Categories
Michezo

Simba yaitafuna Vita hadharani

Miamba wa soka nchini Tanzania,klabu ya Simba Sports club walianza vyema mechi za makundi za kuwania kombe la ligi ya mabingwa Afrika baada ya kuwaangusha AS Vita Club ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo bao 1 bila jawabu katika pambano la kundi A lililopigwa Ijumaa usiku katika uwanja wa Kinsasha.

Bao la mnyama Simba lilitiwa kimiani na mshambulizi Mutshimba Lugalu kupitia mkwaju wa penati  kunako dakika ya 60 na kudumu hadi kipenga cha mwisho.

beki kisi wa Kenya Joash Onyango alipiga dakika zote 90 huku kiungo Francis Kahata akiingia uwanjani kipindi cha pili.

Simba wanaongoza kundi hilo kwa alama 3 ,wakishiriki hatua ya makundi  kwa mara ya pili na ya kwanza  tangu mwaka 2013.

Wekundu wa msimbazi Simba watarejea Dar kujiandaa kwa mkwangurano wa pili watakapowaalika mabingwa watetezi na washindi mara 9 wa kombe hilo Al Ahly  kutoka Misri Februari 23.

Katika pambano la kundi D lililochezwa Cairo,Zamalek walilazimishwa kutoka sare kapa nyumbani dhidi ya MC Alger kutoka Algeria.

Categories
Michezo

Simba SC tayari kumvaa Vita Club huko Kinsasha

Mabingwa wa ligi kuu ya Tanzania bara Simba Sc wameanza mazoezi mjini Kinsasha  Alhamisi jioni  katika jamhuri ya Demokrasia ya Congo kujitayarisha kwa mechi ya kwanza ya makundi kuwania kombe la ligi ya mabingwa Afrika Ijumaa hii dhidi ya wenyeji As Vita Club.

Wekundu wa Msimbazi ambao ni mabingwa mara 21 wa ligi kuu ya kwao wamefuzu kucheza hatua ya makundi ya kombe hilo kwa mara ya pili katika historia na mara ya kwanza tangu mwaka 2003.

Kikosi cha Simba kilicho DRC kinawajumuisha wakenya Francis Kahata na beki kisiki Joash Onyango huku timu hiyo ikiwa ya pekee kutoka ukanda wa East Afrika iliyotinga hatua ya makundi katika kombe hilo .

Baadae tarehe 23 mwezi huu Simba watawaalika mabingwa watetzi na mabingwa mara 9 wa kombe hilo Al Ahly ya Misri,kabla ya kuzuru sudan Machi  5 kuvaana na Al Merreikh na kurudiana nao jijini daresalaam tarehe 16 mwezi uja.

Michuano ya ufunguzi hatua ya nakundi kuwania kombe la ligi ya mabingwa kusakatwa kati ya Ijumaa na Jumamosi.

Categories
Michezo

Ahly kuanza kutetea kombe la ligi ya mabingwa dhidi ya El Merreikh

Washindi mara 9  wa kombe la ligi ya mabingwa Afrika Al Ahly wamejumuishwa kundi A katika droo ya makundi iliyoandaliwa Ijumaa  mjini Cairo pamoja na El Merreikh ya Sudan ,Simba Sc kutoka Tanzania,na As Vita Club ya Drc.

Ahly wataanza ratiba dhidi ya El Merreikh mjini Cairo nao Simba waanzie ugenini dhidi ya Vita Club.

Kundi B linajumuisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini,mabingwa mara tano TP Mazembe kutoka Drc,El Hilal ya Sudan na CR  Belouizdad ya Algeria.

Waydad Casablanca ya Moroko wamejumuishwa kundi C pamoja na Horoya AC ya Guinea,Petro Atletico ya Angola na Kaizer Chiefs kutoka Afrika Kusini huku kundi D likisheheni mabingwa mara 4 Esperance ya Tunisia,mabingwa mara 5 Zamalek ,Mc Alger na Teungueth ya Senegal inayoshiriki kwa mara ya kwanza.

Mechi za raundi ya kwanza hatua ya makundi zitachezwa kati ya Februari 12 na 13 mwaka huu.

