Categories
Burudani

Kazi mpya kutoka kwa Mheshimiwa Professor Jay.

Mwanamuziki wa Tanzania Joseph Haule maarufu kama Professor Jay amerejelea kikamilifu kazi ya muziki ambayo aliiweka pembeni kwa miaka mitano wakati akihudumu kama mbunge wa eneo la Mikumi.

Alichaguliwa kama mbunge wa eneo hilo mwaka 2015 kupitia chama cha CHADEMA kwa kipindi cha miaka mitano kisha akabanduliwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Professor Jay aliamua kurejelea muziki mara moja pale ambapo alishirikishwa na mwanamuziki Stamina kwenye kibao kwa jina “Baba” ambacho kilizinduliwa mwezi Januari mwaka huu wa 2021.

Kibao hicho ni cha ushauri na mafunzo kwa jamii hasa kwa watoto ambao hawatilii maanani ushauri wa wazazi kisha wanapokua wanagonga ukuta na kuanza kulaumu tena wazazi.

Marehemu John Pombe Magufuli ambaye alikuwa rais wa serikali ya muungano wa Tanzania, alipendelea sana kibao hicho kutokana na hatua yake ya kukiitisha wakati alizuru studio za Africa Media Group Tanzania siku chache kabla ya kifo chake.

Na sasa mwanamuziki huyo ana kazi mpya kwa jina “Utaniambia nini”. Kwenye kibao hicho, anaonekana kusifia tajriba aliyonayo katika maisha kwani alianza muziki kitambo, muziki ukampa nafasi kama mbunge na sasa ameurejelea.

Vile vile katika wimbo huo kuna mstari mmoja ambapo anaomba heshima yake au ajichukulie kwa nguvu na anahangaa kuzungumziwa sana katika mitandao ya kijamii kuna maana gani ikiwa wahusika wanapoteza dira.

Hapa anazungumzia wanamuziki ambao hutunga visa vya ajabu ili wasalie kwenye ndimi za mashabiki jambo ambalo hurejelewa kama “Kiki” na watanzania.

Categories
Burudani

Professor Jay arejelea muziki

Joseph Haule maarufu kama Professor Jay amerejelea muziki baada ya kugonga mwamba kwenye siasa na uongozi nchini Tanzania.

Jay ambaye ana umri wa miaka 45 sasa ni mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Aliendeleza kazi hiyo ya muziki iliyompa umaarufu hadi mwaka 2015 alipowania kiti cha ubunge katika eneo la Mikumi na kushinda.

Akihudumu kama mbunge kazi ya muziki aliisimamisha kabisa. Mwaka jana kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Professor Jay na wengine wengi wa chama cha “CHADEMA” walibwagwa. Aliyemshinda katika ubunge wa Mikumi ni Dennis Lazaro wa chama cha CCM.

Tangu wakati huo amesalia kimya hadi maajuzi alipojitokeza tena kwenye ulingo wa muziki kupitia kwa mwanamuziki mwenzake Stamina.

Stamina amemshirikisha Jay kwa ngoma yake mpya kwa jina “Baba” ambayo ilizinduliwa rasmi jana tarehe 13 mwezi Januari mwaka 2021.

Professor Jay alitangaza ujio wa kibao hicho kipya kwenye akaunti yake ya Instagram huku akihimiza mashabiki wakakitazame kwenye akaunti ya Stamina ya You tube.

Duru zinaarifu kwamba sasa jay ambaye anaigiza kama babake Stamina kwenye video ya wimbo huo amerejelea muziki kikamilifu.

Stamina anafungua wimbo huo akimpigia babake simu huku akimzomea na kumlaumu kwa matatizo anayopitia maishani.

Anamuuliza ni kwa nini hakumpeleka mamake akaavye mimba yake kwani anasikia aliikataa hiyo mimba.

Analaumu babake pia kwa ufukara anashangaa ni kwa nini wanaishi nyumba ya kupangisha na hamiliki hata shamba.

Anapoingia babake, anamwelezea kwamba vipimo vilionyesha kwamba yeye sio babake mzazi ila aliamua tu kumlea kama baba mzazi na anashangaa ni kwa nini hakusoma ajitengenezee maisha mazuri.

 

Categories
Kimataifa

Rais Magufuli aapishwa kuongoza Tanzania kwa muhula wa pili

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ameapishwa kuiongoza taifa hilo kwa muhula wa pili.

