Categories
Burudani

Professor Jay arejelea muziki

Joseph Haule maarufu kama Professor Jay amerejelea muziki baada ya kugonga mwamba kwenye siasa na uongozi nchini Tanzania.

Jay ambaye ana umri wa miaka 45 sasa ni mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Aliendeleza kazi hiyo ya muziki iliyompa umaarufu hadi mwaka 2015 alipowania kiti cha ubunge katika eneo la Mikumi na kushinda.

Akihudumu kama mbunge kazi ya muziki aliisimamisha kabisa. Mwaka jana kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Professor Jay na wengine wengi wa chama cha “CHADEMA” walibwagwa. Aliyemshinda katika ubunge wa Mikumi ni Dennis Lazaro wa chama cha CCM.

Tangu wakati huo amesalia kimya hadi maajuzi alipojitokeza tena kwenye ulingo wa muziki kupitia kwa mwanamuziki mwenzake Stamina.

Stamina amemshirikisha Jay kwa ngoma yake mpya kwa jina “Baba” ambayo ilizinduliwa rasmi jana tarehe 13 mwezi Januari mwaka 2021.

Professor Jay alitangaza ujio wa kibao hicho kipya kwenye akaunti yake ya Instagram huku akihimiza mashabiki wakakitazame kwenye akaunti ya Stamina ya You tube.

Duru zinaarifu kwamba sasa jay ambaye anaigiza kama babake Stamina kwenye video ya wimbo huo amerejelea muziki kikamilifu.

Stamina anafungua wimbo huo akimpigia babake simu huku akimzomea na kumlaumu kwa matatizo anayopitia maishani.

Anamuuliza ni kwa nini hakumpeleka mamake akaavye mimba yake kwani anasikia aliikataa hiyo mimba.

Analaumu babake pia kwa ufukara anashangaa ni kwa nini wanaishi nyumba ya kupangisha na hamiliki hata shamba.

Anapoingia babake, anamwelezea kwamba vipimo vilionyesha kwamba yeye sio babake mzazi ila aliamua tu kumlea kama baba mzazi na anashangaa ni kwa nini hakusoma ajitengenezee maisha mazuri.

 

Categories
Burudani

Shishi Baby aomba ukuu wa Wilaya

Mwanamuziki na mjasiriamali wa nchi ya Tanzania Zena Yusuf Mohamed maarufu kama Shilole au ukipenda Shishi Baby ametoa ombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Wakenya wanamfahamu dada huyo kutokana na video iliyosambazwa awali kwenye mitandao ya kijamii ambapo alishindwa kutamka neno, “Subscribe”.

Mwanadada huyo ambaye anamiliki mkahawa kwa jina Shishi Food anasema anatamani sana kuwa mbunge lakini kwa sasa anaomba Rais ampe ukuu wa wilaya.

Amewahi kuwa mwenyeji wa watu mashuhuri kwenye mkahawa huo wake, wa hivi punde zaidi akiwa mwanamuziki tajika wa Congo, Koffi Olomide.

Shishi anakubali kwamba hana kisomo, aliachia darasa la saba, lakini ana kipaji cha uongozi na ikiwa Rais ataona vyema ampatie kazi hiyo ya kusimamia wilaya.

Mwanamuziki huyo alitaja Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bi. Jokate Urban Mwegelo wa miaka 33 ambaye awali alikuwa mtangazaji na mfanyibiashara akisema ikiwa atapatiwa kazi ataifanya kama anavyoifanya Jokate kwa kujitolea.

Siku za hivi karibuni Shilole amekuwa akijitahidi sana kujitafutia yeye na binti zake pale ambapo amekuwa akitangazia kampuni kadhaa biashara zao na inaaminika kampuni hizo zinamlipa vizuri.

Amekuwa pia akihusishwa kwenye tamasha linaloendeshwa na wasafi media ya Diamond Platnumz almaarufu “Tumewasha na Tigo”.