Categories
Michezo

Ratiba ya makundi ya Caf Champions league yakamilika

Mibabe wengi wa bara Afrika walifuzu kwa hatua ya makundi kuwnaia kombe la klabu bingwa barani Afrika msimu huu baada ya kumalizika kwa mechi za mchujo Jumatano usiku.

Timu zilizotinga hatuaya makundi Jumatano ni :-Tp Mazembe kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo,Esperance ya Tunisia,Mc Alger ya Algeria,Simba kutoka Tanzania,As Vita Club kutoka DR Congo,Al Merreikh ya Sudan,Horoya toka Guinea,Petro Atletico ya Angola ,Cr Belouizdad ya Algeria na Wydad Casablanca ya Moroko.

Vilabu vilivyofuzu jumanne ni  Zamalek na Al Ahly zote za Misri,Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs za Afrika kusini na Teungueth ya Senegal.

Kwa jumla vilabu 15 vimefuzu hatua ya makundi ya kombe hilo la kifahari huku nafasi moja iliyosalia ikijazwa na aidha Asante Kotoko ya Ghana au Al Hilal Omdurman ya Sudan baada ya pambano lao marudio jumatano kuahirishwa.

Kijumla Misri itawalishwa na vilabu 2,-Al Ahly na Zamalek,Afrika Kusini 2-,Mamelodi na Kaizer Chiefs,DRC 2-Tp Mazembe na As Vita Club na Algeria 2-Mc Alger  na CR Belouizdad .

Mataifa ya Senegal,Sudan,Guinea,Angola,Moroko,Tanzania  na Tunisia yatakuwa na timu 1 kila moja .

Mechi za makundi zitaanza mwezi ujao.

 

Categories
Michezo

Simba anguruma na kuweka historia ya kutinga makundi ya ligi ya mabingwa

Klabu ya Simba imeandikisha historia baada ya kusajili wa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Platinum Fc ya Zimbabwe  na kufuzu hatua ya makundi ya kombe la ligi ya mabingwa Afrika katika mchuano wa marudio uliosakatwa Jumatano jioni katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.

Difenda Erasto Nyoni aliwanyanyua mashabiki  takriban 30,000 wa wekundu wa msimbazi waliofurika uwanjani   kwa bao la kwanza kupitia mkwaju wa penati wa dakika ya 40  huku wakienda mapumziko kwa uongozi huo.

Kipindi cha pili Mnyama Simba alirejea kwa uchu wa mashambulizi yaliyozalisha goli la pili lililopachikwa kimiani na beki Shomari Kapombe katika dakika ya 61 naye Juma Bocco akapiga bao la tatu dakika ya 91 huku Cletus Chama akifunga karamu kwa bao la nne dakika ya 94.

Simba watakuwa wakipiga hatua ya makundi ya kombe hilo lenye donge nono  kwa mara ya pili na ya kwanza tangu mwaka 2003 ikiwa pia timu ya pekee kutoka Afrika Mashariki kucheza hatua hiyo.

Simba walikuwa wamepoteza duru ya kwanza bao 1-0 ugenini hivyo basi wapiga delji hadi hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Platinum.

Categories
Michezo

Gor yalala chali nyumbani mbele ya Mwarabu CR Belouizdad Nyayo

Ilivyotarajiwa Gor Mahia wameyaaga mashindano ya kombe la ligi ya mabingwa Afrika kwa mara nyingine tena na kukosa nafasi ya kufuzu kwa hatua ya makundi kwa mara ya kwanza baada ya kuambulia kichapo cha mabao 1-2 katika maraudio ya mchujo na CR Belouizdad ya Algeria katika uwanja wa taifa wa Nyayo Jumatano alasiri.

Belouizdad walitinga hatua ya makundi ya kombe hilo kwa mara ya kwanza kwa ushindi wa jumla wa mabao  8-1 baada ya kuigaragaza Kogalo 6-0 katika duru ya kwanza Disemba 26.

Katika mchuano wa Jumatano Gor walianza vyema  pambano hilo huku wakipata la ufunguzi kupitia kwa mshambulizi wa Burundi Jules Ulimwengu katika dakika ya 18 na kumiliki kipindi cha kwanza huku wakiongoza kwa bao hilo hadi mapumzikoni.