Rais Magufuli alitetea wadhifa wake baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ulioandaliwa nchini humo tarehe 28 mwezi Oktoba mwaka huu.

Tume ya uchaguzi nchini Tanzania ilitangaza kuwa Magufuli alipata kura 12,516,252 hii ikiwa ni asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa.

Mwaniaji kiti hicho cha Urais wa upinzani Tundu Lissu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, alikuwa wa pili kwa kuzoa jumla ya kura 1,933,271.

Hata hivyo upinzani nchini Tanzania ulidai kuwa shughuli hiyo ilikumbwa na udanganyifu huku ukitaka zoezi hilo kurudiwa upya.

Raia wa Tanzania walifika katika uwanja wa michezo wa Dodoma, kuhudhuria sherehe hizo kuanzia saa kumi na mbili alfajiri.

Mataifa 12 yaliwakilishwa katika sherehe hiyo sawia na wawakilishi kutoka muungano wa Afrika AU.

Kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo NEC, kati ya watu 29,754,699 waliojiandikisha kupiga kura, ni watu 15,91950 waliojitokeza kupiga kura hizo.

Awamu hii ya pili ya Magufuli itakamilika mwaka 2025.

Categories
Kimataifa

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tanzania, akamatwa kwa madai ya kupanga ghasia

Maafisa wa polisi nchini Tanzania wamemtia nguvuni mwenyekiti wa chama cha upinzani CHADEMA, Freeman Mbowe kwa madai ya kupanga gasia za baada ya uchaguzi nchini humo.

Polisi wamesema Mbowe alikamatwa pamoja na viongozi wengine wawili wa chama hicho kwa madai ya kupanga ghasia wakati wa maandamano dhidi ya matokeo ya uchaguzi yaliyozozaniwa.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa Ijumaa iliyopita, mwaniaji wa chama cha CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alishinda kwa asilimia 84 ya kura zilizopigwa.

Hata hivyo, upinzani unadai uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura na kuwahimiza raia kuandamana kupinga matokeo yake.

Mwaniaji wa upinzani Tundu Lissu anadai mawakala wa chama chake walizuiwa kuingia ndani ya baadhi ya vituo vya kupigia kura ambako masanduku ya kura yalivurugwa.

Mwishoni mwa juma, viongozi wa vyama vya CHADEMA na ACT-Wazalendo waliwarai wafuasi wao kuandamana kwa amani kupinga matokeo hayo.

Hata hivyo polisi wamedai taarifa za kijasusi zinaashiria kuwa waandamanaji hao walinuia kuteketeza masoko na vituo vya petroli.

Categories
Kimataifa

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vyataka uchaguzi mkuu urudiwe upya

Vyama viwili vikuu vya upinzani nchini Tanzania vimeshinikiza kuandaliwa kwa uchaguzi mpya baada ya kupinga uchaguzi wa urais wa  juma lililopita vikisema ulikumbwa na udanganyifu.

Vyama hivyo vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kile cha Alliance for Change and Transparency-Wazalendo (ACT-Wazalend),kwenye mkutano wa pamoja na wanahabari pia vilitoa wito wa maandamano kuanzia siku ya Jumatatu.

Rais John Magufuli alitangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi uliofanyika siku ya Jumatano akiwa amepata asilimia 84 ya kura.

Chama cha CHADEMA kimedai kwamba masanduku ya kura yalivurugwa baada ya maajenti wake kuzuiwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.

Kiongozi wa cha chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe alsiema kuwa uamuzi huo unahusiana na kile alichokitaja kuwa hatima ya nchi hiyo.

Mwaniaji urais wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu alipata asilimia 13 ya kura. Mkuu wa tume ya kitaifa ya uchaguzi, Semistocles Kaijage, alisema kwamba madai ya karatasi bandia za kura hayana msingi. Ujumbe wa uchunguzi wa jumuiya ya Afrika mashariki ulisema kuwa uchaguzi huo ulitekelezwa kwa njia ifaayo.

Hata hivyo ubalozi wa marekani jijini Dar es Salaam ulisema kuwa kasoro pamoja na tofauti kubwa katika asilimia ya kura za mshindi zinaibua shauku kuhusiana na uadilifu wa matokeo hayo.

Categories
Burudani

Mwana Falsafa, Babu Tale, sasa ni wabunge Tanzania

Hamis Mwinjuma mwanamuziki wa mtindo wa Hip Hop nchini Tanzania almaarufu “Mwana Falsafa” au ukipenda “Mwana Fa” sasa ni Mbunge nchini Tanzania.

