Categories
Burudani

Msanii Q Chief atoa ilani kwa Wasafi Media

Msanii wa Bongo Fleva Q Chief ameupa usimamizi wa Wasafi Media na Kampuni ya Tigo muda hadi mwisho wa siku hii leo ili apate maelezo kamili kuhusu sababu ya kuweka jina lake na picha yake kwenye bango la tamasha lao bila idhini yake.

Kupitia Instagram, Q Chief alisema kwamba hakuna yeyote aliwasiliana naye rasmi kutoka kwa kampuni hizo ili kumshirikisha kwenye tamasha hilo la Jumamosi tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2021 almaarufu kama “Wasafi Tumewasha na Tigo”.

Anaendelea kuelezea kwamba mashabiki wake wengi wamekuwa wakimpigia simu kujua ni kwa nini hakuonekana kwenye tamasha hilo ilhali walikuwa wakimtarajia jambo ambalo anasema linaathiri kazi yake ya muziki.

Q Chief anasema amekuwa akijaribu kuwasiliana na usimamizi wa Wasafi Media bila mafanikio huku akiambiwa kwamba wahusika bado wana uchovu wa tamasha la jumamosi.

Hata hivyo wengi wa mashabiki wake kwenye Instagram, wanaonelea kwamba hakustahili kuweka ilani hiyo kwenye mitandao ya kijamii na kwa kufanya vile wanahisi anajitafutia umaarufu.

Hakuna jibu lolote limetolewa na Wasafi Media inayomilikiwa na Diamond Platnumz wala kampuni ya mawasiliano ya rununu ya Tigo kuhusu lalama za Q Chief.

Categories
Burudani

Steve Nyerere akumbuka wema wa Mr. Nice

Jamaa mmoja nchini Tanzania kwa jina Steve Nyerere ambaye ni mchekeshaji amemkumbuka mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Mr. Nice kwa mema aliyomtendea.

Kulingana na Nyerere, yeye na wengine walikuwa walinzi wa Mr. Nice wakati alikuwa maarufu sana na muziki ulikuwa ukimlipa vizuri.

Nyerere anakumbuka kwamba yeye na wenzake walikuwa wakipigwa kila mara walipokuwa wakimpeleka mkubwa wao kwenye matukio mbali mbali.

Anakumbuka wakati mmoja yeye na rafiki yake Ray Kigosi walikuwa na njaa na hawakuwa na la kufanya. Wakahimizana waende nyumbani kwa Mr. Nice kutafuta usaidizi.

Anasema walibisha lango kuu wa muda bila jibu ndiposa wakaamua kuruka ua wa ukuta na kuingia ndani ambapo walimpata Mr. Nice amelala wakamwamsha.

Jambo la kwanza alitaka kujua toka kwao ni jinsi waliingia humo, wakawa wakweli wakasema waliruka ua. Akaita mlinzi kudhibitisha hayo akapata ni kweli.

Baada ya hapo aliwapa sikio ili kujua kilichowaleta kwake na wakamwambia walikuwa wanahisi njaa na hawakuwa na pesa za kununua chakula.

Hawakuamini macho yao pale ambapo Mr. Nice aliwapa kadi yake ya benki, namba za siri na akawaamrisha wakajitolee milioni moja tu pesa za Tanzania kasha wairudishe.

Steve Nyerere anasema waliimba nyimbo za Mr. Nice mwendo wote na kurudi. Anamshukuru mwanamuziki huyo ambaye sikuhizi anasuasua katika kazi yake ya muziki na kumwombea Baraka kwa mwenyezi Mungu.

Mr. Nice ni mmoja kati ya wanamuziki walioanzisha mtindo wa kizazi kipya nchini Tanzania kwa jina Bongo Fleva.

Anasemekana kupata pesa nyingi wakati huo ambazo wengi wanasema hakuwekeza ila katumia vibaya.

Categories
Burudani

Rayvanny kuzindua albamu

Msanii wa Bongo Fleva Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny ama ukipenda vanny Boy ametangaza kwamba ataachilia albamu yake ya kwanza hivi karibuni.

Vanny ambaye anafanya kazi ya muziki chini ya kampuni ya Diamond Platnumz Wasafi Classic Baby – WCB alianza muziki mwaka 2011 akiwa shule ya upili lakini hajawahi kuzindua albamu.

Alijiunga na WCB rasmi mwaka 2015 na mwaka 2016 akaachilia kibao “Kwetu” ambacho kilivuma sana Afrika mashariki.

Mwezi wa pili mwaka 2020 Rayvanny alizindua EP yake kwa jina “Flowers” ambayo ilifanya vyema kwenye mitandao ya kijamii.

EP au ukipenda ‘Extended Play’ ni mkusanyiko wa nyimbo ambazo hazitoshi kuitwa albamu. Mwanamuziki huyo ameteuliwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa.

Ni kati ya wanamuziki wanaofanya vizuri katika WCB na mkubwa wake Diamond aliwahi kufichua kwamba alikuwa akijenga studio zake za muziki isijulikane kama atagura WCB alivyofanya Harmonize.

Diamond alisifia sana studio hizo akisema kwamba zikikamilika zitakuwa bora zaidi Afrika mashariki.

Rayvanny amejulikanisha ujio wa albamu hiyo kwa jina “Sound From Africa” kupitia picha na video ambazo amekuwa akiweka kwenye mtandao wa Instagram lakini hajatangaza tarehe rasmi ya kuiachilia.