Alijihusisha pia kikamilifu na kampeni za chama cha CCM kabla ya uchaguzi mkuu na sasa inasubiriwa kuona ikiwa Rais Magufuli ataridhia ombi lake.

Categories
Burudani

Diamond Platinumz kuzuru Kenya

Msanii wa nchi ya Tanzania Diamond Platinumz au ukipenda Chibu Dangote au Simba anatarajiwa kutua nchini Kenya hii leo kwa kile ambacho kinasemekana kuwa ziara ya mapumziko.

Ama kweli miezi michache ambayo imepita imekuwa ya kazi nyingi kwa msanii huyo kiasi cha kwamba sasa anahitaji mapumziko.

Mwezi Septemba alikuwa anajihusisha na kazi ya kutoa muziki na Bi. Zuchu ambaye alikuwa amejiunga na kampuni ya WCB anayomiliki Diamond. Wawili hao walitoa nyimbo kama vile ‘Cheche’ na ‘litawachoma’ ambazo zilizua minong’ono chungu nzima kwenye mitandao ya kijamii.

Swali ambalo wengi walikuwa wanajiuliza ni la uhusiano kati ya wawili hao kwa jinsi walicheza kwenye video za nyimbo na kuandamana karibu kila sehemu.

Baada ya hapo Diamond na wanamuziki wengine wa WCB waliingilia Kampeni ambapo walikuwa wakikipigia debe chama cha CCM na hasa Rais John Pombe Magufuli.

Uchaguzi ulipokamilika alifanya tamasha nchini Sudan Kusini na nchini Malawi. Aliporejea nyumbani Tanzania alitembelewa na mpenzi wake wa zamani Zari Hassan na watoto wao Tiffah na Nillan. Hakuwa ameonana na watoto hao kwa muda wa miaka miwili.

Na sasa ametangaza likizo yake nchini Kenya ila wengi wanaonelea kwamba anakuja kuona mtoto wake na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna ambaye ni somo wake kwa jina Naseeb Junior.

Ukurasa wa Facebook kwa jina ‘Wasafi News’ unaoaminika kuwa wa Wasafi Media kampuni inayomilikiwa na Diamond Platimumz ndio umetangaza ziara yake ya Kenya na kupachika picha ya awali ya Diamond na Tanasha.

Categories
Burudani

Mwana Falsafa, Babu Tale, sasa ni wabunge Tanzania

Hamis Mwinjuma mwanamuziki wa mtindo wa Hip Hop nchini Tanzania almaarufu “Mwana Falsafa” au ukipenda “Mwana Fa” sasa ni Mbunge nchini Tanzania.

Atawakilisha eneo la Muheza bungeni kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Yeye ni mmoja wa watu zaidi ya elfu kumi ambao walijitosa kwenye kinyanganyiro cha kutafuta tiketi za chama cha CCM mwezi Agosti mwaka huu, ili kutafuta viti vya ubunge kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania.

Baada ya kupata tiketi hiyo Hamis Mwinjuma aliingilia Kampeni, uchaguzi ukafanyika Jumatano 28 Oktoba mwaka huu na akamshinda Yosepher Komba wa CHADEMA.

Mwana Fa alizoa kura 47,578 huku Komba akipata kura 12,034. Sio mengi yanafahamika kuhusu familia ya Mwana Fa ila alifunga ndoa mwana 2016 na binti kwa jina Helga na arusi ilihudhuriwa na watu wachache tu licha ya kwamba yeye ni mtu maarufu.

Mwanamuziki huyo aliingilia fani hiyo mwaka 1995 akiwa bado anasoma shule ya upili na hadi sasa ameendelea kufurahia uungwaji mkono wa mashabiki wake na wapenzi wa muziki nchini Tanzania.

Mhusika mwingine wa sanaa nchini Tanzania ambaye ameingia bungeni kupitia uchaguzi mkuu wa hivi punde ni meneja wa wasanii maarufu kama Babu Tale ambaye ni mmoja wa walioanzisha WCB.

