Categories
Michezo

Timu mbili zitakazocheza AFCON U 17 mwakani kubainika Jumapili

Mataifa mawili yatakayowakilisha ukanda wa CECAFA  katika mashindano ya  kombe la AFCON kwa chipukizi walio chini ya umri wa miaka 17 yatabainika Jumapili katika wilaya ya Rubavu nchini Rwanda wakati wa kupigwa kwa nusu fainli za CECAFA  katika uwanja wa Umuganda.

Chipukizi wa Uganda ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo la CECAFA watashuka uwanjani kwa nusu fainali ya kwanza Jumapili adhuhuri dhidi ya Djibouti kabla wa Ethiopia kupambana na Serengeti Boys  ya Tanzania  katika nusu fainali ya pili mida ya alasiri.

Uganda walitinga nusu fainali baada ya kuongoza kundi A  kwa pointi 6 walipoichakaza Kenya magoli 5-0 kabla ya kuiadhibu Ethiopia 3-0 katika mechi ya pili .

Upande wao Djibouti walitwaa nafasi ya pili kutoka kundi B kwa kutoka sare dhidi ya wenyeji Rwanda na Tanzania.

Tanzania waliongoza kundi B kwa alama 4 kwa kuipiga Rwanda 3-1 kabla ya kuambulia sare  ya 1-1 na Djibouti huku Ethiopia ikisajili sare ya 2-2 dhidi ya Kenya katika kundi A kabla ya kulazwa 3-0 na Uganda.

Washindi wa nusu fainali watajikatia tiketi kucheza kipute cha Afcon mwezi Juni mwaka ujao nchini Moroko na pia kufuzu kucheza fainali ya kombe la Cecafa kesho Jumanne Ijayo.

 

Categories
Michezo

Kenya U 17 yaning’inia Rwanda michuano ya CECAFA

Chipukizi wa Kenya walio chini ya umri wa miaka 17 wanahitaji maombi  mengi  na muujiza Ijumaa  ili kufuzu kwa nusu fainali ya michuano ya CECAFA inayoendelea nchini Rwanda.

Kenya inayofunzwa na kocha Oliver Page itafuatilia kwa karibu pambano baina ya Ethiopia na mabingwa watetezi Uganda ambapo ili Kenya  kufuzu kwa nusfu fainali ni sharti Uganda iwaadhibu Ethiopia mabao 6-0,baada  ya Kenya kuchakazwa mabao 5-0 na Uganda katika mechi  ya kundi A mapema wiki hii.

Uganda inaongoza kundi A kwa  pointi 3 wakifuatwa na  Ethiopia kwa alama 1 sawa  Kenya waliokamilisha mechi zao hususan kufuatia kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Ethiopia katika pambano la ufunguzi.

Timu mbili bora kutoka kundi hilo zitafuzu kupiga nusu fainali dhidi ya timu mbili bora kutoka kundi B  .

Timu ya kwanza na ya pili zitafuzu kushiriki  fainali za AFCON mwaka ujao nchini Moroko.

Categories
Michezo

Tanzania wakwea ndege kupiga kipute cha AFCON mwakani

Mabingwa watetezi wa kombe la Cecafa kwa chipukizi walio chini ta umri wa miaka 20 Tanzania wamefuzu kwa kipute cha Afcon mwaka ujao nchini Mauritania, baada ya kuishinda Sudan kusini bao 1-0 katika nusu fainali ya Cecafa iliyopigwa Jumatatu jioni katika uwanja wa Black Rhino Academy kijini Karatu mji wa Arusha Tanzania.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare tasa timu zote mbili zilirejea kipindi cha pili kwa lengo la kushinda na kutinga michauno ya Afcon mwakani kwa mara ya  kwanza ,huku kosa la mabeki wa Sudan Kusini kunako dakika ya 58 likimpa fursa Kassim Haruna aliyefunga bao kwa wenyeji maarufu kama Ngorongoro Heroes.

Licha ya Sudan kujaribu kila mbinu jitihada zao zilizimwa na kuwapa Tanzania tiketi ya kupiga Afcon mwaka ujao  .

Ngorongoro Heroes watashuka dimbani Black Rhino Jumatano hii kuzindua uhasama wa jadi na Uganda Hippos katika fainali ya kombe hilo walilonyakua mwaka jana nchini Uganda.

Sudan Kusini kwa upande wa pili wa sarafu watapambana  na Kenya Jumatano adhuhuri kuwania nafasi ya tatu na nne.

Categories
Michezo

Kenya yaipiga kumbo Sudan na kutinga nusu fainali Cecafa

Timu ya taifa ya Kenya kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 20, imefuzu kwa nusu fainali ya michuano ya Cecafa inayoendelea mjini Arusha

Tanzania, baada ya kuilaza Sudan mabao 2-1 katika pambano la mwisho la kundi C uwanjani Sheikh Amri Abeid .

