Categories
Habari

Munya:Sheria mpya za kahawa kuwanufaisha wakulima

Waziri wa kilimo, Peter Munya, amesema sheria zilizopendekezwa za sekta ya kahawa zinanuiwa kuwanufaisha wakulima wa zao hilo.

Akiongea na wakulima wa kahawa katika maeneo ya kariene na katheri katika kaunti ya Meru, Munya alisema sheria hizo mpya za sekta ya kahawa zinanuiwa kutokomeza makundi ya ulaghai katika sekta hiyo.

Kama ilivyojiri katika sekta ya majani chai, waziri alisema yuko kwenye ziara ya ushiriki wa umma kote nchini kupokea maoni ya wakulima wa kahawa kuhusu kanuni hizo mpya.

Munya alipongeza bunge la kaunti ya Meru kwa kupitisha mswada wa mchakato wa BBI, akiongeza kusema kwamba hati hiyo inanuiwa kuwanufaisha Wakenya wote.

Munya alisema atakuwa miongoni mwa viongozi wa Meru watakaokuwa mashinani kuwaelimisha watu kuhusu hati hiyo.

Categories
Habari

Raila: Situmii mchakato wa BBI kufika Ikulu

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, amepuuzilia mbali madai kwamba anatumia mchakato wa BBI kuwania urais.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alitaja madai hayo kuwa yasio na msingi kutoka wapinzani wake wa kisiasa.

Badala yake alisema, ikiwa anataka kutwaa uongozi wa kisiasa humu nchini, atatafuta uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura.

BBI sio njia ya mkato kwa Raila kuingia Ikulu. La hasha. Iwapo Raila anataka kuingia Ikulu, wakenya ndio watakaompeleka huko,” alisema Raila

Kulingana na waziri mkuu huyo wa zamani, uamuzi kuhusu atakayemrithi rais Uhuru Kenyatta muhula wake utakapokamilika utaafikiwa na Wakenya kupitia upigaji kura na wala sio kupitia mpangilio mwingine wowote.

Akiwahutubia waombolezaji jana wakati wa mazishi ya mwenda zake mbunge wa Bonchari, Oroo Oyioka ,Raila, hata hivyo alipigia debe mchakato wa BBI akisema unapendekeza kuiwezesha nchi hii kufikia upeo zaidi wa maendeleo.

Kiongozi huyo wa upinzani aliwashukuru wanachama wa mabunge ya kaunti ambao walihakikisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020 unaingia awamu ijayo.Bom

Kadhalika alielezea imani kwamba wabunge watapitisha mswada huo na kutoa fursa ya kuandaliwa kura ya maamuzi ambayo alisema anatumai itabainisha kwamba Wakenya wanaunga mkono kwa dhati mchakato wa BBI.

BBI sasa imefika bungeni kisha itaenda kwa wananchi. Tutakuja kuwaelezea mambo mazuri yaliyo ndani ya BBI. BBI ina manufaa mazuri kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo vya nchi hii,” aliongeza Raila

Categories
Habari

Ruto: Sitishwi na njama za mahasimu wangu

Naibu wa Rais Dkt. William Ruto sasa anasema anafahamu kuna njama ya kumzuia kuwa Rais wa taifa hili.

Ruto alidokeza kuwa mahasimu wake wa kisiasa wanafanya kila wawezalo kuhakikisha azma yake ya kuongoza taifa hili, halifui dafu.

Naibu huyo wa Rais aliyeyasema hayo akiwa katika kaunti ya Nandi hata hivyo alisema hatishwi dhidi ya njama zozote dhidi yake.

Wanapanga njama dhidi yangu Jijini Nairobi, lakini mimi nina watu mashinani. Hakuna tatizo lolote,”alisema naibu wa rais.

Katika kile kinachoonekana kana kwamba alikashifu mkutano uliowaleta pamoja Rais Uhuru Kenyatta,Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa ANC, Charity Ngilu wa NARC na Moses Wetangula wa FORD-Kenya, naibu huyo wa rais alishikilia kwamba uongozi wa taifa hili sio wa kupangiwa katika mikutano ya afisini.

Wanasema watapanga serikali ijayo kutoka Jijini Nairobi, lakini nawaeleza kwamba serikali ya mwaka 2022 haiwezi kupangwa baina ya viongozi wa kikabila,” alifoka naibu wa rais.

Ruto alisema “Serikali ijayo itabuniwa na wakenya wote. Itakuwa serikali inayoelewa maswala yanayowaathiri ‘ma-hustler’.

