Categories
Habari

IEBC yazindua rasmi zoezi la uthibitishaji saini za BBI

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imezindua zoezi la kuthibitisha saini zilizokusanywa na kamati ya BBI katika Ukumbi wa Bomas.

Kupitia taarifa, tume hiyo imesema kuwa makarani 400 walioajiriwa kwa ajili ya zoezi hilo wamepokea kiapo cha siri na wataanza mafunzo mara moja.

IEBC pia imeidhinisha watu 72 wanaowakilisha mashirika sita ambao watakuwa waangalizi wa mchakato wa uthibitishaji wa saini hizo.

Wakati uo huo, tume hiyo ya IEBC imewahimiza maafisa wake, makarani na waangalizi wa mchakato huo kuzingatia kanuni za kujiepusha na maambukizi ya COVID-19 kwa ajili ya usalama kwa wote.

“Mahali pa kuthibitisha saini pameandaliwa kwa vifaa vya kutosha vikiwemo vieuzi na sehemu za kunawa mikono ili kuhakikisha kwamba kanuni za usalama kutokana na COVID-19 zinazingatiwa,” imesema IEBC.

Tume hiyo itapokea kitita cha shilingi milioni 93.7 kutoka kwa Wizara ya Fedha ili kufadhili zoezi hilo, huku makarani wakilipwa shilingi 1,200 kila siku.

Awali, tume hiyo ilikuwa imeomba shilingi milioni 241 kwa ajili ya zoezi hilo lakini serikali ikapunguza fedha hizo hadi shilingi milioni 93.7.

Categories
Habari

Rais Kenyatta awahimiza vijana wachangamkie maswala ya kitaifa

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa vijana kushiriki ipasavyo katika maswala muhimu ya kitaifa.

Rais Kenyatta amesema kuwa wakati umewadia kwa vijana kuchukua ushukani wa maswala ya humu nchini.

Rais amesema kuwa licha ya vijana kuwa zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya Wakenya, hawajashiriki ipasavyo katika uongozi wa taifa hili.

Kiongozi wa taifa amesema hayo katika ukumbi wa Bomas, Jijini Nairobi wakati alipozindua rasmi mjadala wa kitaifa wa vijana kwa jina ‘Kenya ni Mimi’.

Rais ameongeza kuwa vijana wanahitaji kutumia idadi yao kuwania nyadhifa za uongozi nchini.

Amekariri kwamba vijana lazima wawe katika msitari wa mbele kuboresha maisha yao na taifa hili kwa jumla.

“Lazima muwe ndani ya uwanja wala sin je ya uwanja. Lazima mshiriki katika mjadala wa nchi hii kama mtaamua kwamba mnataka kushika usukani wa hatma ya nchi. Mko na nafasi kubwa,” amesema Rais.

Kuhusu mizozo ya kijinsia na tamaduni nyingine zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji na ndoa za mapema, Rais Kenyatta amewahakikishia vijana kuwa serikali haitalegeza juhudi za kukabiliana na maovu hayo.

Aliongeza kwamba serikali yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na wanawake pamoja na vijana katika nyanja zote za kimaendeleo.

Categories
Habari

Hatimaye Ruto atoa mchango wake kwenye mchakato wa BBI

Naibu Rais William Ruto ametoa maoni yake kuhusu maswala kadhaa yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya BBI iliyozinduliwa rasmi leo.

Kwenye hotuba yake katika hafla hiyo, Ruto ameonekana kukosoa baadhi ya vipengele vya marekebisho ya katiba, jambo lililopelekea baadhi ya wajumbe waliofika kwenye hafla hiyo kumzoma.

Ruto ameanza vyema hotuba yake ambapo amekashifu baadhi ya vyombo vya habari baada ya mojawapo kuchapisha taarifa ya kwamba Kiongozi wa ODM Raila Odinga ametangaza kuwania urais 2022, taarifa ambayo Raila mwenyewe pia ameikashifu.

“Kwenye taarifa iyo hiyo, wamesema Ruto atakutana na mashetani Bomas. Najiuliza kama kunayo mashetani yoyote hapa Bomas, au niwaulize oliskia wapi kwamba kuna mashetani ndani ya Bomas?” akasema Ruto.

Baadaye Naibu Rais amekiri kwamba baadhi ya mapendekezo ya BBI yana umuhimu, hasa yale yanayogusia maswala ya vijana na uchumi, akiongeza kuwa swala la ukosefu wa kazi kwa vijana linafaa kuangaziwa zaidi kwenye mjadala mzima.

Baada ya hapo, Ruto ameanza kushtumu baadhi ya mapendekezo ya BBI kuhusu maswala ya uongozi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, Uhuru wa Idara ya Mahakama, Uwakilishi wa wanawake bungeni miongoni mwa maswala mengineyo.