Hata hivyo Belouizdad walirejea kipindi cha pili na mbinu tofauti  huku Amir Sayoud aliyewatesa Algiers kwa kupiga mabao matatu akiisawazisha  kunako dakika ya 74 naye Hamza Belahouel akitikisa nyavu dakika ya 84 na kuwapa wageni ushindi wa 2-1.

Gor waliokumbwa na masaibu mengi  kabla ya mechi hizo mbili dhidi ya Belouizdad ,watasubri kubaini mpinzani wao katika mchujo wa kuwania tiketi kucheza hatua ya makundi ya kombe la shirikisho .

Categories
Michezo

Miamba na limbukeni watinga makundi ya ligi ya mabingwa Afrika CAF

Miamba kadhaa wa soka barani Afrika walifuzu kwa hatua ya makundi kuwania taji ya ligi ya mabingwa Afrika kufuatia mechi za marudio ya michujo ya pili iliyosakatwa Jumanne .

Teungueth

Mabingwa mara 9 wa kombe hilo na mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri walitinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-0 baada ya kuwacharaza SONIDEP ya Niger magoli 4-0 katika mkumbo wa pili uliosakatwa mjini Cairo Misri Jumanne usiku.

Al Ahly

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kusini maarufu kama Masandawana walipata ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana  baada ya kuwapiga wageni Jwaneng mabao 3-1 Jumanne.

Mamelodi Sundowns

Kaizer Chiefs ukipenda Amakhosi ,wakicheza ugenini Luanda walikosa  heshima na kuwapiga kumbo Premeiro De Agosto bao 1-0  na kufuzu kwa makundi ya kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24 ,huku limbukeni Teungueth ambao ni mabingwa wa Senegal wakiwaduwaza miamba Raja Casablanca ya Moroko walipowabandua kupitia penati 3-1 kufuatia sare tasa.

Kaizer Chiefs

Timu nyingine iliyotinga awamu ya makundi kupitia kupewa ushindi wa ubwete kufuatia kujiondoa kwa wapinzani wao ni Zamalek kutoka Misri waliocheza hadi fainali ya mwaka jana,waliopewa ushindi baada ya Gazzelle ya Chad kujiondoa.

Mechi zaidi kupigwa Jumatano ambapo ratiba kamili ya timu 16 kucheza hatua ya makundi itabainika.

 

Categories
Michezo

Gor yatua Algiers tayari kuwakabili CR Belouizdad Jumamosi

Baada ya safari ndefu hatimaye kikosi cha Gor Mahia cha wachezaji 18 na maafisa wa kiufundi , kimetua mjini Algiers kucheza mchuano wa mkumbo wa kwanza hatua ya pili ya mchujo kuwania kombe la ligi ya mabingwa Afrika Jumamosi dhidi ya mabingwa wa Algera CR Belouizdad.

Ujumbe wa Gor ambaoi ulisafiri bila huduma za nahodha Keneth Muguna anayeuguza jeraha, uliondoka nchini muda mfupi kabla ya saa saba usiku wa manane Ijumaa  na kupitia Dubai walikopumzika kwa muda kabla ya kuwasili Algiers mida ya saa tisa unusu Alasiri Ijumaa.

 

Wachezaji wa Gor wakiripoti katika hoteli mjini Algiers

Mkondo wa kwanza wa mechi hiyo utachezwa saa 10 45 pm Jumamosi mjini Algiers, kabla ya mkondo wa pili kuandaliwa hapa Nairobi mapema mwezi ujao huku mshindi wa jumla akifuzu kwa hatua ya makundi ilihali timu itakayoshindwa ikilazimika kucheza mchujo wa kuwania kushiriki hatua ya makundi ya kombe la shirikisho.

Mechi ya Gor na Belouizdad iliahirishwa kutoka Jumatano wiki hii kufuatia kuchelewa kusafiri kwa Gor na kuwalazimu kuiomba CAF kuahirisha mechi hiyo.

Categories
Michezo

Safari ya Gor kwenda Algeria yakumbwa na misukosuko

Safari ya timu ya Gor Mahia  kuelekea Algeria imekumbwa na utata baada ya kudaiwa kukosekana kwa ndege ya usafiri moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Algiers .

