Categories
Kimataifa

Mahakama ya Uganda yaagiza Bobi Wine aachiliwe huru

Mahakama moja nchini Uganda imetoa agizo kwa maafisa wa usalama kuondoka nyumbani kwa mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine.

Hii ni baada ya mahakama hiyo kuitaja hatua ya kumuweka Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, kwenye kifungo cha nyumbani kuwa isiyo halali.

Mwanasiasa huyo hajaweza kutoka nyumbani kwake tangu aliporudi kutoka kituo alikopigia kura katika uchaguzi mkuu nchini humo siku 11 zilizopita.

Agizo la kuachiliwa huru kwa Bobi mapema Jumatatu limetolewa kufuatia uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na mawakili wake ya kupinga hatua ya maafisa wa usalama wa serikali kuendelea kuzingira makazi yake.

Hatua hiyo ilishutumiwa vikali na baadhi ya viongozi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ulimwenguni lakini maafisa hao wakadai kwamba Bobi alikuwa akipewa ulinzi kwa sababu alikuwa mgombea urais.

Tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza Bobi kuwa aliibuka nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro cha urais, baada ya kushindwa na Rais Yoweri Museveni.

Hata hivyo, Bobi alipinga vikali matokeo hayo, akidai kwamba anao ushahidi wa kutosha wa kudhihirishwa kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura hizo.

Categories
Kimataifa

Mtandao warejeshwa Uganda baada ya kufungwa wakati wa uchaguzi mkuu

Huduma ya mtandao imerejeshwa nchini Uganda baada ya kuzimwa kwa siku tano wakati wa uchaguzi mkuu.

kufuatia agizo la serikali, huduma hiyo ilifungwa Jumatano usiku, saa chache kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa siku ya Alhamisi iliyopita.

Hata hivyo, mitandao ya kijamii bado imesalia kufungwa.

Wakati uo huo, msemaji wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Joel Ssenyonyi, amesema afisi ambapo mawakala wake walikuwa wakiandaa stakabadhi za kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo zimevamiwa na wanajeshi.

Ssenyonyi amesema mawakala hao walikuwa wakikusanya fomu za matokeo ya uchaguzi zilizo na ushahidi wa udanganyifu.

Hii ni baada ya makaazi  ya kiongozi wa chama hicho Bobi Wine kuzingirwa na wanajeshi wa serikali.

Bobi alikataa matokeo ya uchaguzi wa urais kama yalivyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Kulingana na matokeo hayo, Rais Yoweri Museveni ndiye aliyeshinda kinyang’anyiro hicho dhidi ya Bobi Wine aliyeibuka wa pili.

Bobi alishtumu vikali jinsi uchaguzi huo ulivyofanywa, huku akidai kwamba ana ushahidi wa kutosha kuhusu visa vya udanganyifu.

Categories
Kimataifa

Bobi Wine sasa adai maisha yake yamo hatarini

Mgombeaji urais wa mrengo wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema anahofia maisha yake.

Hii ni baada ya mgombea huyo kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo ambapo Rais Yoweri Museveni alihifadhi kiti chake.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa alikataa matokeo ya uchaguzi huo, kwani hakutendewa haki, akihoji kwamba ulikumbwa na udanganyifu mwingi.

Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amesema anahofia maisha yake na yale ya mkewe.

Anasema hajaruhusiwa kuondoka  nyumbani kwake kwani nyumba hiyo imezingirwa na maafisa wa usalama.

Licha ya Bobi kudai kuwa kulikuwa na visa vingi vya udanganyifu kwenye uchaguzi huo, Rais Museveni ameutaja kuwa wa huru na haki.

Kampeni za kabla ya uchaguzi huo zilighubikwa na ghasia huku watu kadhaa wakiuawa.

Serikali ilifunga huduma za mitandao kote nchini humo siku ya kuamkia kupiga kura.

Categories
Habari

Rais Kenyatta ampongeza Museveni kwa kuhifadhi kiti cha urais nchini Uganda

Rais Uhuru Kenyatta amempongeza Yoweri Museveni kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Uganda.

Siku ya Jumamosi, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi huo mkuu kwa kujizolea zaidi ya asilimia 58 ya jumla ya kura za urai.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Museveni alimshinda mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, aliyepata asilimia 34 ya kura hizo zilizopigwa mnamo siku ya Alhamisi.

Kupitia ukurasa wa Facebook wa Ikulu ya Kenya, Rais Kenyatta amesema kuchaguliwa tena kwa Museveni ni ushuhuda tosha wa imani waliyonayo wananchi wa Uganda kwa uongozi wake.

Kwenye ujumbe wake wa heri, Rais Kenyatta pia ameahidi kuendelea kushirikiana na Museveni ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na Uganda kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Kiongozi wa taifa pia ameusifu uongozi wa Museveni kwa kuimarisha nchi hiyo na vile vile kuandikisha maendeleo bora ya kiuchumi nchni humo.

