tabuley aliaga dunia mwaka 2013 lakini mwanamuziki Tshala Muana, ambaye anasemekana kuwa mpenzi wake wakati huo, anahuisha miziki yake ambayo amekuwa akirekodi upya.

Kuna pia daktari wa Rhumba kwa jina Verckys Kiamungana Mateta ambaye sasa ana umri wa miaka 76. Verckys alikuwa mwafrika wa kwanza nchini Congo kumiliki kampuni ya kurekodi muziki na kusimamia wanamuziki. Aliwahi kufanya kazi na Franco kwenye kundi la TPOK Jazz lakini baadaye akaanzisha bendi yake kwa jina ‘Ochestre Veve’ nyingine ‘Ochestre Kiam’ na nyingine ‘Ochestre Lipua Lipua’.

Mwanamuziki huyo mkongwe ana mtoto wa kike kwa jina “Ancy Kiamungana” ambaye pia ni mwanamuziki. Kwa sababu ambazo hazijulikani, mwanadada huyo amezamia tu kufanya marudio ya nyimbo za babake na za wanamuziki wengine maarufu kama Koffi Olomide na Fally Ipupa.

Ancy kiamungana

Ancy na babake Verckys walishirikiana kwa kurudia wimbo wake wa zamani kwa jina “Ngai nakomitunaka”. Sikiliza;

Marehemu M’pongo Love, alipata umaarufu kutokana na kibao chake cha mapenzi kwa jina ‘Ndaya’. Mwanadada huyo aliacha kazi kama karani afisini na kuingilia muziki akiwa bado mdogo ambapo alianzisha bendi kwa jina ‘Tcheke Tcheke Love’ .

Kwenye nyimbo zake, alitetea sana wanawake na kukashifu maswala kama ndoa za wake wengi na tabia ya waume kuweka wake wengine kisiri.

M’pongo Love aliaga dunia mwaka 1990 na aliacha watoto watatu wote wa kike. Kifungua mimba wake Sandra Mpongo anasemekana kujaribu kufuata nyayo za mamake kimuziki na pia ameanzisha wakfu kwa jina la marehemu mamake kwa nia ya kusaidia watoto na wanawake walemavu.

Sandra Mpongo

Christy Lova mtoto wa kike wa Dalienst Ntesa ambaye alikuwa akiimba chini ya kundi la TPOK Jazz naye aliingilia muziki na alijulikana sana baada ya kurudia kibao cha babake kwa jina “Bina na Ngai na Respect” yaani cheza nami kwa heshima.

Kando na kibao hicho, Christy ameimba nyimbo zingine kama vile ‘Mytho’, Dolce vita’, na ‘To Bina’.

Ni baadhi tu ya wanamuziki wa Congo ambao watoto wao wamefuata nyayo zao.

Categories
Burudani

Sihitaji walinzi nalindwa na Mungu, Koffi Olomide

Mwanamuziki wa muda mrefu wa nchi ya Congo Koffi olomide au ukipenda Le Grand Mopao au Boss ya Mboka amefichua kwamba yeye huwa hatembei na walinzi kwani anaamini kwamba analindwa na Mungu.

Koffi aliyasema hayo kwenye studio ya Wasafi Fm wakati yeye na Diamond Platnumz walikuwa wanazindua kibao chao kwa jina “Waaa”.

Hapo hapo kwenye kipindi cha ‘The Switch’ ilifichuka kwamba Koffi ana ujuzi wa kiwango cha juu katika mchezo wa Karate maanake ana “Black Belt”.

Alisema kwamba akikasirika yeye huwa mbaya na anaweza kuumiza mtu na ndio maana wakati wote anajituliza na kupoesha hasira.

Ama kweli ana ujuzi huo ikikumbukwa teke aliyomrushia mmoja wa wacheza densi wake katika uwanja wa ndege nchini Kenya kitendo kilichosababisha atimuliwe hata kabla ya onyesho lake.

Boss ya Mboka anatarajiwa kuendelea kukaa nchini Tanzania kwa muda kulingana na usemi wa Diamond kwamba ana video nyingine anafaa kuandaa.

Duru za kuaminika zinaarifu kwamba video hiyo ni ya kibao cha Koffi na Nandy au ukipenda African Princess. Wakati wa mahojiano Koffi alifichua kwamba ameshirikiana pia na Nandy kwenye muziki na dada huyo amekuwa akimsukuma wafanye video lakini akampa Diamond nafasi ya kwanza.