Kogalo walitarajiwa kusafiri Jumapili usiku kwenda Algiers kwa  mkumbo wa kwanza wa mechi ya mchujo kuwania ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa wa Algeria CR  Belouizdad Jumatano jioni ,lakini hadi mapema Jumatatu timu hiyo ilikuwa bado haina uhakika wa kusafiri.

Awali timu hiyo ilikosa tiketi za usafiri kabla ya kampuni Air 748 kutoa shilingi milioni 1 kwa usafiri huku  pia yamkini tiketi zilizonunuliwa hazikutosha kwa wachezaji na maafisa wote wanaohitajika kwenye ziara hiyo.

Pia wachezaji wanadai  kulipwa mishahara yao kabla ya kusafiri na huenda wakosa  kucheza mechi hiyo hatuya ambayo itachangia kupigwa marufuku na kutozwa faini na CAF.

Mkumbo wa pili wa mchuano huo uliratibiwa kuchezwa jijini Nairobi mapema mwezi ujao huku mshindi wa jumla akitinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.

 

Categories
Michezo

Gor Mahia walenga hatua ya makundi ligi ya mabingwa CAF kwa mara ya kwanza

Miamba wa soka nchini Gor Mahia wanalenga kufuzu kwa hatua ya makundi ya kombe la ligi ya mabingwa barani Afrika Caf kwa mara ya kwanza msimu huu.

Kulingana na meneja wa Gor Jolawi Obondo kikosi walicho nacho kwa sasa ni kizuri na pia kina tajriba ya kuweka rekodi kuwa kilabu cha kwanza kutoka humu nchini kucheza hadi hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa baada ya majaribio kadhaa bila ufanisi.

“Ni maombi yetu tucheze hadi hatua ya makundi na hata ikiwezekana hadi hatua ya mwondoano ya ligi ya mabingwa barani Afrika”akasema Obondo

Kwa mjibu wa Obondo Kogalo pia ina fursa ya kwenda mbali msimu huu katika kombe  hilo kutokana  na usaidizi wanaopata kutoka kwa Wizara ya michezo na shirikisho la FKF na kukanusha madai kuwa kikosi cha sasa ni hafifu na hakina uwezo wa kwenda mbali..

“Watu wanasema huenda hatuna kikosi kizuri lakini mimi sikubaliani,tuna kikosi kizuri na tuko na usaidizi kutoka kwa serikali,wizara na  hata shirikisho  sioni kwa nini tushindwe kufika hatua ya makundi” akaongeza Obondo

“Ushindi unataegemea na mtazamo,malengo na pia ushirikiano wa wachezaji ,usaidizi wa na maono ya kocha na nadhani tumejianda kwa hayo yote”akasema Obondo

Nahodha wa kilabu hicho Keneth Muguna pia anaazimia kuingoza Kogalo hadi hatua ya makundi licha ya upinzani mkali watakaopata.

“Tunataka tufuzu ,na kila timu pia inataka kufuzu ,tunajua itakuwa ngumu  lakini mwisho wa siku sisi tunajua sisi ndio tutashinda na kufuzu hatua ya makundi ya Caf Champions League”akasema Muguna

Gor Mahia imeratibiwa kuchuana na mabingwa wa Algeria CR Belouizdad ya Algeria  tarehe 22 mwezi huu mjini Algiers kabla ya kuwaalika wageni hao tarehe 5 mwezi ujao kisha mshindi kijumla afuzu kwa hatua ya makundi ya kombe la ligi ya mabingwa Afrika.

Mabingwa hao mara 18 wa ligi ya Kenya walifuzu kwa raundi ya pili ya mchujo wiki jana baada ya kuibandua APR ya Rwanda mabao 4-3 kwa jumla katika raundi ya kwanza ya mchujo.

Kogallo wamekuwa wakibanduliwa katika hatua ya mchujo ya  ligi ya mabingwa  Afrika kwa misimu mitatu mtawalia iliyopita,baadae wakafuzu kwa hatua ya makundi ya kombe la  shirikisho .

Hata hivyo Gor wameshindwa kuingia hatua ya mwondoano ya kombe la shirkisho katika misimu mitatu iliyopita.

Mabingwa hao mara 18 wa ligi ya Kenya walifuzu kwa raundi ya pili ya mchujo wiki jana baada ya kuibandua APR ya Rwanda mabao 4-3 kwa jumla katika raundi ya kwanza ya mchujo.