Museveni, mwenye umri wa miaka 76, amekuwa uongozini tangu mwaka wa 1986 na ushindi wake sasa unamaanisha kwamba ataiongoza Uganda kwa muda usiopungua miaka 40 kama rais.

Hata hivyo, upande wa upinzani tayari umepinga matokeo hayo, huku Bobi Wine akiahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kwamba kulikuwa na udanganyifu mwingi kwenye shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura hizo.

Categories
Kimataifa

Marekani yagomea uchaguzi mkuu wa Uganda

Marekani haitashiriki katika uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Alhamisi nchini Uganda.

Hii ni kutokana na hatua ya tume ya uchaguzi nchini humo kukataa asilimia 75 ya maombi ya Marekani ya kuwapa idhini waangalizi ili kushiriki katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Balozi wa Marekani nchini Uganda Natalie Brown, tume hiyo haikutoa maelezo kuhusiana na uamuzi huo, licha ya kuwasilishwa kwa maombi kadhaa.

Amesema kuwa ni waangalizi wachache tu ndio walioteuliwa kutoka kwa kundi la watu 88.

Ameongeza kuwa uchaguzi huo mkuu wa Uganda utakosa uwazi na imani ambayo hutokana na kuwepo kwa waangalizi kutoka mataifa ya nje.

Raia wa Uganda watawachagua wabunge wapya na rais katika uchaguzi huo wa Alhamisi.

Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 35, atakuwa akiwania muhula wa sita mamlakani.

Hata hivyo Museveni anatarajiwa kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa upande wa upinzani Bobi Wine.

Categories
Kimataifa

Taharuki ya kiusalama yatanda nchini Uganda kabla uchaguzi mkuu Alhamisi

Vikosi vya usalama nchini Uganda vimesema maafisa zaidi wa usalama watapelekwa katika wilaya zote 39 nchini humo ambako kunakisiwa ghasia za uchaguzi zinaweza kuzuka.

Tangazo hilo ni miongoni mwa mikakati ya matayarisho inayowekwa kabla ya uchaguzi mkuu siku ya Alhamisi.

Haya yanajiri huku Tume ya Mawasiliano nchini humo ikiagiza kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano ya mitandao ya kijamii kufungwa.

Miezi miwili ya kampeni imekumbwa na ghasia na kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao.

Polisi wanasema malori ya kusafirisha mafuta, magari yanayobeba vilipuzi na malori mengine makubwa hayataruhusiwa katikati ya Mji Mkuu wa nchi hiyo Kampala, siku ya upigaji kura.

Maafisa wa usalama wana wasiwasi kwamba vifaa kama hivyo vinaweza kutumiwa na waandamanaji.

Uegeshaji magari kando ya barabara pia hautaruhusiwa mjini Kampala.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Polisi nchini Uganda, Martin Ochola, alionya kwamba yeyote atakayezua vurugu atajuta.

Maafisa wa serikali wanasema kupelekwa kwa maafisa wa usalama kushika doria kunanuiwa kudumisha amani lakini wahakiki wanaonelea kuwa hilo ni jaribio la kuwahangaisha wapiga kura.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kati ya Rais wa sasa Yoweri Museveni na hasimu wake Bobi Wine.

Categories
Kimataifa

Mtandao wa Facebook wafunga akaunti za Museveni

Mtandao wa Kijamii wa Facebook umefunga akaunti kadhaa za chama tawala nchini Uganda cha National Resistance Movement (NRM).

Mtandao huo umedai kuwa kurasa hizo zinalenga kuvuruga mjadala wa umma kabla ya uchaguzi mkuu wa siku ya Alhamisi nchini humo.

Mkuu wa mawasiliano wa mtandao wa Facebook katika eneo la Sub-Saharan Africa Kezia Anim-Addo amesema kuwa walitoa mitandao na kurasa kadhaa nchini Uganda ambayo walidai kuwa ilikuwa inajihusisha na mienendo isiyofaa ikilenga mijadala ya umma kabla ya uchaguzi huo.

Ashburg Kato, ambaye ni mwana blogu mashuhuri wa chama tawala, aliwashtumu wanasiasa wa upinzani na mwaniaji urais Bobi Wine na walinzi wake kwa kuhusika na hatua hiyo.

Bobi Wine hajasema lolote kuhusu madai hayo.

Categories
Burudani

Bobi Wine aangaziwa kwenye Spotify

Mwanamuziki wa nchi ya Uganda Bobi Wine ameangaziwa kwenye kipindi fulani cha sauti tu ambacho kimewekwa kwenye jukwaa la muziki na vipindi vya sauti kwa jina Spotify.

Mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Marekani kwa jina Bas ndiye mtangazaji katika kipindi hicho kilichopatiwa jina la “The messenger” na kitaangazia maisha ya Bobi Wine.

Mbunge huyo wa eneo bunge la Kyandondo Mashariki nchini Uganda ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu anaangaziwa kwa sababu anawania urais nchini Uganda kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 14 mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Safari yake ya uanaharakati na kampeni za urais haijakuwa rahisi na kwa sasa anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa rais wa sasa Yoweri Museveni.

