Categories
Habari

Maafisa wa afya waliofutwa katika kaunti ya Kirinyaga hawatarejeshwa kazini

Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Mumbi Waiguru amesema maafisa wa afya ambao walikuwa wameachishwa kazi na serikali ya kaunti hiyo hawatarejeshwa kazini.

Akiongea kwa njia ya video wakati wa mkutano na kamati ya bunge kuhusu maswala ya afya, gavana huyo alisema nafasi za wahudumu hao tayari zimechukuliwa na wengine.

Alisema kuwa hakuna bajeti ya ziada iliyotengwa kuwaajiri upya huku akiongeza kuwa hawakutuma maombi ya kazi wakati nafasi za ajira kwenye mpango wa huduma ya afya kwa wote zilipotangazwa.

Gavana huyo ,aliongeza kuwa kesi zote zilizowasilishwa mahakamani na chama cha madaktari na wataalam wa meno (KMPDU) pamoja na muungano wa wauguzi nchini  (KNUN) dhidi ya kaunti hiyo hazikufaulu.

Lakini kwenye ujumbe wakati wa kikao hicho,kaimu naibu katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini Dennis Miskellah alishinikiza kuzingatiwa kwa utaratibu wa bodi ya tume ya kuwaajiri watumishi wa umma kuhusu swala hilo.

Alihimiza tume hiyo kuingilia kati swala hilo.

Pia alitoa wito wa kubuniwa kwa tume ya kuwaajiri watumishi wa afya ili itakayoshughulikia maswala ya sekta ya afya.

Categories
Habari

Kaunti ya Kirinyaga yajizatiti kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu

Serikali ya kaunti ya Kirinyaga imeimarisha juhudi za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu unaoendelea kuenea miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo.

Takwimu za idara ya afya ya kaunti hiyo zinaonyesha kwamba kaunti hiyo ina visa vingi vya ugonjwa wa kifua kikuu, ambapo watu 245 kati ya laki-1 walikuwa na ugonjwa huo kufikia mwaka 2018.

Visa vya ugonjwa huo kutoweza kuponywa na dawa viliongezeka kwa asilimia 50 kati mwaka   2016 na 2018, hali ambayo imetokana na kutozingatiwa vyema kwa maagizo ya utumizi wa dawa.

Gavana Anne Waiguru amesema kwamba idara ya afya imekuwa ikiwahamasisha wahudumu wa afya na wale wa kijamii ambao kisha huelimisha wananchi kuhusu kuzuia ugonjwa wa kifua kikuu, kupimwa kwa wakati ufaao na kutafuta huduma za matibabu.

Waiguru alisema serikali ya kaunti hiyo imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa wa kifua kikuu kilicho na vitanda 24 katika hospitali ya Kerugoya.

‘Kituo hicho cha kuwatenga wagonjwa wa kifua kikuu kitasaidia katika uangalizi na pia  kuwatibu wagonjwa wa kifua kikuu,”alisema Waiguru.

Kwa upande wake waziri wa afya wa kaunti hiyo Gladys Kimingi alisema wagonjwa wa kifua kikuu wamekuwa wakipokea matibabu yanayofaa licha ya kuwepo kwa janga la Covid-19.

Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo walio na dalili za kifua kikuu  zinazojumuisha kukohoa kwa muda mrefu kutembelea kituo hicho ili wapimwe na pia kupokea matibabu.

Categories
Habari

COVID-19: Afisi za Kaunti ya Kirinyaga zafungwa kwa muda

Afisi za Serikali ya Kaunti ya Kirinyaga zimefungwa kwa siku 14 baada ya baadhi ya wafanyikazi kuambukizwa virusi vya Corona.

Akitangaza hatua hiyo, Gavana wa Kaunti hiyo Ann Waiguru amesema afisi hizo zitafungwa kuanzia leo ili kuwalinda wafanyikazi na maambukizi ya virusi hivyo.

Waiguru ameongeza kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yameongezeka miongoni mwa maafisa wa serikali ya kaunti licha ya juhudi za kuudhibiti msambao huo.

Waiguru amesema ongezeko la vifo vinavyotokana na ugonjwa huo Kauntini humo pia ni swala la kufadhaisha.