Atawakilisha eneo la Muheza bungeni kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Yeye ni mmoja wa watu zaidi ya elfu kumi ambao walijitosa kwenye kinyanganyiro cha kutafuta tiketi za chama cha CCM mwezi Agosti mwaka huu, ili kutafuta viti vya ubunge kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania.

Baada ya kupata tiketi hiyo Hamis Mwinjuma aliingilia Kampeni, uchaguzi ukafanyika Jumatano 28 Oktoba mwaka huu na akamshinda Yosepher Komba wa CHADEMA.

Mwana Fa alizoa kura 47,578 huku Komba akipata kura 12,034. Sio mengi yanafahamika kuhusu familia ya Mwana Fa ila alifunga ndoa mwana 2016 na binti kwa jina Helga na arusi ilihudhuriwa na watu wachache tu licha ya kwamba yeye ni mtu maarufu.

Mwanamuziki huyo aliingilia fani hiyo mwaka 1995 akiwa bado anasoma shule ya upili na hadi sasa ameendelea kufurahia uungwaji mkono wa mashabiki wake na wapenzi wa muziki nchini Tanzania.

Mhusika mwingine wa sanaa nchini Tanzania ambaye ameingia bungeni kupitia uchaguzi mkuu wa hivi punde ni meneja wa wasanii maarufu kama Babu Tale ambaye ni mmoja wa walioanzisha WCB.

Meneja huyo ambaye jina lake halisi ni Hamisi Shabaan Tale Tale wa chama cha CCM hakuwa na mpinzani katika kuwania kiti cha ubunge eneo la Morogoro Kusini Mashariki na hilo lilisababisha atangazwe mshindi.

Mwaka huu umekuwa wa huzuni na furaha kwake kwani alifiwa na mke wake kwa jina Shammy mwisho wa mwezi juni na sasa amepiga hatua maishani na kuwa kiongozi.

Categories
Burudani

Mwanamuziki Professor Jay ashindwa kutetea kiti cha ubunge

Joseph Haule almaarufu Professor Jay mwanamuziki ambaye aliingilia siasa nchini Tanzania alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge wa eneo la Mikumi katika uchaguzi mkuu ulioganyika jumatano.

Jay wa chama cha CHADEMA alibwagwa na Dennis Lazaro wa chama cha CCM ambaye alizoa kura 31,411 na Professor Jay akapata kura 17,375.

Kiongozi wa chama chake Bwana Tundu Lissu anaonekana kutoridhishwa na shughuli nzima ya uchaguzi akisema ilikumbwa na udanganyifu kwani maajenti wake walizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupiga na kuhesabu kura.

Haule amekuwa mbunge wa Mikumi kwa miaka mitano sasa na alishinda uchaguzi wa mwaka 2015 kupitia chama chake cha CHADEMA.

Wakati huo alijizolea kura 32,259.

Professor Jay ana umri wa miaka 44 sasa na amekuwa kwenye fani ya muziki tangu mwaka 1989 akiwa mmoja wa wasanii katika kundi la “Hard Blasters” na wakati huo alikuwa anajiita “Nigga J”.

Kundi hilo lilizindia albamu ya kwanza iliyojulikana kama “Funga Kazi” na baadaye wakaibuka washindi wa tuzo la kundi bora la muziki wa hip hop.

Alianza kuimba peke yake mwaka 2001 na kufikia sasa ana albamu sita ambazo ni “Machozi, Jasho na Damu”, “Mapinduzi Halisi”, “J.O.S.E.P.H”, “Aluta Continua”, “Izack Mangesho” na “Kazi Kazi” ya mwaka 2016 wakati akiwa mgeni bungeni.

Akiwa anahudumia watu wa Mikumi kama Mbunge, Profesor Jay alionekana kupunguza kazi ya muziki kidogo na sasa inasubiriwa kuona ikiwa atarejea kikamilifu kwenye fani hiyo.

Categories
Kimataifa

Tundu Lissu: Uchaguzi mkuu wa Tanzania ulikumbwa na udanyanyifu

Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia cha Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania Tundu Lissu, amesema uchaguzi mkuu ulioandaliwa Jumatano nchini humo ulikumbwa na udanganyifu.

Mgombea huyo wa urais wa upinzani alidai kuwa mawakala wa upinzani hawakuruhusiwa kuingia katika vituo vya kupiga kura.