Jukwaa la kimitandao la Spotify linatoa fursa kwa watu kupakua na kusikiliza muziki na vipindi popote walipo lakini barani Afrika, linapatikana katika nchi chache.

Afrika Kusini, Morocco, Misri, Algeria na Tunisia ndizo nchi pekee ambazo zimekubalia Spotify kufikia sasa na haijulikani litasambaa lini kwenye nchi nyingine za Afrika.

Hii ina maana kwamba hata Uganda ambayo ni nchi muhimu kwa kipindi hiki cha Bobi Wine haitapata kukisikiliza.

Kipindi kuhusu maisha ya Bobi Wine kimeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Dreamville Studios na Awfully Nice Productions na kilikuwa kipatikane kwa mara ya kwanza kwenye Spotify tarehe 5 mwezi Januari mwaka 2021 siku chache kabla ya uchaguzi mkuu nchini Uganda.

Categories
Burudani

Mlinzi wa Bobi Wine auawa

Mmoja wa walinzi wa mwanamuziki wa Uganda Bobi Wine anasemekana kuaga dunia baada ya kugongwa na lori la polisi katika eneo la Busega.

Francis Ssenteza Kalibala ambaye ni mlinzi wa binafsi wa Bobi Wine mwaniaji urais wa chama cha National Unity Platform NUP, anasemekana kugongwa na gari hilo la polisi wakati kundi la kampeni la Bobi lilikuwa njiani kutoka eneo la Masaka kuelekea jiji kuu Kampala kwa ajili ya kutafutia mwanahabari matibabu zaidi.

Lori hilo la polisi nchini Uganda ambalo nambari ya usajili ni “H4DF 2382” linasemekana kutumika kuzuia msafara wa Bobi Wine uliokuwa katika eneo hilo ukijaribu kuokoa maisha ya mwanahabari.

Mwanahabari huyo wa Ghetto Media kwa jina Ashraf Kasirye naye anasemekana kupigwa risasi kichwani na polisi wakati kundi la kampeni la NUP lilikuwa likielekea Lwengo kwa ajili ya kampeni za siku ya leo.

Francis anasemekana kuaga dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Lubaga. Kufikia sasa hakuna taarifa kuhusu mwanahabari Ashraf aliyepigwa risasi.

Kampeni za Bobi Wine mbunge wa Kyandondo mashariki kwa jina halisi Robert Ssentamu Kyagulanyi huwa zinaingiliwa kila mara na maafisa wa usalama nchini Uganda.

Kwa wakati mmoja Bobi Wine alikamatwa na polisi kwa madai ya kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid 19 jambo ambalo lilizua ghasia na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Yeye ndiye mpinzani wa karibu wa Rais wa sasa nchini Uganda Yoweri Kaguta Museveni kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ingawaje kuna wawaniaji wengine wengi.

Categories
Burudani

Bobi Wine aandaa tamasha la Krismasi

Mwanamuziki wa Uganda Bobi Wine jana tarehe 25 mwezi Disemba mwaka 2020 aliandaa tamasha la muziki saa 12 jioni hadi saa mbili usiku, nyumbani kwake, katika wilaya ya Ntungamo nchini Uganda.

Kulingana na tangazo kwenye ukurasa ulioidhinishwa wa Facebook wa mwanamuziki huyo ambaye pia anawania Urais nchini Uganda, tamasha hilo lilikuwa la kuwasherehekea watu wa kundi lake la kampeni.

Tukio hili lilijiri baada ya Bobi ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, mke wake Barbara na watoto kuungana na waumini katika kanisa katoliki la mtakatifu James Rugarama, wilayani Ntungamo katika Kaunti ya Rushenyi, nchini Uganda kwa ibada ya Krismasi.

Kanisa hilo liko katika kijiji alikozaliwa mke wa Bobi kwa jina Barbie.

Waliohudhuria tamasha hilo walikuwa wamevalia mavazi rasmi ya chama cha National Unity Platform NUP, chake Bobi Wine.

Alishirikiana na mwanamuziki Nubian Li katika kutumbuiza washirika wake wa kampeni huku akiwashukuru kwa kuwa naye kwenye ziara za kampeni ambapo kufikia sasa wamezuru wilaya 95.

Alimtaja mwanahabari mmoja John Cliff Wamala, ambaye alichumbia mpenzi wake maajuzi na akamwimbia wimbo wa mapenzi huku akisema kwamba anatumai jamaa huyo hatafutwa kazi kwa kuangazia kampeni zake.

Nubian alisikika akitoa wito kwa polisi wasiwarushie vitoa machozi na Bobi anasikika akimkata akisema kwamba polisi hawangewasumbua kwani walikuwa nyumbani.

Mbunge huyo wa Kyandondo Mashariki alisikika akihimiza waliokuwa wakihudhuria tamasha hilo wavalie barakoa wakati wote.

Anaonekana kutilia maanani kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona hasa baada ya kukamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kuweka mazingira ya msambao wa corona kwenye kampeni.