Categories
Habari

Kamati ya mswada wa BBI yahimiza Bunge kuiga mfano wa wawakilishi wadi ili kuupitisha

Kamati ya kitaifa ya mpango wa BBI imewapongeza wanachama wa mabunge ya kaunti kote nchini kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.

Kwenye taarifa, kamati hiyo imesema wawakilishi wadi wametekeleza wajibu wao wa kihistoria kwa kukubaliana na mchakato wa marekebisho hayo ya katiba yatakayowezesha taifa hili kusonga mbele.

“Pia tunawashukuru kwa kuisikiliza sauti ya wananchi wakati wa maamuzi yao kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020,” imesema taarifahiyo.

Kamati hiyo pia imewasifu Wakenya kwa kujitolea kwa wingi na kushiriki katika vikao vya ukusanyaji maoni ya umma kuhusu mswada huo, huku wakipuuzilia mbali habari za uongo zinazoenezwa na wanaopinga mchakato huo.

Wanakamati hao wanasema kupitishwa kwa mswada huo kote nchini ni ishara kwamba wananchi wa Kenya wamezungumza kwa sauti moja.

“Ushindi huu mkubwa unaashiria umaarufu wa BBI na ni ishara ya uungwaji mkono wa mswada wa BBI wakati wa kura ya maamuzi,” wakasema.

Na huku mswada huo ukielekea katika hatua ya mbele, kamati hiyo imewaomba wabunge kuzipa kisogo propaganda zinazoenezwa na kuwaiga wawakilishi wadi kwa kupitisha mswada huo katika Bunge la Kitaifa.

Hayo yanajiri huku mabunge zaidi ya kaunti yakiendelea kujadili mswada huo ambao tayari umetimiza masharti ya kikatiba ya kuungwa mkono na angalau mabunge 24 ya kaunti ili kuingia kwenye awamu nyengine.

Kufikia sasa mabunge 41 yamepitisha mswada huo, huku Bunge la Kaunti ya Migori likisalia la pekee lililokataa mswada huo.

Macho sasa yanaelekezwa kwa kaunti tano zilizosalia, ambazo hazijapigia kura mswada huo zikiwemo Nandi, Elgeyo Marakwet, Uasin Gishu, Mandera na Kilifi.

Sheria inasema mabunge ya kaunti yanafaa kuidhinisha rasimu ya mswada huo katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuwasilishwa.

Mswada huo sasa utawasilishwa kwa Spika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa na Ken Lusaka wa Seneti ili kupitishwa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atatia saini na kuuwasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa ajili ya kuandaa kura ya maamuzi.

Categories
Habari

Bunge la Kaunti ya Homabay laidhinisha mswada wa BBI

Bunge la Kaunti ya Homabay limekuwa la tatu kati ya yote 47 kupitisha kwa kauli moja, mswada wa marekebisho ya katiba ya mwaka wa 2020.

Mswada huo wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa (BBI) umewasilishwa katika bunge hilo Alhamisi na kupitishwa na wanachama wa bunge hilo.

Kaunti za Siaya na Kisumu ndizo zilizokuwa za kwanza na pili mtawalia kupitisha mswada huo ambao uliwasilishwa kwenye mabunge yote 47 ya kaunti humu nchini na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili ujadiliwe.

Awali, Bunge la Kaunti ya Homabay lilikuwa limetoa nafasi kwa umma kutoa maoni yao kuhusu mswada huo kufikia Jumatano.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga kukutana na mamia ya viongozi na wajumbe kutoka kaunti hiyo kwenye kikao cha uhamasisho kuhusu BBI.

Mswada huo unahitaji kuidhinishwa na angalau mabunge 24 ya kaunti ili uweze kuelekea kwenye hatua ya kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa na la Seneti.

Mabunge ya Kaunti yana muda wa hadi tarehe 26 mwezi Aprili kufanya maamuzi kuhusu mswada huo wa marekebisho ya katiba.

Categories
Habari

Serikali yatakiwa kuongeza umri wa ruhusa ya utumiaji bidhaa za tumbaku hadi miaka 21

Shirika la urekebishaji tabia na kudhibiti utumiaji wa mihadarati Barani Afrika linataka umri wa chini zaidi wa mtu kuruhusiwa kutumia bidhaa za tumbaku uongezwe hadi miaka 21.

Kwenye rufaa iliyowasilishwa katika Bunge la Seneti na lile la Kitaifa , shirika hilo lisilokuwa la kiserikali limesema hatua ya kuongeza umri huo itazuia kampuni za tumbaku kuchukua fursa ya hali ya vijana kutostahimili tamaa ya kutumia bidhaa hizo.

Shirika hilo limesema hatua hiyo itazuia kampuni za tumbaku kuwauzia vijana bidhaa za tumbaku kwa lengo la kujipatia faida.