Meneja huyo ambaye jina lake halisi ni Hamisi Shabaan Tale Tale wa chama cha CCM hakuwa na mpinzani katika kuwania kiti cha ubunge eneo la Morogoro Kusini Mashariki na hilo lilisababisha atangazwe mshindi.

Mwaka huu umekuwa wa huzuni na furaha kwake kwani alifiwa na mke wake kwa jina Shammy mwisho wa mwezi juni na sasa amepiga hatua maishani na kuwa kiongozi.

Categories
Burudani

Mwanamuziki Professor Jay ashindwa kutetea kiti cha ubunge

Joseph Haule almaarufu Professor Jay mwanamuziki ambaye aliingilia siasa nchini Tanzania alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge wa eneo la Mikumi katika uchaguzi mkuu ulioganyika jumatano.

Jay wa chama cha CHADEMA alibwagwa na Dennis Lazaro wa chama cha CCM ambaye alizoa kura 31,411 na Professor Jay akapata kura 17,375.

Kiongozi wa chama chake Bwana Tundu Lissu anaonekana kutoridhishwa na shughuli nzima ya uchaguzi akisema ilikumbwa na udanganyifu kwani maajenti wake walizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupiga na kuhesabu kura.

Haule amekuwa mbunge wa Mikumi kwa miaka mitano sasa na alishinda uchaguzi wa mwaka 2015 kupitia chama chake cha CHADEMA.

Wakati huo alijizolea kura 32,259.

Professor Jay ana umri wa miaka 44 sasa na amekuwa kwenye fani ya muziki tangu mwaka 1989 akiwa mmoja wa wasanii katika kundi la “Hard Blasters” na wakati huo alikuwa anajiita “Nigga J”.

Kundi hilo lilizindia albamu ya kwanza iliyojulikana kama “Funga Kazi” na baadaye wakaibuka washindi wa tuzo la kundi bora la muziki wa hip hop.

Alianza kuimba peke yake mwaka 2001 na kufikia sasa ana albamu sita ambazo ni “Machozi, Jasho na Damu”, “Mapinduzi Halisi”, “J.O.S.E.P.H”, “Aluta Continua”, “Izack Mangesho” na “Kazi Kazi” ya mwaka 2016 wakati akiwa mgeni bungeni.

Akiwa anahudumia watu wa Mikumi kama Mbunge, Profesor Jay alionekana kupunguza kazi ya muziki kidogo na sasa inasubiriwa kuona ikiwa atarejea kikamilifu kwenye fani hiyo.

Categories
Burudani

Ushindani lazima uwepo, Diamond Platinumz

Mwanamuziki tjika nchini Tanzania, Afrika mashariki, Afrika na hata ulimwenguni Diamond platinumz ameashiria kwamba kule kutopatana au ushindani kati yake na wanamuziki wengine kama vile Ali Kiba kutaendelea kuwepo.

Simba huyo wa muziki nchini Tanzania aliyasema hayo wakati akihojiwa kwenye kipindi kiitwacho “The Switch” cha kituo cha redio cha Wasafi ambacho anamiliki.

Kulingana naye zogo kidogo ni ladha katika ulingo wa muziki ila lisichukuliwe kibinafsi kiasi cha wengine kutaka kudhuru wengine.

” Ni kama sasa tuseme timu ya soka ya Simba iungane na timu ya Yanga, hiyo itakuwa nini sasa? Ndio mpira utakuwa umekufa kabisa.” alisema Diamond.

Msanii huyo anasema lazima ushindani uonekane hasa kwa ubunifu ndio wasanii wajikaze na sanaa iendelee mbele lakini akahimiza kwamba mashindano kama hayo yawe chanya.

“Kwa ukweli vitu kama hivyo lazima viwepo ila watu wasivichukulie kuwa personal watu wasiviingize kwa familia zao, waanze kurogana wataharibu hii sanaa.” alielezea Diamond.