Ruto amekashifu kipengele kinachotoa nafasi kwa baadhi ya vyama vya kisiasa kuchagua viongozi wa tume ya IEBC, akitoa mfano wa timu za kandanda kuteua refa wa kusimamia mechi.

“Ndugu yangu Raila Odinga ni mpenzi wa kandanda. Nataka kuuliza, je, kutakuwa na haki katika ligi ambayo refa ameteuliwa na timu zinazoshiriki, na si timu zote, baadhi ya timu?” akauliza Ruto.

Alipojaribu kuzungumzia swala la kujumuishwa serikalini kwa wanaoshindwa katika uchaguzi, Naibu Rais amepata pingamizi kutokana na kelele za baadhi ya waliohudhuria, na alipouliza kuhusu uwezekano wa kutatua changamoto hiyo, umati ukapaza sauti ya ndiyo.

Kutokana na kelele za watu waliokuwa hawaridhishwi na hotuba yake, Ruto amelazimika kuomba muda kidogo ili amalizie hotuba hiyo ambapo amejibu matamshi ya awali kuhusu mpango wake wa kutoa misaada ya mikokoteni, akitetea mpango huo kuwa unasaidia vijana wasio na ajira.

Hata hivyo Naibu Rais ameunga mkono kipengele cha nyongeza ya mgao wa fedha kutoka serikali kuu hadi zile za kaunti ambapo zitapokea asilimia 35 badala ya asilimia 15 kama ilivyo sasa.

Hatimaye Ruto amehitimisha hotuba yake kwa kumualika Rais Uhuru Kenyatta wakati ambapo umati ulikuwa umeanza kupaza sauti za kumwambia ampe Rais heshima yake.

Categories
Habari

Rais Kenyatta awataka viongozi wapunguze joto la siasa

Rais Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa kisiasa wapunguze kasi ya siasa za mwaka wa 2022 na badala yake watilie mkazo juhudi za kuunganisha Wakenya.

Kwenye ujumbe wake wa moja kwa moja kwa Naibu Rais William Ruto, Rais amesema, japo kwa utani, kwamba Ruto amepoteza dira baada ya kuonekana kuangazia zaidi kampeni za urais katika uchaguzi mkuu ujao.

“Namshukuru Naibu Rais, tumetembea pamoja hadi wakati siasa za 2022 zilipomfanya asahau kila kitu. Watu wanafaa kuwa watulivu kwanza, wakati huo utafika,” amesema Rais.

Amesema hayo kwenye hotuba yake katika hafla ya kuzindua rasmi ripoti ya BBI kwa umma iliyofanyika katika Ukumbi wa Bomas, Jijini Nairobi.

Rais Kenyatta amefananisha hali hiyo na mbio za kupokezana ambapo ameuchekesha umati kwa kusema kuwa badala ya kuendeleza mbio hizo, naibu wake amegeuka na kukimbia akirudi nyuma.

Rais pia ameeleza kuwa alitaka kutumia siku hiyo kumshukuru Ruto, akihoji kuwa amekuwa akimhusisha katika mchakato wa maridhiano na kinara wa ODM Raila Odinga.

“Nataka pia nimshukuru Naibu Rais, katika mchakato huu nimekuwa nikimueleza yaliyokuwa yakiendelea. Amekuwa sehemu ya mchakato huo, huu ni ukweli siwadanganyi, mnaweza kumwuliza yupo hapa. Kwanza alinisaidia kuchagua baadhi ya wazee amabao nimewataja hapa,” akasema kiongozi wa taifa.

Aidha, Rais Kenyatta amemsifu Raila kwa ukarimu wake na kulenga maridhiano, akisema kuwa hakutaka kupewa sehemu ya uongozi serikalini.

Ameongeza kuwa maridhiano yake na Raila yaliyozalisha BBI hayalengi kujipatia nafasi serikalini bali walikuja pamoja kwa lengo la kusitisha mapigano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa humu nchini baada ya kila uchaguzi tangu mwaka wa 1992.

Kenyatta amekuwa wazi kwamba wanataka kuleta kila mtu kwenye mchakato huo ili kuhakikisha kwamba hakuna mkenya anayeachwa nyuma.

Amesema wataendelea kushauriana na viongozi mbali mbali akihoji kuwa kama taifa, Wakenya wanaweza kuiboresha ripoti ya BBI, akiwataka walio na maoni kuhusu ripoti hiyo wayalete mezani.

Categories
Habari

Raila awarai Wakenya kuidhinisha ripoti ya BBI bila ushindani

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amesema kwamba tayari sauti za Wakenya zilizingatiwa kwenye ripoti ya BBI na kilichobaki ni kuipitisha bila upinzani.

Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Raila ameonekana kutoa wito wa kuungwa mkono kwa pendekezo la marekebisho ya katiba bila mvutano.

Akihutubia wajumbe kutoka kaunti zote 47 katika hafla hiyo iliyoandalikwa katika Ukumbi wa Bomas, kiongozi huyo wa ODM amehoji kuwa hakuna haja ya ‘Ndiyo’ au ‘La’ kwenye mchakato huo.

