Categories
Habari

Rais Kenyatta azindua hazina ya kufadhili uchumi wa vijana wa MbeleNaBiz

Rais Uhuru Kenyatta amezindua mpango wa kibiashara wa MbeleNaBiz wa kuwatuza wajasiria mali chipukizi na uzinduzi wa mpango makhsusi wa hazina ya vijana wa mwaka 2020-2024.

Akisimamia uzinduzi huo katika Uwanja wa Michezo wa Moi Kasarani Jijini Nairobi, Rais Kenyatta amesema serikali itatenga shilingi bilioni 1.3 za kufadhili uchumi wa vijana wa taifa hili.

Kulingana na Rais, kati ya pesa hizo, shilingi milioni 900 zitatolewa kwa wajasiriamali 250 kama ruzuku.

“Jumla ya shilingi milioni 900 zitapewa

Rais pia ametumia fursa hiyo kuhimiza vijana kuunga mkono mpango wa maridhiano wa BBI ambao tayari umeungwa mkono na mabunge 40 ya kaunti.

Amesema kupitishwa kwa mpango huo kutawawezesha vijana kupata pesa na kuhakikisha rasili mali zaidi zinawasilishwa katika maeneo ya magatuzi ili kufadhili maendeleo.

Categories
Habari

Biashara zanoga Jomvu kufuatia kupungua kwa visa vya uhalifu

Eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, imeanza kuvutia wawekezaji kutokana na amani inayoshuhudiwa na kupungua kwa visa vya utovu wa usalama katika eneo hilo.

Kulingana na Mbunge wa eneo hilo Badi Twalib, eneo hilo limeshuhudia ongezeko la shughuli za kibiashara na kuwezesha wakazi kupata nafasi za ajira.

Twalib amesema hii ni kutokana na ushirikiano kati ya wakazi, viongozi wa eneo hilo na serikali.

“Jomvu ni eneo salama la kuishi, ndiyo sababu watu wamekuja hapa kufanya biashara. Na kama mbunge, nitahakikisha kazi yangu ni kulinda maslahi ya wananchi wangu na biashara zao,” ameeleza mbunge huyo.

Mbunge huyo alikuwa akiongea alipokabidhi gari la polisi litakalotumiwa kukabiliana na visa vya uhalifu katika eneo la Jomvu.

Amesema eneo hilo lilikuwa likikumbwa na visa vya utovu wa usalama, tatizo alilosema sasa limetokomezwa.

Twalib pia amezuru mradi unaendelea wa ujenzi wa majengo ya kisasa ya makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Jomvu huko Mikindani ambao unafadhiliwa kupitia Hazina ya Ustawi wa Eneo Bunge hilo CDF.

Kwenye ziara hiyo, Twalib amesema majengo hayo yatakuwa na afisi zote za utawala na yataimarisha utoaji huduma kwa wakazi.

“Afisi zote ambazo zinatakikana kuhudumia wananchi wa Jomvu tutaziweka katika jengo moja,” ameongeza Twalib

Categories
Habari

Wabunge washinikiza kuimarishwa kwa biashara kati ya Kenya na Tanzania

Kamati ya Bunge kuhusu Ushirikiano wa Kanda ya Afrika Mashariki imeweka mikakati ya kuimarisha biashara kati ya Kenya na Tanzania.

Akiongea wakati wa ziara mjini Isebania, Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo Ruweida Mohamed amesema biashara kupitia mpaka wa Kenya na Tanzania imekumbwa na changamoto ambazo zimeathiri mazingira ya utendaji biashara baina ya mataifa husika.

Hata hivyo, Ruweida ameeleza kuridhika na upimaji wa ugonjwa wa Korona kwenye mpaka huo ambao umeimarika kwa kiasi kikubwa licha ya changamoto za kisera kwenye mataifa husika.

Aidha ameeleza kufadhaishwa na ukosefu wa ushirikiano kati ya serikali ya taifa na ile ya Kaunti.

Wafanyabiashara wa humu nchini walikuwa wanalalamikia kuhangaishwa na maafisa wa usalama wa Tanzania na kufutiliwa mbali kwa leseni zao za kuhudumu.

Awali, katibu katika idara ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kevit Desai, alisema serikali imejitolea kuwakinga wafanyabiashara dhidi ya athari za ushuru wa juu.

Categories
Habari

Rais Kenyatta amtembelea mwenzake wa Italia, wajadili biashara na vita dhidi ya COVID-19

Rais Uhuru Kenyatta alimtembelea mwenzake wa Italia Sergio Mattarrella wakati huu ambapo anaendelea na ziara rasmi katika makao makuu ya Vatica.

Kwenye ziara hiyo, Rais Kenyatta amekusudia kuboresha uhusiano wa muda mrefu kati ya Kenya na Italia kama mshirika muhimu wa maendeleo.

Viongozi hao wawili wamejadili kuhusu njia za kuimarisha uhusiano wa kibiashara, uwekezaji na utalii.

Aidha, wameshauriana kuhusu namna ambavyo Kenya na Italia zinaweza kubadilishana mawazo kuhusu njia bora za kupambana na msambao wa COVID-19.

Italia ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi kote duniani na ugonjwa wa COVID-19 baada ya kuandikisha vifo vya zaidi ya watu elfu 40.

Jinsi ilivyo hapa nchini Kenya, Italia inapambana na wimbi la pili la ugonjwa wa COVID-19.

Italia ni miongoni mwa nchi zinazotegemewa zaidi Kenya kwa biashara ya utalii na uwekezaji.

Mnamo mwaka wa 2019, Kenya iliuza bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 kwa taifa hilo la Bara Ulaya, kiwango ambacho kilikuwa cha chini kwa kulinganisha na mwaka wa 2018 ambapo pato hilo lilikuwa shilingi bilioni 3.9.

Kenya inatafuta kuboresha zaidi uhusiano wake na Italia  kukiwa na lengo la kuvutia wawekezaji zaidi wa taifa hilo.