Atlas lions ya Moroko ilifanikiwa kuhifadhi kombe la bara Afrika kwa wachezaji wanaosakata soka katika ligi za Nyumbani maaru kama CHAN baada ya kuwagaragaza Mali mabao 2-0 katika fainali iliyopigwa Jumapili usiku katika uwanja wa Ahmadou Ahidjo mjini Yaounde Cameroon.
Fainli hiyo ilisimamiwa na refarii wa Kenya Dkt Peter Waweru ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha JKUAT akisaidiwa na mwenzake Gilbert Cheruiyot huku pia akiandikisha historia kuwa Mkenya.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizikia sare tasa kipindi cha pili timu zote zilirejea kwa lengo la kusaka magoli lakini kipa Anas Zniti wa Moroko alikuwa ange na kuzima mashambulizi yote ya Mali.
Soufiane Bouftini aliwaweka Moroko uongozini kwa bao la dakika ya 69 akiunganisha mkwaju wa kona naye Ayoub El Kaabi akaongeza la pili dakika ya 79.
Moroko waliokuwa wamenyakua kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2018 wakiwa wenyeji, ndiyo timu ya kwanza kuhifadhi kombe hilo huku ikiwa mara ya pili kwa Mali kupoteza katika fainali baada ya kushindwa na DR Congo mwaka 2016 nchini Rwanda.
Soufiane Rahimi wa Moroko aliibuka mfungaji bora kwa mabao 5,lakini Yakoub El Kaabi pia kutoka Moroko akaweka rekodi ya kuwa mfungaji bora tangu kuanza kwa mashindano ya CHAN mwaka 2009 akifunga mabao 12 kwa jumla.
Rahimi pia alituzwa kuwa mchezaji bora wa michuano ya mwaka huu nchini Moroko .
Makala ya mwaka 2022 ya CHAN yataandaliwa nchini Algeria.