Rais John Pombe Magufuli kwenye Kampeni za kutafuta kuchaguliwa tena kupitia chama cha CCM aliwaleta pamoja Ali Kiba, Diamond na Konde Boy almaarufu Harmonize.

Diamond alifichua pia kwamba ametambuliwa kwa mchango wake katika sekta ya burudani na jamii kwa ujumla nchini Tanzania ambapo mwaka 2018 aliambiwa achague mtaa nyumbani kwao ambao utabadilishwa jina na kuitwa jina lake.

Hadi sasa hajachagua mtaa.

jambo lingine ambalo Diamond ameliweka wazi siku za hivi karibuni ni jengo ambalo litakuwa afisi za Wasafi Media ambalo alisema ujenzi wake unakaribia kukamilika.

Jumba hilo “Wasafi Towers” linasemekana kuwa katikati ya mji wa Dar Es Salaam na litakuwa nyumbani kwa kampuni ya muziki ya Wasafi almaarufu WCB, kituo cha runinga na kile cha redio vyote ambavyo viko chini ya Wasafi Media.

Categories
Kimataifa

Wanamuziki kwenye Kampeni nchini Tanzania

Yeyote ambaye amekuwa akifuatilia kampeni za uchaguzi mkuu wa leo eneo la Zanzibar na Kesho katika eneo zima la Tanzania atakubaliana na kauli kwamba wanamuziki wamehusika sana.

Swali ambalo linachipuza sasa ni hili, kwa nini wamejiingiza vile kwenye siasa? Muziki au nyimbo nchini Tanzania ni kitu ambacho huchukuliwa kwa uzito mkubwa.

Vizazi vyote nchini humo vinapenda muziki wa aina fulani na raia nchini humo wanawaenzi na kuwafuatilia kwa karibu wasanii hasa kwenye mtandao wa Instagram ambao ni maarufu sana nchini Tanzania.

Huenda wasimamizi wa mipango katika vyama vya kisiasa walionelea wanamuziki kuwa nguzo muhimu katika kuvutia watu wengi kuhudhuria mikutano ya kampeni.

Wengi wa wasanii ukizingatia mitindo tofauti ya nyimbo, waliandaa nyimbo za kusifia wanasiasa na vyama vya kisiasa kulingana na sehemu ambayo wanaunga mkono.

Bi. Zuchu ambaye ni kitinda mimba wa sasa wa kampuni ya muziki ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platinumz hajaachwa nyuma kwani ana wimbo wa mtindo wa raggae ambao yeye huimba kila akiwa kwenye kampeni za chama tawala cha CCM ambacho wasanii wengi wanaunga mkono.

Mkubwa wake Diamond alibadilisha kidogo maneno kwenye wimbo wake maarufu wa ‘baba lao’ ambapo anarejelea mgombea urais wa CCM Rais Magufuli kama baba lao na pia alibadilisha maneno ya wimbo ‘number one’ akaunda wimbo kwa jina ‘CCM number one’.

Harmonize ambaye aligura Wasafi na kuanzisha ‘Konde Music’ alibadilisha maneno kwenye wimbo wa ‘Kwangwaru’ akaweka maneno ya kusifia utendakazi wa Rais John pombe Magufuli na chama cha CCM. Mwanamuziki huyo ambaye siku hizi anajiita mjeshi ana wimbo mwingine pia wa kusifia CCM kwa jina CC.

Ni baadhi tu ya nyimbo ambazo zimeimbwa na wasanii wa Tanzania katika kuunga mkono chama tawala cha CCM ila ni wengi ambao huwa wanahudhuria mikutano ya chama hicho na kukipigia debe.

Wengine ambao huenda kutumbuiza kwenye mikutano ya CCM ni kama vile Ali Kiba na wengine kutoka kwa kampuni yake ya muziki ya ‘king’s music’, Shilole, Nandy na wengine wengi ambao ni wasanii huru na wa kampuni ya Wasafi.