Alipoulizwa kuhusu kitu ambacho amependa sana nchini Tanzania, Koffi alisema kwamba ni wanawake ambao kulingana naye ni warembo.

Tukio jingine ambalo linatarajiwa kumweka Koffi nchini Tanzania ni ziara inayofanywa na Wasafi Media kwa ushirikiano na Tigo na Pepsi ambapo Diamond alimwalika kwenye ziara ya mwishi mjini Daressalaam. Jana mwanamuziki huyo alikwenda kwenye mkahawa wa Shilole kwa jina Shishi food kwa chakula cha mchana.

Categories
Burudani

Waaaa!! Diamond na Koffi

Hatimaye Diamond Platnumz na Koffi Olomide wamezindua wimbo ambao wamekuwa wakitayarisha. Wimbo wenyewe unakwenda kwa jina “Waaa”.

Diamond ndiye anafungua wimbo kwa maneno, “Anachukua anaweka waaa” ambayo anarudia rudia naye Mopao chini kwa chini anajitambulisha na kutambulisha Diamond kama ‘Le general Dangote’ na ‘Le grand Mopao Boss ya Mboka’, kisha Diamond anaendelea kwa kusifia mwanadada mpenzi wake akisuta mahasidi kwamba lolote wanaloona baya kwa mwanadada huyo haliwahusu.

Mopao anaingia japo kidogo tu kwa sauti yake nzito ndiye anatoa neno ‘Waaa’ ambalo lipo kwenye pambio.

Baadaye Mopao au Koffi anaingia na ile Seben yake ya ‘Papa Mobimba’ naye Diamond anaingia na mtindo wa kusalimiana kwa miguu mtindo ambao ulipendekezwa kama njia ya kuamkuana na kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona. Anashauri watu pia kuzingatia kanuni za kuzuia kusambaa kwa Corona.

Anaimba, “Usiniguse usini touch tusalimiane kwa miguu, usinisalimie, usinikaribie kuna Corona.” mambo yanayokwenda kinyume na msimamo wa serikali ya Tanzania ambayo ilitangaza kwamba hakuna tena virusi vya Corona nchini humo.

Kuna watu kadhaa wa karibu ambao wasanii hao wawili wamewataja kwenye wimbo huo kama vile binti yake Koffi kwa jina Didi Stone na Mama Dangote.

Wawili hao wamejulikanisha sauti ya wimbo tu, video bado.

Kabla ya kuzindua wimbo huo, Koffi alipigia debe wimbo wake kwa jina ‘B’ados’ huku akisihi Wasafi Media wawe wakiucheza.

Simba alimwalika Koffi ahudhurie ziara ya mwisho kwa jina “Tumewasha na Wasafi” ushirikiano wa Wasafi, Tigo na Pepsi ambayo itakuwa Jijini Dar es Salaam.

Categories
Burudani

Ushirikiano wa Koffi Olomide na Diamond Platnumz

Mwanamuziki wa nchi ya Congo Koffi Olomide aliwasili nchini Tanzania ijumaa tarehe 20 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020, ambako alipokelewa na mwanamuziki Abdul Naseeb au ukipenda Diamond Platnumz.

Akihojiwa katika uwanja wa ndege siku hiyo, Koffi, ambaye pia hujiita ‘Mokonzi ya Mboka’ yaani ‘Mfalme wa ulimwengu’ alielezea kwamba alikuwa nchini Tanzania kwa ajili ya ushirikiano wa muziki na Diamond ambaye alimwita mfalme wa muziki nchini Tanzania.

Kwa upande wake Diamond ajulikanaye kwa jina lingine kama Simba, hakutaka kusema lolote kwenye uwanja wa ndege.

Mapema leo wawili hao walichapisha picha na video fupi wakiwa wanarekodi muziki kwenye studio na baadaye Diamond akachapisha tangazo kwenye ukurasa wake wa Instagram akisihi wafuasi na mashabiki watazame Wasafi Tv na wasikilize Wasafi fm kesho saa nne asubuhi na huenda ni uzinduzi wa wimbo wao utafanyika.

Kulingana na video hiyo, huenda wimbo wenyewe ni ‘remix’ ya wimbo kwa jina ‘Papa Ngwasuma’ wake Koffi. Wadadisi wanasema kwamba collabo hiyo, itakuwa kwenye albamu ya nne yake Diamond Platnumz.

Mida ya saa nane hii leo, Koffi alipachika kipande cha video ambayo wanatayarisha.