Waziri Mkuu huo wa zamani amesema BBI inaipa nchi hii nafasi nyengine ya kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye katika ya mwaka wa 2010.

Akiwahimiza wale wanaotilia shaka yaliyomo kwenye ripoti hiyo ili waiunge mkono, Raila amesema mpango huo una lengo la kuipeleka nchi hii mbele, kwa kuwa umetilia maanani mashauriao yaliyofanywa na Wakenya.

Amehoji kuwa BBI inatoa fursa ya kutathmini yale yanayokosekana katika katiba ya sasa ambayo ameisifu kwa ubora wa kimataifa, akisema ajenda hiyo ndiyo iliyopelekea kuridhiana na mpinzani wake wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta.

“Hii ndiyo sababu tulikuja pamoja. Baadaye tuliipa kamati hii jukumu la kuchukua maoni kutoka kwa Wakenya. Kutoka hapo tukaanza safari mpya. Tulitembelea sehemu mbali mbali za nchi hii na watu wakazungumza,” amesema Raila.

Amesema mpango huo pia una madhumuni ya kuleta usawa kwa Wakenya ambao wanapaswa kupata mahitaji ya kimsingi kama chakula na huduma za afya.

Kuhusu umoja wa taifa, Raila amewapa changamoto Wakenya kutupilia mbali maswala ya kikabila.

“Sote tunapaswa kuwa wamoja kama Wakenya. Hiyo ndiyo sababu tuko katika mchakato huu.”

Odinga pia ameonekana kumkosoa Naibu Rais William Ruto kwa kufanya kampeni za mapema za uchaguzi wa mwaka wa 2022, hatua ambayo ameitaja kama inayoleta taswira kwama serikali ya Rais Kenyatta haijatimiza ajenda zake za kimaendeleo.

Amesema Ruto hawezi kujitenga na serikali iliyo mamlakani sasa.

Categories
Habari

Halfa ya uzinduzi wa ripoti ya BBI yang’oa nanga Bomas

Uzinduzi wa ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa BBI unaendelea katika Ukumbi wa Bomas, jijini Nairobi.

Hafla hiyo inaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga miongoni mwa viongozi wengine mbali mbali humu nchini.

Ripoti hiyo hiyo inanuiwa kurekebisha baadhi ya sehemu za katiba ya mwaka 2010 ambapo inapendekeza sheria na marekebisho kadhaa kwa sheria zilizoko ili kuziba mianya iliyoko.

Uzinduzi wa ripoti hiyo unajiri baada ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika Ikulu Ndogo ya Kisii Jumatano wiki iliyopita.

Wale wanaozungumza kwenye shuhuli hiyo wamepongeza hatua hiyo wakisema wakati umewadia wa kushughulikia tofauti za muda zilizoko.

Wale ambao wametoa hotuba zao ni pamoja na Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu, Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyikani nchini COTU Francis Atwoli, miongoni mwa viongozi wengine wanaowakilishamakundi mbali mbali nchini.

Kilele cha hafla hiyo ni hotuba ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga kabla Naibu Rais William Ruto pia kutoa hotuba yake na kumkaribisha Rais Uhuru Kenyatta.

Categories
Habari

Oparanya awasihi Wakenya kuunga mkono ripoti ya BBI

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliffe Oparanya, amewataka Wakenya kuunga mkono ripoti ya Mchakato wa Maridhiano (BBI) iliyokabidhiwa rasmi Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega alisema ripoti hiyo inalenga kuongeza mgao wa mapato kwa Kaunti kutoka asilimia 15 hadi asilimia 35.

Oparanya ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano na Makatibu  wa Kaunti 47 Jijini Nairobi, alisema pesa hizo zitasaidia serikali za Kaunti kuanzisha miradi zaidi  itakayokuwa na  manufaa makubwa ya ustawi  katika kaunti hizo.

Katika kile kinachoonekana kupiga jeki mfumo wa ugatuzi nchini, ripoti hiyo inapendekeza kubuniwa kwa  Hazina ya Wadi  itakayosimamiwa kisheria.

Vile vile inapendekeza kuongezwa kwa  rasilimali za  Kaunti kutoka  mgao wa mapato wa asili-mia 15 ya sasa hadi angalau  asiili-mia 35 na kuhakikisha kuwa lengo lake kuu  ni utoaji wa huduma katika maeneo yaliyo na watu  na  yanayohitaji kuhudumiwa, pamoja na  kushughulikia watu wanaoishi kwenye mipaka ya mbali katika   kila Kaunti.

Jopo lililoandaa ripoti hiyo linatarajiwa kukutana  katika   ukumbi wa  Bomas  mnamo   Jumatatu ili kuwafafanulia  Wakenya yaliomo katika  ripoti hiyo.

.