Naibu wa rais alisema hana nia ya ugawanaji wa mamlaka ya kisiasa, akisisitiza kuwa ataendelea kuhubiri ujumbe wake wa ‘hustler’ kote nchini.

Wanauliza nitaeneza vipi ajenda yangu. Jibu langu kwao ni kwamba nilimsaidia Raila Odinga kuwa waziri mkuu na nikamsaidia Uhuru Kenyatta kuwa rais wa taifa hili. Ninajua ninachofanya,” alisema Ruto.

Kuhusu swala la BBI,naibu wa rais William Ruto alisema wakenya hawapaswi kulazimishwa kuunga mkono marekebisho ya katiba nchini. Naibu wa rais ambaye alikuwa akiongea huko Kapsabet katika kaunti ya Nandi, aliwatahadharisha baadhi ya viongozi dhidi ya kuwalazimisha wananchi kuegemea upande fulani katika mchakato wa kurekebisha katiba.

Dkt. Ruto aliwapuuzilia mbali wale wanaojaribu kumsukuma kuongoza kampeini za kupinga mchakato huo wa kurekebisha katiba huku akisema kuwa Kenya ni taifa linalozingatia maongozi ya kidemokrasia na maoni ya kila mmoja ni muhimu.

Alisema kuwa wakenya wanapaswa kuachwa kufanya maamuzi yafaayo kuhusu maswala yanayoathiri maisha yao.

Categories
Habari

Viongozi wa kisiasa kuwaelimisha wakenya kuhusu ripoti BBI

Viongozi wa vyama vya kisiasa wameahidi kuwaelimisha wakenza katika juhudi za kuwahamasisha kuhusu fursa zilizopo kwenye ripoti ya BBI.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao waliwahimiza wakenya kuweka kando tofauti zao na kushirikiana katika kujenga kenya bora kwa vizazi vijavyo.

Kuhakikisha sauti ya kila mkenya inasikika na kuwezesha kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake, tutawaelimisha wakenya ili kuwahamasisha kuhusu fursa zilizopo katika taifa hili kupitia mpango huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Viongozi hao waliokutana katika Ikulu ya Nairobi siku ya Alhamisi, walielezea mpango wa kuwa na mkutano wa pamoja kati ya wabunge na viongozi wa kaunti tarehe 9 mwezi Machi mwaka huu.

Huku wakishukuru mabunge ya kaunti kwa kuunga mkono mswada wa BBI, viongozi hao wa vyama vya kisiasa walisema hatua hiyo ya mabunge hayo iliweka msingi ambapo taifa hili litaboresha usawa wa kijinsia, usawa wa fursa kwa wote sawia na kila mkenya kufurahia ufanisi unaoafikiwa nchini.

Jinsi wawakilishi wa kaunti walivyodhihirisha, sasa ni wakati kwa wakenya wote kuweka kando tofauti zao na kuungana pamoja katika kuboresha taifa hili, kwetu sisi, watoto wetu na kwa vizazi vya nchi hii vijavyo,” walisema viongozi hao.

Categories
Habari

Kaunti ya Nandi yakatalia mbali mswada wa BBI

Kaunti ya Nandi imekuwa ya pili kukatalia mbali mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.

wakati wa zoezi la kupigia kura mswada huo siku ya Alhamisi, wanachama 23 wa bunge la kaunti hiyo walipiga kura kupinga mswada huo huku 13 wakiunga mkono mswada huo.

Kaunti ya Nandi sasa inajiunga na kaunti ya Baringo kwa kupinga mswada huo wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.

Hata hivyo mswada huo tayari unaelekea kwa kura ya maamuzi baada ya kuafikia kiwango kinachohitajika ili kujadiliwa katika bunge la taifa na lile la Senate. Zaidi ya mabunge 40 ya kaunti yamepiga kura kuunga mkono mswada huo.

Siku ya Jumatano jopo linalosimamia mpango wa maridhiano humu nchini BBI, lilitoa wito kwa kaunti zilizosalia kuunga mkono mswada huo.

Ushindi mkubwa wa mswada huo ulioshuhudiwa ni ishara tosha kuwa utaungwa mkono katika kura ya maamuzi,” lilisema jopo hilo.

Jopo hilo liliwahimiza wabunge kupuuzilia mbali propaganda na kuiga mfano wa wawakilishi wodi katika kuunga mkono mswada huo.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alielezea matumaini kwamba ripoti hiyo ya BBI itaidhinishwa na wakenya bila pingamizi na hivyo kuleta mageuzi yanayopendekezwa

Baada ya kukamilika kwa zoezi la kupigia kura mswada wa marekebisho ya katiba, tunakaribia kuwapa wakenya marekebisho wanayohitaji ili kubuni taifa lenye umoja, dhabiti, linalowajumuisha wote na linalokabiliana vilivyo na uhalifu na ufisadi,” alisema kiongozi huyo wa chama cha ODM.