Koffi alikuwa na tamasha nchini Tanzania tarehe saba mwezi Marchi mwaka huu na kampuni ya Diamond Wasafi Media ndiyo ilimpa huduma za matangazo na huenda wazo la kushirikiana lilizaliwa wakati huo.

Diamond Platnumz amekuwa akishirikiana na wasanii wakubwa ulimwenguni katika muziki na wa hivi karibuni kabisa ni Alicia Keys ambaye amemsifia sana Diamond.

Categories
Burudani

Tshala Muana akamatwa na baadaye kuachiliwa

Mwanamuziki wa nchi ya Congo Mama Tshala Muana alikamatwa jumatatu mchana mjini Kinshasa nchini Congo.

Duru zinaarifu kwamba Malkia huyo wa Mutuashi alitiwa mbaroni kutokana na wimbo ambao alirekodi na kuuzindua kwa jina “Ingratitude” maanake kutokuwa na shukrani. Alizindua wimbo huo wiki jana na tangu wakati huo, umekuwa ukizungumziwa sana nchini Congo.

Maneno ya wimbo huo yanasemekana kumlenga Rais wa sasa wa nchi ya Congo Felix Tshisekedi kwa kile ambacho kinasemekana kumgeukia mwandani wake Rais wa zamani wa nchi hiyo Joseph Kabila ingawaje hakuna majina ambayo yametajwa.

Mtayarishaji wa Tshala Muana wa muziki kwa jina Claude Mashala alielezea kwamba maafisa kutoka kitengo cha “National Intelligence Agency, ANR, walimkamata kama mhalifu bila kuheshimu umri wake na kujali afya yake.

Hivi maajuzi kulisambazwa picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha Mama Tshala Muana akiwa anaugua hospitalini.

Inasemekana kwamba Kabila alimsaidia Tshisekedi kuunda serikali ya muungano hata kama muungano huo haujakuwa ukifanya vyema.

Tshala Muana wa umri wa miaka 62 sasa, ni rafiki ya Kabila na alikuwa pia akipigia debe chama chake cha People’s Party for Reconstruction and Democracy,PPRD.

Uhusiano wao unaonekana kujengwa na hatua ya babake Joseph Kabila, Laurent Kabila ya kumteua Tshala Muana kama mbunge wakati akiwa mamlakani.

Kukamatwa kwa mwimbaji huyo wa kibao maarufu ‘Nasi Nabali’ kulisababisha wanawake kadhaa kuandamana katika barabara za mji wa Kinshasa wakitaka aachiliwe huru.

Mama huyo ambaye ni kiungo muhimi katika muziki wa nchi ya Congo aliachiliwa jana jumanne baada ya chama chake cha PPRD kufanya kila juhudi kuhakikisha uhuru wake.

Tshala Muana akiwa amezingirwa na wafuasi wake muda mfupi baada ya kuachiliwa huru
Categories
Burudani

Kibao cha kuenzi mamake Koffi olomide kuzinduliwa leo

Wiki moja baada ya mazishi ya mamake mzazi, mwanamuziki wa nchi ya Congo Koffi Olomide yuko tayari kuzindua kibao cha kusifia na kumkumbuka mwenda zake.

Kupitia akaunti zake kwenye mitandao ya kijamii, Koffi kwa jina halisi Antoine Christophe Agbepa Mumba alitangaza hayo.

“Hamjambo marafiki. Nashukuru kwa kuniunga mkono na jumapili hii tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020 saa mbili usiku mtapokea rasmi video ya kibao cha ‘Mama Amy’ kwenye akaunti yangu ya Youtube. Wimbo ambao nilimwimbia mama. Usikose” Ndiyo maneno yake Koffi.

 

Mama Amy ambaye ni mama mzazi wa Koffi Olomide aliaga dunia tarehe tatu mwezi huu wa Oktoba mwaka 2020 na akazikwa tarehe 16 huko ufaransa.

Wanamuziki wenza kama vile Fally Ipupa walihudhuria mazishi hayo yaliyosheheni majonzi mengi. Koffi kwa wakati mmoja alizidiwa na kuangua kilio.

Wakati mamake aliaga dunia, Koffi alikuwa anajitayarisha kuzindua kibao kipya kwa jina “Danse ya ba congolais” yaani densi ya watu wa nchi ya Congo.

Koffi pia ametangaza tamasha atakaloandaa mwezi februari mwakani huko ufaransa.