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizikia kwa sare tasa ,Fortune Omoto aliondoa ukame  wa mabao kwa bao la dakika ya 62 kwa Kenya , lakini zikisalia dakika tano mechi ikatike Ali Gozoli Nooh akavunja nyoyo za wakenya kwa bao kusawazisha .

Hata hivyo Benson Ochieng alipachika bao la dakika ya 92  na kuhakisha Kenya maarufu kama rising stars ,wanamaliza kwenye nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 6 kutokana na mechi mbili na kufuzu kwa nusu fainali ya Jumatatu  dhidi ya Hippos kutoka Uganda huku Tanzania walioongoza kundi A wakiweka miadi ya kumenyana na  Sudan kusini katika nusu fainali ya pili pia Jumatatu.

Nahodha wa Kenya na Sudan wakiwa na waamuzi kabla ya mechi

Timu ya kwanza na ya pili katika michuano hiyo ambayo fainali yake  itapigwa Disemba 2 zitafuzu kushiriki mashindano ya kombe la Afcon kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka ujao nchini Mauritania.

Rising Stars walikuwa wamesajili ushindi wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya kundi hilo dhidi ya Ethiopia.

 

Categories
Michezo

Uganda Hippos wabanwa mbavu na Sudan Kusini CECAFA

Uganda walilazimishwa kwenda sare tasa dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya ufunguzi ya kundi B kuwania kombe la Cecafa kwa vijana walio chini ya umri wa  miaka 20 iliyochezwa Jumatatu jioni katika uwanja wa Black Rhino Academy Complex.

Ilikuwa mara ya  tatau mtawalia kwa timu ya Uganda kutatizwa na  Sudan Kusini,baada ya Uganda Cranes kuhitaji bao la dakika ya mwisho kabla ya kuishinda Sudan Kusini katika pambano  kufuzu kwa kombe la Afcon jijini Kampala kabla ya kucharazwa na Sudan Kusini bao 1-0 kwenye mechi ya marudio iliyochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Uganda maarufu kama Hippos  watarejea uwanjani Jumatano kwa mechi ya pili dhidi ya Burundi mechi ambayo lazima washinde ili kufuzu kwa nusu fainali.

Mashindano ya Cecafa yataingia siku ya tatu Jumanne kwa mchuano mmoja wa kundi  A kati ya Djibouti na Somalia katika uwanja wa Black Rhino Academy Complex kuanzia saa kumi alasiri.

Mechi za makundi zitafikia tamati Ijumaa kabla ya nusu fainali kung’oa nanga Novemba 30 ikifuatwa na fainali ya Disemba 2.

Timu bora kutoka kila kundi na timu bora ya pili kutoka makundi yote matatu zitafuzu kwa nusu fainali ilihali timu mbili bora zikifuzu kuwakilisha ukanda wa Cecafa katika mashindano ya kombe la mataifa ya afrika Afcon mwaka ujao nchini Mauritania.

Categories
Michezo

Tanzania waitemea Djibouti ‘cheche za moto’ CECAFA

Mabingwa watetezi Tanzania wajulikanao kama Ngorongoro Heroes wameanza vyema kutetea kombe la Cecafa baada ya kuwachachafya  Djibouti mabao 6-1 katika mchuano wa ufunguzi wa kundi A uliosakatwa Jumapili alasiri katika uwanja wa Black Rhino Academy Sports Complex.

Wenyeji walijikuta taabani katika kipindi cha kwanza baada ya limbukeni Djibouti kuwafunga bao la dakika ya 14 kupitia  free kick ya  mshambulizi Kassim  na kudumu hadi kipenga cha mapumziko.

Kipindi cha pili Ngorongoro Heroes walirejea kwa vishindo huku Teps  Evans akikomboa bao katika dakika ya 54  naye Abdul Seman akawaweka wenyeji kifua mbele kwa goli la dakika ya 65  akijibu tobwe lililotemwa na kipa wa Djibouti na kurejea kwa bao la tatu kunako dakika ya 72.

Mabao mengine matatu ya Tanzania yalifungwa na Khelfin Salum ,Razack Shekimweli na Abdul aliyefunga penati na kufunga mechi kwa mabao matatu.

Mashindano hayo kuendelea Jumatatu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid  kwa pambano la kundi B Uganda dhidi ya Sudan Kusini saa kumi alasiri ,mechi itakayotanguliwa na ile ya kundi C baina  ya Kenya Rising Stars dhidi ya Ethiopia kuanzia saa saba adhuhuri katika uwanja wa Black Rhino Academy .

Mashindano hayo yanayoshirikisha mataifa 9 yatakamilika Desemba 2 huku timu mbili bora zikifuzu kwa mashindano ya Afcon mwaka ujao nchini Mauritania.