Kunao wengine ambao wamechagua kuunga mkono vyama vya upinzani kama vile Roma Mkatoliki na Ney wa Mitego.

Mhadhiri wa chuo kimoja kikuu nchini Tanzania Dakta Viscencia Shule alizungumza na BBC ambapo alielezea kwamba mara nyingi utakuta wanamuziki hawajiingizi kwa kampeni kwa hiari ni vile inabidi.

Kulingana naye serikali ya Tanzania iliweka sheria kali za kudhibiti maadili katika sekta ya burudani ambazo zimewagusa wasanii kwa njia moja ama nyingine.

Wengi wameadhibiwa na Baraza La Sanaa La Taifa almaarufu BASATA kwa nyimbo au vitendo ambavyo vinaonekana kukiuka maadili na hivyo lazima wajiweke upande wa serikali wasionekane waasi.

Categories
Kimataifa

Jumbe na simu za kufikia watu wengi kwa wakati mmoja vyapigwa marufuku kwa muda nchini Tanzania

Nchi ya Tanzania inapoendelea kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa Jumatano wiki ijayo, mabadiliko yanaendelea kushuhudiwa. Wapiga kura wapatao milioni 29 watapiga kura siku hiyo kuchagua Rais na Wabunge baada ya kukamilika kwa kipindi cha siku 64 cha Kampeini.

Serikali ya Tanzania sasa imeingilia wanaotumia mitandao ya kijamii na simu za rununu. Jana serikali hiyo ya Chama Cha Mapinduzi yaani CCM ilitoa ilani kwa kampuni za mawasiliano ya rununu inayozitaka kusitisha mara moja huduma za kutuma jumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja na za kupiga simu kwa watu wengi kwa wakati mmoja.

Marufuku hiyo ni kati ya tarehe 24 mwezi huu wa Oktoba na tarehe 11 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020.

“kwa kuzingatia athari ya utumizi mbaya wa jumbe nyingi kwa pamoja na simu kwa watu wengi kwa wakati mmoja kwa uchaguzi mkuu, na kulingana sheria ya tatu ya ratiba ya pili ya sheria ya mamlaka ya kusimamia mawasiliano nchini Tanzania, mamlaka hii inawaagiza mfunge kwa muda huduma hizo.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye barua iliyotumwa kwa kampuni za mawasiliano.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini Tanzania Bwana James Kilara alifafanua kwamba wanaotumia jumbe hizo kwa ajili ya usalama, maswala ya serikali na huduma za fedha wanakubaliwa kuendelea.

Kabla ya hapo kuliibuka tetesi kwamba jumbe zozote fupi ambazo zilikuwa na jina Tundu Lissu au herufi za kuashiria majina ya mgombea huyo wa urais kupitia CHADEMA hazikuwa zinaenda.

Categories
Kimataifa

Rais Magufuli atetea hatua ya kutangua uteuzi wa Gambo kuwa Mkuu wa Mkoa

Rais wa taifa la Tanzania Dakta John Pombe Magufuli ambaye anawania kipindi cha pili uongozini kupitia chama cha CCM ametetea hatua ya kutangua uteuzi wa Bwana Mrisho Gambo kuwa mkuu wa mkoa.

Akizungumza katika eneo la Arusha ambapo alipeleka kampeni jana, Rais Magufuli alifafanua kwamba chama cha CCM ni chama ambacho kinapenda haki.

Kulingana naye wote ambao walikuwa wakifanya kazi za serikali na wakaonyesha nia ya kuingia siasa kutafuta kuchaguliwa walipoteza nafasi zao za kazi serikalini.

Magufuli alisema hakumfukuza Gambo kazini na kwamba yeye mwenyewe alimwomba amwachishe kazi ili aende kugombea ubunge wa Arusha.