Lissu ametoa wito kwa jumuiya za kikanda zikatalie mbali matokeo ya uchaguzi wa Tanzania aliyoyataja kuwa haramu.

Hata hivyo tume ya uchaguzi nchini Tanzania imepuuzilia mbali madai hayo ya Lissu ikiyataja yasiyo na msingi wowote.

Mkuu wa tume hiyo ya uchaguzi Semistocles Kaijage, alisema madai kwamba kulikuwa na karatasi bandia za kupiga kura si ya ukweli.

Vyombo vya habari nchini Tanzania viliripoti kuwa shughuli ya upigaji kura Tanzania bara na visiwani Zanzibar ilikuwa ya Amani.

Rais wa nchi hiyo John Magufuli anawania awamu ya pili katika uchaguzi huo.

Categories
Kimataifa

Mjue Mpinzani Mkuu wa Magufuli, Tundu Lissu, kwenye uchaguzi wa urais Tanzania

Uchaguzi mkuu wa Tanzania 2020, utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba, unatarajiwa kushuhudiwa ushindani mkubwa katika kinyang’anyiro cha urais nchini humo.

Rais wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli anaazimia kuchaguliwa kwa awamu ya pili kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, CCM, ambacho kimekuwa uongozini tangu mwaka wa 1977.

Hata hivyo, Magufuli anacho kibarua kigumu atakapokabiliana na mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, Tundu Lissu.

Je, mgombea huyu ni nani?

Tundu Antiphas Mughwai Lissu alizaliwa tarehe 20 Januari mwaka wa 1968, akiwa na umri wa miaka 52 sasa.

Ni mkazi-asili wa eneo la Singida lililoko umbali wa takribani maili 200 Kaskazini-Magharibi mwa mji mkuu wa Dodoma.

Tundu Lissu ni Mwanasheria ambaye kutokana na ushupavu wake katika taaluma hiyo, alichaguliwa katika wadhifa wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania na pia Mwanasheria Mkuu wa chama cha Chadema.

Lissu alianza kupata umaarufu katika ulingo wa siasa alipogombea kiti cha ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki mwaka wa 2010 na kufaulu katika uchaguzi huo kwa tiketi ya Chadema.

Lissu anatajwa kama mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, asiyeogopa kukosoa serikali na hasa Rais Magufuli, ambaye ameonekana kutofautiana naye tangu kuchaguliwa kwake mwaka wa 2015.

Kutokana na msimamo wake mkali na matamshi ya kuupinga uongozi wa nchi hiyo, Lissu amepitia masaibu mengi ukiwemo msururu ya visa vya kukamatwa kwake na kushtakiwa kwa madai ya uchochezi miongoni mwa mashtaka mengine mengi.

Mnamo tarehe saba Septemba mwaka wa 2017, genge la watu wasiojulikana lilimvamia Tundu Lissu nyumbani kwake Dodoma na kumjeruhi vibaya kwa kumpiga risasi mara kadhaa mwili mzima.

Kufuatia kisa hicho, viongozi na wafuasi wa upinzani nchini Tanzania waliulaumu utawala wa nchi hiyo, wakiukashifu kwa uwezekano wa kuhusika katika kitendi hicho.

Hata hivyo, Rais Magufuli alijitokeza na kushtumu kitendo hicho mbali na kuagiza uchunguzi ufanywe ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria lakini hadi sasa, hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa kukamatwa kufuatia kisa hicho.

Lissu alikimbizwa hadi Hospitali Kuu ya Dodoma alikopokea matibabu ya dharura kwa masaa machache kabla kusafirishwa kwa ndege hadi Hospitali ya Aga Khan katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi.

Alitibiwa kwa miezi kadhaa kabla kusafirishwa tena hadi nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ya kuimarisha viungo vyake ambako anasemekana kufanyiwa upasuaji mara 19 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg.

Mnamo Julai mwaka huu, Tundu Lissu alirejea nchini Tanzania na kupokelewa na umati mkubwa wa wafuasi wake, ujio ambao ulipandisha joto la siasa za uchaguzi wa urais nchini humo.

Tarehe tatu Agosti 2020, wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema walipiga kura ya kumtafuta mgombea wa chama hicho atakayekabiliana na Rais Magufuli katika kinyang’anyiro cha urais.