Kwa sasa mtu anapofikia umri wa miaka 18, anazingatiwa kuwa na ujuzi unaohitajika kufanya maamuzi ya busara kuhusu uvutaji sigara.

Hata hivyo kwa mujibu wa rufaa ya shirika hilo, utafiti unaashiria kuwa watu wa umri huo hawana ukomavu wa kutosha wa kudhibiti hisia zao, kustahimili shinikizo za marafiki na kutambua hatari inayotokana na uvutaji sigara.

Categories
Habari

Moto wateketeza Jengo la Bunge la Kaunti ya Garissa

Mali ya thamani isiyojulikana imeharibiwa kufuatia mkasa wa moto katika jengo la Bunge la Kaunti ya Garissa.

Ukumbi wa vikao na afisi zilizoko karibu iliharibiwa na moto huo ambao chanzo chake hakijabainika.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Garissa, Mohamed Ali, moto huo uliteketeza takriban nusu ya jengo la bunge hilo.

Juhudi za wananchi za kuzima moto huo ziliambulia patupu kwani kulikuwa na zulia na dari la mbao kwenye jengo hilo.

Makundi kadhaa yakiwemo maafisa wa jeshi na wale wa idara ya wazima moto yalijitokeza kukabiliana na moto huo.

Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mkasa huo.

 

Categories
Habari

IEBC yaidhinisha mswada wa BBI

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imeidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020, kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa (BBI).

Kwenye taarifa, tume hiyo imesema kuwa imethibitisha saini za kutosha zinazohitajika kikatiba kuruhusu mswada huo kujadiliwa bungeni.

Kati ya saini zilizowasilishwa kwa tume hiyo na kamati ya kitaifa ya BBI mnamo tarehe 10 mwezi Desemba mwaka uliopita, jumla ya saini 1,140,845 zimethibitishwa kuwa sahihi.

IEBC sasa inapanga kutuma mara moja, nakala za mswada huo kwa mabunge ya kaunti zote 47 ili yaujadili ndani ya miezi mitatu.

Baadaye kila spika wa mabunge ya kaunti hayo atawasilisha ripoti ya uaumuzi kwa Spika wa Bunge la Kitaifa na wa Seneti.

Ikiwa angalau mabunge ya kaunti 24 yatapitisha mswada huo, basi wabunge na maseneta pia wataujadili na wakiupitisha, maandalizi ya kura ya maamuzi yatafuata.

Categories
Habari

Kuria amtaka Rais aunde kamati ya Bunge ili kuokoa mapendekezo muhimu ya BBI

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, sasa anamtaka Rais Uhuru Kenyatta kubuni kamati maalum ya Bunge ili kujadili namna ya kupitisha mapendekezo yenye manufaa katika mpango wa BBI.

Kuria amesema hatua hiyo itasaidia kuepusha hali ya mpango huo kutupiliwa mbali kwa kukosa uungwaji mkono.

Kuria amedumisha kwamba nchi hii haistahili kupoteza mapendekezo kadhaa muhimu katika mpango wa BBI, kama vile kuongezwa kwa kiwango cha fedha zinazotolewa kwa kaunti na kubuniwa kwa maeneo bunge mapya kwenye kaunti ambako hakuna uwakilishi wa kutosha.

Amekariri kwamba juhudi za kuandaa kura ya maamuzi kuambatana na hali ilivyo sasa humu nchini zitasababisha BBI kukosa uungwaji mkono wa kutosha kote nchini.

Akiongea katika eneo la Gatundu Kaskazini baada ya hafla ya mazishi katika Kijiji cha Kang’oo, Kuria ametoa wito kwa kiongozi wa taifa kuandaa mkutano wa kundi la wabunge wa vyama mbali mbali ili kujadili uwezekano wa kupitisha bungeni mapendekezo muhimu kwenye ripoti hiyo ya BBI.

Amesema ijapo ripoti hiyo ni nzuri, taratibu zinazohitajika kabla ya kufanyia katiba marekebisho hazijafuatwa.

Aidha, Kuria amesema inasikitisha kuona kwamba kutokana na tamaa za kibinafsi, baadhi ya wanasiasa wametumia ripoti ya BBI kama chombo cha kuzua ghadhabu miongoni mwa Wakenya wengi.

Categories
Habari

Wabunge wahitilafiana kuhusu pendekezo la BBI la kubuni Maeneo-Bunge 70 zaidi

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Kitaifa wameibua wasi wasi kuhusiana na mfumo mpya unaopendekezwa wa kugawanya maeneo-bunge mapya yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya BBI.

Wabunge hao hasa kutoka kaunti zilizo nje ya Nairobi, wakiongozwa na Mbunge wa Mwingi Magharibi Charles Nguna, wanapinga pendekezo la kuongeza maeneo bunge 12 mapya katika kaunti ya Nairobi wakisema ipo haja ya kuendeleza maeneo yote ya kijiografia.