Gavana hiyo pia amemuagiza Afisa Mkuu wa Afya wa serikali ya kaunti hiyo kuwafanyia upimaji wa jumla wafanyikazi wa idara zilizoathirika na kuharakisha utoaji wa matokeo ya vipimo hivyo ili kuwezesha familia za watakaopatikana na ugonjwa huo zijitenge.

Amesema juhudi za kuendelea na shughuli za serikali ya kaunti afisini huku wafanyikazi wakitangamana kwa kuzingatia masharti ya kudhibiti Korona hazijafua dafu na akatoa wito kwa wafanyakazi hao kuandaa vikao vyao ‘kidijitali.’

“Wakati wa kufanyia kazi nyumbani, maafisa wa kaunti watafanya mikakati ya kuhakikisha idara za kutoa huduma muhimu zinaendeshwa kwa kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya za kuzuia maambukizi,” akasema Waiguru.

Amesema mawasiliano yatafanywa kwa njia ya simu au barua-pepe.

Categories
Habari

Balozi wa Marekani ashtumu hatua ya kutumia vijana kuzua vurugu humu nchini

Balozi wa Marekani humu nchini Kyle McCarter amesema nchi yake haitabakia kimya na kutazama vijana wakiendelea kuchochewa na wanasiasa kuzua vurugu humu nchini.

Wakati uo huo, Kyle amekanusha madai kwamba nchi yake inapanga kufutilia mbali hati za Visa za maafisa wa ngazi za juu serikalini, kwa kukatiza uhuru wa kujieleza, kutangamana na kujikusanya pamoja humu nchini.

Balozi huyo ambaye alikuwa akiongea wakati wa ziara ya kutoa mchango wa barakoa kwa utawala wa Kaunti ya Kirinyaga, amesema hafahamu lolote kuhusu habari hizo huku akitaja madai hayo kuwa ya uongo.

Akiwa ameandamana na Gavana wa Kirinyaga Ann Mumbi Waiguru, Kyle pasipo kutoa maelezo zaidi amesema hakuna uamuzi wowote kama huo ambao umeafikiwa na nchi yake, na akahimiza WaKenya kupuuza uvumi wa aina hiyo.

Pia amesema kwamba wale watakaopatikana na hatia kufuatia kupotea kwa fedha za kupambana na janga la COVID-19, watakabiliwa na hatua kali kutoka kwa serikali yake.

Kuhusu usalama, Kyle amesema kwamba serikali za Marekani na Kenya zinashirikiana kwa karibu ili kushinda kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Categories
Habari

Wasichana katika kaunti ya kirinyaga kunufaika na visodo kutoka kwa Gavana Waiguru

Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru ameanzisha zoezi la kutoa visodo kama njia mojawapo ya kuimarisha mtoto msichana.

Katika hafla iliyoandaliwa katika shule ya upili ya Kiamugumo  Alhamisi, gavana huyo alitoa visodo kwa takribani wasichana 500 katika eneo hilo.

Hii sehemu ya pakiti 27,000 za visodo vinavyonuiwa kuwasaidia wasichana 9,000.

Waiguru alisema zoezi hilo ni mpango wa serikali ya kaunti hiyo ya kuimarisha mtoto msichana utakaowawezesha kusalia shuleni wakati wa hedhi.

Gavana huyo alisema wasichana watatu kati ya kumi hukosa kwenda shuleni kila mwezi wakati wa hedhi.

“Hedhi ni jambo la kawaida ambalo halipaswi kusababisha wasichana kukosa shule. Tunafanya bidii kuhakikisha mtoto wa kike anapata fyrsa sawa ya kwenda shuleni sawia na mtoto wa kiume,” alisema Waiguru.

Mpango huo unatekelezwa na wizara ya elimu ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na ile ya jinsia ambao umekuwa ukisambaza visodo na kuwashauri wasichana katika kaunti hiyo.

Gavana huyo alisema akiwa gavana mwanamke wa pekee katika eneo la mlima Kenya, atakuwa kielelezo kwa wasichana na kuwapa motisha ya kuafikia ndoto zao maishani.

“Wasichana wanaweza kuafikia ndoto zao sawa na wavulana iwapo watatia bidi,” alisema gavana huyo.

Gavana huyo alikuwa ameandamana na wawakilishi kadhaa wa kaunti hiyo pamoja na mawaziri wa wa kaunti hiyo.