Categories
Habari

Gavana Mutua awataka wanaopinga BBI kukoma kuwapotosha Wakenya

Kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap Dkt. Alfred Mutua ametoa wito kwa wale wanaopinga mswada wa BBI kukoma kuwapotosha Wakenya.

Akiongea wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika eneo la Mwala, Mutua ambaye pia ni gavana wa Kaunti ya Machakos, amesema kuwa katiba haibadilishwi kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi bali inafanyiwa marekebisho ili kuiboresha.

Dkt. Mutua ameongeza kuwa katiba mpya itaongeza pesa zinazotengewa kaunti na kuimarisha maslahi ya Wakenya.

“Mnadanganywa kwamba eti tunabadilisha katiba,  hatubadilishi katiba. Hii ni kuongezea vipengele tu kwa katiba iliyopo,” amesema Mutua.

Ametoa wito kwa kaunti zilizosalia kupitisha mswada huo ili uwasilishwe bungeni na baadaye kwa wananchi ambao watatoa uamuzi wa mwisho kupitia kwa kura ya maamuzi.

Categories
Habari

Wakili Kanjama aitaka mahakama itupilie mbali mchakato wa BBI

Wakili Charles Kanjama amewasilisha kesi mahakamani ya kupinga mchakato wa kuidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020.

Kwenye ombi lake, wakili huyo anasema ana sababu za kuamini kuwa utaratibu uliotumiwa kukusanya na kuthibitisha saini za mpango wa maridhiano wa BBI haukutimiza masharti ya kikatiba.

Anaitaka mahakama ifutilie mbali uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba ilithibitisha saini zilizokusanywa na kupata kwamba mswada huo uliungwa mkono na zaidi ya wapiga kura milioni moja.

Aidha, Kanyama anataka hatua ya Tume ya (IEBC) ya kutuma mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020 wa katika mabunge ya kaunti ibatilishwe.

Wakili huyo anadai kwamba aliiandikia barua IEBC akitaka taarifa iwapo tume hiyo ilithibitisha saini za BBI kwa kulinganisha na saini zilizopo tayari na iwapo orodha ya wapiga kura iko na saini za wapiga kura.

Kanjama amesema IEBC ilimjibu kwamba haikuwa na uwezo huo na kwamba haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kufanya uthibitisho wa saini za wapiga kura.

Kulingana na wakili huyo, hatua ya mabunge ya kaunti kuendelea kujadili na kupitisha mswada huo inaibua wasiwasi kuhusu mchakato mzima na kwamba inafaa kusitishwa mara moja kwa sababu mchakato huo unafanyika kinyume cha katiba.

Categories
Habari

Kamati ya mswada wa BBI yahimiza Bunge kuiga mfano wa wawakilishi wadi ili kuupitisha

Kamati ya kitaifa ya mpango wa BBI imewapongeza wanachama wa mabunge ya kaunti kote nchini kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.

Kwenye taarifa, kamati hiyo imesema wawakilishi wadi wametekeleza wajibu wao wa kihistoria kwa kukubaliana na mchakato wa marekebisho hayo ya katiba yatakayowezesha taifa hili kusonga mbele.

“Pia tunawashukuru kwa kuisikiliza sauti ya wananchi wakati wa maamuzi yao kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020,” imesema taarifahiyo.

Kamati hiyo pia imewasifu Wakenya kwa kujitolea kwa wingi na kushiriki katika vikao vya ukusanyaji maoni ya umma kuhusu mswada huo, huku wakipuuzilia mbali habari za uongo zinazoenezwa na wanaopinga mchakato huo.

Wanakamati hao wanasema kupitishwa kwa mswada huo kote nchini ni ishara kwamba wananchi wa Kenya wamezungumza kwa sauti moja.

“Ushindi huu mkubwa unaashiria umaarufu wa BBI na ni ishara ya uungwaji mkono wa mswada wa BBI wakati wa kura ya maamuzi,” wakasema.

Na huku mswada huo ukielekea katika hatua ya mbele, kamati hiyo imewaomba wabunge kuzipa kisogo propaganda zinazoenezwa na kuwaiga wawakilishi wadi kwa kupitisha mswada huo katika Bunge la Kitaifa.