Rais Magufuli alijipigia debe na kumpigia debe pia Mrisho Gambo ambapo alihimiza wapiga kura wa Arusha wamchague ili awaletee maendeleo.

Shughuli za Kampeni zinaendelea kushika kasi nchini Tanzania ikitazamiwa kwamba uchaguzi wa tarehe 28 mwezi huu wa oktoba uko karibu.

Tume inayosimamia uchaguzi nchini Tanzania ilitangaza kwamba kampeni zitafanyika kati ya tarehe 26 mwezi Agosti na tarehe 27 mwezi oktoba mwaka huu wa 2020.

Categories
Kimataifa

Tanzania

Nchi ya Tanzania awali ikijulikana kama Tanganyika ambayo ni nchi ya eneo la Afrika mashariki ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni mwaka 1961 na Uhuru kamili ukaja mwezi wa Disemba mwaka huo.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliongoza ukombozi wa Tanzania alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania.

Alichaguliwa kupitia chama cha Tanzanian African National Union TANU, ambacho mwaka 1977 kiliungana na chama tawala cha Zanzibar cha “Afro Shirazi Party ASP na pamoja wakaunda Chama Cha Mapinduzi.

Kwa muda mrefu Tanzania ilikuwa nchi ya chama kimoja almaarufu ‘one party state’ hadi mwezi Februari mwaka 1992 ambapo vyama vingi vilikubaliwa chini ya uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi wakati huo. Kufuatia hayo, vyama vya kisiasa 11 viliandikishwa nchini Tanzania.

Chaguzi mbili ndogo za mwaka 1994 ndizo zilikuwa za kwanza kuwahi kuandaliwa chini ya sheria ya kukubalia vyama vingi na chama tawala cha sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilishinda viti hivyo viwili.

Mwezi wa Oktoba mwaka 2000, Tanzania iliandaa uchaguzi wa kwanza mkuu chini ya vyama vingi. Mwaniaji wa chama cha CCM Benjamin Mkapa aliibuka mshindi ambapo aliwapiki wapinzani watatu wakuu. Chama cha CCM kilishinda viti vya ubunge 202 kati ya vyote 232.

Katika eneo la Zanzibar Abeid Amani Karume alichaguliwa Rais baada ya kumshinda Seif Shariff Hamad wa chama cha Civic United Front (CUF).

Zanzibar ni eneo ambalo awali lilidhamiriwa kijisimamia kama nchi huru lakini likawianishwa na Tanzania mwaka 1964. Kwa hiyo inajisimamia kwa kiasi lakini bado iko chini ya Tanzania. Zanzibar ina bunge na ina Rais. Ina uwakilishi pia katika bunge la Tanzania.

Kufikia sasa nchi ya Tanzania ina vyama 22 vya kisiasa kama vile Chama Cha Mapinduzi CCM, Civic United Front CUF, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Union for Multiparty Democracy UMD kati ya vingine.

Rais Ali Hassan Mwinyi alikuwa wa CCM na aliongoza Tanzania kwa miaka kumi kati ya mwaka 1985 na mwaka 1995. Alifuatiwa na Benjamin Mkapa wa CCM vilevile ambaye aliongoza pia kwa miaka kumi hadi mwaka 2005.

Jakaya Mrisho Kikwete aliingia afisini kama Rais wa Tanzania mwisho wa mwaka 2005 hadi mwaka 2015. Rais wa sasa John Pombe Magufuli alishika hatamu za uongozi wa Tanzania mwaka 2015 hadi sasa.

Wote ambao wamehudumu kama marais nchini Tanzania ni wa chama cha CCM.

Mwaka huu wa 2020 nchi ya Tanzania itaandaa uchaguzi mkuu tarehe 28 mwezi huu wa Oktoba. Kulingana na matukio, kinyanganyiro cha Urais kina ushindani mkali kati ya Rais wa sasa John Pombe Magufuli wa chama cha CCM na Tundu Lissu wa chama cha CHADEMA.