Kamati kuu ya Chadema ilikuwa imeidhinisha majina ya wagombea watatu ambao walipigiwa kura ya mchujo.

Tundu Lissu aliibuka mshindi kwa kuzoa jumla ya kura 405 kati ya 442 zilizopigwa, na kuwapiku wagombea wenza Lazaro Nyalandu aliyepata kura 36 na Dkt. Mayrose Majige aliyepata kura moja.

Kufuatia matokeo hayo basi, Tundu Lissu alitangazwa kama mgombea atakayepeperusha bendera ya Chadema.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa nchini humo, uteuzi wa Lissu kukabiliana na Magufuli ulitokana na msimamo wake mkali wa kisiasa.

Chama hicho kilikuwa na nia ya kurudisha imani ya wafuasi wake baada ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho kuhamia chama tawala kinachoongozwa na Magufuli baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2015.

Aliyekuwa mgombea wa Chadema katika uchaguzi huo wa uraisi Edward Lowassa pia alihamia CCM baada ya kushindwa na Magufuli, hatua iliyowaghadhabisha wafuasi wa Chadema.

Kampeni za kuelekea uchaguzi wa mwaka huu zilipamba moto, huku Rais Magufuli akiwahakikishia wananchi wa Tanzania maendeleo zaidi katika awamu ya pili iwapo watamchagua tena.

Naye Lissu amepata umaarufu mkubwa hasa miongoni mwa vijana, akiahidi kuinua uchumi wa nchi hiyo, kuongeza mishahara kwa wahudumu wa sekta ya umma, kuwafidia waliomizwa na serikali iliyo mamlakani na kuanzisha mchakato wa mageuzi ya katiba ndani ya siku 100 za kwanza uongozini.

Hata hivyo, masiabu ya Lissu yalianza kumkabili tena mwishoni mwa mwezi jana alipotakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi nchini humo baada ya kusikika akisema tume hiyo ina njama ya kuiba kura za urais kwa faida ya Magufuli.

Juma moja baadaye, Lissu alipewa adhabu ya marufuku ya kutofanya kampeni kwa siku saba zilizofuata baada ya kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi kwenye mojawapo ya mikutano yake ya kampeni.

Huku wananchi wa Tanzania wakielekea debeni Jumatano, kitendawili kilichopo ni iwapo Tundu Lissu ataweza kumbwaga Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kuandikisha historia ya kuking’atua madarakani chama tawala cha CCM ambacho kimeongoza taifa hilo tangu kuundwa kwake mwaka wa 1977.

Categories
Kimataifa

Jumbe na simu za kufikia watu wengi kwa wakati mmoja vyapigwa marufuku kwa muda nchini Tanzania

Nchi ya Tanzania inapoendelea kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa Jumatano wiki ijayo, mabadiliko yanaendelea kushuhudiwa. Wapiga kura wapatao milioni 29 watapiga kura siku hiyo kuchagua Rais na Wabunge baada ya kukamilika kwa kipindi cha siku 64 cha Kampeini.

Serikali ya Tanzania sasa imeingilia wanaotumia mitandao ya kijamii na simu za rununu. Jana serikali hiyo ya Chama Cha Mapinduzi yaani CCM ilitoa ilani kwa kampuni za mawasiliano ya rununu inayozitaka kusitisha mara moja huduma za kutuma jumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja na za kupiga simu kwa watu wengi kwa wakati mmoja.

Marufuku hiyo ni kati ya tarehe 24 mwezi huu wa Oktoba na tarehe 11 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020.

“kwa kuzingatia athari ya utumizi mbaya wa jumbe nyingi kwa pamoja na simu kwa watu wengi kwa wakati mmoja kwa uchaguzi mkuu, na kulingana sheria ya tatu ya ratiba ya pili ya sheria ya mamlaka ya kusimamia mawasiliano nchini Tanzania, mamlaka hii inawaagiza mfunge kwa muda huduma hizo.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye barua iliyotumwa kwa kampuni za mawasiliano.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini Tanzania Bwana James Kilara alifafanua kwamba wanaotumia jumbe hizo kwa ajili ya usalama, maswala ya serikali na huduma za fedha wanakubaliwa kuendelea.

Kabla ya hapo kuliibuka tetesi kwamba jumbe zozote fupi ambazo zilikuwa na jina Tundu Lissu au herufi za kuashiria majina ya mgombea huyo wa urais kupitia CHADEMA hazikuwa zinaenda.