Hayo yanajiri huku mabunge zaidi ya kaunti yakiendelea kujadili mswada huo ambao tayari umetimiza masharti ya kikatiba ya kuungwa mkono na angalau mabunge 24 ya kaunti ili kuingia kwenye awamu nyengine.

Kufikia sasa mabunge 41 yamepitisha mswada huo, huku Bunge la Kaunti ya Migori likisalia la pekee lililokataa mswada huo.

Macho sasa yanaelekezwa kwa kaunti tano zilizosalia, ambazo hazijapigia kura mswada huo zikiwemo Nandi, Elgeyo Marakwet, Uasin Gishu, Mandera na Kilifi.

Sheria inasema mabunge ya kaunti yanafaa kuidhinisha rasimu ya mswada huo katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuwasilishwa.

Mswada huo sasa utawasilishwa kwa Spika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa na Ken Lusaka wa Seneti ili kupitishwa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atatia saini na kuuwasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa ajili ya kuandaa kura ya maamuzi.

Categories
Habari

BBI yapita magatuzini, sasa yaelekea Bunge la Kitaifa

Mswada wa marekebisho ya katiba ya mwaka 2020 kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa (BBI) umetimiza uungwaji mkono wa mabunge 24 yanayohitajika kikatiba ili uelekezwe katika Bunge la Kitaifa kujadiliwa.

Hii ni baada ya mabunge ya Kaunti 12 zaidi kupitisha mswada huo siku ya Jumanne na hivyo kutimiza matakwa ya kikatiba ya kupitishwa na angalau mabunge ya kaunti 24 ambayo ni zaidi ya nusu ya mabunge yote ya kaunti 47 nchini.

Kufikia Jumatatu alasiri, mabunge 12 yalikuwa tayari yamepitisha mswada huo, yakiwemo Homabay, Siaya, Kisumu, Pokot Magharibi, Busia, Trans Nzoia, Kajiado, Kisii, Vihiga, Nairobi, Laikipia na Samburu, huku kaunti ya Baringo ikiwa ya pekee iliyokataa mswada huo.

Mabunge mengi ya kaunti yalikuwa yameratibu kujadili mswada huo Jumanne huku yale ya Kakamega, Narok, Makueni, Nyamira, Taita Taveta, Murang’a, Bungoma, Kitui, Nyeri, Lamu, Nyandarua na hivi sasa Garissa pia limepitisha mswada huo na kutimiza idadi ya 24.

Haya yanajiri huku kaunti zengine zikiendelea kujadili msawa huo na zengine zikiwa bado zinachukua maoni ya wananchi.

Categories
Habari

Kura ya maamuzi yanukia huku kaunti zikiendelea kupitisha BBI

Siku ya Jumanne huenda ikaamua mwelekeo wa mchakato wa marekebisho ya katiba humu nchini, huku mabunge kumi ya kaunti yakitarajiwa kuidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Mabunge ya Kaunti za Narok, Makueni na Machakos yamesema yako tayari kuunga mkono mswada huo utakapowasilishwa siku hiyo na hivyo kuongeza uwezekano kwamba hitaji la kikatiba la kuwa na angalau kaunti 24 zilizouithibisha mswada huo litatimizwa.

Bunge la Kaunti ya Samburu ndilo la hivi punde kupitisha mswada huo na kufikisha 12, jumla ya kaunti zilizopitisha mswada huo.

Kaunti hizo ni pamoja na Siaya, Homabay, Kisumu, Busia, Pokot Magharibi, Trans Nzoia, Kajiado, Kisii, Vihiga, Nairobi, na Laikipia, huku Baringo ikisalia kaunti ya pekee kukatalia mbali mswada huo.

Hivi leo Gavana wa Kaunti ya Makueni Kivutha Kibwana ameonekana kubadili msimamo akisema ataunga mkono mchakato huo n ahata kuwahimiza wawakilishi wadi wa kaunti hiyo kufuata mkondo huo.

Mabunge ya kaunti kadhaa za eneo la Mlima Kenya yanatarajiwa kujadili mswada huo Jumanne, unaohitaji kuungwa mkono na angalau mabunge 12 zaidi ili kutoa fursa ya marekebisho ya katiba.

Kaunti zengine zinazotarajiwa kujadili mswada huo wiki hii ni Tharaka Nithi, Nakuru, Nyeri, Embu, Murang’a, Migori, Bungoma, Kakamega na Taita Taveta.

Awali, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga alikuwa alisema ana imani kwamba kufikia Jumanne wiki hii, mswada huo utakuwa umeungwa mkono na idadi ya kaunti zinazohitajika kikatiba.