Amesema ataendesha kampeini ya kupinga mpango wa BBI iwapo mfumo huo wa kugawanya maeneo mapya ya ubunge hautachunguzwa upya.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya amesema kuwa kubuniwa kwa maeneo mane mpya katika Kaunti ya Kilifi hakutasuluhisha changamoto ya uwakilishi akisema kuwa kulingana na takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Kaunti ya Kilifi inahitaji maeneo bunge sita mapya.

Amesema kuwa mpango huo wa BBI pia haujashughulikia jinsi ya kugawanya pesa za Hazina ya Usawazishaji Maendeleo.

Hata hivyo Mbunge wa Funyula Oundo Ojiambo ameunga mkono kubuniwa kwa maeneo bunge 70 mapya akisema ni bora kuliko kuunganisha maeneo bunge madogo.

Mbunge wa Endebbes Robert Pukose amekosoa pendekezo la kuongeza idadi ya wabunge bila kuelezea jinsi usawa wa kijinsia utakavyoafikiwa katika Bunge la Kitaifa.

Categories
Habari

Baadhi ya wanawake wakataa BBI

Kundi moja la wanawake limepinga marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano wa BBI.

Kundi hilo limesema marekebisho ya katiba yatahujumu ufanisi ambao umeafikiwa na wanawake kufuatia katiba ya mwaka wa 2010.

Wanawake hao wamedai kwamba marekebisho hayo yanatumiwa kuwafumba macho wanawake kwani hayaelezei jinsi suala la jinsia litakavyoshughulikiwa kwenye Bunge la Kitaifa.

Wakiongozwa na Daisy Amdany, wanawake hao wamesema watahamasisha wanawake wengine na Wakenya kwa jumla kupinga mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

“Ningependa kuomba akina mama wote wa Kenya tusimame pamoja tukatae BBI,” amesema mwanaharakati huyo.

Wamekashifu vikali mpango huo, wakihoji kuwa unanuiwa kuhujumu haki za kikatiba na uhuru wa wanawake.

Wamesema pendekezo la kuhakikisha uwakilishi sawa wa jinsia katika Bunge la Seneti ni hatua ya kuwafumba macho wanawake kwani watanyimwa fursa ya kuingia kwenye Bunge la Kitaifa ambalo litahusisha serikali pana.

Aidha wanawake hao wameisifu Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007.

Wamehimiza idara hiyo kutumia mifumo ya jumla kushughulikia maovu yaliyotekelezwa hapa nchini bila kushawishiwa kisiasa.

Categories
Habari

Wabunge washinikiza kuimarishwa kwa biashara kati ya Kenya na Tanzania

Kamati ya Bunge kuhusu Ushirikiano wa Kanda ya Afrika Mashariki imeweka mikakati ya kuimarisha biashara kati ya Kenya na Tanzania.

Akiongea wakati wa ziara mjini Isebania, Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo Ruweida Mohamed amesema biashara kupitia mpaka wa Kenya na Tanzania imekumbwa na changamoto ambazo zimeathiri mazingira ya utendaji biashara baina ya mataifa husika.

Hata hivyo, Ruweida ameeleza kuridhika na upimaji wa ugonjwa wa Korona kwenye mpaka huo ambao umeimarika kwa kiasi kikubwa licha ya changamoto za kisera kwenye mataifa husika.

Aidha ameeleza kufadhaishwa na ukosefu wa ushirikiano kati ya serikali ya taifa na ile ya Kaunti.

Wafanyabiashara wa humu nchini walikuwa wanalalamikia kuhangaishwa na maafisa wa usalama wa Tanzania na kufutiliwa mbali kwa leseni zao za kuhudumu.

Awali, katibu katika idara ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kevit Desai, alisema serikali imejitolea kuwakinga wafanyabiashara dhidi ya athari za ushuru wa juu.

Categories
Habari

Bunge la Seneti kujadili hotuba ya Rais

Bunge la Seneti leo linatarajiwa kujadili hotuba ya kuhusu hali ya taifa la Kenya iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi wiki iliyopita.

Kulingana na katiba, Bunge linapaswa kujadili yaliyomo kwenye hotuba hiyo kati ya siku tatu na nne baada ya Rais kuhutubu.

Maseneta wataangazia maswala mbali mbali ikiwemo ripoti ya saba ya kila mwaka kuhusu hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana katika harakati za kuafikia maadili ya kitaifa na misingi ya uongozi.

Ripoti ya kila mwaka kwa Bunge kuhusu usalama wa kitaifa na ripoti ya pamoja ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ya miaka ya kifedha ya 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020 pia zitajadiliwa.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta aliangazia maswala kadhaa ya kitaifa ikiwemo ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, juhudi za kupambana na janga la Corona na ufunguzi wa shule.

Rais aliwahakikishia Wakenya kwamba hali ya taifa hili iko imara licha ya changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga la ugonjwa wa COVID-19.